Tafuta

Hija ya Kitaifa ya 25 nchini Burikna faso katika madhabahu ya Mama Yetu wa Yagma . Hija ya Kitaifa ya 25 nchini Burikna faso katika madhabahu ya Mama Yetu wa Yagma . 

Burkina Faso:Hija ya 25 huko Yagma:nchi inataka kujipatanisha,haki na amani!

Tarehe 15 Agosti 2020 nchini Burkina Faso imefanyika hija ya kitaifa ya 25 katika Madhabahu ya Bikira Maria Mama Yetu wa Yagma.Katika fursa hiyo Kardinali Ouédraogo amesema nchi inataka mapatano,haki na amani na kumwomba Mungu awaepushe na matatizo mengi katika nchi hiyo hasa ya mashambulizi kutoka kwa magaidi.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Pamoja na Mama wa Yagma,tushangwere na kutangaza maajabu ya Mungu, ndiyo ilikuwa kauli mbiu iliyoongoza maandamano ya siku ya Jumosi tarehe 15 Agosti 2020 nchini Burkina Faso kwa kufanya hija ya kiutamaduni ya 25 katika Madhabahu ya Bikira Maria Mama Yetu wa Yagma. Siku ya hiyo ni sikukuu kubwa kwa Mama Kanisa kuadhimisha Siku Kuu ya Kupalizwa mbinguni kwake Bikira Maria,  Mwili na Roho yake. Lakini Kanisa la Burkina Faso katika siku hiyo ilichaguliwa kama ishara muhimu ya hija ya kitaifa ambapo hata mwaka huu wamekuwa na fursa ya kujumuika na kusali kwa pamoja.

Nchi inatafuta maridhiano, haki na amani

Mwaka huu tukio hili limekuwa lenye maana kwa namna ya pekee ikiwa ni hija ya 25 tangu kuanza kwake na kwa maana hiyo ni Yubilei ya shaba! Katika fursa hiyo, Kardinali Philippe Ouédraogo, Askofu Mkuu wa Ouagadougou nchini Burkina Faso aliongoza Misa Takatifu na katika mahubiri yake ameinua sala za kumshukuru Mungu na kuwaalika waamini wakati huo huo wamwombe “Bwana kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu ili alinde Nchi ambayo imo katika harakati za kutafuta mapatano, haki na amani. “Mungu atuokoe na ukosefu wa usalama na mashambulizi ya magaidi,  Kardinali Ouédraogo, ameongeza maombi yake ili kuokolewa na janga la virusi vya Corona na kuwajalia zawadi ya uchaguzi mkuu wa urais na viongozi tawala wa serikali  wapenda amani, wanaoaminika na wanaokubalika kwa watu wote ulimwenguni. Kuhusiana na uchaguzi wa rais na viongozi unatarajiwa kufanyika tarehe 22 Novemba mwaka huu.

Udhaifu kibinadamu umefunuliwa na covid-19

Kwa mujibu wa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Ouagadougou, Askofu Léopold Médard Ouédraogo, amesisitiza jinsi janga la Covid-19 lilivyo funua udhaifu wa ubinadamu licha  ya kuwa na idadi kubwa ya uvumbuzi wa kisayansi uliofikiwa na mahitaji,  kwa maana hiyo amesisitiza kwamba  waamini hawana budi kumwelekea Bikira Maria. Hata hivyo hija hiyo imekuawa na jambo jingine muhimu hasa la kukabidhiana kati ya Msimamizi wa Madhabahu hiyo Padre Narcisse Guigma, kwa mfuasi wake , Padre Jules Pascal Zabré.  Kwa ishara ya kwanza ilikuwa ni kukabidhi ramani ya Madhabahu na pia chombo kinachotunza funguo za eneo hilo la ibada na sala.

Madhabahu ilijengwa kwa imani na nguvu ya waamini

Madhabahu hiyo ilijengwa kwa imani na matendo ya dhati ya waamni amekumbusha Padre Gigma. Chini ya usumamizi wake, kiukweli eneo la Maria limeonesha ukamilisho kabisa wa ujenzi wa Kanisa Kuu dogo na kuanzisha ujenzi wa ukuta wa kuzunguka  madhabahu yote na nyumba ya mahujaji. Kwa upande wa msimamizi mpya wa madhabahu, Padre Zabré amebainisha kuwa yuko tayari kujikita katika huduma kwa sababu kuhani kila mahali aendapo anaitwa kuhudumia. Hija hiyo ilihitimishwa kwa maandamano na kupanda mti mahali ambapo wanatarajia  kujenga kikanisa wakati  ujao kwa ajili ya nyumba ya hija.

Jiwe la msingi liliwekwa mwaka 1978

Madhabahu ya Mama Yetu wa Yagma inapatikana katika kilima ambapo walijenga kwa mfano wa Groto ya Lourdes. Jiwe la kwanza la msingi liliwewa kunako mwaka 1978. Mwanzoni mwa kazi ya ujenzi wa Kanisa hilo ulibarikiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa ziara yake ya pili ya Kichungaji kunako mwaka 1990 na kuweka tarehe mwaka 1991,  wakati kunako 1998, Baraza la Maaskofu nchini humo walitangaza Yagma kuwa kituo cha hija kitaifa.

Asilimia 85 ya gharama za ujenzi ni kutoka kwa waamini

Madhabahu hiyo imejengwa kwa karibu miaka 22 na kugharimu milioni za kifranki za Uswiss na limesaidiwa kwa karibia asilimia 85 na waamini mahalia. Ndani ya Kanisa kuna nafasi za kukaa watu 2,000. Tarehe 15 Agosti 2013 madhabahu hiyo ilipewa heshima ya kuwa Kanisa Kuu dogo. Na ni vema kukumbuka kwamba tarehe 2 Februari mwaka huu nchini Burkina Faso imewekwa wakfu katika Moyo safi wa Bikira Maria, Mama Yetu wa Yagma.

18 August 2020, 13:59