Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 19 ya Mwaka A wa Kanisa: Wazo kuu: Injili ya Imani na Matumaini kwa Mwenyezi Mungu hata nyakati za dhoruba kali! Yeye yupo daima pamoja na waja wake. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 19 ya Mwaka A wa Kanisa: Wazo kuu: Injili ya Imani na Matumaini kwa Mwenyezi Mungu hata nyakati za dhoruba kali! Yeye yupo daima pamoja na waja wake. 

Tafakari Jumapili 19 Mwaka A: Injili ya Imani na Matumaini

Ujumbe wa Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Mungu wetu ni Mungu wa utulivu, amani na mapendo kwa waja wake. Hili linajidhihirisha jinsi Mwenyezi Mungu alivyomtokea Eliya na kuongea naye katika upepo wa utulivu katika mlima horebu na jinsi Yesu alivyotuliza dhoruba katika ziwa Galilaya na kuwaokoa wanafunzi wake: Imani na Matumaini!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 19 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya domenika hii unasema: Mungu wetu ni Mungu wa utulivu na amani. Hili linajidhihirisha jinsi Mungu alivyomtokea Eliya na kuongea naye katika upepo wa utulivu katika mlima horebu na jinsi Yesu alivyotuliza dhoruba katika ziwa Galilaya na kuwaokoa wanafunzi wake.  Somo la kwanza la kitabu cha Wafalme linatusimulia jinsi Nabii Eliya alivyokutana na Mungu katika katika pango mlimani Horebu alipokimbilia kwenda kujificha, akimkimbia Yezebeli mke wa Ahabu mfalme wa Israeli aliyetafuta kumuua kwa kusababisha manabii wa Baali wauawe na watu baada ya kuwa wameshindwa katika shindano lililofanyika ili kujua Mungu wa kweli ni yupi kati ya Mungu wa Israeli au Baali. Akiwa ndani ya pango Mungu anamuuliza, unafanya nini hapa? Naye akasema, Naona uchungu na wivu, ewe Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue! (1Waf. 19:10).

Mungu alipojifunua kwa watu wake katika Agano la Kale, alitumia ngurumo na radi, moto na matetemeko ya nchi kuwafanya watu watambue ukuu na uwezo wake. Alipokuwapo Eliya ndani ya pango palitokea dhoruba kubwa, radi na tetemeko la nchi, lakini Mungu hakujitokeza kwake kupitia ishara hizi, bali alijionesha katika upepo mtulivu. Mungu akaongea na Eliya kama mtu anavyoongea na rafiki yake; kwa sauti ya upole na utulivu akimwambia kuwa yupo pamoja naye hata kama yuko kimya. Mungu anamwonyesha Eliya kuwa hawakomboi watu kwa kuwapatiliza kwa moto, matetemeko, upepo mkali, kwa kuwatesa au kuwauwa. Si Mungu wa kisasi ni Mungu wa msamaha na amani. Ndiyo maana Mungu hajionyeshi katika kelele ya upepo mwingi wa nguvu uliyoipasua milima na kuivunjavunja miamba, wala katika tetemeko la nchi wala katika moto kama Eliya alivyofikiri bali katika sauti ndogo ya utulivu. Imani ya nabii Eliya kwa Mungu iliimarika, akawa na ujasiri wa kusimama mbele za Mungu. Hata hivyo Mungu alimtaka amchague mrithi wake ambaye ni Elisha. Licha ya kuona makuu ya Mungu aliyoyatenda kupitia Eliya wengi katika Israeli walirudi tena kuabudu miungu ya uwongo. Hata hivyo imani ya Eliya kwa Mungu ilibakia imara ndiyo maana anakumbukwa kama nabii mkubwa zaidi baada ya Musa ndiyo maana wote wawili walitokea wakati wa kugeuka sura kwa Yesu mlimani Tabor (Mt. 17:3).

