Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 27 ya Mwaka A wa Kanisa: Waamini wanaalikwa kuzaa matunda mema yanayomwilishwa katika haki jamii. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 27 ya Mwaka A wa Kanisa: Waamini wanaalikwa kuzaa matunda mema yanayomwilishwa katika haki jamii. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 27: Matunda Mema Na Haki Jamii

Mwana anayezungumziwa katika Injili ni Yesu Kristo. Wakati wa mavuno, ndio saa ile ya neema na wokovu ambayo Mungu daima anaingilia kati ili kutuweka sisi karibu naye. Mungu daima hafurahii kifo cha mtu mwovu bali atubu na kuiacha njia yake mbaya ili aishi. Yesu anasema: “Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake’’.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Shamba la mizabibu, ndio hasa neno tunalolisikia likijirudia si tu katika somo la Injili bali hata kutoka kwa somo letu la kwanza la leo kutoka Nabii Isaya. Ni wimbo wa mapenzi, katika Agano la Kale, shamba la mizabibu ni lugha ya picha inayowakilisha mwanamke anayependwa, kutoka Kitabu cha Wimbo Ulio bora, mke anatambulishwa kama mzabibu uliochanua maua. Lakini pia shamba la mizabibu linawakilisha taifa lile teule la Wanawaisraeli.  Wimbo huo wa mapenzi tunaona pale mwanzoni unatoa maneno mazuri na ya kuvutia lakini mwishoni ni maneno ya kukatisha tamaa kwani badala ya matunda mema, shamba lile likazaa zabibu-mwitu. Mshangao kwa upande wa Mungu aliyekuwa anasubiri na kutegemea matunda mema kutoka katika shamba lake la mizabibu: Badala ya kuona hukumu ya haki (mishpat kwa Kiebrania), akaona dhuluma (Mispah kwa Kiebrania); alitarajia kuona haki (sedaqah kwa Kiebrania), na badala yake akaona kilio (se’aqah kwa Kiebrania). Somo la Injili ya leo kama somo la kwanza pia tunasikia mfano wa shamba la mizabibu. Yesu anatumia lugha hiyo kwa hakika iliyoeleweka vyema kwa wasikilizaji wake. Tofauti na Nabii Isaya, katika somo la Injili hatusikii juu ya Mungu kuwa ni mmiliki wa shamba la mizabibu na badala yake ni mwenye nyumba.

Shamba la mizabibu kadiri ya Nabii Isaya lilizaa mizabibu-mwitu ila katika somo la Injili lilizaa zabibu nzuri lakini wakulima waliwatenda jeuri watumwa wa mwenye shamba na hatimaye hata na mwana wa mwenye shamba kwa kuwa walimwona ni tishio zaidi kama mrithi.  Na hitimisho lake pia ni tofauti kwani mwenye nyumba halitelekezi shamba lake bali anawapa wakulima wengine wanaokuwa waaminifu kwa kukusanya matunda kiaminifu kwa mwenye nyumba. Yesu leo anazungumzia juu ya mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima na kusafiri. Mwenye nyumba au mmiliki wa shamba kama ilivyokuwa enzi zile kwa desturi alikodisha wakulima na yeye aliishi maeneo ya mijini na hivyo kutuma watumishi wake kwenda wakati wa mavuno ili kupata sehemu ya kodi yao. Cha kushangaza wakulima wale wakawatenda jeuri watumwa wa mwenye nyumba. Yawezekana waliwatenda jeuri kwa kuwa hawakupata matunda mengi na mazuri, au labda hakuwa tayari kutoa sehemu ya jasho la kazi yao kwa mmiliki wa shamba lile kwa tamaa zao, yawezekana pia hawakuwajibika vema na hivyo kukosa cha kumpa mwenye shamba.

Watumwa wa mwenye shamba walipotumwa na mwenye nyumba tunasoma kuwa wakawakamataka watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Hata baada ya kuwatendea mabaya tunaona mwenye nyumba bado analipenda shamba lake na anategemea matunda kutoka katika shamba lake, hakukata tamaa au hakusita kuacha kutuma watumwa wake shambani ili kukusanya matunda. Tena anatuma wengi zaidi kuliko awali, lakini hata na hawa nao wanatendwa jeuri na wakulima wale. Kama jaribio lake la mwisho anaamua sasa kumtuma mwana wake, lakini hata naye wakulima wale wakamkamata na kumuua kwani walijua huyu ndio mrithi wa shamba, ndio kusema walikuwa si tu na nia ya kutokutoa matunda bali hata na kujimilikisha shamba lile ili liwe lao. Kwa kweli kama ilivyokuwa kwa somo la kwanza la leo, hata katika somo la Injili tunaweza kuona kila muhusika wa mfano huo una maana na ujumbe kwetu kama Wakristo.

