Tafuta

Vatican News
Sala ni imani inayomwilishwa katika matendo. Sala ni imani inayomwilishwa katika matendo. 

Tafakari Jumapili 20 Mwaka A: Sala Inayomwilishwa Katika Matendo

‘’Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie’’ ni sala ya mwanamke yule mkananayo, ni sala isiyokuwa na mashaka katika wema na upendo wa Mungu, ni mfano wa sala ya mmoja mwenye kuwa na hakika bila mashaka yoyote kwa Mungu, pamoja na kuwa mtu wa mataifa anamtambua Yesu kuwa ni Bwana, kuwa ni Mungu na anafika na kumsujudia, ndio kumwabudu. Sala na Imani.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Ni siku chache tu zimepita tangu tuliposikia habari mbaya na za kusikitisha juu ya mlipuko mkubwa uliopelekea kuondoa uhai wa mamia ya watu na mamia mengine wakiachwa majeruhi katika mji mkuu wa Lebanoni yaani Beiruti. Tuwaombee ndugu zetu wa Lebanoni wanaopitia kipindi hiki kigumu cha majaribu makubwa ili Yesu aliyefika katika nchi ile miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita akiwa katika mwili wake wa nyama, aweze pia kuwa nao leo na hasa katika kipindi hiki kwa namna ya pekee. Injili ya leo inaelezea Yesu aliondoka huko na akaenda kando pande za Tiro na Sidoni, ndio kusema sehemu zile leo zinazotambulika kama Lebanoni. Na akiwa pale tunaona mhusika mwingine mkuu anayesikika leo ni mwanamke mkananayo wa mipaka au maeneo yale ya Siro Foinike, ndio sehemu zilizokuwa zinakaliwa na wageni kwa maana ya watu wa mataifa, yaani pia wapagani, watu wasiokuwa wa taifa lile teule. Wazo kuu katika masomo ya Dominika ya leo ni jibu litokanalo na ukweli kuwa wokovu ni kwa ajili ya watu wote na sio tu kwa taifa lile teule la wanawaisraeli.

Nabii Isaya katika somo la kwanza anaonesha jinsi mpango wa Mungu ni kuwakomboa wanadamu wote bila kujali rangi wala kabila wala taifa lao. ‘’Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu…Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu…’’ (Isaya 56). Nabii Isaya katika sura ile ya 66:21 anakwenda mbali zaidi na kusema; ‘’Pia nitawachagua baadhi yao kuwa Makuhani na baadhi yao kuwa Walawi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema’’.  Dhana hii haikukubalika na wala kupokelewa na wayahudi wote kwani baadhi bado waliamini kuwa wokovu ni kwa ajili ya wao tu kama taifa teule la Mungu. Hata kati ya waamini wakristo wale wa kwanza, waliompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wao, nao pia baadhi walipata shida hiyo (Matendo 10 na 11 masimulizi ya Petro na Kornelio na nyumba yake), ‘’Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waamini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu na kusema. Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula nao!’’ (Matendo 11:1-3)

Ni swali lililokuwa linawasumbua hasa waamini wale wa mwanzo wenye asili ya Kiyahudi. Je, wokovu ni kwa ajili ya watu wote au kwa ajili wana wa Abrahamu tu? Na kutokana na uelewa finyu kati yao kukaanza kuzuka kila aina ya mgawanyiko na hata magomvi na makundi. Kwani walikuwepo na dhana kuwa Injili haina budi kuhubiriwa kwa wana pekee wa taifa teule na kwa kutetea msimamo wao wakawa wanafanya kurejea ukweli kuwa Yesu katika utume wake wa miaka mitatu alibaki ndani ya mipaka ya Palestina na kusisitiza somo la Injili ya Mathayo 10:5-6, ‘’Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria. Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo’’. Ni kutokana na mitazamo tofauti na kushindwa kutafsiri vema kauli hiyo ya Yesu tunaona migawanyiko katika Kanisa lile la mwanzo 1 Wakorintho 1:10-12; Wagalatia 2:11-14. Kulikuwa na wale wenye mtazamo wa kati wakisema kuwa Injili ilipaswa kuhubiriwa kwanza kwa wana wa Israeli kwa nafasi ya kwanza na kisha kuhubiri kwa watu wa mataifa yaani wageni na ndio wapagani kwa nafasi ya pili ya mwisho (Mathayo 22:1-6 na 8-10).

