Tafuta

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT kudumisha nidhamu, maadili na utu wema kama utambulisho wao. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT kudumisha nidhamu, maadili na utu wema kama utambulisho wao. 

Askofu mkuu Nkwande "Atema cheche" Chuo Kikuu cha SAUT

Ni wajibu na dhamana ya wakleri wanaosoma Chuoni hapo kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwa ni mifano bora ya kuigwa, kimaadili, kiutu na kitaaluma, kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku hapo chuoni. Wawe ni mfano bora kwa maneno na mtindo wao wa maisha. Wanafunzi wanahitaji kutambua kwamba, wanapendwa, wanaheshimiwa na kuthaminiwa.

Na Nikas Kiuko, Nuriath Abdallah, Mwanza na Pd. R. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Chuo Kikuu cha Kikatoliki, kinaundwa na Jumuiya ya walimu, wanafunzi na wafanyakazi wanaojisadaka kwa ajili ya elimu na maisha! Hii ni Jumuiya inayopaswa kushikamana na kutembea kwa pamoja; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kurithisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu, kijamii na kitamaduni kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, waweze kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Huu ni mwaliko wa kuwa wazi kwa tamaduni nyingine zinazowazunguka ili kutajirishana kwa njia ya majadiliano ya kina! Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ni Jumuiya ambayo kila mtu anawajibu na dhamana ambayo anapaswa kuitekeleza kama njia ya kukamilishana, kwa kutambua kwamba, Mwalimu wao ni mmoja tu naye ni Kristo Bwana, wanayepaswa kufuata nyayo zake, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, dhamana inayotekelezwa kwa uvumilivu na unyenyekevu, daima wakijitahidi kujenga uhusiano wa karibu na Kristo Yesu.

Ili kuweza kufundisha kwa dhati kwanza kabisa, kuna haja ya kujifunza, kwani mwanafunzi ni yule ambaye anafuata nyayo na mifano wa mwalimu wake, makini katika mafundisho ili aweze kuyaboresha na ikiwezekana kumpita hata mwalimu wake, hali inayowafanya wadau mbali mbali katika elimu kuwa wanyenyekevu na watu wanaohitaji neema na baraka ya Mungu katika maisha yao, ili kuweza kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Kufundisha na kujifunza ni mchakato unaokwenda taratibu sana katika maisha, lakini muhimu katika ujenzi wa upendo na ushirikiano na Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, kusaidia kukamilisha kazi ya uumbaji. Dhamana hii takatifu anasema Baba Mtakatifu Francisko inasaidia kufahamu na kuboresha wema uliomo ndani ya kila kiumbe kwani kinaakisi na kupendwa na Mungu.

Kutokana na dhamana hii, Jumuiya ya Chuo kikuu inategemeana na kukamilishana, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake; kwa kutambua wito na mwelekeo wa maisha yake ili Chuo kikuu kiweze kupeta na kung’ara si tu kitaaluma, bali kama shule ya maadili na utu wema! Lengo la Chuo Kikuu cha Kikatoliki ni kusaidia kuwafunda wainjilishaji na wainjilishwaji, ili kwa kukutana na Kristo Bwana, waweze kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika uhalisia na vipaumbele vya watu, kielelezo cha Injili hai kati ya walimwengu, ili watu kwa kuona mifano bora ya maisha, waweze kumwongokea Mungu na hivyo kuwa ni viumbe wapya! Wanafunzi wajifunze kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha, kwa kujikita katika upendo na ukarimu, kwani ufanisi wao mwisho wa siku, utapimwa kwa kuzingatia nyenzo hizi.

Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, waweze kupata ufunuo wa ukweli wote ambao ni Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Roho Mtakatifu awasaidie wanafunzi kukuza na kudumisha majadiliano kati ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na tafiti za kisayansi, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa linalohimizwa kwenda ulimwenguni kote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, hivi karibuni alikitembelea Chuo Cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) na kubahatika kukutana na kuzungumza na Majaalimu pamoja na wakleri wanafunzi wanaoendelea kunolewa Chuoni hapo.

Askofu mkuu Nkwande amesema, Chuo Kikuu cha SAUT kinaheshimiwa sana ndani na nje ya Tanzania. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya wakleri wanaosoma Chuoni hapo kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwa ni mifano bora ya kuigwa, kimaadili, kiutu na kitaaluma, kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku hapo chuoni. Wawe ni mfano bora kwa maneno na mtindo wao wa maisha. Wanafunzi wanahitaji kutambua kwamba, wanapendwa, wanaheshimiwa na kuthaminiwa. Uwepo wa wakleri Chuoni hapo, iwe ni chachu ya maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Wanafunzi wengine, waguswe na ushuhuda huu, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu, chemchemi ya wema na utakatifu wa maisha!

Kwa upande wake, Padre Charles Bundu, Mlezi wa wanafunzi wa SAUT, Mwanza, amemhakikishia Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande kwamba, uwepo wa Wakleri Chuoni hapo, imekuwa ni chachu inayoimarisha akili, maadili na maisha ya kiroho kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha SAUT. Kwa sasa kuna Mapadre 16 kutoka Majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki ndani na nje ya Tanzania. Kuna watawa 85 kutoka katika Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume. Orodha hii inakamilishwa na Mabruda 3 wanaoendelea kunolewa Chuoni hapo, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Chuo Kikuu cha SAUT, kinatoa majiundo makini yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Wakati huo huo, Padre Titus Amigu, Jaalimu chuoni hapo ameongeza kwamba, mafundisho ya Kikristo ni utambulisho pekee unaokitofautisha Chuo Kikuu cha SAUT na vyuo vingine vyote nchini Tanzania. Kuendelea kujikita katika utambulisho huu ni changamoto kubwa, kwa sababu wanafunzi wanatoka katika mazingira tofauti ya malezi na makuzi yao: kiroho na kimwili! Wote hawa wanahitaji uvumilivu na subira, ili kuweza kuwanoa kikamilifu kadiri ya miongozo inayotolewa na Mama Kanisa mintarafu dhamana na wajibu wa Vyuo Vikuu vya Kikatoliki. Katika mahojiano maalum na Amina Rashidi, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa BAMC, amekiri kwamba, wanafunzi wengi Chuo Kikuu cha SAUT wanajivunia malezi na majiundo yanayotolewa Chuoni hapo: kiakili, kiroho, kimaadili na kiutu. Licha ya kwamba, SAUT kinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, lakini, wanafunzi wanao uhuru mkubwa wa kuabudu, kama sehemu ya haki zao msingi! Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, amekipongeza Chuo Kikuu cha SAUT kwa kuendelea kutoa elimu bora kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Ametumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Mapadre wanaosoma Chuoni hapo kwa kusaidia kutoa huduma za kichungaji kwenye Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Mwanza, kadiri ya nafasi zao!

SAUT Mwanza
08 July 2020, 14:04