Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XIV ya Mwaka A wa Kanisa: Sala ya Yesu inasimikwa katika unyenyekevu wa moyo! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XIV ya Mwaka A wa Kanisa: Sala ya Yesu inasimikwa katika unyenyekevu wa moyo! 

Tafakari Jumapili 14 ya Mwaka: Sala: Unyenyekevu wa Moyo!

Sala hii ya Yesu ni ya shukrani na sifa kwa Mungu Baba si tu ni ya kipekee bali inabeba ujumbe mkubwa kitaalimungu. Ili kuelewa vema sehemu ya sala hii na hivyo kuweza kutafakari kwa kina yafaa pia kufahamu mazingira yaliyotangulia kabla ya sala hii ya shukrani ya Yesu mwenyewe. Aya zinazotangulia sehemu hii ya Injili ya leo, tunaona Yesu anakataliwa katika miji ile tajiri, miji ya kibiashara.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Somo la Injili ya leo ni Sala ya Yesu akimshukuru Mungu, na ni sala pekee ya Yesu tunayokutana nayo katika Injili zile pacha, kwani Sala ya ‘’Baba Yetu’’, ni sala ambayo Yesu anatufundisha sisi wanafunzi wake kusali. Pia mara kadhaa japo hatuambiwi sana aina ya sala tunakutana na Yesu akisali, mfano alipokuwa Getsemani na pale juu Msalabani alimwita Mungu Baba na kumlilia, ingawa Wainjili wanatupa kwa ufupi sana sala hizo za Yesu. Sala hii ya shukrani na sifa kwa Mungu Baba si tu ni ya kipekee bali inabeba ujumbe mkubwa kitaalimungu. Ili kuelewa vema sehemu ya sala hii na hivyo kuweza kutafakari kwa kina yafaa pia kufahamu mazingira yaliyotangulia kabla ya sala hii ya shukrani ya Yesu mwenyewe. Aya zinazotangulia sehemu hii ya Injili ya leo, tunaona Yesu anakataliwa katika miji ile tajiri, miji ya kibiashara miji ya ufukweni ya ziwa lile Galilaya: Korazini, Betsaida na hata Kafarnaumu, miji iliyokataa Neno na hata miujiza aliyoifanya katikati yao.

Sura hii inaanza na mashaka makubwa hata kutoka upande wa Yohane Mbatizaji. Yohane baada ya kusikia anayoyatenda Yesu, naye anakwazika na kujawa na mashaka juu ya Yesu na hivyo anatuma baadhi ya wafuasi wake kwenda na kumuuliza Yesu: ‘’Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?’’ (Mt 11:3). Yesu anaonesha jinsi ilivyo ngumu kwa kizazi kile kubadili vichwa vyao na kukutana na sura halisi ya Mungu kupitia Yeye, aliye Mwana pekee wa Mungu. Mashaka yalikuwepo si tu kwa watu wa kawaida bali hata kwa mtangulizi wake, Yohane Mbatizaji. Yesu si tu anakataliwa na watu wa kawaida bali na hata wale waliojitambulisha kuwa ni wenye akili na hekima, wale wanaoamini kuijua vema Sheria ya Musa, wanaijua katika ukamilifu wake na hivyo ni wao waliojiona kuwa na wajibu wa kuwafundisha wengine kuishika Sheria ya Musa. Nabii Isaya 5:20-21 anaonya: ‘’Ole wao wanaojiona kuwa wenye hekima ambao wanajiona kuwa wenye akili’’.

Yesu si kwamba anawatenga hao wenye akili na hekima katika ufalme wake, bali leo anatutaka sote kubadili vichwa vyetu, na kuwa watoto wachanga, wanyenyekevu, wapole, maskini, watu wanaokuwa wa mwisho kabisa kadiri ya vipimo vya ulimwengu huu. Wale wanaokuwa tayari kumpokea Yesu na Neno lake ndio wanaotambulishwa leo kama ‘’watoto wachanga’’, ndio wale wanaotambua udogo wao na hivyo kujitegemeza katika huruma na upendo wa Mungu. Yesu anamshukuru Mungu kuwafunulia siri za mbinguni watoto wachanga, hasemi wajinga au wasiokuwa na uelewa bali wale wanaokuwa na moyo kama wa watoto wachanga. Hivyo, yafaa tukumbuke kujua siri za mbinguni na kuzipokea haimaniishi kuwa sisi tu wajinga, tusiokuwa na akili au ufahamu bali tunaokuwa na kubaki watoto wachanga mbele ya Mungu.

