Tafuta

Vatican News
Padre Gaston George Mkude: Tafakari Kuhusu Uhusiano Uliopo Kati ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Ndoa Takatifu. Padre Gaston George Mkude: Tafakari Kuhusu Uhusiano Uliopo Kati ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Ndoa Takatifu.  (Vatican Media)

Uhusiano Kati ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Ndoa Takatifu

Ni katika muktadha huu naona ni vema tukachukua nafasi kidogo kutafakari fumbo la Ekaristi takatifu na kweli za maumbile yetu kama wanadamu. Mwanadamu ni kiumbe mwenye roho na mwili, hivyo hatuna budi kila mara kumwona katika ukamilifu wake na kamwe tusikae moja bila upande mwingine, mwanadamu sio mwili tu na pia sio roho tu bali ni muunganiko kamili wa mwili na roho.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Zawadi ya mwili ina nafasi ya pekee katika imani yetu ya Kikristo. Lakini leo naomba tunapoadhimisha sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo tutafakari kwa pamoja juu ya Mwili wa Kristo na miili yetu mintarafu maumbile ya uzazi na dhana nzima ya maumbile yetu ya kijinsia. Naelewa kuwa sio mada rahisi na hasa inapoletwa mbele yetu na mmoja ambaye ni mseja na kasisi wa kikatoliki kama mimi kwani mtakuwa na maswali juu ya uzoefu wangu katika eneo hilo. Na kwa kweli hapa lengo langu sio sana kujadili au kutafakari juu ya Fumbo la Ekaristi Takatifu bali zaidi sana tuone mahusiano ya Mwili wa Kristo na dhana nzima ya miili yetu ya kibinadamu mintarafu maumbile ya uzazi. Leo tunapoishi katika ulimwengu wa utawandazi hatuwezi kusema kuna miiko ya kujua mambo kadha wa kadha yanayohusu eneo hilo la maumbile yetu ya kijinsia. Na hata nathubutu kusema kile ambacho kilionekana kuwa ni miiko na siri kubwa leo hii hakuna tena siri wala miiko ile tunapoingia na kuishi katika ulimwengu wa utandawazi.

Leo ndoa nyingi zinavunjika na kuparaganyika kisa tu mitandao ya kijamii au teknolojia ya mawasiliano, leo simu na mitandao imekuwa ni kichocheo kikubwa na cha haraka za mahusiano na hivyo aidha kujenga mahusiano lakini pia hata kuyabomoa na kuyaangamiza kabisa. Ni katika muktadha huu naona ni vema tukachukua nafasi kidogo kutafakari fumbo la Ekaristi takatifu na kweli za maumbile yetu kama wanadamu. Mwanadamu ni kiumbe mwenye roho na mwili, hivyo hatuna budi kila mara kumwona katika ukamilifu wake na kamwe tusikae moja bila upande mwingine, mwanadamu sio mwili tu na pia sio roho tu bali ni muunganiko kamili wa mwili na roho. Naona kuna haja Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ituasaidie pia kutafakari juu ya uhalisia wetu kama wanadamu na hasa eneo hilo la maumbile ya kijinsia. Kanisa mara nyingi limepoteza hata mvuto katika ulimwengu huu wa leo wa teknolojia na utawandazi na hasa kuhusu mafundisho yake kuhusu elimu ya jinsia ya kimaumbile.

Ulimwengu hata umekosa kutenda haki kwa Kanisa kwa kuona kuwa Kanisa kazi yake ni kuweka sheria na maagizo nini kinaruhusiwa na nini kinakatazwa. Pamoja na ukweli kuwa maisha ya mwadamu karibu katika kila eneo kuna sheria na makatazo yake ila ili kuelewa vema juu ya maumbile yetu ya kijinsia haitoshi kubaki katika sheria na makatazo tu bali kuingia na kuona hasa ukweli na umaana wa maumbile hayo ya kijinsia. Mimi sio mwanamichezo ila natumaini akija mchezaji mmoja makini na mzuri wa mpira wa miguu kama kijana Jonas Mkude wa timu ya Simba, na akaanza kutueleza uzuri wa mchezo wa soka kwa kutueleza sheria zake, sidhani kama tutaonja uzuri wa mchezo huo. Mmoja hapendi kuucheza au kuungalia kwa kuwa anapenda sheria za mchezo huo ila kwa hakika mpira wa miguu ni zaidi ya sheria. Na hata wachezaji wake hawaanzi kucheza kwa kujua sheria zake na hivyo hivyo hata kwa sisi mashabiki tena wa ngazi kama yangu ambao uelewa wa sheria zake nyingi wala ukiniuliza sizijui ila napenda kuuangalia na kuushabikia.

