Tafuta

Mama Kanisa tarehe Mosi, Oktoba ya Kila mwaka anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Mama Kanisa tarehe Mosi, Oktoba ya Kila mwaka anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. 

Kumbukumbu Ya Mtakatifu Theresia Wa Mtoto Yesu! Utume!

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu katika maisha na utume wake alisema daima kwamba, wito wake ni upendo kwa Mungu na jirani. Siri kuu ya utakatifu wa maisha yake ni fadhila ya imani, matumaini na mapendo. Tangu mwanzo alijijenga katika tunu msingi za Kikristo, akazama zaidi katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; akajipambanua katika maisha ya sala, sadaka na uvumilivu.

Na Sr. Veronica Silvester Buganga, CMTBG - Roma.

Kila mwaka ifikapo tarehe 1 Oktoba, Mama Kanisa  humwadhimisha  Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kwa heshima ya Bikira na Mwalimu  wa Kanisa na tangu mwaka 1927 aliteuliwa kuwa ni msimamizi wa wamisionari wote duniani pamoja na Mtakatifu Francisko Xsaveri. Kanisa katika kipindi cha Mwezi wa Oktoba linapenda kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika kuombea shughuli za kimisionari pamoja na kuchangia kwa hali na mali mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni mwamko na ushuhuda wa kimisionari kama kielelezo cha imani tendaji na mapendo kamili kwa Mungu na jirani.

KUZALIWA: Theresia wa Mtoto Yesu alizaliwa tarehe 2 Januari 1873  Alencon na baadae kuhamia Lisieux nchini Ufaransa.  Theresia ni mtoto wa tisa kuzaliwa na kitinda mimba kwenye familia ya Mzee Luigi Martin  na Zeria Guerin ambao sasa Kanisa limewaweka kuwa mfano na kioo  kwa familia zote za Kikristo. Tarehe 19 Oktoba 2008 walitangazwa kuwa ni Wenyeheri na mwaka 2015 Kanisa limewatangaza kuwa watakatifu kwa kuzingatia walivyoishi na kuwalea watoto kiimani na katika maadili ya kikiristo. Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu aliaga dunia tarehe 30 Septemba  1897, akatangazwa Mtakatifu mwaka 1925, mnamo mwaka 1927 Papa Pius XI akamtangaza kuwa ni msimamizi wa utume wa Kanisa.

WITO: katika maandiko yake anasema wito wangu ni Upendo. Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu katika umri mdogo amekutana na matatizo mengi na majaribu makubwa, kama vile kuuguliwa na wazazi, kwanza mama hadi akashindwa kumnyonyesha,  pia kubaki yatima baada ya kifo cha mama yake. Akaanza kumzoea dada yake mkubwa lakini akapatwa na uchungu wa kutengana nae mwaka 1882 Paulina alipoingia kwenye Shirika la Wakarmeli. Theresia alitamani na yeye aingie utawani mapema iwezekanavyo ila kwa umri wake mdogo hakuweza kupokelewa kwenye monasteri kwa kuzingatia ugumu wa maisha ya sadaka za utawa wa ndani. Hakukata tamaa, mwaka 1887 akaenda hadi Roma kuhiji ili akutane na Papa LEO wa XIII, ili ampe ruhusa, Papa Leo XIII alimsikiza na kumshauri asubiri bado ni mdogo, alisikitika ila akapokea kwa matumaini na utulivu.

Kuingia Utawa wa Wakarmeli: Mungu hakukawaia kumwonjesha furaha ya uvumilivu na matumaini yake, mara baada ya hija Askofu alimruhusu, Theresia aliingia kwenye monasteri ya Wakarmeli tarehe 9 Aprili1888 akiwa na umri wa miaka 15.  Aliweka Nadhiri za kwanza tarehe 8 Septemba 1890 sanjari na Sikukuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria. Aliifurahia siku hiyo kwa kuwa ni Bibi arusi wa Yesu na mama wa roho za watu, tayari kujitoa kama sadaka ya kuteketezwa na upendo wa Mungu. Siku hiyo aliomba pia neema ya kuendelea kubaki akiwa mnyenyekevu na mtu mwenye kiasi. Katika monasteri yake alijishughulisha na kazi ndogo ndogo alizopewa na mkubwa wake. Kunako mwaka 1893 aliteuliwa kuwa mlezi wa wanovisi, akafanya utume huu kwa bidii. Alitamani kuona upendo unakuwa ni msingi wa maisha na utume wake, ili aweze kuwa yote kwa ajili ya wote.

