Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukuu na Utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukuu na Utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! 

Tafakari Jumapili 29 Mwaka A: Utukufu na Ukuu wa Mungu!

Maandiko Matakatifu ya dominika hii ya 29 ya mwaka A wa Kanisa yamezungumza juu ya uwiano unaopaswa kuwapo kati ya mahitaji ya kimwili ya mwanadamu na yale ya kiroho. Kristo amelifupisha fundisho hilo aliposema “mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari na mpeni Mungu yaliyo yake Mungu”. Mwenyezi Mungu apewe nafasi yake katika maisha ya mwamini! Je, viongozi?

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 29 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Is 45:1, 4-6) ni kutoka Kitabu cha Nabii Isaya. Ni somo linalozungumzia kitu ambacho kwa kiasi fulani kinashangaza. Koreshi alikuwa ni mfalme wa Waajemi. Ni yeye aliyewashinda Babeli katika vita na hivyo kuwa mtawala wa himaya yote ambayo Babeli alikuwa akiitawala. Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho taifa la Israeli lilikuwa utumwani Babeli. Sasa kwa vile Koreshi alikuwa amemshinda Babeli, basi ni yeye sasa aliyekuwa mtawala wa Israeli au mkoloni wao wote Babeli na Israeli. Kitu kinachoshangaza katika somo hili ni kuwa Mungu anamwita mtawala huyu kuwa ni mteule wake na mpakwa mafuta wake. Huyu alikuwa ni mtawala wa taifa pagani na tena taifa ambalo lilikuwa limewaweka utumwa watu wake Israeli. Anampa cheo ambacho kilikuwa kimetengwa kwa manabii, makuhani na wafalme wa taifa lake teule Israeli.

Kitu hiki cha kushangaza, Mungu mwenyewe anakifafanua na kusema amekifanya hivyo “kwa ajili ya Yakobo mtumishi wake na Israeli mteule wake”. Ameamua kumtumia mtawala huyo mpagani na hata asiyemjua Mungu kuwa ni chombo chake cha kuwarudishia uhuru watu wake waliokuwa utumwani. Na historia ya taifa teule inatuthibitishia hilo pale inapoonesha kuwa Waisraeli walipata kurejeshwa katika nchi yao kutoka utumwani Babeli katika kipindi cha utawala wa huyu huyu Koreshi. Somo letu hili, pamoja na jambo lake la kushangaza, linapenda kuonesha mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni kuonesha ukuu na utukufu wa Mungu. Mungu ni mkuu na mtawala wa mataifa yote, mafaifa yanayoliheshimu Jina lake na hata yale ambayo hayaliheshimu Jina lake. Na kwa ukuu wake, ni Yeye anayewatawala wakuu na watawala wote na anaweza kuwatumia kadiri apendavyo. 

Kwa Waisraeli kutambua kuwa Koreshi, mtawala aliyeogopwa dunia nzima ni mtawala anayetimiza makusudi ya Mungu wao, lilikuwa ni jambo la kuwaongezea imani kwa Mungu wao. Jambo la pili ambalo somo hili linaonesha ni kuwa mipango ya Mungu itabaki kuwa ni ya Mungu. Ni Yeye ajuaye afanye nini na kwa njia ipi kwa ajili ya watu wake. Mungu anaweza kutumia hata maadui wa watu wake ili kuwafundisha watu wake hao fadhila na hata kuwaonesha njia ya kuufikia wokovu. Ni namna nyingine ya kusema kuwa hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Yeye anaweza kugeuza jambo ambalo machoni pa wanadamu si jema na akalitumia kuonesha utukufu wake.

Somo la pili (1Thes 1:1-5B) ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike. Waraka huu ndio unaosemekana kuwa ndio waraka wa kwanza kuandikwa na Paulo kati ya nyaraka zake zote ambazo zipo katika Agano Jipya. Ni hapa ndipo alipoanzisha utamaduni wa kuwaandikia waamini wa makanisa aliyohubiri ili pamoja na kuwasalimu aweze kuendelea kuwalisha Neno la Mungu lililo Habari Njema ya wokovu. Katika somo hili la leo, Mtume Paulo anawakumbusha Wathesalonike kuwa Injili aliyowahubiria haikuwa ni maneno matupu. Ilikuwa ni Injili iliyo na nguvu na iliyo na Roho Mtakatifu na hivi kuweza kuamsha ushawishi ndani yao. Anawakumbusha watambue utofauti kati ya tangazo la Injili na tangazo la propaganda nyingine za kielimu au za kisiasa ambazo walikuwa wamezisikia kutoka kwa wengine. Injili haisambazwi kwa ufundi wa maneno wala ufasaha wa mtangazaji. Injili inasambazwa kwa sababu yenyewe ina nguvu ya Roho Mtakatifu, nguvu iwezayo kuleta wokovu kwa wote wanaoiamini na kuipokea.

