Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Kashfa ya Msalaba inakuwa ni kikwaszo kwa Mtakatifu Petro. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Kashfa ya Msalaba inakuwa ni kikwaszo kwa Mtakatifu Petro.  (ANSA)

Tafakari Jumapili 22 ya Mwaka A. Mt. Petro na Kashfa ya Msalaba!

Kristo Yesu alimtambulisha Mtume Petro kuwa ni ‘’Petros’’, kuwa ni jiwe la msingi katika mcahakato wa ujenzi wa Kanisa. Lakini leo anapoteza sifa hiyo na badala yake anakuwa ni jiwe la kujikwaa na kuanguka. Leo Mtume Petro anakuwa jiwe lile linalojulikana kwa lugha ya Kigiriki kama ‘’Scandalon’’, ni jiwe ambalo kwalo mmoja anajikwaa na kuanguka. Hii ndiyo Kashfa ya Fumbo la Msalaba!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! ‘’Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu’’, (Matendo 14:22), ni maneno ya Mitume Paulo na Barnaba kwa Kanisa la Antiokia, wakiwa na nia ya kuwaimarisha katika imani. Ni ufupisho wa ujumbe wa Dominika ya leo kwa kila rafiki na mfuasi wa Yesu Kristo. Ni Injili ya Dominika ya leo inatoa jibu kwa nini Yesu aliwakataza wasimwambie mtu kuwa Yeye ni Kristo. Ni Dominika iliyopita Simon Bar Yona anapewa jina jipya la Kefa au Petro, likiwa na maana ya jiwe lile la kwanza katika msingi na leo tunaona anageuka na kuwa jiwe la kujikwaa, jiwe la makwazo kwani anawaza kinyume na Kristo, kinyume na mpango wa Mungu, kinyume na mantiki ya Masiha wa Mungu. Simon anatambulishwa kama Mwana wa Yona, Yona aliyekwenda kinyume na mpango wa Mungu lakini baadaye akakubali kutii na kuongozwa na Mungu mwenyewe.

Na hiki ndicho kinachojiri pia kwa Simon Petro ambaye mwanzoni tunaona bado hajaelewa vema umasiha wake Yesu Kristo na ni baada ya Fumbo lile la mateso, kifo na ufufuko kwa msaada wa ujio wa Roho Mtakatifu anabadilika na kuanza kuwa shahidi wa Kristo aliyeteseka, kufa na kufufuka. Ni mwaliko kwa maisha ya kikristo ambao unakwenda kinyume na mantiki ya ulimwengu wetu wa leo, ulimwengu wa kusaka raha za kila aina, madaraka na nafasi za heshima iwe kiuchumi au hata kisiasa. Ni kinyume na mantiki ya kuponda maisha, kwani Yesu leo anatuambia kila anayetaka kuwa mfuasi wake basi hana budi kubadili kichwa na moyo wake, kuwaza kadiri ya mantiki ya Injili, kadiri ya Neno la Mungu na si kadiri ya mantiki zetu za dunia hii. Ni mwaliko wa kubadili namna zetu za kufikiri, kutenda na kuishi.

Somo la Injili ya Dominika iliyopita, Petro alimkiri Yesu kuwa ni Kristo lakini Yesu anawasisitiza kwa kusema; ‘’Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote ya kwamba yeye ndiye Kristo’’. Na leo tunapata nafasi ya kutafakari zaidi kuona sababu za kutowaruhusu kuwashirikisha wengine juu ya ukweli huo. Mtume Petro alitambulishwa kuwa ni ‘’petros’’, kuwa ni jiwe la msingi, lile jiwe la kwanza kabisa katika ujenzi, lakini leo anapoteza sifa hiyo na badala yake anakuwa ni jiwe la kujikwaa kwa kushindwa kubadili kichwa chake, kwa kutaka bado kuendelea kuongozwa na mantiki ya dunia hii, mantiki inayokinzana na ile ya mpango na mapenzi ya Mungu.  Leo Mtume Petro anakuwa jiwe lile linalojulikana kwa lugha ya Kigiriki kama ‘’scandalon’’, ni jiwe ambalo kwalo mmoja anajikwaa na kuanguka.

