Tafuta

Vatican News
Utunzaji bora wa mazingira ni muhimu katika asili yake Utunzaji bora wa mazingira ni muhimu katika asili yake 

Siku ya Utunzaji bora wa Mazingira:Maaskofu wa Cei wanahimiza kuongozwa na Laudato sì!

Baraza la Maaskofu nchini Italia(Cei)wametangaza ujumbe wao katika fursa ya Siku ya 15 ya kitaifa kwa ajili ya Utunzaji bora wa Mazingira,itakayofikia kilele chake tarehe Mosi Septemba.Maaskofu wanatoa ushauri kwa maparokia na vyama vya kitume kwamba inatakiwa mitindo mipya ya maisha katika mwanga wa Laudato sì.Mwaliko ni kuanzisha matendo yanayojikita kwenye mantiki ya utunzaji wa mazingira.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Italia katika Siku ya 15 ya Kitaifa kwa ajili ya utunzaji bora wa Mazingira, siku ambayo inaadhimishwa kila tarehe 1 Septemba, wanasisitizia juu ya mitindo mipya ya maisha hasa kwa kuongozwa na Wosia wa Kitume Laudato sì wa Papa Francisko. Katika ujumbe wao wanasema “Ni kipindi cha kufikiria kwa upya mantiki nyingi za maisha yetu pamoja, dhamiri ya kile ambacho kinafaa na kinaleta maana, katika kutunza maisha yenyewe, yenye thamani, umuhimu wa uhusiano kijamii na kiuchumi.

Ukosefu wa msimamo na udhaifu ni msingi wa ujenzi wa mfumo bora wa afya na siyo maslahi binafsi

Ujumbe wa maaskofu umefanyiwa kazi na Tume ya Baraza la Maaskofu kwa ajili ya matatizo ya kijamii na kazi, haki na amani kwa kushirikiana na Tume ya Maaskofu kwa ajili ya Uekumene na Majadiliano ya kidini ambapo wameupatika kauli mbiu kutoka katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Tito :“Tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa”  (Tt2,12). Kwa ajili ya mitindo mipya ya maisha”. Ujumbe huu unasisitiza kuwa janga la Covid-19 umeweza kuonesha hali nyingi zilizo na utupu kiutamaduni, hali za ukosefu wa mahali pa kuegemea na ukosefu wa haki, ambao lazima uweze kupata muafaka na kwamba katika muktadha  wa ukosefu wa msimamo na udhaifu, vyote hivyo vinageuka kuwa msingi wa ujenzi wa mfumo bora wa kiafya ambao unapaswa usimike msingi  wake juu ya  mwanadamu na siyo maslahi binafsi.

Janga la kiafya limeweka wazi mifumo dhaifu ya kijamii na kiuchumi

Maaskofu wa Italia wanasema kwamba dharura ya kiafya imeangazia mfumo wa kijamii na kiuchumi ulioonyeshwa kutokuwa na usawa na ubaguzi, ambapo  mara nyingi wadhaifu sana ni rahisi zaidi kubaki bila kutetewa, lakini pia uwezo mkubwa wa mwamko wa nguvu kwa watu, na nia ya kutaka kushirikiana. Maaskofu wa Italia pia wanaalika wanaparokia na vyama vya kitume vya Kanisa  kutazama uhusiano wao na mazingira kwa kuzingatia kuwa yote yamesukana  (LS 138) na janga la virusi vya corona , liimekuwa ni ishala wazi kwamba dunia imeugua kama alivyokuwa amekwisha sema Papa Francisko katika sala yake tarehe 27 Machi 2020, na kama matokeo ya uhusiano endelevu na mazingira yote.

Kuongozwa na Wosia wa Kitume wa Papa Francisko Laudato sì

Kwa mujibu wa Maaskofu wa Italia uchafuzi mkubwa wa mazingira, machafuko ya mifumo mingi ya mazingira na uhusiano usio wa kawaida kati ya banuai vinaweza kuwa vimeongezea  katika  janga hilo au kuzidisha matokeo ya athari zake na kwa hivyo wanawaalika  kakabiliana na mgogoro huu wa mazingira. “Mara nyingi tulifikiria sisi ni mabwana na kuharibu kila kitu, tumeharibiwa, na kuchafua maelewano ya kuishi mahali ambamo tumewekwa”,  wanasisitiza maaskofu na kwa maana hiyo tunatakiwa  kujikita katika  mafundisho ambayo Papa Francisko anafafanua katika Wosia wake wa Laudato si’.

Miaka mitano ya Laudato sì:mwaka maalum wa Laudato sì

Miaka mitano baada ya kutangazwa kwa Laudato sì na katika fursa ya mwaka huu maalum uliowekwa kwenye maadhimisho ya kumbukumbu yake kuanzia tarehe  24 Mei 2020 - 24 Mei 2021, ujumbe unaendelea “ ni muhimu kwamba katika Majimbo yetu, katika maparokia, katika vyama vyote na harakati zote za kikanisa ziweze kuelewa juu yake. Hii ni kwasababu   Wosia huo bado unangojea kupokelewa kwa pamoja ili uweze kuwa maisha, matarajio ya wito katika hatua mbali mbali za kubadilika katika uhusiano na kazi ya uumbaji, liturujia, na  utukufu kwa Mungu”.

Maelekezo ya kichungaji

Hatimaye katika ujumbe wa Maaskofu wanatoa baadhi ya maelekezo ya kichungaji kwa maana ya kutangaza uzuri wa uumbaji; kulaani vipingamizi vya mpango wa Mungu katika kazi yake ya uumbaji; kuelimisha utambuzi, kufundisha namna ya kufanya mang’amuzi,  na kusoma ishara za kazi ya uumbaji; kufanya mabadiliko katika mitazamo na tabia ambazo haziendani na mfumo wa ekolojia; kuchagua kujenga nyumba ya pamoja ambayo ni matunda ya  moyo uliopatanishwa; kujiunga katika  mtandao wa chaguzi mahalia, ikiwa na maana ya kufahamishana mazoea mazuri ya mapendekezo endelevu ya mazingira na kuhamasisha mipango katika maeneo mahalia;  kuhamasisha liturujia za kidini juu ya utunzaji wa kazi ya uumbaji  hasa katika ‘Kipindi cha Kazi ya Uumbaji’ (kuanzia Septemba 1 -Oktoba 4); kuhamasisha mkakati wa kielimu fungamani, ambao unajikita katika masuala ya  kisiasa na kijamii; kuwa na mkakati wa kushirikiana na wale walio katika jamii za kiraia ambao wanajitahidi katika masuala ya maisha ya kiroho; kuhamasisha uchaguzi wenye nguvu kwa usalama utunzaji bora wa mazingira.

05 June 2020, 13:01