Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ufalme wa Mungu ni Wokovu ambao Mwenyezi Mungu amewaandalia watu wote! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ufalme wa Mungu ni Wokovu ambao Mwenyezi Mungu amewaandalia watu wote! 

Tafakari Jumapili 17 ya Mwaka A: Ufalme wa Mungu: Wokovu wa Wote

Yesu anaonesha kuwa ufalme wa Mungu ni kitu chenye thamani kubwa kama ardhi iliyo na madini ambapo mtu akigundua anakwenda kuuza vyote alivyonavyo ili ainunue ardhi hiyo. Kumbe, kuushughulikia ufalme wa Mungu ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele kwa sababu ya thamani yake kwa wokovu wa mtu. Ni mwaliko wa kutumia rasilmali zake kuupata ufalme wa Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 17 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (2Fal 3:5, 7-12) ni kutoka Kitabu cha Pili cha Wafalme. Somo hili linalotoa chimbuko la mfalme Solomoni kuwekwa kama mfano wa mtu mwenye hekima kupita wote katika Israeli. Kama vile ambavyo mapokeo yamemuweka mfalme Daudi kama mtunzi wa Zaburi vivyo hivyo mfalme Sulemani anawekwa kama mtu mwenye busara na mtoaji wa mafundisho na maamuzi ya hekima katika Israeli. Chimbuko hilo sasa linalotolewa na somo la leo ni kuwa Mungu mwenyewe alimtokea Sulemani katika ndoto na kumtaka aombe chochote kile anachotaka na Mungu angemjalia. Sulemani ambaye ni kwa kipindi kifupi tu, alikuwa ameurithi ufalme kutoka kwa baba yake Daudi alijiona bado hatoshi kulingana na kile ambacho Daudi alikuwa amekifanya katika Israeli.

Tutakumbuka kuwa Daudi alikuwa amefanikiwa kuinganisha Israeli kama taifa moja na alifanikiwa kabisa kuwashinda maadui waliokuwa wakiwazunguka na hivi kuifanya Israeli kuwa taifa lililo katika amani. Sulemani haombi kitu kingine chochote isipokuwa hekima itakayomsaidia katika utendaji wake. Mungu anapendezwa sana na ombi hilo la Sulemani. Yeye mwenyewe anamwambia Sulemani “hukuomba miaka mingi ya kuishi, wala hukuomba utajiri wa mali wala kuangamiziwa adui zako bali umeomba hekima”. Mungu akamtamkia kuwa atampa hekima na hatakuwapo mwingine mwenye hekima kuliko yeye. Hivi ndivyo Maandiko Matakatifu yanavyoeleza chimbuko la Sulemani kuhusishwa na hekima. Hapohapo somo hili linaonesha kuwa hekima iliyo kuu na ipitayo hekima zote ni ile hekima inayotoka kwa Mungu. Hali kadhalika somo linatupatia nasi changamoto ya kujua ni nini tunachoweza kuomba kutoka kwa Mungu. Tunaoneshwa kuwa pamoja na kuomba kwa Mungu yale tunayoyahitaji katika maisha, tuinue mioyo kuomba pia mapaji ambayo yatatusaidia kuwasaidia wengine. Hekima aliyoiomba Sulemani si hasa kwa ajili yake bali ilikuwa kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Somo la pili (Rum 8: 28-30) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili Mtume Paulo anazungumzia juu ya mpango wa wokovu ambao Mungu alikuwa nao tangu awali. Anasema, tangu mwanzo Mungu aliwajua watu wake, akawachagua ili awafananishe na mwanae. Paulo anaendelea kuonesha pia kuwa hao ambao tangu mwanzo Mungu aliwachagua aliwaita,  na hao aliowaita aliwahesabia haki na hao aliowahiesabia haki akawatukuza.  Namna hii ya uandishi ambayo Mtume Paulo anaitumia hapa inalenga tu kuonesha kuwa wokovu ambao Paulo anawahubiria warumi umekwishaandaliwa tayari na Mungu mwenyewe. Na kuhusu wokovu huu, sio kwamba Mungu tayari amekwishateua watu ambao ni lazima waokolewe na wengine ambao ni lazima waangamie hata kama wakifanya nini.  Kuna kipindi somo hili lilipata tafsiri hiyo kutoka kwa baadhi ya wahubiri kuwa Mungu amekwishapanga na kuchagua tangu mtu anapozaliwa kuwa huyu ni wa kwenda mbinguni na huyu ni wa kwenda motoni.