Wayahudi wa nyakati zile za Yesu walikuwa wanamtegemea na kumsubiri Masiha atakayebadili maisha yao na kuyafanya kuwa bora zaidi, maisha yaliyosheheni amani na haki (Ezekieli 49). Marabi waliwafundisha watu kuwa siku za Masiha, nchi yao itageuka na kuwa bustani nzuri, bustani zitakuwa misitu, na ardhi yao itatoa mazao mara elfu, kutakuwa na utajiri na ustawi kwa wote kama siku zile za uumbaji wa ulimwengu katika bustani ile ya Paradiso. Hii ilikuwa ni mtazamo si tu wa wayahudi wengine bali hata wale waliokuwa wafuasi na rafiki zake Yesu. Ulikuwa ni mtazamo na matarajio hata ya wale rafiki wa karibu wa Yesu yaani mitume akiwemo Mtume Petro. Kwa bahati mbaya bado hata katika nyakati zetu wapo wahubiri wengi na wenye wafuasi wengi wakihubiri Injili ya mafanikio, Injili ya utajiri, Masiha anakuja ili kututimizia mahitaji yetu ya kidunia. Injili ya mafanikio inakuwa sawa na mantiki ya ulimwengu wetu wa leo, ulimwengu wa mashindano ya kiuchumi, usalama wake unatokana na uwingi wa mali na vitu mmoja anavyojilimbikizia.

Na ndio walikuwa wanatarajia kuyaona haya kwa ujio na uwepo wa Bwana na Mwalimu wao Yesu wa Nazareti, waliomtambua na kumkiri kuwa ni Kristo, mpakwa mafuta na Masiha wao. Na ndio tunaona matarajio yao ni kuziona siku zile za utukufu na swali pekee kichwani mwao ni nani atakuwa na nafasi ya kwanza, nafasi za heshima kwa cheo, nafasi za kipekee zaidi baina yao. Na ndio tunasoma; ‘’Lakini wao wakanyamaza, maana njiani walikuwa wamebishana ni nani aliyekuwa mkubwa kati yao’’ (Marko 9:34). Ni mjadala ambao labda hata nyakati zetu katika jumuiya zetu bado unatusumbua na hata kutupelekea kugawanyika na mbaya zaidi hata kuchukiana na kupoteza sifa ya mwanafunzi na mfuasi wa Yesu. Mabishano juu ya ukubwa na heshima yapo katika familia zetu, jumuiya zetu za makuhani maparokiani, majimboni na hata katika Kanisa zima la ulimwengu. Ukubwa ni mantiki ya ulimwengu huu lakini sisi tulio wanafunzi na wafuasi wa Yesu tunaalikwa kuwa watumishi na sio mabwana wakubwa na waheshimiwa.

Ni katika muktadha huu Yesu anawaalika wanafunzi wake kubadili vichwa vyao, namna zao za kufikiri, kubadili mantiki zao. Yesu anawaambia kwa kuwaonya kuwa anapaswa kwenda Yerusalemu na sio katika utukufu waliokuwa wanaoufikiri wao, anakwenda Yerusalemu sio kufanyika mfalme kama yalivyokuwa matarajio yao bali ili apate mateso mengi, kufa na hatimaye siku ya tatu kufufuka. Yesu haendi Yerusalemu ili akatawazwe mfalme na kuishi katika majumba ya kifahari, bali kupokea kikombe cha mateso, kifo na hatimaye kufufuka siku ya tatu. Mateso, kifo na ufufuko ndio kusema matarajio na matazamio yao yote yamekuwa ni bure, ni sawa na kusema wamepoteza muda wao kumfuata mtu ambaye hatima yake ni hii ya kushindwa mbele ya macho ya mwanadamu. Mitume wanabaki na mfadhaiko akilini na hata mioyoni mwao, ni kauli ya kukatisha tamaa kwani walikuwa na matarajio makubwa kiasi cha kuwapelekea hata kubishana kati yao juu ya nani ni mkubwa zaidi ya wengine, nani atakuwa katika nafasi za heshima. Kwao walielewa kuwa ujio wa Masiha, ni ujio wa maisha bora kabisa na zaidi sana kwao waliokuwa rafiki wa karibu na huyu Kristo. Kristo anakuwa ni kikwazo kwao, kwani ni kinyume na matarajio na matazamio yao.

