Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXIII ya Mwaka A wa Kanisa. Waamini wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kushughulikia ustawi, maendeleo na wokovu wa jirani zao. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXIII ya Mwaka A wa Kanisa. Waamini wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kushughulikia ustawi, maendeleo na wokovu wa jirani zao.  (AFP or licensors)

Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka A: Ustawi Na Wokovu wa Jirani

Kama Nabii Ezekieli, tunakumbushwa nasi kuwa damu ya mmoja wa ndugu yetu anayeangamia itatakwa kwetu iwapo tulikuwa na nafasi ya kumsaidia hata kwa ushauri aiache njia yake mbaya amrudie Mungu. Injili inauweka wajibu huu katika neno la upatanisho. Inatuonesha kuwa ipo njia ya kupita kufikia upatanisho kati ya ndugu na ndugu. Muhimu ni uvumilivu na upendo wa kidugu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 23 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Ez 33:7-9) ni kutoka kitabu cha Nabii Ezekieli. Mungu anamwambia Ezekieli kuwa kazi yake ya unabii ni sawa na ile ya mwangalizi au mlinzi. Katika Israeli ya wakati huo, miji ilijengwa kwa kuzungushiwa kuta kwa ajili ya usalama. Kuta hizo zilikuwa pia na mnara ambamo ndani yake walikaa kwa zamu walinzi wa miji. Hao walikuwa na kazi moja kubwa, kupaza sauti endapo kuna adui anakaribia au endapo kuna hatari yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wa mji. Mungu anapomwambia Nabii Ezekieli kuwa yeye pia ni mwangalizi anamtwika wajibu huu kwa wana wote wa Israeli aliokabidhiwa. Yeye kama Nabii anatakiwa kuwatahadharisha ndugu zake juu ya maadui au hatari zinazoweza kuangamiza roho zao.

Hatari hizi zinaweza kuwa ni zile za kutoka ndani, yaani mienendo ya watu wenyewe lakini pia zinaweza kutoka nje, yaani katika mazingira yanayowazunguka. Mungu anamkumbusha Nabii Ezekieli kuwa yeye kama Nabii azingatie kuwa atawajibishwa kutokana na namna alivyoutekeleza wajibu wake. Endapo atakaa kimya au kwa sababu yoyote ile akaacha kupaza sauti yake na watu wakaangamia, basi damu ya watu wale itakuwa juu yake. Lakini atakapopaza sauti yake na watu wenyewe wakaipuuza, wataangamia na damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao wenyewe. Wajibu ambao nabii anaitiwa kwa watu wake si wajibu anaoubeba nabii peke yake. Katika jumuiya ya watu wa Mungu, jumuiya ya familia ya Mungu yaani Kanisa, kwa ubatizo sote tunashirikishwa kazi ya unabii pamoja na ile ya ukuhani ya ya ufalme wa Kristo. Kumbe kila mmoja wetu anaalikwa kutambua kuwa anao wajibu kwa ajili ya wokovu wa mwenzake.

Somo la pili (Rum 13: 8-10) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili, Mtume Paulo anachota kutoka katika hazina ya mafundisho ya Agano la Kale mwelekeo mpya wa mafundisho yake kwa Wakristo wa Roma. Anawaalika Wakristo wa Roma kuijenga jumuiya yao katika msingi wa upendo. Anawaambia msiwe na deni lingine lolote isipokuwa upendo. Waswahili husema “dawa ya deni kulipa”. Mtume Paulo kwa kuufananisha upendo na deni anawaalika kutambua kuwa kwa mkristo upendo ni wajibu ambao anapaswa daima kuutimiza kwa jirani yake. Kutoka katika hazina ya mafundisho ya Agano la Kale anakazia kusema kuwa upendo ndio ukamilifu wa sheria na Torati zote. Anayeishi upendo amezishika sheria na Torati zote. Mtakatifu Augustino katika kufafanua mafundisho haya ya Mtume Paulo alisema “ishi upendo kisha fanya unachotaka”. Ndani yake ni fundisho kuwa ndani ya upendo, ulio upendo wa kimungu, hakuna ovu.