SIRI YA UTAKATIFU : Utakatifu wake umetokana na fadhila ya: imani, matumaini na upendo wa kina kwa Yesu Kristo uliomwezesha kufanya mang’amuzi na kuiishi njia yake ndogo ya: unyenyekevu , uvumilivu pamoja na kujiachia kabisa katika mikono ya Yesu na Bikira Maria. Aliamini na ndio ilikuwa dira ya maisha yake kuwa kila tendo hata kama ni dogo kiasi gani ukilifanya kwa upendo linaleta baraka na neema kubwa. Theresia wa Mtoto Yesu anatufundisha kuwa ni kwa njia ya sadaka ndogondogo tunapata utakatifu,  matendo madogo ya kila siku kuyafanya kwa upendo thabiti yanamfurahisha Mungu. Mtakatifu Theresia alijitoa mzima mzima kwa Mungu. Aliunganisha mateso yake ya kila siku na yale ya Yesu Msulibiwa pamoja na dhoruba nyingi akajaliwa wepesi uliong’ara kwenye uso wake.  Aliteseka bila kupoteza furaha maana alishirikiana na Yesu kwa kila hali, alijisemea “Theresia peke yake hawezi kitu, Theresa na Yesu anaweza yote. Alionja na kuitegemea huruma ya Mungu, kiasi kwamba alijisikia kuwa Yesu ni rafiki yake wa karibu. Katika kutafakali fumbo la Umwilisho, katika sehemu ya mwisho ya maandishi yake kwenye picha ya Mtoto Yesu anasema “siwezi kumwogopa Mungu aliyejifanya mdogo hivi kwa ajili yangu…Mimi nampenda! Kwa kuwa yeye ni upendo na huruma tu!”

MAISHA YAKE YA KIROHO: Theresia wa Mtoto Yesu, tangu utotoni alijengeka katika tunu msingi za Kikristo, akazama zaidi katika fumbo la Utatu Mtakatifu. Alikuwa na kiu kubwa ya kuwa mtakatifu, aliongozwa na Maandiko Matakatifu, hasa Injili na Nyaraka za Mtume Paulo.  Alisoma maisha ya watakatifu akaona elimu yao kuwa ni ya hali ya juu na akatafuta na kuvumbua njia iliyomfikisha haraka mbinguni. Ngazi iliyomsaidia kupanda kila siku kwenda juu, “Njia ndogo” inaakisiwa  katika Injili ya Mathayo 18,3, “Msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo hamtaingia katika ufalme wa mbingu”. Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu anasema sikimbilii ile nafasi ya kwanza bali ya mwisho, kama kielelezo cha unyenyekevu, imani na matumaini kama ya mtoto mikononi mwa baba alivyo salama, Theresia alimpenda saana baba yake na baba alimlea kama Malkia wake, Theresia anamfananisha na kumchukulia Mungu kama mfalme wake.

MAISHA YA SALA: Ni muungano wa karibu kabisa na Mungu , maneno yaliyotawala muda wa sala binafsi ni kumwambia “Yesu nakupenda, Mungu wangu nakupenda” aliziimba kwa furaha sifa kuu za Mungu, kwa Mtakatifu Teresia sala na sadaka ndizo nguzo kuu ambazo zilimwimarisha. “Sala ya 8 Septemba 1890”. Ee Yesu mpenzi wangu wa kimungu! Nisaidie nisipoteze vazi langu la pili la ubatizo! Nizuie utakapoona naelekea kutenda dhambi kwa makusudi hata kama ni ndogo, nisitafute kikingine isiopokuwa wewe, viumbe visiwe na thamani kwangu na mimi kwao ila wewe Yesu uwe yote, …Yesu nakuomba amani ya ndani na upendo ambao sio mimi ila wewe ndani yangu, niko radhi kufa shahidi kiroho au kiroho na kimwili ili kutimiza mapenzi yako na kuifikia sehemu ambayo ulitangulia kuniandalia. Yesu niwezeshe kuokoa roho nyingi, leo isipotee hata moja na roho zote za toharani  zivushwe kwenda mbinguni. Amina.

