Tafuta

Askofu Agapiti Ndorobo Fidelis wa Jimbo Katoliki la Mahenge anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Ya Uaskofu kunako mwaka 1995. Askofu Agapiti Ndorobo Fidelis wa Jimbo Katoliki la Mahenge anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Ya Uaskofu kunako mwaka 1995. 

Askofu Agapiti Ndorobo Jubilei ya Miaka 25 Ya Uaskofu Mahenge!

Askofu Agapiti Ndorobo Fidelis alipadrishwa tarehe 6 Desemba 1980. Tarehe 3 Machi 1995 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mahenge na kuwekwa wakfu tarehe 16 Juni 1995 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Amejipambanua katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Mahenge!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ya Mungu nchini Tanzania na kwa namna ya pekee kabisa Jimbo Katoliki la Mahenge, Tanzania, linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, ukuu na shukrani kwa Askofu Agapiti Ndorobo Fidelis kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mahenge, Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Askofu Ndorobo alizaliwa tarehe 14 Agosti 1954 huko Kidulo, Parokia ya Haubi, Jimbo Katoliki la Kondoa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 6 Desemba 1980 akapewa daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki la Dodoma. Tarehe 3 Machi 1995 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mahenge na kuwekwa wakfu tarehe 16 Juni 1995 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Vatican News anapenda kuchukua fursa hii, kumpongeza Askofu Agapiti Ndorobo Fidelis kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mahenge. Miaka 25 ni kipindi chenye changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika nchi za kimisionari. Anamshukuru Mungu kwa kumpatia nguvu, neema, baraka na afya ya kuweza kuendelea kuwatakatifuza, kuwaongoza na kuwafundisha watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mahenge kwa ari na moyo mkuu.

Kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lina mpongeza Askofu Ndorobo kwa kushikamana katika urika wao kama Maaskofu. Wanatambua mchango wake mkubwa alioutoa katika Idara ya Caritas Tanzania, kiungo muhimu sana cha Injili ya huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ameonesha moyo wa ukarimu wa kimisionari katika maisha na utume wake, kwa kusoma alama za nyakati na kuona mahitaji ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mahenge, kiasi cha kuridhia Jimbo Katoliki la Mahenge kugawanywa na hivyo hapo tarehe 14 Januari 2012, Jimbo Katoliki la Ifakara likaundwa.

Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge aliwakumbusha waamini kwamba, kumegwa kwa Jimbo la Mahenge na kuundwa kwa Jimbo Katoliki la Ifakara kunapania kuboresha huduma za kichungaji kwa Familia ya Mungu Jimboni humo, changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Ifakara ni kuonesha ushirikiano wa dhati na Askofu Salutaris Melchior Libena. Itakumbukwa kwamba, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 8 Desemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko alimteua Mheshimiwa Padre Filbert Felician Mhasi wa Jimbo Katoliki Mahenge, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, lililoko Kusini mwa Tanzania.  Hadi  uteuzi huo Askofu mteule Padre Filbert Felician Mhasi alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Kanisa Kuu la Kwiro, Jimbo Katoliki Mahenge. Katika muktadha huu, Askofu Filbert Felician Mhasi ni matunda ya ukomavu wa imani na umisionari wa Jimbo Katoliki la Mahenge.

Askofu Ndorobo amekuwa bega kwa bega na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mchakato wa huduma ya elimu na afya kwa kusaidia mchakato na hatimaye kukamilika kwa Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT, "College of Health and Allied Sciences", SFUCHAS, ambacho kimekuwa ni msaada mkubwa katika maboresho ya huduma ya tiba na afya nchini Tanzania. Jimbo Katoliki la Mahenge katika maisha na utume wake, limewekeza sana katika sekta ya elimu. Ni kati ya Majimbo ambayo yamekuwa yakitoa majaalimu kwenye Seminari na taasisi za elimu ya juu zinazoongozwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, Askofu Ndorobo ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Kiaskofu hasa miongoni mwa Maaskofu vijana. Ishara ya uzee wenye matumaini katika kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Huu ni wakati wa kuyaangalia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini na kwamba, mapambano bado yanaendelea kabisa! Jimboni Mahenge kumenoga hadi raha!

Askofu Ndorobo

 

17 October 2020, 16:21