Mwenye nyumba ni Mungu mwenyewe, ndiye anayelipenda na kulitunza shamba lake la mizabibu yaani jumuiya ya waamini, Kanisa lake ili lizae matunda na kuyakusanya kwake. Akalizungushia ugo ndio kusema ili libaki salama kutoka maadui, na ugo unamaanisha hazina kubwa ambayo jumuiya hii inaachiwa na Mungu ndio Neno lake. Ni kwa msaada wa Neno lake jumuiya ile inaweza kuenenda katika njia inayokuwa salama, yenye uhakika kwa asilimia zote. Wakulima wale tunaweza kuwafananisha na viongozi wa kidini na kisiasa, wenye wajibu wa kuwaongoza watu ili kuzaa matunda mema na kwa kuyakusanya kwa mwenye shamba kwa wakati muafaka. Kama tulivyosoma katika somo la kwanza, matunda yaliyokuwa yakitarajiwa ni matendo ya upendo na haki jamii. Makundi mawili ya watumwa waliopelekwa kukusanya matunda tunaweza kuyafananisha na makundi ya Manabii waliotumwa kabla na baada ya uhamisho wa Babeli.

Hata baada ya uhamisho alituma Manabii wengi kuliko kabla ili kuwasaidia Waisraeli wajibu wao wa kutunza maagano ya uaminifu na Mungu aliyewatoa katika nchi ya utumwa na kuwapa nchi ile ya maziwa na asali. ‘’Tangu siku ile wazee wenu walipotoka nchini Misri hadi leo, sijakoma kuwatuma kwenu watumishi wangu, manabii. Lakini hamkunisikiliza wala kinitegea sikio, ila mlizidi kuwa wakaidi, mkawa waasi kuliko hata wazee wenu’’ Yeremia 7:25-26. Na watumwa wale tunasoma kutoka Kitabu cha pili cha Mambo ya Nyakati 24:21 ‘’Lakini wakamfanyia njama; na kwa amri ya mfalme, wakampiga mawe kwenye ua wa nyumba ya Mwenyezi Mungu wakamuua’’. Mwinjili Mathayo anapoandika Injili hii anaakisi hali iliyokuwepo kati ya Kanisa lile la Mwanzo na watu wa taifa lile teule. Msuguano uliokuwepo na madhulumu waliyopitia kama Kanisa kutoka kwa Wayahudi kwa Kanisa lile la mwanzo. Wakulima wale hawataki kumpa mwenye shamba nafasi yake anayostahili ya kukusanya matunda kwani ni matunda ya shamba lake, ndio kusema wanataka kujimilikisha shamba lile. Kujimilikisha ni sawa na kuenenda kama vile Mungu au mwenye shamba la mizabibu kana kwamba hayupo. Ni maisha yetu kila mara tunapokataa kuongozwa na Mungu kwa kuishi kadiri ya matakwa na matamanio yetu, tukikataa kuongozwa na Neno lake na kubaki kufuata mantiki zetu za kibinadamu.

Mwana anayezungumziwa katika somo la Injili ni Yesu Kristo. Wakati wa mavuno, ndio saa ile ya neema, saa ile ya wokovu ambayo Mungu daima anaingilia kati ili kutuweka sisi karibu naye. Mwishoni mwa somo la Injili ya leo, Yesu anawauliza wasikilizaji wake juu ya mtazamo wao juu ya wakulima wale waovu. Jibu lao linaakisi pia mtazamo wa kibinadamu. “Wakamwambia, atawaangamiza vibaya wale wabaya, na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake’’. Lakini tunasoma na kushangazwa na jibu la Yesu kwao, Yesu hakuwa na jibu la kuangamiza na kuteketeza kwa ukali kwani Mungu daima hafurahii kifo cha mtu muovu bali atubu na kuiacha njia yake mbaya ili aishi. Na ndio Yesu anawaambia; “Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake’’. Kabla ya hitimisho tunaona Yesu anatumia maneno yanayomrejelea yeye mwenyewe; “Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu’’. Ni maneno yanayozungumzia juu ya kifo na ufufuko wa Yesu. Ni yeye aliyekamatwa na wakuu wa watu na kuteswa na kuuawa. Ni wakuu wa watu waliomkamata na kumtupa nje ya shamba lile la mizabibu la Baba yake.