UTUME wake wa pekee ni kumfanya Yesu ajulikane na apendwe na watu wa nchi zote, alifanya hivyo kwa njia sala na sadaka ndogondogo.Theresia alikuwa na shauku kubwa ya kuwa mmisionari, alitamani afike duniani kote akihububiri upendo wa Mungu katika Fumbo la Msalaba na ufufuko wa Bwana harusi wake Yesu Kristo, hakuweza kwenda kimwili kwa vile alikuwa mtawa wa ndani pia afya yake kwa muda mrefu ilikuwa ni tete sana hivyo akatolea mateso ya ugonjwa na mateso mengine aliokutana nayo kwa ajili ya wamissionari, aliwaandikia barua kuwatia moyo na zaidi Theresa amefika duniani kote kwa njia ya sala. Katika kufanikisha adhima yake ya kumfanya Yesu atambulike na apendwe na watu wa mataifa yote alijitoa mhanga kwa ajili ya wongofu wa wakosefu wakubwa, akiamini katika upendo wa Mungu wenye huruma isiyo na mipaka. Aliwaombea wakosefu neema ya toba na wongofu wa ndani. Bwana Franzini alikuwa mfungwa aliyehukumiwa kunyongwa, Theresia alisoma katika gazeti habari zake na akapata uchungu kuwa hii roho inakaribia kuangamia maana Franzini hakuwa mchamungu, Mtakatifu Theresia akamsihi Yesu  amguse amjalie neema ya kutubu dhambi zake ili baada ya adhabu ya kifo, roho yake isiende motoni. Yesu aliisikiliza sala ya Theresia na kumpa ishara ya wongofu wa huyo mfungwa Franzini ambaye alibusu Msalaba ishara ya toba na wongofu wa ndani.  

KUWAOMBEA MAPADRE: Siku iliyotangulia nadhiri zake, mbele ya Yesu wa Ekaristi Takatifu alijitafiti na kusema nimekuja kwenye Monasteli ya Wakarmeli kwa ajili ya kuziokoa roho, kusali hasa kuwaombea mapadre. Alitamani kuishi upendo wa kidugu katika jumuiya.  Alipenda kukaa karibu na masista wenzake hasa wale wasio mvutia na waliokuwa wanamsababishia mateso, wazee walalamishi aliwachukulia kwa upendo, kuwavumilia na kuwasamehe. Hamu kubwa ya Mtakatifu Theresia ilikuwa ni kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu, kukutana na kukaa na Yesu mpenzi wa moyo wake  kila siku na katika uzima wa milele.  Maneno ya mwisho ya  Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kabla ya kukata roho kwa ugonjwa wa Kifua kikuu, TB,  uliomtesa kwa muda  kitandani anasema  “Mungu wangu nakupenda”. Maneno yaliyotawala maandishi yake yote “ Yesu Nakupenda” kabla ya kifo aliahidi akisema  “Nitakaa mbinguni nikiwatendea watu mema duniani, ndizo neema tele kabisa  nitakazowanyeeshea mvua ya mawaridi. Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa katika maisha yake yameandikwa kwanza kwa lugha ya Kifaransa na baadaye yakafsiriwa kwa lugha mbalimbali.  Kwa lugha ya Kiswahili Kitabu cha maisha yake kinaitwa  “Ua la Upendo” na kwa “Kihaya cha ndani kabisa” kinaitwa  “Akamuli ke ngonzi”, yaani hadi raha katika masuala ya utamadunisho! Imekaa vizuri!

Theresia wa Mtoto Yesu
30 September 2020, 16:26