‘’Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, hasha, Bwana, hayo hayatakupata’’, Ndio kusema Petro anamchukua na kumtenga na wengine ili yeye achukue nafasi ya kuwa mwalimu, ya kumwelekeza Kristo juu ya matarajio yao kwake. Kwao walifundishwa na marabi kuwa Masiha hawezi kufa, na kwa ujio wake basi wafu watafufuka kutoka makaburini ili waweze kuungana na walio wazima katika kufurahia ujio wake. Petro anasahau nafasi yake na kutaka kumtangulia yule aliye mwalimu na Bwana wetu, anachukua nafasi ya kuwa mwalimu na kuacha kumsikiliza mwalimu wa kweli, anatangulia mbele badala ya kufuata njia ya Masiha. Jibu la Yesu linatustua sana kwa jinsi anavyotumia maneno makali; ‘’Akageuka, akamwambia Petro, nenda nyuma yangu, shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu’’. Kurudi nyuma haina maana kuwa Petro akae mbali na Yesu hapana bali hapaswi kwa sasa kujichukulia nafasi ya kuwa mwalimu na badala yake akae nafasi ya nyuma ili ajifunze kutoka kwake, kutoka kwa yeye aliye Bwana na Mwalimu wetu, kwa kuifuata njia yake.

Petro anapoteza nafasi yake kama nilivyotangulia kusema hapo juu kwa kutaka yeye awe mwalimu wa Yesu, kwa kutaka kumfundisha mpango na mapenzi ya Mungu kwa kuongozwa na mantiki ya kibinadamu. Kosa la Mtume Petro sio dogo kwani alipotea njia, akasahau kujifunza kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa kukubali kuongozwa na mantiki za dunia hii na sio ile ya Mungu. Petro anapoteza mwelekeo kwa kwenda njia inayokinzana na ile ya Masiha. Petro anaongozwa na mantiki ile ya yule mwovu aliyekwenda kwa Yesu na kumshawishi ili amsujudie ili kumpatia mali za ulimwengu huu. ‘’Hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu. Hapo, Yesu akamwambia, Nenda zako Shetani’’ (Mathayo 4:8-10). MtumenPetro aliyepewa jina la Kefa, manake jiwe la msingi, leo anapoteza sifa ile kwa kuwa jiwe la kujikwaa, jiwe la makwazo(scandalon), jiwe linalopoteza mwelekeo sahihi kwa kukubali kuongozwa na mantiki ile ya ulimwengu huu, mantiki ya utukufu, utajiri, mafanikio, nafasi za heshima na ukubwa, mantiki ambazo zinakinzana na hata kututoa katika mwelekeo sahihi, ramani ya kutupeleka katika urafiki na ukaribu na Mungu.

Ni hapa mara baada ya kumkemea Mtume Petro, sasa Yesu anawageukia wanafunzi wake wengine wote na kuwafundisha, akiwaalika kubadili vichwa vyao kwa kuanza kuongozwa sio tena na mantiki ya dunia hii bali ile ya Kristo, ya mateso, kifo na hatimaye kufufuka pamoja naye. Ni mwaliko wa kukubali kuwa wanafunzi wake na kujifunza kutoka kwake kwa kufuata njia ile aliyoipitia yeye mwenyewe. Mwanafalsafa Erasmus wa Rotterdam (1469-1536)  akijaribu kuelezea sehemu ya Injili ya leo alisema; “Multi me sequuntur pedibus magis quam imitazione’’ ni maneno ya kilatini nitajaribu kutoa tafsiri yangu kuwa; ‘’Wengi wananifuata zaidi kwa miguu yao kuliko kwa kuiga mifano yangu’’. Ni ufuasi unaokosa uhalali, kwani mfuasi wa kweli ni yule anayeenenda kama mwalimu wake, ni anayefikiri na kuenenda kadiri ya mafundisho ya mifano halisi ya mwalimu wake. Haitoshi kuwa wakristo wa Dominika tu au wa majina tu bali maisha yetu hayana budi kuakisi Injili ya Kristo, ni kwa kulishika na kuliishi Neno lake hapo tunakuwa kweli wafuasi, hivyo tusiishie kuwa wakristo wa jina tu wakati maisha yetu yakiwa bado yanaongozwa na mantiki za ulimwengu huu.

