Tafuta

Wanafunzi,wazazi na walimu wakiandamana mara baada ya mauaji ya watoto shule moja huko Kumba nchini Kamerun tarehe 24 Oktoba 2020. Wanafunzi,wazazi na walimu wakiandamana mara baada ya mauaji ya watoto shule moja huko Kumba nchini Kamerun tarehe 24 Oktoba 2020.  

Kamerun:Mauaji ya watoto huko Kumba ni tendo unyama mkubwa!

Jumamosi tarehe 24 Oktoba 2020 kundi la wanaume wenye silaha walivamia shule na kuvunja madarasa ya shule ya msingi nchini Kamerun,watoto nane kunzia miaka 9 hadi 12 walifariki Dunia.Askofu wa Jimbo katoliki la Kumba amesema hili ni tendo la unyama.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ni siku ya kusikitisha zaidi kwa mujibu wa barua iliyoripotiwa na “La Croix Afrique”, kutoka kwa askofu wa Kumba, nchini Kamerun, Askofu Agapitus Enuyehnyoh Nfon, ambaye anafafanua mauaji ya watoto yaliyotokea katika jimbo lake, Jumamosi  tarehe 24 Oktoba 2020, wakati kundi la Wanaume wenye silaha walivunja madarasa ya shule ya msingi ya Taasso ya Mama Francisca na kuwapiga wanafunzi hao wadogo kwa silaha za moto na mapanga. Inakadiliwa watoto 8 wa  shule wameuawa, wote wakiwa na umri wa kati ya miaka 9 na 12.

Kwa sababu ya kitendo hiki cha kinyama amesema kiongozi huyo kwamba  watu wa Kumba wamelia machozi na jimbo zima linaomboleza, mioyo yao imevunjika kwa sababu watoto wao wasio na hatia hawapo tena. Kwa njia hiyo ametoa wito kwa serikali ya Kamerun na kwa jamumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za kumaliza mauaji mengi ya raia katika eneo la (Anglophone) linalozungumza kiingereza nchini Kamerun, pia Askofu Nfon anauliza swali “Je Mamlaka itabaki bila kufanya lolote kwa muda gani? Watoto wetu watalazimika kufa tena kabla halijafanyika kitu chochote?” Hatimaye Askofu pia ametangaza kwamba, Ijumaa tarehe 30 Oktoba 2020 waataadhimisha Misa Takatifu katika Kanisa kuu la jiji, lililowekwa wakfu kwa Moyo Mtakatifu  wa Yesu kuwaombea marehemu wote na majeruhi.

Kwa sasa, wahusika wa shambulio hilo hawajatambuliwa. Inachukuliwa, hata hivyo, kwamba wanaweza kuwa washiriki wa vikundi vya kujitenga katika mkoa unaozungumza Kiingereza. Kiukweli, nchini Kamerun, nchi yenye watu wengi wanaozungumza Kifaransa, tangu 2017 kumekuwa na mapigano na machafuko kati ya vikosi vya usalama vya serikali na watenganishi wa kiingereza ambao miaka mitatu iliyopita walitangaza uhuru wa kile kinachoitwa “Ambazonia”. Hadi sasa, mzozo wa ndani umesababisha zaidi ya waathiriwa 3,000 na karibu watu 70,000 waliohamishwa ndani.

Kufuatia na tukio hili la kinyama naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres ameelezea kushtushwa kwake na ripoti  juu ya mashambulizi hayo kwenye mji wa Kumba kusini magharibi mwa Kamerun. Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa, tarehe 25 Oktoba 2020 jijini New York, Marekani, imemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa katika tukio hilo watoto wengine kadhaa walijeruhiwa na kwamba “shambulio hilo la kuchukiza ni kumbusho juu ya gharama kubwa ambayo raia wakiwemo watoto wanalipa huku wakinyimwa haki yao ikiwemo elimu. Mashambulio dhidi ya maeneo ya shule lazima yakome kwa kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto.” 

Bwana Guterres ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za watoto waliopoteza maisha na huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi. Bwana Guterres amesihi mamlaka za Kamerun  zifanye uchunguzi wa kina ili wahusika wa shambulio hilo wafikishwe mbele ya sheria. Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa pande zilizojihami zijizuie kufanya mashambulizi dhidi ya rai ana ziheshimu sheria za kimataifa za kibindamu na za haki za binadamu. Bwana Guterres amesihi kwa dhati pande zote kuitikia wito wake wa sitisho la mapigano duniani huku akisema kuwa, “Umoja wa Mataifa upo kusaidia mashauriano jumuishi yanayoweza kuleta suluhu ya kudumu kwenye mzozo huko kaskazini-magharibi mwa Kamerun.”

Duru za habari zinasema kuwa kile kilichoanza kama harakati za raia wa kusini mwa Kameruni kusaka usawa zimeongezeka na kuwa janga kamili ambapo vikundi vya waasi vinavyosaka kumaliza kile kinachodaiwa kuwa udhibiti wa watu wa Kameruni wanaozungumza lugha ya kifaransa kwenye maeneo ya Wakamerun wanaozungumza lugha ya kiingereza vimebeba silaha dhidi ya vikosi vya serikali. Mapigano hayo yamesababisha mamia ya watu kupoteza maisha huku makumu ya maelfu wakilazimika kukimbia makazi yao. Viwanda vimechomwa moto, barabara hazipitiki, bohari za kuhifadhi bidhaa zimeteketezwa, huku madereva wa malori wakiwa wanatekwa mara kwa mara na watekaji kudai fedha ili wawaachie huru

26 October 2020, 16:25