Ni Yesu aliyeonekana kuwa anakufuru kwa kujiita Mwana wa Mungu, mtu aliye najisi aliyestahili kutupwa nje ya mji ule mtakatifu wa Yerusalemu. Lakini Mungu akamuinua kwa kumfufua kutoka wafu na kumuweka kuwa mkuu wa shamba lake, amekuwa jiwe kuu la pembeni walilolikataa waashi kwalo Kanisa lake likapata kujengwa na kuwepo. Yafaa tukumbuke hata nasi na kuzingatia kuwa kila mara tunapokosa kuzaa matunda ni sawa na kushiriki katika kumnyima Mungu nafasi yake kama mwenye nyumba. Ni kushiriki katika kuliangamiza Kanisa lake kwa maisha yetu yasiyozaa matunda mema, kukosa kuwa mashuhuda wa Injili ni kumkataa Mungu aongoze na kuyapa dira maisha yetu. Matunda mema ni maisha mema yanayotarajiwa kutoka kwa kila mmoja wetu, ni sisi tunaopendwa na Mungu kiasi cha kutuwekea ugo ili tubaki salama, ugo ni Neno la Mungu, mnara ni Neno la Mungu linalotuhakikishia kila mara kujilinda na adui yetu ambaye ni mwovu shetani, Yesu ametuwekea pia Sakramenti za Kanisa ili daima tubaki salama. Ni kwa msaada wa Neno lake na maisha ya Kisakramenti kila mbatizwa anabaki salama dhidi ya adui muovu.

Mwinjili Mathayo kama nilivyotangulia kusema anatutahadharisha hata nasi kwani kila mmoja kwa ubatizo wetu tunaalikwa kufanya kazi katika shamba la mizabibu na hivyo kutarajiwa matunda mema. Mwinjili Mathayo zaidi ya kutoa onyo kwa wakuu wa Wayahudi bali hata kwetu nasi Wakristo, kukumbuka kuwa hata nasi tunaweza kuwa hao wakulima wabaya na wakatili. Huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu ni wa kushangaza kwani Mungu haliachi au kulitelekeza shamba lake bali daima anatafuta wengine wanaoweza kufanya kazi kiaminifu na kutoa matunda kwa wakati. Na ndio tunaona Kanisa la Kristo linazidi kushamiri na kukua popote duniani hata kama wale waliopokea mwanzoni imani wamekuwa wakulima wabaya kwa kukataa kuzaa matunda mema. Daima Mungu anaingilia kati kuona kuwa shamba lake linabaki, taifa lake linabaki na ndio Jumuiya ya waamini, yaani Kanisa. Kanisa ni shamba la mizabibu nasi wabatizwa ni wakulima tunaotumwa kufanya kazi katika shamba hilo zuri na kutoa matunda mema kwa wakati.

Katika karamu ya mwisho Yesu anatumia tena lugha ya mfano ya mzabibu na hapa anajitambulisha Yeye mwenyewe kuwa ni mzabibu. “Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda yeye huliondoa, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi’’ (Yohane 15:1-2). Bado mwaliko wa Yesu ni ule ule wa kuzaa matunda, ni kwa kuishi kwa kujishikamanisha naye ndio njia pekee inayotuhakikishia sisi kuzaa matunda, tukiwa mbali naye hakika hatuwezi kitu, ni kwa neema na msaada wake tunahakikishiwa kuzaa matunda. Ni kwa kukubali kuongozwa na Neno lake na kushiriki maisha ya Sakramenti tunaweza kuzaa matunda mema katika maisha yetu. Kwa kweli ujumbe kusudiwa kutoka somo la Injili ya leo hatuupati kwa wale wakulima wakatili, bali hasa kutoka shamba la mizabibu lenyewe na mwenye nyumba, hasa upendo wake mkubwa kwa shamba lake la mizabibu na hivyo kila mara kusaka wakulima wengine na kuwakabidhi shamba lake. Ndio kusema kama sisi tutakosa kuwa waaminifu na kushindwa kuzaa matunda basi daima mwenye nyumba atasaka wengine na kuwakabidhi shamba lake la mizabibu.

Wakulima wale wabaya walitamani kujimilikisha shamba na ndio kilikuwa kishawishi chao kikubwa kwa kutenda jeuri na hata hatimaye kumuua mwana wa mwenye shamba. Ni kishawishi hata kwetu leo yafaa tukumbuke sisi sio wamiliki bali ni wakulima tunaotumwa kufanya kazi kiaminifu katika shamba, shamba ni la Mungu mwenyewe, Kanisa sio mali yetu bali ni la Mungu mwenyewe, hakuna hata mmoja anayepaswa kupata kishawishi cha kufikiri kuwa sisi ni wamiliki, kwani kwa kufikiri na kutenda kama sisi ni wamiliki basi nasi tutaishia kuwa wakulima wabaya, kwani tutashindwa kuongozwa kadiri ya mapenzi ya mwenye shamba bali kwa mapenzi yetu wenyewe, na ndio wakawatenda jeuri manabii kwani hawakutaka Mungu aongoze maisha yao. Nasi leo hatuna budi kukumbuka kuwa maisha yetu daima lazima yaongozwe na Mungu mwenyewe, kwa kulisoma na kulishika Neno lake, ni Mungu anaongea nasi katika Maandiko Matakatifu. Nawatakia tafakuri na Dominika njema.

03 October 2020, 14:46