Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 28 ya Mwaka A wa Kanisa: Ndani ya Adhimisho la Ekaristi Takatifu kuna mwaliko wa kuingia katika Ufalme wa Mungu. Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 28 ya Mwaka A wa Kanisa: Ndani ya Adhimisho la Ekaristi Takatifu kuna mwaliko wa kuingia katika Ufalme wa Mungu. 

Tafakari Jumapili 28 Mwaka A: Ekaristi Takatifu: Karamu Ya Upendo

Liturujia ya Neno la Mungu: Karamu hii ya Bwana ni ile ambayo inaandaliwa kwetu katika Adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ndani ya adhimisho la Ekaristi Habari Njema hutangazwa na mwaliko wa kuuingia ufalme wa Mungu hutolewa. Kwa namna ya pekee kabisa, adhimisho la Ekaristi ni kiashirio hicho cha karamu ya Ufalme wa Mungu ambayo tunaanza kuishiriki tukingali hapa duniani.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 28 ya mwaka A wa Kanisa. Ni masomo yanayotoa matumaini ya ujio wa neema za Mungu kwa watu wake, Neema hizi ndio Habari Njema ya Ufalme wake na Habari hii inazotolewa kwa wote walio tayari kuipokea lakini pia neema hii ni mwaliko unaohitaji mwitikio chanya na wa mtu binafsi kwa wote wanaoalikwa kuzipokea. Somo la kwanza (Is 25:6-10A) ni kutoka Kitabu cha Nabii Isaya. Katika somo hili nabii anazungumza juu ya karamu ya vinono iliyoandaliwa kwa watu wote, karamu ambayo imeandaliwa katika mlima wa Bwana. Akingali anazungumza juu ya karamu, hapo hapo anatambulisha kitu kipya. Anaongea juu ya kuondoa utando uliowaweka mateka watu wake pamoja na kuyahukumu mataifa. Ni kitu gani sasa ambacho Nabii Isaya anakizungumzia?  Huu ni unabii ambao Isaya anautoa katika kipindi ambacho Waisraeli wako utumwani Babeli.

Nabii Isaya anapowapa waisraeli ujumbe wa sherehe ambayo Mungu atawaandalia, na tena sherehe itakayofanyika katika mlima wa Bwana, anamaanisha kuwapa matumaini kuwa utumwa wao utaisha na watarudi katika nchi yao. Huo mlima wa Bwana anaouzungumzia ndio mlima Sioni ambapo ndipo lilipokuwa limejengwa Hekalu, alama ya uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Ujumbe huu unakwenda snjari na kutangazia hukumu kwa mataifa. Haya ni yale mataifa watesi wa Waisraeli waliokuwa wamewachukua mateka. Mungu anawatangazia neema watu wake ikiwa ni pamoja na kuwaondolea vikwazo vinavyowazuia wasiufurahie uwepo wake kati yao. Mungu anajitambulisha na kujidhihirisha kwao kuwa ni Mungu anayeokoa.

Somo la pili (Waf. 4:12-14, 19-20) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Mtume Paulo anauandika waraka huu akiwa kifungoni Roma. Katika somo la leo, Mtume Paulo anawapitisha Wafilipi katika historia yake: mambo aliyopitia na jinsi alivyoweza kukabiliana na hali mbalimbali katika maisha yake. Anakiri kuwa ameishi  katika vipindi vya kukosa mahitaji na ameishi pia katika vipindi vya kuwa na kila kitu alichohitaji, ameishi katika vipindi vya majonzi lakini pia ameishi katika vipindi vya furaha. Anakiri kuwa katika yote hayo amefanikiwa kwa sababu ya tumaini lake kwa Mungu. Kauli mbiu iliyomwongoza ndiyo hii “nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu”. Mtume Paulo anajua wazi kuwa kwake kifungoni kutakuwa kumewahuzunisha sana waamini wake. Kwa sehemu kubwa anapenda kuwatia moyo wasione kifungo chake kama ni kushindwa kwa kazi nzima ya uinjilishaji. Kwa Mtume Paulo, hali rahisi na hali ngumu ni mapito katika kazi ya uinjilishaji. Anawaasa wasife moyo bali waimarike kama yeye alivyoimarika tangu mwanzo kwa hali mbalimbali alizozipitia.

Injili (Mt 22:1-14) Injili ya dominika hii ya 28 ya Mwaka A wa Kanisa ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Katika injili hii, Yesu anaendelea kutoa mifano kuhusu ufalme wa Mungu. Ufalme huu anauelezea kama sherehe ya harusi ambayo mfalme mmoja alimwandalia kijana wake. Kitu cha kushangaza katika harusi hiyo ni kwamba wageni walioalikwa kuja hawakuja. Wengine waliupuuzia na wengine basi tu waliendelea na shughuli zao. Mfalme alikasirika, akatuma majeshi yake yakaenda kuwaangamiza wageni wale na kuchoma moto miji yao. Baada ya hilo, akatuma watumishi wake waende katika njia kuu kukusanya yoyote watakayemwona aje kwenye harusi. Njia hiyo ikafanikiwa na harusi ikajaa watu. Tatizo linatokea pale ambapo mfalme anapita kuwaangalia wageni wake, akagundua kuna mmoja ameingia akiwa hana vazi la harusi. Akaamuru afungwe mikono na miguu na kutupwa katika giza la nje ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.

