Tafuta

Vatican News
Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Bukoba asema, Padre ni zawadi ya Mungu kwa ajili ya watu wake! Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Bukoba asema, Padre ni zawadi ya Mungu kwa ajili ya watu wake!  (AFP or licensors)

Askofu Desiderius Rwoma: Padre Ni Zawadi kwa Watu wa Mungu!

Padre ni rafiki ya Mungu na watu. Ni mhudumu wa Sakramenti za Kanisa. Padre afahamike jinsi anavyoishi: Awe ni mtu wa sala na msikivu wa Neno la Mungu na mwajibikaji. Padre mzuri ni yule anayejitahidi kuyaishi kikamilifu yale anayofundisha na kuwashauri wengine wafanye. Padre ni chombo cha ukombozi wa dunia na chemchemi ya haki, amani na upendo wa Kimungu kwa watu!

Na Padre Deogratias Makuri, Singida,

Jimbo Katoliki la Singida tarehe 8 Agosti 2020 limezawadiwa zawadi ya Padre Higinius Daghoo, katika Parokia ya Ilongero. Upadrisho huo ambao ulifanyika katika Parokia ya Ilongero unafungua mlango kwa mashemasi wanaotarajiwa kupadirishwa mwaka huu wa 2020. Katika mahubiri yake yalijikita katika thamani ya Ekaristi na Padre ambapo Baba Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba alisisitiza muungano wa Kristo na sisi kwa sisi katika Ekaristi Takatifu uwe ni alama ya zawadi ya Mungu kwa binadamu. Baba Askofu Rwoma ambaye aliongoza maadhimisho hayo alisisitiza maana ya Upadre kuwa ni zawadi ya Mungu ambayo kwayo kijana “hutwaliwa katika wanadamu na kuwekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu (Ebr. 5:1) Askofu Rwoma alitaja wajibu wa Kiekaristi wa Padre kuwa ni pamoja na kutoa matoleo na dhabihu, kujitakasa, kutafakari kwa kina na kuamini maneno ya kiekaristi yanayotumika wakati wa mageuzo, kuwa mnyenyekevu katika maadhimisho ya Kiekaristi. Padre anaingia katika mahusiano ya mafumbo matakatifu na Muungano wa kipekee na Kristo Yesu aliyempatanishi na Mungu, kuunganisha mateso yake sanjari na mateso ya Kristo katika utume wake, kukaa huku akiwa ameunganika na Kristo na kupenda kusali na kuabudu Ekaristi Takatifu.

Askofu Rwoma aliwaasa mapadre kuwa kuna mazingira ambayo Mapadre hutoa huduma zao za kitume lakini hazitambuliki, hata hivyo wanaendelea kuitoa pasipo kuchoka. Lakini upendo wao kwa watu wote bila kujali dini wala kabila unaonekana wazi. Tusemeje tena juu ya uaminifu wa kijasiri kabisa ambao Mapadri wengi wanauonesha katika wito wao, licha ya matatizo mengi na pengine kutoeleweka vizuri na watu wanao wahudumia? Licha ya matatizo na changamoto zote hizo, Mapadri wengi wanaendelea kuwa waaminifu kwa maisha na wito wao wa kuwa “Marafiki” wa Kristo “aliyewaona, akawaita na kwa namna ya pekee, wakachaguliwa, na kutumwa. Ni matumaini ya Askofu kwamba wengi wao wana kumbukumbu nzuri ya Mapadri wao, waliowabatiza, waliowafundisha kwa maneno na mifano yao mizuri ya kujitoa bila ubinafsi na wengine hata kutoa uhai wao kwa ajili ya huduma yao ya kipadri.

Askofu Rwoma aliendelea kuasa akisema, “Katika nyakati zetu hizi, lazima itambulike kuwa Padre ni rafiki ya Mungu na rafiki ya watu, Padre ni Sakramenti ya Upatanisho, Padre afahamike jinsi anavyoishi maisha yake, Padre awe mtu wa sala na msikivu wa Neno la Mungu, Padre awe mwajibikaji, Padre mzuri ni yule anayejitahidi kuyaishi kikamilifu yale anayofundisha na kuwashauri wengine wafanye, Padre ni mtumishi wa Mungu na watu, Padre ni chombo cha ukombozi wa dunia, Padre ni chemchemi ya haki na upendo wa Kimungu. Padre anapaswa kuwa mkarimu kwa watu wote, Padre awe kipenzi cha Mungu na watu. Padre ni chombo kitakatifu cha Yesu, Padre asemehe yote na apokee yote, Padre akubali kukosolewa na awe wazi, Padre ni mganga wa maisha ya roho, Padre awe kimbilio la maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Padre awe shujaa na mwenye busara, Padre aishi kati ya watu kwa ajili ya watu katika mambo matakatifu Padre awe mpenda haki kwa watu wote.”

Padre ni chombo cha haki, amani na mwalimu wa sala na maisha matakatifu. Padre asiwe na chuki na watu, bali awe ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu! Askofu Rwoma alitaja baadhi ya majukumu ya Padre kuwa ni pamoja na kuwa mhudumu wa dhabihu, Mhudumu wa Neno, Sakramenti za wokovu, mwombezi na mlezi wa Taifa la Mungu, mweka wakfu taifa la Mungu na zaidi ni mtetezi wa taifa la Mungu. Askofu Rwoma alimalizia kwa kumuasa Padre mpya kuwa “ukitaka kuwa na amani na furaha na upadre wako, fanya yafuatayo: thamini na penda wito wako, kuwa na muungano na Askofu.  Usifanye jambo kubwa bila kumshirikisha Askofu wako, kuwa na muungano na mapadre wenzako na daima sali kwa bidii sala za Kanisa na hasa sala maalum za kipadre.

Naye Askofu Edward Mapunda wa Jimbo la Singida, aliyeshiriki Ibada hiyo ya Misa Takatifu alimshukuru kwa dhati Askofu Rwoma kwa kukubali kuja kuadhimisha Misa hii na kukubali kumpa Daraja ya Upadre, shemasi Higinius Daghoo aliyekuwa mlezi wake tangu awali. Padre Higinius amepangiwa kuanza utume wake katika Seminari Ndogo ya Msingi ya Mtakatifu Wiliam, Diaghwa kama Baba wa kiroho, mlezi na mwalimu. Tunamtakia mwanzo mwema na mafanikio mema katika utume wake huu mpya.

Upadrisho Singida

 

14 August 2020, 08:35