Leo Kristo anatualika kuwa kila mmoja wetu anayetaka kuwa mfuasi wake basi hana budi kuzingatia mambo matatu; ‘’Na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate’’. Ufuasi ni kuwa tayari kupitia njia ile aliyopitia Yesu Kristo. Njia ya Kristo ndio ile inayoelekea Golgota na si katika majumba ya kifalme au ya kikuhani pale Yerusalemu, bali ni njia inayofikia ukomo na kilele chake pale juu msalabani, kifo cha aibu na fedheha, kifo cha kujivua kila aina ya utukufu wa dunia hii. Kujikana, ndio kusema kuacha kujipa nafasi ya kwanza katika maisha. Ni hulka ya mwanadamu kujifikiria yeye katika maisha ila kuwa mfuasi wa Kristo tunaalikwa kuacha kujiweka nafasi ya kwanza, kujisahau mimi ili nafasi hiyo nimpatie Kristo kwa njia ya huyu jirani. Mantiki ya ulimwengu wetu ni kupambana ili kila kitu chema kiwe changu, iwe ni cheo, mali, nafasi na kadhalika. Ni ulimwengu unaoongozwa na mantiki ya ubinafsi na umimi. Sifa ya kwanza ya mfuasi wa kweli wa Yesu ndio kujikana, kutojipa nafasi ya kwanza, kutokuangalia masilahi binafsi, hata ikiwa katika upande wa maisha ya kiroho.

Hatutendi mema ili kujihakikishia nafasi mbinguni, au kukua na kupiga hatua katika maisha yetu ya kiroho, kwani huko bado ni kutenda kibinafsi. Bali kumpenda mwingine bila kutarajia chochote kwa upande wetu. Najua hapa wengi wataniuliza inawezekanaje hili? Ndio kupenda kama Mungu anavyotupenda sisi, upendo usiojitafuta au kutaka manufaa yake hatimaye, bali kupenda bila masharti, ni kumpenda mwingine bila kuweka masharti kwa kuwa ni mwanafamilia, ndugu au rafiki au mjuani au basi nitanufaika na kitu fulani baadaye, maana huo sio upendo kwa jirani bali unageuka kuwa ni umimi na ubinafsi. Upendo wa kweli ni ule usiohesabu faida kwa anayependa iwe yoyote ile. Katika jamii za Kiyahudi kulikuwa na mfano juu ya upendo usio na masharti; Mkulima mmoja alijikuta akiwa katika mgahawa mmoja pamoja na marafiki zake. Baada ya kubaki katika ukimya kwa muda, alimgeukia mmoja wa marafiki zake na kumuuliza: Hebu niambie kidogo: unanipenda au hapana? Na rafiki yake akamjibu mara moja na kumwambia: Ndio, nakupenda! Na hapo mkulima alisema: Wewe unaniambia kuwa unanipenda, na bado haujui mpaka sasa nini ninahitaji.

Ikiwa kweli unanipenda, hakika ungelijua hitaji langu. Hakika kumpenda mwingine ni pamoja na kujua mahitaji yao na hata kuteseka pamoja nao’’ Ni simulizi dogo lakini linalotualika kujitafakari, maana tunaishi katika ulimwengu wa kila mmoja na lwake, ulimwengu wa kujali mambo yangu tu na ya wengine hayanihusu, ni ulimwengu wa mmoja anakula na kunywa hata kusaza na jirani yetu anakosa hata mlo mmoja kwa siku, kila mmoja aangalie maisha yake. Ni watu wangapi leo wamekata tamaa ya maisha, na hawana mtu wa kuwasikiliza au hata kuwapa neno la faraja? Ajitwike msalaba wake, ndilo agizo la pili ili tuweze kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Kubeba msalaba haimaanishi hata kidogo kuvumilia mateso ya kimwili au madhulumu yawe madogo au makubwa au maumivu. Mtaniuliza hata hapa ila yafaa tukumbuke kuwa mkristo au mfuasi wa Yesu haalikwi kusaka mateso au maumivu bali anaalikwa kupenda. Msalaba hapa ni ishara ya upendo, kujitoa mzimamzima bila kujibakisha.

