Tafuta

Vatican News
Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda Tanzania "ametia nia" kuimarisha ari, mwamko na ushirikiano wa kimisionari kati ya Jimbo la Mpanda na Jimbo kuu la Dar es Salaam. Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda Tanzania "ametia nia" kuimarisha ari, mwamko na ushirikiano wa kimisionari kati ya Jimbo la Mpanda na Jimbo kuu la Dar es Salaam. 

Askofu Eusebius Nzigilwa Atia Nia ya Kimisionari Jimbo la Mpanda

Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa katika salam zake za shukrani kwa Mwenyezi Mungu na familia ya watu wa Mungu nchini Tanzania katika ujumla wake, ameonesha kwamba, kipaumbele chake cha kwanza Jimboni Mpanda ni kuendelea kupyaisha wongofu, ari na mwamko wa kimisionari, kwa kutumia uzoefu na mang’amuzi yake ya shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Dar Es Salaam! Umisionari

Na Padre Agapito Mhando na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Tanzania, amesimikwa rasmi Jumapili tarehe 2 Agosti 2020 katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora na mahubiri kutolewa na Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Ibada hii ya Misa Takatifu ilitanguliwa na Masifu ya Jioni yaliyoongozwa na Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Pamoja na nia mbali mbali zilizokuwepo, lakini kama familia ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda, limetoa Ibada ya Misa hii kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mzee Benjamin William Mkapa. Katika sherehe hizi, Rais John Pombe Magufuli amewakilishwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Mizengo Kayanza Peter Pinda.

Hii ni sehemu ya mahojiano maalum kati ya Radio Vatican na Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Anasema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linatumwa na Mwenyezi Mungu, ili liwe ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Na kwa kudaiwa na wajibu wa ndani wa ukatoliki wake na kwa kulitii agizo la Kristo Yesu, linajibidisha kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wote, huku wakifuata mifano ya Mitume ambao Kanisa limejengwa juu yao, hali wakifuata nyayo za Kristo Yesu walihubiri Neno la kweli na kuanzisha Makanisa. Kumbe, waandamizi wao wanawajibika kuendeleza kazi hii, ili kweli Neno la Mungu liendelee kutukuzwa na Ufalme wa Mungu kutangazwa na kusimikwa duniani kote!

Kumbe, Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa katika salam zake za shukrani kwa Mwenyezi Mungu na familia ya watu wa Mungu nchini Tanzania katika ujumla wake, ameonesha kwamba, kipaumbele chake cha kwanza Jimboni Mpanda ni kuendelea kupyaisha wongofu, ari na mwamko wa kimisionari, kwa kutumia uzoefu na mang’amuzi yake ya shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Angependa kuona umoja na mshikamano wa kimisionari kati ya Jimbo Katoliki la Mpanda na Jimbo kuu la Dar Es Salaam vinaimarishwa kwa njia ya: Utoto Mtakatifu ambao kimsingi ni chachu ya uinjilishaji ndani ya familia na kati ya watoto wenzao. Ushirikiano wa kwaya ili kuweza kusaidia mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji. Mtakatifu Augustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa alikuwa anasema, kuimba ni kusali mara mbili.

Ushirikiano huu wa kimisionari unapania kuwahusisha pia WAWATA yaani Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam. WAWATA wamekuwa mstari wa mbele katika kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali, kwa njia ya uwepo na ushiriki wao mkamilifu. Ushirikiano huu wa kimisionari unalenga pia kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano mazuri yaliyojengeka kati ya Askofu Nzigilwa na Wakleri wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa takribani miaka 25 iliyopita. Lengo ni kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kujikita katika wongofu wa shughuli za kimisionari, kwani Wakristo wote wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Mpanda ni sehemu ya Jimbo kuu la Tabora. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora katika utangulizi wa Ibada ya kumsimika Askofu Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda amegusia historia nzima ya uinjilishaji katika eneo hili, dhamana na utume uliotekelezwa na Wamisionari wa Afrika, “White Fathers”. Walipata changamoto kubwa ya kimisionari walipotaka kwenda kuinjilisha nchini Rwanda. Wakati ule, Ujiji, Kigoma, ilikuwa ni kitovu cha biashara. Tabora yalikuwa ni Makao makuu Mtemi Mirambo wa Unyanyembe, Tabora na dini ya Kiislam ilikuwa imeshamiri sana katika eneo hili. Kunako mwaka 1886, Kalema ikawa ni kimbilio la Wamisionari wa Afrika na kujenga ngome yao mahali hapa. Eneo la Kalema likawa ni kitovu cha uinjilishaji maeneo ya Sumbawanga, Mbeya na Rukwa kwa wakati huu. Eneo hili limehudumiwa na Maaskofu 12 na kwa sasa Askofu Eusebius Afred Nzigilwa anakuwa ni Askofu wa tatu kuongoza Jimbo Katoliki la Mpanda. Waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, wameonesha shauku ya kufanya hija ya kiroho, ili kuweza kujifunza mengi zaidi kuhusiana na eneo la Kalema.

