Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Jengeni Ufalme wa Mungu hapa duniani katika haki, amani, ukweli na mshikamano! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Jengeni Ufalme wa Mungu hapa duniani katika haki, amani, ukweli na mshikamano! 

Tafakari Jumapili 29 Mwaka A: Jengeni Ufalme wa Mungu Duniani!

Masomo ya domenika hii yanatueleza kuwa licha ya kuwa kwa ubatizo tumekuwa raia wa ufalme wa Mungu mbinguni, maadamu bado tuko duniani tunawajibu wa kuujenga ufalme wa Mungu dunia huku tukizitii mamlaka za falme za kidunia zilizo halali. Ujumbe huu umefumbatwa na maneno ya Yesu: Mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na Kaisari yaliyo yake Kaisari! Ufalme wa Mungu!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 29 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika ya 28 mwaka A yalitukumbusha kuwa kwa ubatizo tumestahilishwa kuingia katika karamu ya ufalme wa Mungu mbinguni kwa kuvikwa neema ya utakaso kama vazi maalumu. Masomo ya domenika hii yanatueleza kuwa licha ya kuwa kwa ubatizo tumekuwa raia wa ufalme wa Mungu mbinguni, maadamu bado tuko duniani tunawajibu wa kuujenga ufalme wa Mungu dunia huku tukizitii mamlaka za falme za kidunia zilizo halali. Ujumbe huu umefumbatwa na maneno ya Yesu: Mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na Kaisari yaliyo yake Kaisari. Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya linasimulia kuitwa na kutumwa kwa Koreshi mfalme mpagani wa Uajemi, kuwaweka huru wana wa Israeli kutoka uhamishoni Babeli. Kuitwa na kutumwa kwa Koreshi ni fundisho kuwa Mungu wa Israeli ni Mungu wa mataifa yote na ni mkuu juu ya miungu yote.

Katika kumwita Koreshi Mungu alimwahidia ushindi dhidi ya taifa la Babeli. Baada ya kushinda Koreshi aliwaamuru waisraeli, warudi katika nchi yao wakalijenge upya Hekalu na mji wao wa Yerusalemu. Mpango huu wa Mungu ni kinyume kabisa na matarajio ya Wayahudi waliotegemea kwamba siku moja wangewekwa huru kutoka utumwani na mfalme kutoka katika nyumba ya Daudi. Hii inatuonyesha kuwa mpango wa Mungu kwa mwanadamu ni fumbo lisiloeleweka kwa akili za kibinadamu bali imani tu yaelewa kwa njia ya ufunuo. Kumbe ili kuikamilisha mipango yake, Mungu mara nyingine anawatumia viongozi wa kisiasa kwa kuwapa mamlaka, nguvu na uweza. Kwa hiyo mamlaka halali ya kidunia yanatoka kwa Mungu katika hekima yake na upendo wake kwa watu wake. Kwa hiyo mamlaka yoyote ya kiserikali maadamu inafanya yaliyo mema na inawasisitiza watu wake wamuongokee Mungu mamlaka hii yatoka kwa Mungu na hainabudi kuheshimiwa.

Katika somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike, mtume Paulo anaeleza furaha yake kwa kazi ya uinjilishaji ilivyofanikiwa kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu. Paulo anatueleza kuwa kazi yake ya kutangaza habari njema ilipata mafanikio kwakuwa ilifanyika katika maongozi ya Roho Mtakatifu. Hivyo anatukumbusha kusali na kumshukuru Mungu daima kwa neema anazotujalia na pia anatuonesha kwamba kazi yeyote ya uinjilishaji wa habari njema inayofanyika kwa nguvu na uwezo wa mwenyezi Mungu huzaa matunda mema. Mungu ndiye anayetufanikishia utume wetu nasi hatupaswi kuwa na mashaka tunapotumwa kwani Mungu anakuwa nasi daima akitutegemeza. Katika Injili ilivyoandikwa na Mathayo, inatuonyesha jinsi Mafarisayo wanavyopanga kwa chuki namna ya kumwangamiza Yesu kwa kuweka wazi unafiki wao katika maisha ya kiimani na kijamii na hivyo wanapanga kumuingiza katika malumbano yao kuhusu ulipaji wa kodi. Tukumbuke kuwa Wisraeli walipokuwa uhamishoni Babeli walilipa kodi kwa mfalme wa Babeli. Baada ya kurudi kutoka uhamishoni Babeli waliendelea kulipa kodi kwa mfalme Koreshi wa Uajemi.

Nyakati za Yesu walilipa kodi kwa mfalme wa Kirumi na pesa iliyotumika kulipa kodi ilikuwa ni pesa ya Kirumi ambayo ilikuwa ina sanamu ya mfalme wa Warumi na iliandikwa divus kumwonesha mfalme huyo kama mungu wao. Hivyo kwa Myahudi hii ilikuwa ni kufuru kwani sanamu za kila aina zilikatazwa katika amri ya kwanza ya Torati, na sanamu au mtu kupewa jina la utakatifu ilikuwa ni kufuru tosha.  Hivyo majadiliano mazito yaliibuka kati ya viongozi wa siasa na viongozi wa dini kuhusu uhalali wa Myahudi kulipa kodi kwa Serikali ya kikoloni. Kikundi cha Wazeloti waliwashawishi Wayahudi wasilipe kodi kwa Warumi kwa kuwa kufanya hivyo ni dhambi. Kikundi cha Waherodi ambao walishikamana na Warumi, walihalalisha Myahudi kulipa kodi kwa Warumi na wao ndio walikuwa wakusanya kodi na watoza ushuru.