Kujitwika upendo na hapo tunaweza kumfuasa Yesu Kristo, hata kama yatupasa kufa tufe kwa sababu tunampenda Mungu na jirani. Kumfuasa Kristo ni kupenda kama Kristo, ni kukubali kuongozwa na Injili yaani Neno lake, ni kuacha kutawaliwa au kuongozwa na mantiki ya ulimwengu huu. Ni kupenda hata ikibidi kutolea sadaka maisha yangu. ‘’Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayeipoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona’’. Marabi walikuwa na msemo maarufu uliosema; ‘’Mwanadamu anapaswa kufanya nini ili aishi? Kujiua yeye mwenyewe! Na nini mwanadamu anapaswa kufanya ili afe? Ni kuishi kwa ajili yake mwenyewe!’’ Ndio kusema ubinafsi na umimi ni utumwa na kifo, kujali maisha yako ni sawa na kuyaangamiza kwani inageuka kuwa sawa na kujiweka kifungoni au gerezani. Ni vema tukajaribu kujiuliza kila mmoja wetu aina ya maisha ninayoishi au unayoishi ni je naishi kwa ajili yangu mwenyewe au kwa ajili ya wengine? Ninajali mambo yangu tu kana kwamba wengine hawaishi? Je kuishi kwangu kunagusa vipi maisha ya wengine?

Tunaalikwa kupoteza nafsi zetu kwa ajili ya Kristo. Ndio mwaliko wa kupenda bila kujibakiza, iwe ni nguvu zetu, vipaji au mali zetu, muda au uwezo wetu fulani kwa ajili ya wengine, hapo kweli tunakuwa wafuasi wa Yesu Kristo. Mantiki ya dunia hii inatualika kusaka na kujilimbikizia, kumiliki na hata kutawala wengine, lakini tunajua sote mwisho wake ni mahangaiko na mateso nafsini mwetu hivyo leo anatualika kuyapoteza ndio kusema ni kwa kuyatoa maisha yetu na vyote tulivyo navyo kwa ajili ya wengine hapo tunapata amani na furaha ya kweli. Mantiki ya Kikristo ni kinyume na kanuni za kiuchumi wa dunia hii kwani sisi tunayapata maisha ya kweli kwa kuyapotea, kwa kujitoa, kwa kupenda bila kusaka faida binafsi, upendo ni kujitoa mzima kama Kristo alivyojitoa pale juu msalabani. Ukristo unatudai kuishi kwa ajili ya wengine na kamwe si kwa ajili yetu. ‘’Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake?’’.

Hapa kwa nafsi katika Biblia ndio sawa na kusema mwanadamu mzima, mwili na roho, ukamilifu wake, maisha yake na hata hatima yake baada ya maisha ya hapa duniani, na upande wa pili tunaona Yesu akizungumza juu ya kuupata ulimwengu mzima, ndio kusema vitu vya dunia hii kama vile, ndio sanamu za nyakati zote yaani madaraka, utajiri, mafanikio, utukufu binafsi, malimwengu na raha za dunia hii na kadhalika. Injili leo inatualika kubadili vichwa vyetu kwa kufanya maamuzi sahihi kwa kukubali kuongozwa na mantiki ya Kristo, kinyume na tofauti na mantiki ya dunia yetu. ‘’Anifuate’’, ndilo agizo la tatu na la mwisho ili kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Kumfuasa hapa kama nilivyotangulia kuonesha katika maneno ya Erasmus wa Rotterdam, sio kwa miguu bali kwa kukubali kuifuata njia ile ya Kristo. Kukubali kuwa sehemu ya mpango na misheni ya Kristo, kukubali kumpenda mwingine kama anavyopenda Yeye. Mtu maskini na wa haki hana kitu cha kukitegemea na kwacho kuweka moyo wake zaidi ya kwa Mungu, lakini ni ngumu kwa mtu tajiri na mbinafsi kumtegemea Mungu kwani mali na vitu vyake daima vinampigia kelele: Nitegemee mimi! Ni mwaliko kwetu leo kuangalia je kweli sisi ni wafuasi wa Yesu, tunaongozwa kweli na mantiki ya Kristo au ya ulimwengu huu? Kuwa mfuasi daima lazima kujikana, kujitwika msalaba na kumfuata.

Nawatakieni tafakari na Dominika njema.

28 August 2020, 07:45