Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXIII ya Mwaka: Maonyo ya kidugu, msamaha na upatanisho wa kweli! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXIII ya Mwaka: Maonyo ya kidugu, msamaha na upatanisho wa kweli!  (ANSA)

Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka A: Kuonyana na Msamaha wa Kidugu!

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Mchakato wa maonyo kati ya ndugu na hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia msamaha na upatanisho wa kweli kama kielelezo cha ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Kukosa na kukoseheana ni sehemu ya ubinadamu, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa utakatifu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 23 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika hii yanatukumbusha wajibu wa kila mbatizwa katika kuishuhudia Injili kwa maneno na matendo katika maisha ya kila siku katikati ya ndugu zake wabatizwa na wasio wabatizwa. Wajibu huu ni pamoja na kuwaongoza wakosefu ili wapate kutambua na kutubu makossa yao na kurudi katika njia ya haki ya kumpendeza Mungu na jirani. Mwongoza wa kutimiza wajibu huu unatolewa na Yesu akisema ndugu yako akikukosea, mwonye, patana naye, mrudishe kwa Mungu pia tunaitwa kuwa walinzi wa maisha yetu na maisha ya watu wengine kiroho na kimwili. Katika somo la kwanza, Mungu anamwita nabii Ezekieli kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli. Ezekieli aliitwa kuwa nabii, wakati waisraeli wakiwa utumwani Babeli. Kama nabii alipewa jukumu la kuwa mlinzi. Jukumu lake lilikuwa kulipokea neno la Mungu na kwa neno hili kuwaonya wana wa Israeli dhidi ya maovu yao. Awaonye watu watendao maovu waiache njia yao mbaya.

Mungu anamwambia Ezekieli kuwa asipomwonya mtu huyo aiache njia yake na mtu huyo akifa katika uovu wake basi Mungu atamdai damu ya mtu huyu. Lakini akimwonya mtu mbaya kusudi aiache njia yake, lakini huyo mtu mbaya asiiache basi atakufa katika uovu wake na kuhukumiwa lakini nabii atajiokoa roho yake. Hii ni kazi ambayo Mungu alimwitia nabii Ezekieli aikamilishe. Kazi yake ilikuwa kuwaonya na kuwaongoza wakosefu wa taifa la Israeli watubu. Na alimwambia asipoitimiza kazi hii atakuwa na lawama mbele ya Mungu na wakosefu wasipomsikiliza watakuwa pia na lawama mbele za Mungu. Ndivyo anavyoitwa kufanya kila mbatizwa kwani kwa njia ubatizo sote tunashirikishwa ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Dhana ya kuonyana kidugu na kusameheana Yesu anaitilia msisitizo kwa jinsi ilivyo muhimu kwa maisha ya kikristo na anatoa mwongozo wa maisha haya ya kidugu na kusameheana akisema; ndugu yako akikukosea nenda ukamwonye asipokusikiliza chukua pamoja nawe mtu mmoja au wawili ili kwa ushahidi wa watu wawili au watatu kila neno lithibitike. Asipowasikiliza liambie Kanisa na asipolisikiliza Kanisa na awe kwako kama mtu wa mataifa na watoza ushuru.

Ili kuonesha jinsi ilivyo muhimu msamaha wa kidugu Yesu anasisitiza na kusema; Yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni (Mt. 18:18, Yoh 20:22-23). Na akaongeza kusema; wawili wenu watakapopatwa duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwa na Mungu kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu nami nipo kati kati yao. Kumbe, wakati wa kumwonya ndugu aliyekosa, tunapaswa kufanya hivyo kwa upendo na kwa hatua. Hatua ya kwanza inatudai kumsahihisha mtu aliyekosa kwa faragha tukiheshimu hadhi na utu wake pamoja na kulinda jina lake hata kama ni mkosaji ili mkosefu huyu atambue na kuonja upendo wa kidugu. Hatua hii ya kwanza ikishindikana tunapaswa kuomba msaada kutoka kwa mtu mwingine anayeweza kumshauri mkosefu kwa upendo ili abadili njia zake mbaya. Na kama hatua hii ya pili ikishindikana ndipo hapo tunapaswa kuripoti kwa mzee wa Kanisa. Kama mkosaji huyu atakaza shingo na kuziba masikio yake basi jumuiya ina haki ya kumtenga huku ikimuombea kwa Mungu ili shetani amwachie.