Ndio mfano wa karamu ya harusi iliyoandaliwa lakini wale walioalikwa wakakosa kufika na mwishoni mfalme kuwatuma watumwa wake kwenda kuwaalika kutoka barabarani ili kuwaalika wote watakaokutana nao. Israeli kama Taifa teule hakika lilikuwa na nafasi ya mzaliwa wa kwanza lakini haikuwa na maana kuwa ni taifa pekee la wana wa Mungu (Sira 36:11 na Yeremia 3:19). Mwinjili Mathayo katika hitimisho la Injili yake na hasa kuonesha wakati wa neema ulipofika na sasa ni baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Mfufuka anawaalika wanafunzi wake; ‘’Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu’’ (Mathayo 28:19). Hata Yesu wakati wa utume yake katika nchi ile ya Palestina pamoja na kuhubiri Injili ndani ya mipaka yake bado alishaonesha juu ya uwigo wa utume na misheni yake kuwa sio tu kwa taifa teule bali hata na watu wa mataifa mengine. Na moja ya ishara ya wazi juu ya hilo ndio tukio la Injili ya Dominika ya leo ambapo Yesu anasikia kilio na sala ya mwanamke mkananayo, mwanamke mgeni au wa kipagani, wa kimataifa asiyekuwa myahudi kwa dini wala kwa utaifa.

Kwa Wayahudi, Wakananayo si tu watu wa mataifa na wageni bali ni watu hatari na maadui. Hatari na uadui wao ni kutokana na historia yao kuwa mara kadhaa waliwafanya wayahudi kuacha imani yao kwa Mungu na kugeukia na kuabudia miungu yao ya uongo kama Baali na Astarte. Katika muktadha huu hata wanafunzi wa Yesu pale wanapokutana na mwanamke yule Mkananayo walibaki kuona mwitikio wa Bwana na Mwalimu wao kwa mtu mgeni na mpagani utakuwa wa aina gani. Je, Yesu anatii sheria zao za kukaa mbali na wapagani na kuwakatakaza hata kuwasogelea kwa karibu au atamsikiliza na hivyo kuenenda kinyume na sheria zao?  Mwinjili Mathayo katika somo la Injili anatuonesha mjadala ulioibuka wa mwanamke yule na Yesu. Mwanamke yule anapaza sauti yake, na si kusema lolote bali anasali tena sala inayomkiri na kumtambua Yesu kuwa sio mtu wa kawaida bali mwenye uwezo wa kimungu ndani mwake, anayeweza kurehemu maana ni Bwana na Mwana wa Daudi.

Ni hapo nasi tunabaki na mshangao kwani pamoja na kusikia mwanamke yule alipaaza sauti yake lakini Yesu alimwacha bila kumpa jibu lolote kana kwamba hakukisikia kilio chake. Na ndio hali hii tunakutana nayo mara nyingi katika sala na maombi yetu kwa Mungu hata pale tunapopaaza sauti na kumlilia mara nyingi na hata tunapoingia na kusali mbele yake tukiwa na hakika tupo sisi na Yeye tu hivyo lazima atatusikia na kutujibu sala zetu. Labda baadhi yetu inafika wakati tunakata tamaa ya kuendelea kumwamini na kumtumaini Yeye pekee.  Ni katika kipindi hicho wanafunzi wa Yesu ndio wanapoingilia kati. Ni wao wanaoona ni heri kuingilia kati kwa kutoa ushauri kwa Yesu wakisema ‘’Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu’’. Kwa kweli ushauri wao ndio kusema mfukuze, akae mbali nasi asitusumbue na kutughasi kwa makelele na vilio vyake. Ni hali ya kujimilikisha Kristo, anapaswa ahusike na mambo yangu tu na sio ya wengine, ni mali yangu na familia yangu na watu wangu tu, au kabila langu tu au jumuiya yangu, au nchi yangu tu au bara langu tu au watu wa imani yangu tu, na kadhalika na kadhalika. Kwa Mungu hakuna sera ya ubinafsishaji, ni vema tukakumbuka hata tunaposali lazima kutambua sala ni kitendo cha upendo hivyo kusali sio kwa ajili yetu tu au wale wanaokuwa karibu yetu tu bali kwa wengine wote pia, hata tusiowajua na watu wanaotuchukia na kutunenea mabaya kati ya watu.