Baada ya Yesu kuwanyamazisha Mafarisayo kwa unafiki wao katika majadiliano yaliyotangulia, wao waliamua kuwatuma baadhi ya wanafunzi wao kumhoji kuhusu uhalali wa kulipa kodi kwa Serikali. Wanafunzi hawa wanampatia Yesu sifa nyingi kuwa ni mtu wa haki, mkweli, hajali cheo cha mtu, kwa kuwa hatazami sura. Lakini sifa hizi zilikuwa ni kumpamba kusiko na ukweli ambako kunadhihirishwa na swali lao la kimtego wakisema: Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi ama sivyo? (Mt. 22:17. Ni swali la mtego kwelikweli kwasababu endapo Yesu angesema si halali, angepingana na utawala wa Kirumi, hivyo angefanya kosa la uhaini na kustahili kifo, na kama angesema ni halali angepingana na sheria za torati kwani kulipa kodi ilikuwa ni sawa na kumuabudu Kaisari aliheshimiwa kama mungu ndiyo maana sarafu ya kulipia kodi ilikuwa inachapa yake, ishara ya kumuabudu yeye na pia angejipinga mwenyewe kwakuwa alitangaza kuwa yeye ni Masiha, Mwana wa Mungu na hivi hawezi akaunga mkono uabudu wa sanamu.

Yesu akitambua nia yao ovu mioyoni mwao, anawaambia waziwazi; mbona mnanijaribu enyi wanafiki? Kisha akawaomba dinari, fedha ya kulipia kodi nao walipompatia aliwauliza; Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia: Ni ya Kaisari. Yesu akawaambia: Mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu (Mt. 22, 21). Kumbe kwa kuwa walitumia fedha ya Kaisari kwa faida yao, walipaswa kulipa kodi kwa Kaisari, ambayo ilitumika kwa maendeleo yao. Lakini pia wajibu wao kwa Mungu sio sababu ya kutotimiza wajibu wao kwa serikali. Zaidi ya hayo wao kuwa chini ya utawala wa kigeni ni dhambi zao za kumuasi Mungu ndio maana Yesu anawaambia wampe Mungu yaliyo yake Mungu. Jibu hili linatukumbusha wajibu wetu wa kutii mamlaka halali ya kiserikali inafanya yaliyo halali kwa maendeleo ya watu wake. Ndiyo maana katika nyaraka zao, Petro na Paulo, walitoa maelekezo makini kwa Jumuiya za Kikristo wakiwaongoza jinsi wanavyopaswa kujihusisha na mamlaka za kiraia. Wakristo wanapaswa kuheshimu na kutii mamlaka halali, (Rum. 13, 1) (1 Pet. 2, 13-14); walipaswa pia kuiombea mamlaka halali katika utendaji wake, (1 Tim. 2: 1-2), na kulipa kodi kwa mamlaka halali (Rom.13:7).

Ni pale tu, mamlaka ya kisiasa inapotoa amri ambayo ni kinyume na sheria ya Mungu, wakristo walilazimika kutotii mamlaka ile, wakifuata mfano wa Petro ambaye aliwajibu wazee wa Baraza la Wayahudi {Sanhedrin}: Tunapaswa kumtii Mungu kuliko mwanadamu (Mdo 5:29). Ndiyo maana wakristo wa mwanzo walikuwa tayari kufa mashahidi kuliko kutolea ubani kwa wafalme, walipoamriwa na watawala dhalimu, kwani ilikuwa kinyume na imani yetu kwa kuwa wafalme hao walijiweka mahali pa Mungu. Kama vile Maherodi na mafarisayo walivyotaka kuchochea uhasama kati ya dini na Serikali kwa kutaka kumnyamazisha Yesu baada ya kuwanyamazisha wao, ndivyo ilivyo hata nyakati zetu pale wanasiasa wanapotaka kuwanyamazisha viongozi wa dini wanapowakemea juu ya uovu wao wakiwataka wanyamaze kwa kusema waache siasa. Jibu la Yesu lilionyesha wazi kuwa dini na Serikali havipaswi kupingana kwani ni taasisi mbili ambazo zinamshughulikia mtu yuleyule katika kumletea maendeleo ya kimwili na kiroho ili aweze kuishi maisha mema na ya kumpendeza Mungu. Hivi tusiwe watu wa kuchanganya mambo.

Tumpe Mungu yale yaliyo yake na Kaisari yale yaliyo yake. Kwa kuwa hakuna jamii inayoweza kuishi pasipo sheria, basi sheria zinapaswa kulenga kutafuta manufaa ya kila mmoja, wakati kila mwananchi analazimika kufuata sheria na kuchangia usitawi wa jamii husika anakoishi. Jambo hili ni wazi kwa kila mtu, lakini ukweli kwamba Mkristo ni raia wa falme hizi mbili: Ufalme wa Mungu maana kwa ubatizo tumefanywa kuwa raia wa ufalme wa Mungu na Ufalme wa dunia yaani nchi fulani au taifa fulani kwa kuwa tuko duniani. Tutambue kuwa falme za kidunia pamoja na kuwa na tofauti katika muundo, historia na mfumo zinaongozwa na sheria, taratibu, kanuni, miongozo na maadili. Hivyo tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atuangazie tuweze kuzitambua mamlaka zilizo halali na kuzitii huku tukitimiza wajibu wetu kwa Mungu na kwa Kanisa. Tumsifu Yesu Kristo. 

Jumapili 29
16 October 2020, 16:12