Yesu leo anamshukuru Mungu kwa sababu ya hawa watoto wachanga, kwa Kigiriki ni ‘’nèpioi’’, wanaojaliwa na kufunuliwa siri za mbinguni. Zaburi 131 ‘’Ee Mwenyezi Mungu, sina moyo wa kiburi…ila nafsi yangu imetulia na kuwa na amani, kama mtoto mchanga alivyotulia na mama yake, ndivyo nafsi yangu ilivyo tulivu’’. Mtoto mchanga hapa isieleweke kumaanisha unyonge na uduni tu bali hali ya kutumaini na kujikabidhi kwa imani kubwa kama vile mtoto mchanga mikononi mwa mama yake. Mtoto mchanga ndio yule anayejitegemeza tena kwa imani kuu mikononi mwa baba yake na mama yake, anayejifunza kila kitu kwa utii mkubwa kutoka kwao. Ni ile hali ya kujiona hawezi lolote bila baba au mama yake. Na ndio tunaona Yesu anatualika wanafunzi wake ili kuurithi ufalme wa mbinguni hatuna budi kuwa kama watoto wadogo (Mathayo 18:3).

Watoto wachanga pia katika Maandiko Matakatifu wanatambulishwa kama ‘’maskini’’. Maskini ndio wale wanaoweka pia tumaini lao na nguvu yao katika Mungu pekee. Ndio wale ambao wanaipokea Habari Njema ya wokovu (Mathayo 11:5 na 5:3). Mfuasi wa kweli ndio yule anayemtegemea Mungu katika kila hali, anayeweka kando majivuno yake, ubinafsi wake, kujikweza kwani anatambua udogo na uduni wake mbele ya Mungu. Anayekuwa tayari kusikia Neno na kuliweka katika maisha yake, anayeruhusu kuongozwa na Mungu mwenyewe kupitia Neno lake. Katika nyakati za Yesu, mtoto mchanga hakuwa anahesabiwa kama mwanadamu kamili kisheria, alieonekana kama sawa na kitu tu, na Yesu leo tunaona anawaalika wasikilizaji wake kubadili mitazamo yao, wabadili vichwa vyao ndio namna zao za kufikiri na kuenenda. Anayekuwa mdogo kama mtoto mchanga, huyo Yesu anatuambia ndiye anayekuwa mkubwa (Mathayo 18:4).

Ni kwa kuwa watoto wadogo hapo tutaweza kumjua Mungu kuwa ni Baba yetu, na kumuita ‘’Abbà’’. Ni yule tu mwenye moyo na mtazamo kama watoto wachanga anaweza kumjua Mungu kuwa ni Baba yetu.  Ni kishawishi cha wengi wetu hata leo kuwa Mungu ni rafiki ya watu wema na wenye haki, wenye kutenda yaliyo mema na kuwavumilia tu waovu na wadhambi. Huyu ni Mungu wa wenye hekima na akili, Mungu anayekidhi na kuingia katika mantiki na vigezo vyao vya kibinadamu. Cha kushangaza, Baba wa Yesu kinyume chake anawapokea mikononi mwake na kuwakumbatia wale ambao sisi tunawatupa jalalani, wale waliodharauliwa, wasiojaliwa na mtu yeyote, wadhambi na watoza ushuru (Mathayo 11:19), makahaba (Mathayo 21:31), kwa sababu ni hawa wenye uhitaji mkubwa wa huruma na upendo wake wa Kimungu.

Matajiri, walioshiba na kutosheka, wenye hekima na akili, hawa wanajiona wana kila kitu, hivyo hawana uhitaji wa Mungu mwenye huruma na upendo na badala yake wanakuwa na picha potofu ya Mungu. Hata nao wanaalikwa leo kubadili vichwa na kuwa na mtazamo mpya, wa kukubali kuwa watoto wachanga na maskini. Sehemu ya pili ya Injili ya leo: ‘’…wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia’’. Kitenzi ‘’kujua’’ katika ulimwengu wa kiyahudi hakimaanishi kufahamu mara baada ya kukutana naye mara kadhaa au mara nyingi bali ni kuonesha mahusiano ya ndani kabisa, kitenzi hicho pia kinatumika kuonesha mahusiano ya wanandoa kati ya mume na mke, ni mahusiano yanayojengeka katika upendo wa kweli, upendo wa kujitoa sadaka kwa ajili ya mwingine.

Musa pamoja na kutaka kuuona uso wa Mungu anaishia kukumbushwa kuwa: ‘’Lakini hutaweza kuniona uso maana hakuna mwanadamu yeyote atakayeniona na kuishi’’ (Kutoka 33:20). Ni Yesu pekee anayemjua Mungu Baba, anayekuja ili kutufunulia uso wa Mungu katika ukamilifu wake. Ndio uso wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote, kwa watu wanaokubali kuwa watoto wachanga mbele yake. Hivyo anayemjua Mungu Baba kikamilifu ni Mwana, kwani ni umoja na Mungu Baba, ni Baba ndani ya Mwana na Mwana ndani ya Baba katika ukamilifu wake, na ni muungano wa hizi nafsi mbili za Mungu, wanaunganishwa na ule upendo wa Kimungu ndio Roho Mtakatifu, ndiyo pumzi ya upendo itokayo kwa Baba na Mwana. Ila nasi kwa kukubali kufanyika watoto wachanga tunaweza kuingia katika mahusiano ya kumjua Mungu, kumtambua kama ‘’Abbà’’. Waandishi, marabi, waliamini kuwa wao kwa kuijua vema Sheria ya Musa basi pia walimjua Mungu. Walijiona wao wanaijua Sheria na hivyo kuwa walimu wa wengine, kwani wao ni wenye hekima na akili.