Mfano huu ambao Yesu anautoa unaacha maswali mengi hasa kwetu sisi wasikilizaji na wasomaji wa leo. Kwa nini wageni wote wapuuzie mwaliko wa harusi? Kwa nini mfalme awaue waliokataa kuja harusini na achome miji yao? Ametuma watu katika njia kuu wakusanye yeyote watakayemuona aje harusini, kwa nini alimwondoa na kumtupa nje yule ambaye hakuwa na vazi la harusi? Na mwisho Je? Ilikuwa ni kawaida kwa jambao kama hili kutokea? Ndugu zangu, kuuelewa mfano huu ni muhimu kuzingatia kuwa Yesu hazungumzii tukio moja bali anarejea historia nzima ya wayahudi katika kuupokea ufalme wa Mungu. Anazungumza juu ya matukio yaliyopita, matukio yaliyopo na yale yajayo kuhusu ufalme wa Mungu. Harusi yenyewe ndiyo Habari Njema ya wokovu ambayo Mungu anaitangaza na kuwaalika watu wote waipokee. Huko nyuma, Wayahudi hawakuipokea Habari hii njema. Waliipuuzia na kila mmoja akaendelea kushika njia ya maisha yake kama kawaida. Hata Mungu alipotuma wajumbe wake manabii kuamsha dhamiri zao hakuna aliyeutilia maanani mwaliko wao. Kwa sababu hiyo, Mungu aliwaacha washambuliwe na adui zao ambao waliwaua, walichoma moto miji yao na kuwapeleka utumwani. Hiyo yote ilikuwa ni kuwasaidia kuamsha dhamiri zao ili wamrudie na kupokea mwaliko wake.

Wakati huo sasa umepita. Wayahudi wapo katika wakati ambapo wajumbe wa Habari Njema wanazunguka katika njia kuu wakiwaalika watu kuipokea Habari Njema. Mwaliko huu ni wa jumla na ni wa wote, ila jibu lake daima ni la mtu binafsi. Kila mmoja anapaswa kuuitikia kama mtu binafsi, akiufungua moyo wake na kuutayarisha ili Habari hiyo Njema ipate kuzaa matunda ndani yake. Kushindwa kufanya hivyo ni sawa na kukosa vazi la harusi. Na itakapofika sasa ambapo mfalme atakuja kuwapokea wageni wake na akamkuta mmoja hajautayarisha moyo wake basi atafungwa mikono na miguu na kutupwa nje kutakakokuwa na kilio na kusaga meno.  Ndipo hapo Yesu anaongeza na kusema, “waitwao ni wengi lakini wateule ni wachache” kuonesha kuwa mwaliko daima ni wa wote lakini kila mmoja anapaswa kuushughulikia kama mtu binafsi kwa kuuandaa moyo wake na kwa kujitahidi kuyageuza maisha yake ili astahilishwe kuwa miongoni mwa wateule atakapokuja Bwana.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu ya dominika hii ya 28 ya mwaka A wa Kanisa yamezungumza juu ya mwaliko wa Karamu ambayo ni Mungu mwenyewe anawaandalia watu wote na kuwaalika wote ili waishiriki. Ufafanuzi wa masomo haya umetuonesha kuwa karamu inayozungumzwa katika Maandiko Matakatifu ni Habari Njema ya ufalme wa Mungu na hapo hapo ni mwaliko wa kuuingia. Karamu hii ya Bwana ni ile ambayo inaandaliwa kwetu katika Adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ndani ya adhimisho la Ekaristi Habari Njema hutangazwa na mwaliko wa kuuingia ufalme wa Mungu hutolewa. Kwa namna ya pekee kabisa, adhimisho la Ekaristi ni kiashirio hicho cha karamu ya Ufalme wa Mungu ambayo tunaanza kuishiriki tukingali hapa duniani. Ni mwaliko wa wote na sote tunaalikwa kuujongea tukiwa na moyo safi kama lile vazi la harusi linalotakiwa katika karamu. Leo tunaona waziwazi kuwa kuiishi Ekaristi ipasavyo ni kuuishi mwaliko wa Karamu ya Ufalme wa Mungu. Tujibidiishe basi kuadhimisha, kushiriki na kupokea Ekaristi Takatifu mara kwa mara ili tuendelee kukaa ndani ya mwaliko wa Karamu ya Ufalme wa Mungu na tustahili kuhesabiwa kati ya wateule wake.

Liturujia Jumapili 28

 

 

 

 

09 October 2020, 15:48