Tunapoendelea kusoma tunaona ni kama Yesu anafuata ushauri wao kwa kuzidi kuwa mgumu katika kujibu sala na kilio cha yule mama mpagani. ‘’Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyuma ya Israeli’’. Kundi la kondoo lilipotea katika Agano la kale, kundi lililokosa mchungaji daima lilimanisha taifa teule la Israeli (Ezekieli 34:6,11,16 na Isaya 53:6). Mwanamke yule mkananayo alilitambua hilo vema lakini bado aliamini katika wema na upendo wa Mungu sio tu kwa taifa lile teule pekee bali hata kwa watu wa mataifa mengine. Mwanamke mkananayo aliamini katika wema na upendo wa Mungu na si katika mitazamo duni ya kibinadamu, mitazamo ya mipaka na kugawa wana wa Mungu kwa rangi, makabila, mataifa na mambo yafananayo na hayo. ‘’Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie’’ ni sala ya mwanamke yule mkananayo, ni sala isiyokuwa na mashaka katika wema na upendo wa Mungu, ni mfano wa sala ya mmoja mwenye kuwa na hakika bila mashaka yoyote kwa Mungu, pamoja na kuwa mtu wa mataifa anamtambua Yesu kuwa ni Bwana, kuwa ni Mungu na anafika na kumsujudia, ndio kumwabudu. Sala zetu hazina budi kuwa pia ni matendo ya imani, na ndiyo sala haswa. Kusali ni kuamini! Kusali sio kwa sababu tuna shida na mahangaiko katika maisha yetu bali tuna imani kwa Mungu. Kusali ni kumkiri Mungu na kumpenda Mungu kwa dhati.

‘’Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa’’ Ni jibu bado la kukatisha tamaa kabisa kutoka kwa Yesu kwa mwanamke yule mkananayo. Ndio kusema Waisraeli ni kundi, ndio taifa na wengine wote walitambulikana nao kama mbwa. Kwa kweli jina ‘’mbwa’’ lilionesha kuwa wapagani na watu wa mataifa wasiokuwa wanawaisraeli ni sawa na wanyama tu au takataka. Ni mtazamo uliokuwepo kati yao na hata Yesu anatumia mtazamo wao ule kutoa katekesi katika Dominika ya leo. Lakini pia hata kati yetu katika ulimwengu wa leo na yawezekana hata katika jumuiya zetu za waamini, je, tunawaona watu wote kuwa ni sawa na sisi na kuwatendea kwa haki kama wana wa Mungu au tunaangalia watu kwa hali zao labda za kiuchumi, kielimu, nafasi zao katika jamii, kirangi, kikabila na hata kidini? Jina mbwa hatulisikii tu kutoka katika kinywa cha Yesu pekee bali tunakutana nalo mara kadhaa hata katika Agano Jipya. ‘’Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua nyinyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga’’ (Mathayo 7:6). Na pia tunasoma; ‘’Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo watakaa nje ya mji’’. (Ufunuo 22:15). ‘’Jihadharini na hao watendao maovu, hao mbwa…’’ (Wafilipi 3:2). Jina mbwa lilitumika hata katika Kanisa lile la mwanzo kuonesha kila aina ya maisha yanayokinzana na Injili.