Sehemu ya tatu ya Injili yetu ya leo (Aya 28-30), inaonesha jinsi walio wadogo, watu wa kawaida, maskini wanavyopata mateso kutoka kwa wenye hekima na akili. Ni hawa wenye hekima na akili yaani, waandishi na mafarisayo na wakuu wa makuhani waliojiona kuwa na uwezo wa kuitafsiri na kuwafundisha wengine nini cha kushika na kutenda na nini cha kuepuka mintarafu Sheria ya Musa. Ni wao walioifanya dini ile ya kiyahudi kuwa mzigo mzito usiobebeka kirahisi. (Luka 11:46) ‘’…Na ninyi waalimu wa sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku ninyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia(kuigusa?)’’. Ndio dini ya sheria na masharti mazito na magumu, dini inayokuwa mzigo kwa wengi wetu, ni dini inayotisha na kuogofya kwa uwingi wa sheria na masharti. Ni dini inayopoteza ladha ya kuwa Habari Njema!

Sheria ya Mungu inakuwa mzigo mzito usiobebeka kirahisi kama tunavyoona kutoka Kitabu cha Hekima ya Sira 6:24-28 ‘’Tia pingu za hekima miguuni mwako, na ukosi wake shingoni mwako…’’ Ni katika muktadha huu dini ile ikageuka kuwa mzigo kwa wengi na hivyo kuwakatisha tamaa wadogo na maskini, watu wa maisha ya kawaida. Si tu watu wa kawaida walianza kujiona mbali na dini ile bali mbaya zaidi walijiona wapo mbali na Mungu. Waliishia kujiona ni watu walio mbali na ufalme wa Mungu, kwa wingi na ukali wa Sheria ya Mungu. Ni kwa hawa waliojiona wapo mbali si tu na dini yao bali pia na Mungu ambao Yesu leo anawageukia na kuwatia moyo, kuwapa tena matumaini. Yesu anawaalika hawa wanaosumbuka na kulemewa na mizigo mizito ya sheria, wanaosumbuka kwa kukataliwa na kutengwa na dini yao. Sheria anayowapa Yesu sio tena utitiri wa sheria bali ni moja na inayokuwa laini, si nyingine bali ndio ile ya Upendo. Ni kwa kuishika amri hii mpya ya upendo tunajikuta kuwa karibu na Mungu na jirani.

Nira katika Agano la Kale ilikuwa ni ishara ya Sheria ya Musa na makandokando yake yote au mahitaji ya sheria hiyo. Si kwamba amri mpya inatuacha bila wajibu mkubwa na mgumu bali Yesu anaitambulisha kuwa laini. Nira ya upendo, upendo unaoakisi pia asili yetu kama wanadamu kwani tumeumbwa kupenda na kupendwa, ni sheria isiyotoka nje yetu bali ipo ndani mwetu. Nira yake ni laini, kwani Yesu hatuamrishi kuishika bali Yeye mwenyewe anakuwa wa kwanza kuishika. Ndio asili ya Mungu mwenyewe kwani Mungu ni upendo kadiri ya Mwinjili Yohana. Yeye anakuwa wa kwanza kutuonesha kumpenda Mungu na jirani. Ni Yeye anayekubali kumwilika ili atukomboe sisi, ila kwa nafasi ya kwanza kutumiza mapenzi ya Baba yake. Kumwilika kwa Yesu ndio kusema kunaonesha upendo wake kwa Mungu Baba na kwetu sisi tunapokubali kufanyika watoto wachanga. ‘’…mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo’’. Kujifunza kwake ndio kusema kuacha kuwafuata wenye hekima na akili, wale wanaojitegemea wenyewe badala ya kumtumaini Mungu na kumsikiliza na kulishika Neno lake, wale wanaomuhubiri Mungu anayekuwa mbali na wadogo na wanyonge, hasa wadhambi na walio wa mwisho.

Mpole na mnyenyekevu wa moyo, upole na unyenyekevu unaozungumziwa hapo sio ujinga, bali ni kuwa tayari hata kuteseka bila kulipa uovu kwa uovu, bali kupenda katika hali zote hata nyakati zile tunapokuwa na hakika ya kupokea madhulumu na mateso. Kujifunza kutoka kwa Yesu mwenyewe aliyekubali kuteseka na hata kufa bila kulipa ovu kwa ovu bali kwa huruma na upendo. Yesu anatualika leo kutambua kuwa Yeye yupo upande wa walio wadogo, walio wanyonge na duni, walio wa mwisho na kutengwa katika ulimwengu huu. Yafaa leo katika tafakari yetu kujiuliza ikiwa kama tuna uso wa Mungu kama ule wa marabi na mafarisayo au ile anayotufunulia Yesu mwenyewe. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

04 July 2020, 07:26