Kanisa daima linafundisha na kuangalia juu ya dhana nzima ya maumbile ya kijinsia likijikitaka katika sheria ya asili (Natural law), ndio sheria ya kushiriki katika sheria ile ya milele ya Mungu mwenyewe. Pamoja ndio sheria mama inayotuongoza katika maswala ya sheria zihusuzo maumbile ya kijinsia ila bado inatupa muono unaokuwa finyu kwa kiasi fulani kwani mara nyingi tunaishia kuona maumbile ya kijinsia nia na lengo kubwa ni katika kuzaana na kuujaza ulimwengu. Hivyo hata tendo la ndoa linaonekana kuwepo kwa ajili ya nia kubwa ya kuzaliana na kuujaza ulimwengu. Na hivyo leo badala ya kujikita na kuanzia katika sheria ya asili ya maumbile (Natural Law) bali tutatafakari kwa kuanzia katika kiini cha imani yetu yaani Karamu ile ya mwisho, Ekaristi Takatifu ile ya kwanza ya Yesu pamoja na wanafunzi wake. Usiku ule Yesu akiwa pamoja na wanafunzi wake, alitwaa mkate, akaubariki, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, ‘’Huu ni Mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu’’.

Hivyo kiini hasa cha imani yetu ni zawadi ya Mwili wake Bwana wetu Yesu Kristo. (Corpus Domini au wengine wanaiita pia Corpus Christi yaani Mwili wa Kristo). Labda swali linakuja mara moja Ekaristi Takatifu au Mlo ule wa karamu ya Mwisho unaakisije maumbile yetu ya kijinsia? ‘’Huu ni Mwili wangu’’, ndio maneno anayotamka Yesu katika karamu ile ya mwisho au Adhimisho la kwanza la Ekaristi Takatifu kati ya Yesu na wanafunzi wake. Mara nyingi katika imani yetu tunaona kuna kusahau na hata kuudharau mwili na kukazia zaidi roho. Na ndio utasikia hata kuna misemo kuwa huyu ni mtu wa kiroho au hata kusikia mwili unafaa nini mbele ya roho yangu na mitazamo mingi ya namna hiyo tunaweza kuwa na mifano mingi hapa kadiri ya maisha ya kila mmoja wetu. Mwanafalsafa wa Kifaransa wa karne ya 17 aliyejulikana kama Renè Descartes katika kutumia njia yake ya mashaka ili kuwa na hakika na uwepo wake anaongozwa na maneno yale: ‘’Cogito ergo sum’’ ni maneno ya kilatini yenye maana hasa kuwa kwa kuwa nawaza au nafikiri na nina hakika ninafanya kitendo hicho basi nina hakika ya uwepo wangu. Nipo kwa kuwa nina hakika kuwa ninafikiri, uwepo wangu unahakikiwa na uwezo wangu wa kufikiri, wa kuwaza.

Kuna kishawishi cha kufikiri namna hiyo na hivyo kujikuta kwetu mwili hauna umuhimu kwani itoshe kuwa roho tu na hapa hata mawasiliano yetu yanakuwa katika namna ya juu zaidi kuliko sasa tunapokuwa mwili na roho. Mawasiliano kati ya malaika hakika ni ya juu zaidi kuliko yetu sisi wanadamu kwani wao ni roho tu, hivyo malaika mmoja na mwingine hakuna jinsi wala namna ya kuficha kwa mwingine mawazo na fikra zake. Naomba hili liwe la mjadala wa siku nyingine. Karamu ya mwisho leo inaturejesha na kuwaza kwa namna nyingine. Ni kwa njia ya mwili Yesu anatuonesha jinsi tunavyoweza kuingia katika mahusiano iwe na Mungu na hata kati yetu. Ni kwa njia ya miili yetu hapo tunaweza kuingia katika mahusiano na mwanadamu mwingine. Tunaona, kusikia, kunusa na hata kugusa mwingine kwa kuwa tuna mwili. Hivyo ni kwa njia ya miili yetu kunakuwa na mawasiliano yetu ya kibinadamu kati yetu, miili yetu ndio chanzo na njia pekee ya mawasiliano kati yetu kama vile simu na vifaa vingine vya mawasiliano.