Tafsiri hii haiwezi kuendelea kupokelewa kwa sababu Mungu anakusudia watu wote waokolewe. Anachokifanya ni kumwacha mwanadamu atumie uhuru wake kuchagua kuokolewa ili wokovu usionekane kama ni kitu ambacho mtu amelazimishiwa au amepangiwa kama maji yanavyolazimika kupita kwenye bomba bali kama kitu ambacho mtu amestahili kwa uchaguzi wake huru. Maneno haya ya Mtakatifu Paulo yanaakisi maneno ya Zaburi 33:11 yanayosema “makusudi ya moyo wake ni ya vizazi na vizazi”. Ni makusudio ya wokovu ambapo wote kabisa bila kubagua Mungu amewajua, akawachagua, akawaita, akawahesabia haki na akawatukuza. Yeye Mungu amekwisha maliza upande wake wa kuwaandalia watu wokovu. Unabaki upande wetu wa kuupokea wokovu huo. Na huu ni mwaliko sasa wa kutumia vema uhuru ambao Mungu ametupa ili kuufikia wokovu huo.

Injili (Mt 13:44-52) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo.  Yesu anatoa mifano miwili kuelezea ufalme wa Mungu. Hii ambayo tunaiita mifano, kama ambavyo anaitumia Yesu, kimsingi ni hadithi au masimulizi ambayo Yesu anayatoa ili kwa kutumia lugha ya vitu ambavyo watu wanavifahamu awafanye wapige picha ya kile ambacho hawakifahamu. Kwa mfano leo anatumia masimulizi ya ununuzi wa kito chenye thamani na ya mvuvi wa samaki ili kutoa mfanano na ufame wa Mungu. Tunaona wazi katika mifano hiyo Yesu anaonesha kuwa ufalme wa Mungu ni kitu chenye thamani kubwa kama ardhi iliyo na madini ambapo mtu akigundua anakwenda kuuza vyote alivyonavyo ili ainunue ardhi hiyo. Na hii inawavuta wasikilizaji wake kuona kuwa kuushughulikia ufalme wa Mungu, kuutafuta ufalme wa Mungu ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele kwa sababu ya thamani yake kwa wokovu wa mtu.

Lakini pia mfano huu unatoa mwaliko wa mtu kutumia rasilmali zake alizonazo kuupata ufalme wa Mungu. Katika mfano wa pili Yesu anatoa picha nyingine ya ufalme wa Mungu. Picha hiyo ni kuwa kama mvuvi anavyokusanya samaki wazuri na wale wabaya katika wavu au kokoro kama linavyoitwa katika maeneo mengine, ndivyo hivyo ambavyo katika kuingia ufalme wa Mungu utafanyika uchaguzi kati ya watu wema na wale wasio wema. Wema watapewa nafasi ya kuingia na wale wasio wema watabaki nje ambapo Yesu anasema kutakuwa na kilio na kusaga meno. Hapa pia Yesu anatoa mwaliko wa kujibidiisha kuwa wema ili kustahili kuchaguliwa kuingia katika ufalme wa Mungu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News,  masomo ya leo yanailekeza tafakari yetu kuhusu ufalme wa Mungu. Neno hili Ufalme wa Mungu linajumuisha ndani yake vitu vingi. Leo ufalme wa Mungu unazungumziwa kama wokovu ambao Mungu amewatayarishia watu wake na ambao wote wanaitwa kuuingia kwa kufanya uchaguzi sahihi katika maisha. Ndiyo maana katika nafasi ya kwanza masomo yameonesha kazi aliyoifanya Mungu kuwaandalia wanadamu ufalme huo. Katika hili, Mtume Paulo ameeleza kuwa Mungu amewachagua, akawaita, akawahesabia haki na akawatukuza wale aliowajua. Hili tumelieleza katika ufafanuzi wa somo lenyewe kuwa halihusu kundi fulani teule bali ni mwaliko ulio wazi kwa wote.

Katika nafasi ya pili masomo yanatuonesha wajibu sasa ambao mwanadamu anaachiwa aufanye ili astahili kuuingia ufalme huo ambao Mungu ameuandaa. Ni uamuzi unaojijenga katika uhuru kamili wa mwanadamu. Hata hivyo uhuru huu pia unahitaji kusaidiwa na neema ya Mungu. Mfano wa Solomoni anayeomba Hekima kutoka kwa Mungu ni mwaliko wa mwanadamu kuendelea kuomba msaada wa Mungu katika kufikia mang’amuzi sahihi maishani hasa pale anaposongwa na kutingwa na yale yanayoonekana kuushinda uwezo wake. Makusudi ya moyo wake ni ya vizazi na vizazi (Zab 33:11) naye ameuandaa ufalme wake ili sote tuuingie. Tuzidi kuomba neema zake ili tustahili kuuingia ufalme huo wa wokovu wetu.

Liturujia J17 Mwaka A
24 July 2020, 08:27