Lakini yafaa bado na hata tunabaki na maswali iweje Yesu atumie lugha kali kiasi kile tena kwa mwanamke anayekuja kwake kwa heshima na imani kubwa kiasi kile. Mwanamke ambaye tunaona mara tatu anamuita na kumtambua Yesu sio kama mtenda miujiza bali kama ‘’Bwana’’, anamtambua kuwa ni Masiha, kuwa ni Kristo, kuwa ni Mungu iweje basi Yesu atoe jibu lenye ukali wa maneno kiasi kile? Je, ndio kusema Yesu naye alikuwa na mtazamo kama wayahudi wengine wa nyakati zake, na kama sio bado swali linabaki kwa nini lugha ile ya kuona wapagani ni sawa na mbwa? Bado mwanamke yule mkananayo aliendelea kumjibu Yesu; ‘’Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao’’. Na hapo Yesu anamjibu nasi tunabaki na mshangao; ‘’Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile’’. Yesu hajawahi kutamka wazi wazi juu ya ukubwa wa imani kwa Myahudi yeyote yule ila kwa mwanamke huyu mgeni, mwanamke mpagani. Ni hapo sasa tunapata jibu la swali lile lililokuwa linatusumbua awali. Ilikuwa ni nia ya Yesu kuwaalika wanafunzi na wafuasi wake wenye asili ya Kiyahudi kubadili vichwa vyao, kubadili mitazamo yao ya kibinadamu na kuwa na kichwa kipya, kuvaa mtazamo wa Kimungu, Mungu ni wa wote na kamwe hana taifa wala kabila wala rangi.

Na ndio tunaona Kanisa la Kristo linabeba na kuvaa mantiki mpya ya Mungu kuwa wa watu wote bila ubaguzi wa aina yoyote ile. ‘’Kwa njia ya imani, nyinyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu kwa kuungana na Kristo. Nyinyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja kwa kuungana na Kristo Yesu. Ikiwa ninyi ni wa Kristo, basi ni uzao wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu’’ (Wagalatia 3:26-29). Ni kwa njia ya Kristo sisi sote tunafanyika wana wa Mungu, Taifa lake teule na la kifalme, wana wa Abrahamu. Ahadi zake zote zinatimia kwa wale wote wanaokubali na kumpokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wao. Kristo amekuja kuondoa kila aina ya matabaka na makundi mbele ya Mungu kwani ni kwake nasi tunafanyika warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu, yaani Kristo. Mwanamke mkananayo leo anasimama kama kielelezo cha mfuasi wa kweli wa Kristo, mfano wa sala na jinsi gani tunapaswa kuhusiana na Mungu. Leo tunaishi katika ulimwengu kwenye mtanzuko mkubwa juu ya maana ya sala.

Sala ni kitendo cha imani; ni kilio na makelele kwa wengine; ni kupoteza muda kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu. Imekuwa hivyo kwani wengi tunafikiri tunasali ili Mungu atende tutakavyo sisi na sio ili mapenzi yake yatimizwe katika maisha yetu na hatuna budi kutambua kuwa mapenzi ya Mungu kwetu daima ni mema, hivyo tubaki na imani na matumaini katika sala zetu. Sala zaidi ya kuwa kitendo cha imani, ni kitendo pia cha matumaini na upendo kwa Mungu. Ni katika sala tunakutana na Mungu na kamwe hatupaswi kupoteza mwelekeo kwa kusikiliza wengine wanasema nini juu yetu bali tuongozwe na imani ya kweli kwa Mungu aliye wema na upendo wote. Sala ni kitendo cha imani, na kamwe tusiingie katika sala tukidhani Mwenyezi Mungu atatujibu kwa kuwa ni mastahili na haki yetu. Kusali ni kukubali upendo na wema wa Mungu kwetu na kamwe sio mastahili au haki yetu. Mwanamke Mkananayo hakujiona kuwa mwenye mastahili wala mwenye haki bali alibaki mwenye imani na matumaini makubwa kwa wema na upendo wa Mungu. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

14 August 2020, 13:41