Mwili wa mwanadamu ndio mlango wa mawasiliano kati yetu. Ni kwa njia ya miili yetu tunaweza kuhusiana kati yetu. Pamoja na kutumia lugha kwa mawasiliano bado mawasiliano yetu yanachangiwa kwa nafasi kubwa kabisa na ile lugha ya mwili, uso unaongea, macho yanaongea, mikono inaongea, hivyo lugha ni kutusaidia na kutuingiza zaidia katika mawasiliano zaidi ila lugha ya kwanza inayomuunganisha mwanadamu na mwingine ni ile lugha ya mwili. Mtoto mchanga kabla ya kujifunza kuongea anawasiliana na mama kwa lugha ya mwili na hivyo mara baada ya kuzaliwa mara anapoanza kuona mtoto anawasiliana na mama na watu wanaomzunguka nakuanza hata kutabasamu! Chakula ni mojawapo ya kiunganishi muhimu sana ya mahusiano baina yetu. Familia inakaa na kushiriki pamoja meza ya chakula, marafiki hali kadhalika katika kuonesha urafiki wao kwa hakika wanaalikana kushiriki chakula pamoja, hivyo chakula kinatuunganisha kwa namna ya pekee kabisa. Huwezi kusema mmoja ni rafiki yangu halafu huwezi hata kutenga au kuona jinsi ya kushiriki naye chakula, hakika marafiki zetu tutapambana kuona aidhan tunawaalika majumbani kwetu au kukaa nao mahali na kushiriki nao chakula. Nafasi ya kukaa na kula pamoja ni fursa inayoturudisha na kukumbuka nyuma lakini pia kushiriki hali zetu za sasa na huku tukiangalia kesho yetu kwa matumaini.

Na ndio Yesu wakati anapoweka Agano Jipya kati ya Mungu na mwanadamu, anawakusanya na kuwaalika wanafunzi wake katika mlo ule wa jioni, karamu ile ya mwisho pamoja nao kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake. Alitwaa mkate, akaubariki, kuumega na kuwapa wale. Hapa kula haikuwa tena kama vile mlo wa kawaida wa kibaiolojia bali sasa kuonesha muungano wa Agano Jipya unaojengeka katika Upendo kamili kabisa kati ya Mungu na mwanadamu. Na ndio hivyo hivyo hata katika uwanda wa maumbile yetu ya kijinsia. Kwa kuwa sisi wanadamu tu viumbe tunaotumia lugha, hivyo mahusiano ya kijinsia yanapewa maana ya kina zaidi. Ni kwa njia ya mahusiano hayo wawili wanaonesha muunganiko wa pekee kabisa. Ni kwa lugha ya miili, wawili wanaingia katika mahusiano ya mapendo. Miili inaongea hata kabla ya maneno ya lugha ya kawaida na hata kukubaliana kabla ya kauli za kutoka kinywani. Ni kwa njia ya miili basi mwanadamu anawasiliana kwa namna ya ndani na kina kabisa. Mwili umeumbwa kwa mawasiliano, sura imeumbwa kwa kuwasiliana baina ya wanadamu. Sura ndio mlango wa nyumba ya mwili, ni kwa njia ya sura mmoja anaingia katika mawasiliano na mahusiano na mwingine.