Kwa upande wake, Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma ambaye ametoa mahubiri katika Ibada hii, amekazia, umuhimu wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda kumpokea Askofu Nzigilwa kama zawadi maalum kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Zawadi hii ni jibu la sala ambayo wamekuwa wakimwomba Mwenyezi Mungu tangu tarehe 21 Desemba 2018, Mwenyezi Mungu alipoingilia mipango yao, kwa Baba Mtakatifu Francisko kumteuwa Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo Katoliki la Mpanda wakati huo, kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya. Katika sala yao, watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda, wamemwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwapatia mchungaji: mnyenyekevu na mpole wa moyo atakaye wafundisha, waongoza na kuwatakatifuza. Mwenyezi Mungu amejibu ombi lao na kuwazawadia Askofu Eusebius Afred Nzigilwa ambaye katika nembo yake ya kiaskofu anaongozwa na kauli mbiu: Unyenyekevu na Upendo.

Ili Jimbo Katoliki la Mpanda liweze kupata tija, ustawi na maendeleo fungamani kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, tunu zinazosimikwa katika misingi ya imani, matumaini na mapendo. Askofu Joseph Roman Mlola amwosia Askofu Nzigilwa, apende kudumisha utamaduni wa sala, tafakari ya Neno la Mungu na Ibada mbali mbali, kwa kutambua kwamba, Uaskofu ambao ni utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre ni huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hii ni huduma inayopaswa kutolewa na kupokelewa kwa moyo wa upendo na shukrani. Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye ndiye aliyehamishwa kutoka Jimbo Katoliki la Mpanda na kupelekwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya, amewapongeza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda kwa kumpata mchungaji mkuu. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linafahamu fika mateso na mahangaiko ya Jimbo ambalo halina mchungaji mkuu, ndiyo maana, wamekuwa bega kwa bega na watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda, ili kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwapatia mchungaji mwema na mnyenyekevu wa moyo!

Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Mizengo Kayanza Peter Pinda kwa niaba ya Rais Magufuli amelipongeza Kanisa kwa huduma makini katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya watanzania wengi tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji wa awali eneo la Kalema na matunda ya mchango huu yanaendelea kuonekana bayana. Kanisa limechangia pia amani, utulivu na maridhiano kati ya watanzania wote kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli Tanzania iweze kuwa “Kisiwa cha Amani, Ustawi na Maendeleo ya wengi”. Kanisa limesaidia sana katika malezi na makuzi ya watu kwa kujikita zaidi si tu katika imani, bali hata katika misingi ya maadili na utu wema. Kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imekwisha kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa reli na bandari, reli kutoka Kaliua mpaka Kalema pamoja na bandari yake ili hatimaye ujenzi reli na bandari uweze kusaidia kuhudumia mizigo mingi kutoka Kalema na kutoka DRC.

Kumbe, wananchi wa Mpanda ni walengwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano. Hapa anasema Mzee Mizengo Kayanza Peter Pinda kuna umuhimu kwa wananchi kuwa na moyo wa shukrani kwa hatua mbali mbali za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali. Radio Vatican inapenda kumtakia heri na baraka Askofu Nzigilwa anapoanza kuandika historia ya maisha na utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda.  Tunapenda kumshukuru sana Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa sadaka na majitoleo yake, yaliyofanikisha mahojiano haya maalum kwa njia ya simu!

Bp Nzigilwa
03 August 2020, 13:29