Imani ya Nabii Eliya kwa Mungu ilimfanya awe mwaminifu katika kazi ya Mungu. Kumbe, ni katika utulivu na ukimya wa kutafakari ndipo Mungu anajitokeza na kuongea nasi. Ili tukutane na Mungu na kuongea naye tunahitaji utulivu wa ndani mwa mtima wetu, tunahitaji sio tu ukimya wa kutokuongea bali pia utulivu wa nafsi na akili katika kumtafakari Mungu na makuu yake. Sala za kelele, kulialia na kurukaruka ni fujo mbele za Mungu na haziwezi kusikilizwa. Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake kwa Warumi anaeleza huzuni aliyonayo moyoni akisema; nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Paulo ana huzuni kwa kuwa Wayahudi waliokirimiwa kipekee na Mungu kwa kupewa Neno la Mungu, zawadi bora kupita zote ya Masiya kuzaliwa kwao, lakini wao wakamkataa yeye aliye njia pekee ya wokovu ambaye torati na manabii walitabiri kuja kwake na ametoka katika ukoo wao. Je, sisi tu tofauti na wayahudi? Tujitafakari mienendo yetu kama kweli baada ya kulipokea neno la wokovu Bwana wetu Yesu Kristo kwa sakramenti ya ubatizo na mafundisho mengi tunayopata tumebadilika na kuziacha njia zetu mbovu na ovu au tumekaza shingo na kuwa wakaidi kuliko tulivyokuwa mwanzo.

Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo inasimulia jinsi Yesu alivyotembea juu ya maji ili kudhihirisha umungu wake kwani kadiri ya Agano la Kale walisadiki kuwa ni Mungu tu anaweza kutembea juu ya maji. Kutembea kwake Yesu juu ya maji kulikuwa hakikisho kwa mitume wake kuwa yeye ni Mungu nao wakamsujudia wakisema, hakika wewe ni Mwana wa Mungu. Petro anaomba naye atembee juu ya maji, anataka kufanana na Mungu. Yesu anamruhusu lakini mara akaanza kuzama, sababu alikosa imani. Imani yetu kwa kristo inapaswa kuendelea kukua siku kwa siku. Injili inaonesha wazi kujali kwa Yesu katika kuimarisha imani ya mitume kwake. Haitoshi kuonesha imani yetu kwa Yesu wakati tunajisikia furaha, bali imani yetu kwa Yesu inaoneshwa vizuri wakati wa majaribu; maisha yetu yote yanapaswa kuwa ungamo la imani kwa Yesu. Imani inatuonesha nguvu ya Yesu; hakuna kisichowezekana tunapoweka matumaini yetu kwa Yesu. Tunarudia hili tena na tena na tunaamini tunachosema lakini mang’amuzi yanatuambia kuwa wakati tunapojaribiwa, imani yetu inaonesha kuwa tu dhaifu kuliko tunavyofikiria na tunashindwa kirahisi kwa vishawishi na majaribu.

Pale msaada wa binadamu unaposhindwa ndipo sala yetu; Bwana niokoe, tunapoisali mara moja. La kusikitisha ni kwamba tunachelewa mara nyingi kutamka hili. Yesu hayuko mbali wala hasahau kujihusisha na sisi katika majaribu yetu. Hachelewi kuja kutuokoa. Mang’amuzi yanatufundisha kuweka matumaini yetu kwake. Yesu atakaa katika nyua za jumuiya na familia zetu kama kuna umoja na upendo kati yetu. Kama tukimsukumia mbali kwa mgawanyiko, mashua zetu hazifiki popote. Yesu anawaambia mitume wasiogope. Sisi pia tukikosa imani tunazama katika matatizo na mahangaiko.Yesu anatumbia tusiogope. Mtume Petro anatuambia kuwa Yesu alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenyehaki” (Pet 2:23). Ni katika utulivu wake, upole wake, unyenyekevu wake na utii wake aliweza kutukomboa. Je, mimi na wewe tunapotukanwa tunafanya nini? Je, tunapotendewa vibaya tunafanya nini? Tukumbuke kuwa sheria ya jino kwa jino itatuacha wote vibogoyo na ya jicho kwa jicho itatufanya sote vipofu. Kristo anatuambia Jifunzeni kwangu maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.” Tusiwe watu wa mapambano na kisasi. Tumwombe Mungu atulize ghasia za Maisha yetu. Kama alivvyomtokea Elia katika sauti ya utulivu alipokuwa katika dhoruba na matatizo vivyo hivyo atatuliza dhoruba zetu na kutuletea utulivu. Kama Kristo alivyotuliza dhoruba katika ziwa na kuwaokoa mitume vivyo hivyo atafanya na kwetu. Baada ya dhoruba kuna utulivu; Baada ya dhiki kuna faraja.