Hivyo kinywa na hata maneno au busu hivyo vinakamilisha kile ambacho tayari sura tayari ilishawasilisha. Hivyo kama Kanisa kuanza kuzungumzia juu ya dhana nzima ya maumbile ya kijinsia kwa kuanza kuzungumzia nini kinaruhusiwa na nini kinakatazwa na Kanisa ni kuanzia mahali pasipofaa sana. Maadili ya Kanisa sio juu ya nini kinaruhusiwa na nini kitakatazwa na Kanisa, bali jinsi ya kuhusiana na wengine kwa namna ile ambayo Mungu katika uumbaji ametaka tuhusiane na kuwasiliana. Maadili sio makatazo bali ni kuniwezesha kuishi na wengine kwa namna ile Mungu ametuumba kuhusiana na kuwasiliana. Kitendo ni kibaya sio kwa sababu kinakatazwa bali kwa kuwa kinakinzana na uhalisia na ukweli wa mahusiano baina yetu kama wanadamu. Hivyo Yesu leo anabadili mtazamo mzima wa mitazamo yetu yahusuyo Maadili na maisha yetu wanadamu kwani anaingia katika Agano na mwanadamu kwa njia ya zawadi ya Mwili wake (Corpus Domini). Ni kwa njia ya Mwili wake anatualika kuingia katika mahusiano ya pekee kabisa na Mungu. Huu Mwili unatolewa kwa ajili yenu, Mwili wake ni zawadi kwetu. Labda tutafakari nini maana yake kutupa Mwili wake kama zawadi kwetu.

Hii inaweza kungumu kueleweka hasa pale mwili tunapoushusha na kudhani kuwa unaweza kuwa mali ya mtu mwingine. Mitazamo kama ile ya mume kuwa ni mmiliki si tu mwili wake bali pia wa mke wake. Hivyo mwanaume angeweza kufanya lolote na mwili wa mke wake na mke kamwe hawezi kuumiliki mwili wake kama vile mume awezavyo. Na ndio utaona hata katika jamii zetu mke akikutwa katika uzinzi au akikosa uaminifu hapo inakuwa ni kosa kubwa sana na hata kupelekea ndoa nyingi leo kuvunjika na kama ni mume anakosa uaminifu basi mke hana budi kusamehe kwani mume ana haki na mume wake, ila mke ni mali ya mume. Yesu leo anatoa Mwili wake kuwa zawadi yetu. Mwili wa Kristo ni zawadi kwa Kanisa lake, kwa ajili ya uzima wa milele. Anapotoa Mwili wake anatualika nasi kuwa na uelewa mpya juu ya miili yetu. Kuwa ni mwili daima kunikumbushe kuwa mimi ni zawadi itokanayo na upendo wa wazazi wake na hatimaye sote ni zawadi ya Mungu aliye Bwana na Muumbaji wetu sote. Sisi ni zawadi! Hivyo hata mahusiano ya ndoa hayana budi kujengeka katika ukweli huo kuwa kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake wa ndoa. Na pia mwingine hana budi kumpokea mwenzake kama zawadi na kamwe si kama mali yake anayoimiliki au kuitawala.

Ni mahali ambapo wawili wale wanajifunza kujitoa zawadi kamili bila kujibakiza, huku wakijitoa wakiongozwa na imani na uaminifu kati yao. Ni mahali pakujifunza kupokea zawadi sio kama zawadi nyingine zozote tunazoweza kuzifikiria katika ulimwengu huu, kwani hapa zawadi sio kitu bali ni mwingine.  Hivyo lazima kupokea zawadi hii ya juu kabisa kwa shukrani na hata kwa heshima kubwa. Mwingine kamwe si kitu bali ni mtu hivyo huna budi kumpokea kwa heshima kubwa na shukrani ya pekee. Hivyo maneno ya Kristo katika karamu ya mwisho yanatuongoza leo katika mahusiano ya kindoa kati ya mume na mke. Maisha ya ndoa ni maisha ya muunganiko, hivyo hayana budi kuakisiwa na kitendo cha kujitoa baina ya hawa wawili hivyo hawana budi kama nilivyosema hapo juu kujitoa na kupokeana kwa kila jambo kwa shukrani na heshima. Karamu ya mwisho, Yesu anapotoa Mwili wake kuwa zawadi kwetu anakutana na hali kinzani isiyokuwa rafiki sana kwake.