Hivyo basi, ili kumsaidia mkosaji hatupaswi kuwa wepesi wa kueneza uovu na makosa yake kwa kuwatangazia wengine wala kutoa adhabu kubwa kwake kwa kukataa kutoa msamaha. Kutangaza makosa ya mkosaji hata kabla ya kumuonya na kumsahihisha ni dalili wazi kuwa mwenendo wetu hauongozwi na upendo wa kidugu. Mtume Paulo akiwaandikia Warumi barua yake kabla hajaenda kuwatembelea akijua kuwa ndugu wengi wa jumuiya ile walikuwa bado wapagani na ni wachache tu kati yao aliofahamu lakini aliwataka watambue upendo na huruma kuu Mungu aliowajalia kwa kuwaita na kuwaalika kumwamini Kristo na hivyo kuwafanya wachukue nafasi ya wayahudi waliomkataa Yesu. Mtume Paulo aliwafanya wakristo wa Roma watambue deni walilonalo kwa Kristo aliyewakomboa kutoka utumwa wa dhambi na kuwapa roho mtakatifu na kuwafanya kuwa watoto wa Mungu na kuwaweka katika njia ya kufika mbinguni kwenye uzima wa milele.

Hata hivyo Mtume Paulo anawaambia kuwa wanapaswa kulipa deni walilokopeshwa na Kristo kwa kuwatendea jirani zao kwa mapendo, na hasa ndugu zao katika Jumuiya ya kikristo. Ushauri wa Paulo kwa wakristo wa Roma kuhusu upendo kwa ndugu wa jumuiya unatuhusu sisi pia. Katika kujaribu kulipa deni la kukombolewa toka utumwa wa dhambi, tunapaswa kuzingatia haya; Deni letu la upendo kwa Mungu sasa limekuwa deni kwa ndugu zetu; ni deni ambalo hatuwezi kulilipa vilivyo kwa vile hakuna kiasi cha upendo kwa upande wetu kinachoweza kulingana na upendo wa Mungu aliotuonesha. Hatupaswi kupima upendo na ukarimu wetu kwa wengine ndiyo maana anachotudai Mungu ni upendo kwa jirani zetu na hii ndiyo amri yake pekee wala si kingine (Yoh 13:34). Mtume Paulo anasisitiza kuwa hakuna sheria yoyote ile inayoweza kuchukua nafasi badala ya upendo; siyo kusali masaa mengi, siyo kufunga muda mrefu, siyo kutoa mali zetu, hii itakuwa yote bure, kama tutakapomtenga ndugu yetu na upendo wetu (1Kor 13:1-3). Upendo unadai kuwasamehe, kuwapokea wanaotukosea kama walivyo, upendo unatudai kuwajali maskini, kushiriki furaha na machungu yao, kuwa na amani na watu wote, kukwepa kisasi, kulipa ovu kwa jema (Rom 13:14-21).

Kumbe, kama Mungu alivyomweka Nabii Ezekieli kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli ili kuwaonya wakosefu watubu, nasi pia kwa ubatizo tumetumwa kuwa walinzi wa wenzetu, kuwaonya wanapokosea na kuwasamehe wanapoomba msamaha. Tuwaonye na kuwaongoza wakosefu wapate kutubu. Sisi tulipobatizwa, tulifanywa kuwa wafuasi wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tulipewa jukumu la kushuhudia injili kwa maneno na matendo yetu ya kila siku. Tulipewa jukumu la kuwaleta wengine kwa Kristo kwa matendo yetu mema. Kwa maneno mengine tulifanywa kuwa walinzi wa imani. Watu wakiona matendo yetu wamtukuze Mungu Baba yetu aliye mbinguni. Kwa kuwa kwa Ubatizo tulifanywa kuwa walinzi wa ndugu zetu, tulifanywa kuwa manabii wa kuonya na kuwaongoza wakosefu ili watubu na kumrudia Mungu, tusipofanya hivyo tutakuwa na lawama mbele ya Mungu maana ndivyo Mungu alivyomwambia nabii Ezekieli. Mungu atatudai kwa nini tumeacha roho ya mkosefu ipotee. Lakini kazi hii si rahisi inadai sadaka. Katika kuifanya tutapata madhulumu na mapingamizi.

Wakati mwingine wakosefu wanavichwa na shingo ngumu na masikio yao hayasikii lakini hatupaswi kukata tamaa, bali kuendelea kuwaonya, ndio maana Yesu alisema asipokusikiliza chukua pamoja nawe mtu mmoja au wawili na asipokusikiliza liambie Kanisa kwa maana kwamba tusikate tamaa katika kuwaonya wakosefu ili waweze kutubu, kuongoka na hatimaye kumrudia tena Muumba wao.

03 September 2020, 15:54