Mtume Petro anampa Yesu masharti ya kumwamini akisema “Kama ni wewe niamuru nikufuate juu ya maji. Nisipoweza kutembea juu ya maji sitakuamini. Hata sisi wakati mwingine tunafanya majaribio ya namna hiyo: Kama ni wewe mponye mtoto wangu. Asipopona sikuamini tena. Kama ni wewe ongeza mshahara wangu. Kama si hivyo, siji kanisani tena. Kama ni wewe nipatie pesa la sivyo sitoi sadaka. Hii ni imani ya Mikate. Imani ya miujiza. Kumfuata Kristo hakumalizi matatizo ya maisha: Petro alipoomba kumfuata Yesu akitembea juu ya maji, Yesu alimruhusu lakini hiyo haikuzuia upepo kuendelea. Hivyo, hata tukiamua kumfuata Kristo matatizo yataendelea tena inawezekana yakaongezeka kwasababu hata Petro aliogopa zaidi alipokuwa akitembea juu ya maji zaidi ya alivyokuwa akiogopa wakati yupo katika mtumbwi. Lakini upepo ulipozidi akaona shaka akaanza kuzama. Hata sisi katika maisha yetu ya kumfuasa Kristo yanaanza tukiwa motomoto lakini matatizo yanapotujia tunaona shaka na hivyo, tunapotea. Pengine tunasema nitamtegemea Mungu katika shida zangu. Lakini matatizo yanapozidi tunajiuliza hivi kweli Mungu peke yake atanisaidia, au nitumie na njia nyingine? Hivi sala peke yake itasaidia kuongeza biashara yangu au nitumie na njia nyingine nyingine?’

Tukumbuke kuwa palipo na Yesu hakuna dhoruba itakayotushinda. Licha ya matatizo kuongezeka, tukimuita Kristo atatusaidia. Daima Kristo yupo tayari kutusaidia katika shida zetu. Aliona kutoka mbali kwamba mitume wanahangaika. Akaja mbio kuwasaidia. Mungu hawezi kutuacha tujaribiwe zaidi ya nguvu zetu. Aliwaacha mitume wapigwe na upepo lakini alikuwa karibu kuwasaidia. Petro alipoona mambo yamekuwa magumu alimlilia Yesu naye akamponya. Tuwe na imani na kumwendea Kristo katika shida zetu kwasababu yuko tayari kutusaidia. Inawezeka katika maisha yetu kuna dhoruba na matatizo mbalimbali: hatuelewani katika familia, katika ndoa, katika vikundi vyetu, katika jumuiya zetu. Mwambie Kristo “Bwana niokoe” Yeye atatuliza shida zote maana yeye ni Mungu wa utulivu. Nabii Eliya, Mtume Petro na Mtume Paulo waliweka matumaini yao kwa Mungu; hawakujuta kwa kufanya hivyo. Adui wa imani ni ubinafsi. Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kuruhusu majaribu yatujie, yanatusaidia tutambue jinsi imani yetu ilivyo haba. Matumani yetu kwa Kristo yanapaswa kukua siku kwa siku, yeye ana nguvu na ni mwaminifu, mang’amuzi yaliyopita yanaonesha kwamba anastahili matumaini yetu bila masharti yoyote. Ni Yesu peke yake anayeweza kuendesha mashua ya maisha yetu hadi mahali tunapokwenda; mbinguni. Tukifika pale, tutaacha imani nje ya mlango na kupewa badala yake uzima wa milele.

 

 

07 August 2020, 07:50