Yesu anashiriki mlo na karamu ile pamoja na Yuda Iskariote ambaye alimuuza kwa vipande vya fedha, anashiriki pia pamoja na Petro ambaye alimkana mara tatu na hata mitume wengine ambao kwa sehemu kubwa walikimbia na kujiweka mbali na Bwana na Mwalimu wao. Pamoja na hali hizi kinzani bado Yesu hasiti kuutoa Mwili wake kwetu hata leo. Pamoja na ukweli kuwa mara nyingi tunakuwa mbali naye bado Yesu anatoa Mwili na Damu yake kuwa chakula chetu kwa ajili ya uzima wa milele. Ni kwa kumwangalia Yesu katika mlo na karamu ile ya mwisho nasi pia na hasa wanaokuwa katika mahusiano ya kindoa kuiga na kujifunza kutoka kwake. Yesu anatoa Mwili wake katika mazingira yake ya kusalitiwa, kukanwa na hata kukimbiwa sio na watu wa mbali bali wale aliowapa Mwili wake wale na Damu yake wanywe. Ni kwa kumwangalia Yesu tu katika karamu ile ya mwisho hapo kila mmoja anayeingia katika mahusiano ya kindoa anapata nguvu ya kusonga mbele pamoja na changamoto au magumu yanayoweza kutokea katika maisha ya muunganiko wa mume na mke. Maumbile ya kijinsia hasa ni kwa ajili ya kuwaunganisha mtu mume na mtu mke.

Lugha ya mwili inawaunganisha wawili hawa, inawaleta pamoja. Lakini tumeona katika karamu ya mwisho mmegeko na kukosekana kwa muunganiko kamili baina ya Yesu na wanafunzi wake. Yuda anamsaliti Yesu, hamwoni tena Yesu kama Rafiki na Mwalimu wake bali anamuona kama kitu au bidhaa ya kuwekwa na kunadiwa au kuuzwa sokoni kwa vipande 30 vya fedha. Petro anamwahidia Yesu kuwa yupo tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya Mwalimu na Rafiki yake, lakini wakati wa majaribu ulipofika hakuweza kusimama na kuishi kiapo chake. Petro anamkana Yesu mara tatu kuwa hamjui na wala hana mahusiano na mtu huyu. Hata katika mazingira haya ya kusalitiwa na kukanwa Yesu anabaki kimya. Hana la kusema. Na hivyo hivyo hata katika mahusiano ya ndoa leo adui yake mkubwa ni usaliti na uongo, ni kukosa uaminifu wa dhati.

Mfalme Daudi alipolala na Batsheba aliyekuwa mke wa Uria, dhambi au kosa lake halipo katika kuzini tu bali katika uongo na hujuma. Na ndiyo Maadili ya Ndoa katika Kanisa linawaalika wanandoa kuwa wakweli na miili yao na hivyo kuepuka uongo na hujuma. Kushiriki tendo la ndoa na mwingine ni sawa na kusema ‘’najitoa mwili wangu kama zawadi kwako bila kujibakiza, sasa na daima, na pia nakupokea nawe mwenzangu kama zawadi kwa heshima na shukrani kubwa’’. Hata hivyo bado Maadili ya Ndoa yanawataka wanandoa kuwa na maneno ya kuponyana pale wanapoanguka katika uongo na hujuma. Ni kuwa na maneno yanayoweza kuponya madonda na machungu yaliyosababishwa na uongo na kukosa uaminifu. Hivyo anayekosa uaminifu haitoshi tu ila kwa kutumia busara kubwa na hekima kuona pia kujipatanisha na mwenzake, narudia hapa lazima kutumia hekima na busara hivyo kuepuka madhara zaidi. Ila hasa pale mwingine anapogundua bila mashaka kuwa mwenzake amekosa uaminifu basi hapo aone jinsi ya kujipatanisha na Mungu na mwenzake wa ndoa pia.

Katika karamu ya mwisho Yesu anakuwa ni muhanga wa uongo na usaliti kama tulivyoona hapo juu. Ananunuliwa na wenye pesa na wenye nguvu na mamlaka. Anachukulia kwa nguvu na maaskari na kumuwamba pale juu msalabani. Yesu hakujibu dhuluma na usaliti kwa mabavu na nguvu bali aliyapokea yote kama mmoja aliye mnyonge na duni kabisa. Alijikabidhi katika mikono ya wanafunzi wake, hivyo alikataa kujitetea Yeye mwenyewe. Hata kama walimsaliti na kumkana, Yeye alibaki mwaminifu mpaka dakika ya mwisho. Baadhi ya ndoa leo zinagubikwa pia na ubabe au mabavu na unyanyasi wa kila aina. Tunaweza kuona pia Mfalme Daudi kwa Uria ni ubabe na mabavu, alitumia madaraka yake katika kumdhulumu Uria. Hebu angalia jinsi wanawake leo wanavyonyanyasika kijinsia kwa kubakwa iwe majumbani, makazini, na kwa bahati mbaya nikiri na niseme hata makanisani matukio yao ya aibu kubwa yanasikika leo wanawake wanaotumika kingono. Dhuluma za kingono leo dhidi ya watoto si tu zinasikika huko nje bali hata kati yetu makasisi wa Kanisa Katoliki tunadhulumu watoto wengi ulimwenguni kote wa kike na kiume kwa kutumia nafasi zetu au madaraka yetu au nguvu na mabavu yetu.