Injili (Mt 22:15-21) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Ni Injili ambayo Yesu anatangaza “mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari na mpeni Mungu yaliyo ya Mungu”. Tunaona waziwazi katika Injili hii ni upinzani ambao Yesu anazidi kuupata anapoendelea kutekeleza utume wake. Upinzani huu unaozidi kukua unajidhihirisha leo katika mtego ambao Mafarisayo na Maherode wanamtegea ili akijikwaa katika majibu yake wapate sababu ya kumshtaki. Na mtego huo ulikuwa ni juu ya kulipa kodi kwa Kaisari. Kodi hii ambayo Waisraeli walipaswa kuilipa kwa Kaisari ilikuwa kidogo ni tofauti na kodi ambayo wananchi huwajibika kutoa kwa serikali yao. Kwanza, Kaisari hakuwa Myahudi, alikuwa ni Mrumi aliyetawala Israeli kama koloni lake. Hii peke yake iliwafanya Waisraeli kumchukia na kumwona kama: mkoloni na mtawala mgeni ambaye hapaswi kulitawala taifa teule la Mungu. Sababu ya pili ilikuwa ni ya kidini.

Wapo walioona kumtii Kaisari ni sawa na kumdharau Mungu. Sasa, endapo Yesu angejibu moja kwa moja kuwa watu watoe kodi angejikuta katika mgogoro na Wayahudi walio wengi waliouchukia utawala wa Kaisari. Lakini pia endapo angesema moja kwa moja kuwa Wayahudi hawapaswi kutoa kodi kwa Kaisari, basi wangeenda tu kumshtaki kwa Kaisari kama mpinzani wa utawala wake. Yesu anautambua mtego huo na ndipo anawapa jibu hilo kuwa “mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari na mpeni Mungu yaliyo ya Mungu”. Jibu hili ambalo Yesu analitoa halikuwa tu ni kwa sababu ya kukwepa kuingia katika mtego bali alilenga pia kutoa fundisho. Na fundisho hilo ni kuwaalika wafuasi wake kutafuta siku zote ulinganifu kati ya wajibu wao wa kidini na wajibu wao kwa viongozi na mahitaji ya kijamii. Mwanadamu ni mwili na roho. Sio mwili tu bila roho na wala sio roho tupu bila mwili. Uwiano sahihi kati ya vyote viwili ndio unaomfikisha mwanadamu katika ukamilifu ule alioukusudia Mwenyezi Mungu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu ya dominika hii ya 29 ya mwaka A wa Kanisa yamezungumza juu ya uwiano unaopaswa kuwapo kati ya mahitaji ya kimwili ya mwanadamu na yale ya kiroho. Kristo amelifupisha fundisho hilo aliposema “mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari na mpeni Mungu yaliyo yake Mungu”. Kama tulivyopata nafasi ya kufafanua masomo yetu haya ya leo, tumeona jinsi ambavyo Mungu mwenyewe anaonesha ukuu wake kwa kutumia mamlaka za mataifa kuyatimiza makusudi yake kwa watu wake. Kuutafakari ujumbe huu wa kumpa Kaisari yaliyo yake na kumpa Mungu yaliyo yake katika ulimwengu mamboleo ni muhimu kusisitiza pia kuwa si halali kumpa Kaisari yaliyo ya Mungu na si halali pia kumpa Mungu yaliyo ya Kaisari. Tunapaswa kulisisitiza hilo kwa sababu Mungu kwa asili yake huridhika na humuhitaji mwanadamu kumpa iliyo haki yake. Lakini hali sio sawa kwa Kaisari, yaani viongozi na watawala wa kidunia.

Wao mara kwa mara hawajaridhika kupewa iliyo haki yao na mara nyingi sana wamewataka watu kuwapa pia ile iliyo ya Mungu. Hili wamelifanya kwa kuingilia: uhuru wa kidini; uhuru wa dhamiri za watu, haki ya watu kumuabudu Mungu wa kweli kwa kuweka mazingira magumu ya kuabudu na kumtukuza Mungu. Wameendelea kuvuka mipaka hadi kujitwalia haki ya kuwa waamuzi juu ya uhai kwa kuendeleza utamaduni wa kifo katika kupitisha sheria juu ya utoaji mimba, kuruhusu kifo laini (eutanasia), kuchochea vita, mauaji ya kimbari; kwa kutengeneza, kuuza na kulimbikiza silaha za maangamizi na mengine mengi kama hayo, kwa maneno machache, huku ni kukumbatia utamaduni wa kifo. Kristo Yesu, leo anapotualika kumpa Mungu yaliyo ya Mungu na kumpa Kaisari yaliyo yake kwa namna ya pekee anatualika sisi tulio wafuasi wake kulinda pia mipaka ya iliyo haki ya Mungu ili kwa namna yoyote ile isinajisiwe na Kaisari asiyeridhika kamwe kupokea iliyo yake pekee.

Liturujia J29
16 October 2020, 16:27