Injili (Mt 18:15-20) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo.  Katika somo hili, Yesu anazungumza juu ya upatanisho kati ya ndugu na ndugu. Katika Uyahudi, neno ndugu lilimaanisha katika nafasi ya kwanza watu walio na undugu wa damu kama kaka na dada. Lakini pia lilikuwa na maana pana kiasi cha kujumlisha taifa zima la Waisraeli kwani wote walijiona kuwa ni watoto wa baba mmoja, yaani Mwenyezi Mungu. Na maana hii pana ya udugu katika Israeli ilikuwa imeenea sana. Kumbe, hata hapa Yesu anapozungumzia upatanisho kati ya ndugu hajibani tu kuzungumzia ndugu wa damu bali ndugu katika maana pana ya jumuiya nzima. Anasema, ndugu yako akikukosea tafuta nafasi uzungumze naye ninyi wawili na kujaribu kumaliza tatizo. Akikusikia utakuwa umempata, yaani umemwokoa. Asipokusikia tafuta mtu mwingine mmoja au wawili mwende mkazungumze na ndugu yako. Akiwasikia mtakuwa mmemwokoa. Asipowasikia liambie Kanisa. Na kama hatalisikiliza na Kanisa basi awe kwenu kama mtu wa mataifa au kama mtoza ushuru. Neno hilo kuwa kama ndugu hatalisikiliza Kanisa basi atendewe kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru linaweza kuchukuliwa kama ni hukumu ya kumtenga mtu moja kwa moja. Kwa kweli sivyo. Nje ya mafundisho ya Yesu au kabla ya Yesu, watu wa mataifa na watoza ushuru walionekana kama ni wadhambi na walikuwa ni watu ambao Wayahudi hawakuwa na ukaribu nao.

Ni Yesu katika mafundisho yake ameonesha umuhimu wa kupiga hatua kuwasogeza na kuwaonesha Wayahudi kuwa hata wao wamo katika mpango wa Mungu wa wokovu. Na tena mara nyingi katika mifano yake, Yesu ameonesha namna gani watu wa mataifa na watoza ushuru walivyo na imani na walivyo tayari kumpokea. Kumbe, ni kundi la watu ambalo halipaswi kuachwa pembeni bali ni kundi ambalo linahitaji msaada wa kipekee ili liufikie wokovu. Kumbe, Yesu anaposema kama ndugu yako halisikii Kanisa na awe kwenu kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru hamaanishi kumtenga ndugu bali kumwona kama ni mtu anayehitaji zaidi msaada wa upatanisho ili aweze kuokolewa. Yesu katika Injili ya leo anazungumzia upatanisho kama kumwokoa mkosaji kwa sababu ndugu na ndugu kukosana na kutokupatana huwa na uchungu ule ule sawa na wa kifo.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika ya leo yanatukumbusha juu ya wajibu tulionao kwa wenzetu. Binadamu wote na kwa namna ya pekee sisi tunaounganishwa na imani moja kwa Kristo tunaalikwa kushughulikia ustawi na wokovu wa wenzetu. Kama Nabii Ezekieli, tunakumbushwa nasi kuwa damu ya mmoja wa ndugu yetu anayeangamia itatakwa kwetu iwapo tulikuwa na nafasi ya kumsaidia hata kwa ushauri aiache njia yake mbaya amrudie Mungu. Injili inauweka wajibu huu katika neno la upatanisho. Inatuonesha kuwa ipo njia ya kupita kufikia upatanisho kati ya ndugu na ndugu. Yesu ameiwekea njia hiyo hatua nyingi za kupita. Hatua zote hizo lakini ni hatua zinazohitaji uvumilivu zikiongozwa na upendo wa kidugu. Njia ya upatanisho kati ya ndugu kamwe haina njia ya mkato na wala haielekezi kwenye hukumu. Ni njia inayofikia mwisho pale tu ndugu anapofanikiwa kumpata na kumwokoa ndugu yake.

Liturujia J23 Mwaka A

 

04 September 2020, 16:14