Nikiri pia hata nasi Makasisi mara ngapi tumetumia nafasi zetu kudhulumu ndoa za watu kwa kuingia katika mahusiano na wake za watu, hapo hakika tunafanana na Mfalme Daudi alivyomdhulumu Uria. Tunaweza kukubaliana kuwa ili kuzungumzia Maadili yanayohusu maumbile yetu ya kijinsia haitoshi kuzungumzia nini kinakatazwa na nini kinaruhusiwa na Kanisa.  Kama Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kuwa hata mume anaweza kumbaka mke wake. Hii inashangaza tunaposikia kwa mara ya kwanza ila yafaa tukumbuke kila mara tendo la ndoa ni tendo la upendo hivyo wawili wote kwa pamoja lazima wajitoe kama zawadi na kamwe isiwe kwa ajili ya kutimiza matakwa ya mmoja tu. Hebu tufikirie watoto wangapi leo wanalazimishwa na hata kuuzwa katika soko la kitalii la ngono karibu duniani kote, hebu fikiria watoto sio tu wa kule Thailand na Ufilipin bali hata katika miji yetu ya kitalii katika Afrika Mashariki na hata Afrika kiujumla. Hivyo kila mara katika mahusiano ya kijinsia panapokuwa na mabavu na ukubwa wa aina yeyote ile hapo mahusiano hayo yanapoteza maana na uhalisia wake kadiri ya mpango wa Mungu.

Karamu ya mwisho inatukumbusha kuwa kiini cha mahusiano ya kijinsia ni kukataa kila aina ya manyanyaso na badala yake ni maelewana na usawa. Mmoja anapotamani mwili wa mwingine basi isiwe kwa namna ile ya kibanafsi kama vile ni mmiliki wa mwili wa mwingine bali wanapaswa kuingia katika mahusiano ya upendo na kujitoa kwa heshima na shukrani na kamwe sio kama simba atamanivyo nyama kwa kuirarua na kuisambaratisha. Tamaa ile haina budi kuamsha furaha kwa mwingine, hivyo mwingine kujiona ni wa thamani na kamwe sio kujisikia duni na mnyonge na hivyo anashiriki kwa lengo la kumfurahisha huyu mwenye nguvu aidha kifedha au kimadaraka au hata nguvu za kimwili. Ni kitendo kinapaswa kuamsha furaha na thamani kwa wote wawili na kamwe asiwepo mmoja anayetumia ukubwa au nafasi yake kwa kumtumia mwingine, mmoja asijesikie kamwe kuwa anatumika kwa ajili ya mwingine bali wote wawili wanajitoa kwa heshima na shukrani kubwa. Mtume Paulo anasema: ‘’Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo’’. (1Wakorintho 7:4)

Tamaa ile haina budi kuwepo kwa wote wawili. Kila mmoja anatamani kutamaniwa, na hapo kuthamini pia tamaa ya mwingine. Daima kuna furaha kuona mwingine anakufurahia, unaona fahari kuona mwingine anaona fahari pia juu yako. Anasema Askofu mkuu mstaafu Rowan Williams wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye yeye ameoa na ana mke: Katika mahusiano ya kindoa hapo sina dhamana juu ya mwili wangu mwenyewe. Kila mara ninapokuwa katika matamanio ninabaki na hali ifuatayo: Siwezi kujitimilizia tamaa na mahitaji zangu nikibaki mwenyewe. Tunakuwa katika hali ya kutoweza kujisaidia pale tunapobaki wenyewe bila mwingine. Ili mwili wangu uweze kuwa sababu ya furaha kwa mwingine, kumpokea mwingine kwangu hapo lazima awepo mwingine, ambaye namuona au kumgusa, kumpokea na kumthamini, ndio kusema mimi nakuwa zawadi na chanzo cha furaha kwa mwingine. Kutamani furaha yangu ni sawa na kutamani furaha ya yule anayenitamani. Furaha yangu ya kimwili ni faraha ya kimwili ya mwingine.

