Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetuma salam za rambi rambi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kufuatia msiba mzito wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Ben William Mkapa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetuma salam za rambi rambi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kufuatia msiba mzito wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Ben William Mkapa. 

Maaskofu Katoliki Tanzania: Salam za Rambirambi: Ben William Mkapa

Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge, ndiye aliyepewa heshima ya kuliwakilisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika kutoa salam za rambirambi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Kanisa Katoliki linaungana kwa dhati kabisa na watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mzito ambao umeligusa taifa, Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. RIP!

Na Padre Nikas Kiuko, Dar Es Salaam na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa, Jumapili tarehe 26 Julai 2020 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mzee William Benjamin Mkapa, Mkristo Mkatoliki aliyekuwa anaishi katika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Upanga, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ni kiongozi aliyeshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Parokia yake ya Upanga. Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge, ndiye aliyepewa heshima ya kuliwakilisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kutoa salam za rambirambi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania na kuonesha kwamba, Kanisa Katoliki lilikuwa limeungana kwa dhati kabisa na watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mzito.

Huu ni msiba ambao umeligusa taifa, Kanisa la Tanzania na Ulimwengu katika ujumla wake, kutokana na ushuhuda wa wema na unyoofu wa maisha ya Marehemu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Askofu Ndorobo, amewafariji watu wa Mungu kwa maneno kutoka katika sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 6: 37 “Wote anipao Baba watakuja kwangu, nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu”. Amewafariji wote katika imani ya Kanisa kuhusu ufufuko wa wafu na uzima wa milele. Kwa sababu hawajui siku wala saa, ni vyema kila mwamini akatumia muda wake vyema kwa ajili ya kujiandaa kukutana na Kristo Yesu, Hakimu mwenye huruma, haki na mapendo. Tanzania imegubikwa na majonzi makubwa kwa kifo cha Mzee Benjamin Mkapa na kwamba hawataweza kupata tena yale mambo ambayo walizoea kupata kutoka kwake, yaani: maono, ushauri na ushiriki wake katika maisha ya kila siku. Ni kiongozi aliyependwa na watanzania na Afrika katika ujumla wake. Alibarikiwa kuwa na kipaji cha kusikiliza shida za watu wake na kuwasaidia kadiri ya nafasi na uwezo wake. Huu ni upungufu ambao Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye anayeweza kuujaziliza.

Ni kiongozi aliyejituma bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Askofu Ndorobo amesema kwamba, alikutana na Rais Mkapa wakati wa maandalizi ya Ujio wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania kunako mwaka 1990. Wakati huo, Askofu Ndorobo alikuwa ni Padre aliyekuwa anatekeleza majukumu yake kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Akiwa Jimbo Katoliki Mahenge, alimkaribisha na kukubali kuchangia katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Regina Mundi. Watanzania wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na huduma ya kutukuka iliyotolewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini William Mkapa. Watanzania wataendelea kumwombea ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumpokea miongoni mwa watakatifu na wateule wake mbinguni!

Wakati huo huo, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kennedy Gastorn amesema kifo cha Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin William Mkapa, sio pigo kwa Tanzania tu bali kwa Jumuiya ya Kimataifa. Balozi Gastorn amesema kuwa hayati Mkapa alikuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia nguli na tayari salamu za rambirambi kufutia msiba wake zinaendelea kumiminika kutoka kwa balozi za nchi mbalimbaki kwenye Umoja wa Mataifa na kwa Katibu Mkuu Bwana Antonio Guterres. Umoja wa Mataifa umepokea tarifa za msiba wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa kwa mshituko mkubwa sana. Hakika ni pigo kubwa sana kwa taifa Tanzania, kwa Bara la Afrika na kwa Dunia nzima katika ujumla wake. Alipokuwa Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania alikuwa Mwenyekiti wa kampeni katika Umoja wa Mataifa zilizofanikisha kumchagua Dkt. Salim Ahmed Salim wa Tanzania kuwa Rais wa 34 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1979 hadi mwaka 1980.

Historia yake kwa ufupi inaonesha kwamba, Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa aliongoza awamu ya tatu kutoka Oktoba 1995 hadi Novemba 2005. Alikuwa Rais wa kwanza aliyechaguliwa katika uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi vya siasa tangu mfumo huo uliporejeshwa nchini Tanzania kunako mwaka 1992. Mheshimiwa Mkapa alizaliwa Masasi, Mkoani Mtwara tarehe 12 Novemba, 1938. Alipata elimu ya msingi na sekondari kati ya mwaka 1945 – 1956 katika shule za Lupaso, Ndanda, Kigonsera na Pugu. Alipata shahada ya kwanza ya Lugha ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda mwaka 1962, na shahada ya Uzamili ya Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Columbia, Marekani mwaka 1963. Aliajiriwa kama Ofisa Tawala na hatimaye Ofisa Mambo ya Nje. Kati ya mwaka 1966 na 1976 alifanya kazi katika Taasisi mbalimbali za umma.

Baadhi ya nyadhifa alizoshika kati ya Mwaka 1976 hadi Septemba mwaka 1995 ni pamoja Balozi wa Tanzania nchini Nigeria 1976; Balozi wa Tanzania nchini Canada 1982 – 1983; Mbunge wa Nanyumbu na Waziri wa Mambo ya Nje 1977 – 1980 na 1983-84; Waziri wa Habari na Utamaduni 1980 – 1982; Waziri wa Habari na Utangazaji 1990; Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu mwaka 1992 – Septemba 1995. Ratiba elekezi ya mazishi ya Mzee Benjamin Mkapa inaonesha kwamba, atazikwa Jumatano tarehe 29 Julai 2020, majira ya saa 8 mchana kwenye Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara.

TEC: Salam za Rambirambi
27 July 2020, 13:40