Tafuta

Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania: Waraka Kuhusu Uchaguzi Mkuu Nchini Tanzania tarehe 28 Oktoba 2020 Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania: Waraka Kuhusu Uchaguzi Mkuu Nchini Tanzania tarehe 28 Oktoba 2020 

Waraka wa Kichungaji Kuhusu Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020

Askofu mkuu Isaac Amani ameandika Waraka wa Kichungaji mintarafu Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba 2020. Anachambua kisa cha Esau kuuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza na baraka zake, wajibu wa mpiga kura; mambo wanayopaswa kuzingatiwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu pamoja na madhara ya kutoa na kupokea rushwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika roho ya mwondoko, kuwajibika na kushirikiana katika Kristo Yesu, Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania, ameandika Waraka wa Kichungaji kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Arusha akiwashirikisha kisa cha Esau na Yakobo nduguye, mintarafu Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba 2020. Katika Waraka huu, Askofu mkuu Isaac Amani anachambua kisa cha Esau kuuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza na baraka zake kwa bakuli la dengu nyekundu! Dhamana na wajibu wa mwananchi mpiga kura; mambo wanayopaswa kuzingatiwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu pamoja na madhara ya kutoa na kupokea rushwa!

Askofu mkuu Amani kwa ufupi kabisa, anabainisha kinzani zilizokokuwepo kwenye familia ya Mzee Isaka na mkewe Rebeka pamoja na watoto wao Esau ambaye alikuwa ni mwindaji na Yakobo alikuwa ni mkulima. Isaka alimpenda sana Esau kwa sababu alipenda kula mawindo yake lakini Rebeka alimpenda Yakobo. Naye Yakobo kwa kusaidiwa na Mama yake akamlaghai baba yake na hivyo kuchukua haki ya mzaliwa wa kwanza na baraka, hali ambayo ilisababisha chuki na uhasama kiasi cha Esau kuweka kisasi cha kutaka kumuua ndugu yake Yakobo. Rej. Mwa. 25: 24-41. Askofu mkuu Amani anasema, uchaguzi mkuu ni fursa adhimu ambayo watanzania wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Amani kwamba, raia wenye uzalendo tayari wamekwisha kujiandikisha na hata kuhakiki majina kwenye Daftari ya Mpiga Kura, ili waweze kutumia haki yao Kikatiba kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu nchini Tanzania. Kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha hekima na ukomavu wa kisiasa, ili uchaguzi uweze kuwa: wa wazi, huru na wa kweli, ili hatimaye, Tanzania iweze kuwapata viongozi waliochaguliwa na wananchi wenyewe! Mwananchi mwenye sifa anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi. Lakini, ikumbukwe kwamba, haki na wajibu ni sawa na chanda na pete. Haki ya kupiga kura inaandamana na wajibu!

Wapiga kura wahakikishe kwamba, wale wanaowapigia kura wanazo sifa za kuwaongoza watanzania; wanayo nia thabiti ya kutekeleza malengo waliyobainisha wakati wa kampeni. Wananchi wawasikilize viongozi wanapoendelea kunadi sera na Ilani za vyama vyao, ili waweze kuwa na busara ya kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo fungamani. Wasimamizi wahakikishe kwamba, wanasimamia mchakato mzima kwa haki, uwazi na uhuru kamili. Ili baada ya matokeo viongozi wapya husimikwa na wale waliopata kura chache waungane na viongozi wapya pamoja na wananchi ili kuijenga Tanzania. Hii ndiyo njia makini ya kupata viongozi sanjari na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watanzania. Watanzania wajitahidi kuwa ni wachamungu na kamwe wasikubali kuuza haki yao kwa “bakuli la pilau”, bali wasimame kidete katika uhuru na ukweli kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao na usalama wa watanzania wote.

Askofu mkuu Amani anawataka watanzania kuwaogopa wale wote wanaotafuta madaraka kwa njia ya rushwa, wale wanaotaka kuhatarisha amani na usalama; wale wanaotaka kuwalaghai watanzania kwa kutaka “kujimwambafai” lakini ni sawa na “debe tupu” kwani ni watu wasiokuwa na uzalendo. Watanzania wakumbuke daima kwamba, rushwa ni adui wa haki; kwani kuomba na kututoa rushwa ni sawa na mpiga kura kuuza haki yake msingi kwa kuidharau na kumchagua mtu asiyekuwa na sifa na matokeo yake, atakuwa mtumwa. Kwa ufupi, rushwa ni biashara ya kuuziana haki! Matokeo yake ni kuenea kwa uhalifu dhidi ya haki. Huu ni ugonjwa mbaya sana unaoweza kufananishwa na mkorogo wa sumu na asali: kwa maonjo ni mtamu, lakini kwa hakika unaua.

Watanzania wasiposimama kidete, rushwa itaisambaratisha amani ya nchi. Lakini “haki ikitekelezwa, watu wema hufurahi, lakini watu wabaya hufadhaishwa”. Meth. 21:15. Umefika wakati kwa watanzania kuchagua viongozi wenye sifa, kwa uelewa na kwa uhuru bila kufuata mkumbo. Watanzania wathubutu kuchagua Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; wasimame kidete kuchagua uhuru na haki, kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kudumisha amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Moyo wa uzalendo upewe kipaumbele cha kwanza!

Jimbo kuu la Arusha
12 September 2020, 14:16