Karamu ya mwisho ni mwaliko kwetu kushiriki uduni wa Kristo, kwa jinsi alivyojikabidhi mikononi mwa wanafunzi wake aliowaalika kuutwa Mwili wake na Damu yake. Ni udhaifu wake wa daima kwani anabaki mpaka leo kujitoa kwetu tulio wanyonge na wadhambi. Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake na kuwaonesha makovu ya madonda yake, ndio kusema anabaki daima hata katika utukufu wa milele akiwa na makovu ya madonda yale kama ishara ya unyonge na uduni wake, ishara ya Upendo wa Mungu kwetu. Ni kumbukumbu ya Upendo wa milele wa Mungu kwangu na kwako. Je, nasi mara ngapi tumekubali kubaki na makovu ya madonda yatokanayo na gharam ya upendo wetu kwa wengine? Kuamini katika ufufuko maana yake ni kuamini katika kupenda hata kwa kupata madonda na makovu kwani tunajua mwisho wetu sio kifo bali kushiriki maisha ya utukufu wa milele pamoja na KRISTO mwenyewe. Usawa na upendo kamili kati ya wanandoa si tu ni Injili inayoishi bali ni kielelezo cha jamii zetu zinazokuwa na kishawishi cha tofauti na matumizi mabaya ya madaraka na mamlaka, iwe katika jamii za kiraia bali hata zile za kikanisa.  

Mahusiano mazuri na yenye afya ya kindoa yanatoa changamoto kubwa hata katika taasisi za kisiasa katika ulimwengu mamboleo. Kama tangu nyumbani tayari watoto wanaonja usawa na hali ya kuheshimiana basi hata wanapokuwa watu wazima na kuchukua wajibu mbali mbali hawatakuwa na kishawishi cha kugandamizana au kuona kuwa mmoja anabudi kuwa chini na kutawaliwa tu. Na ndio maana hata leo Mama Kanisa anajitathimi kuona kuwa linaweza kuwa na mapadre wanaothamini sadaka ya useja ikiwa tangu katika familia wamepokea malezi ya kuthamini maumbile na tofauti za kujinsia. Wasemari leo hawapaswi kulelewa tena kwa kukaa mbali na wanawake badala yake kuwa msaada mkubwa katika kuwasadia kukomaa katika mahusiano. Pamoja na usaliti, tunaona Yesu anageuza usaliti ule kwa kujitoa Mwili na Damu yake kama zawadi kwa wanafunzi wake. Kila adhimisho la Ekaristi ni adhimisho la uaminifu, na ndio kila Maadili ya Kanisa yanajengeka katika uaminifu. Tunajitoa wenyewe, miili yetu, maisha yetu, matumaini na hata hofu zetu, kwa mwingine bila kujibakiza sasa na daima. Na hili tunalishuhudia katika maagano ya wana ndoa kuwa wanajitoa na kupokeana siku zote za maisha yao. Lakini hii leo imeonekana kuwa changamoto kubwa katika jamii zetu.

Taasisi ya ndoa leo imekuwa ni moja ya taasisi inayokosa udumifu. Tunaishi katika ulimwengu wenye utamaduni wa kila kitu ni kwa mkataba tena wa muda mfupi, iwe kazini na hata majumbani. Na hii inazaa matatizo na sintofahamu nyingi katika jamii zetu na hasa kwa wanakanisa. Leo hata baadhi ya maaskofu wanaona labda Kanisa halina budi kubadili baadhi ya mafundisho yake mintarafu sakramenti ya ndoa. Na si tu wenye maisha ya ndoa bali hata kwa sisi tulioingia katika maisha ya wakfu kama makasisi na utawa, bado leo kuna wengi wanatoka katika maisha ya ukasisi na utawa kana kwamba siku ile ya kuwekwa wakfu tuliweka maagano au mkataba wa muda mfupi tu au basi ngoja kwanza niingie nione nikiona kama mambo hayaendi basi nitarudi na kusema natoka! Ni utamaduni wetu wa leo hakuna anayetaka kuingia katika mahusiano ya kudumu na ya kiaminifu bila kujali hali au nyakati kuwa ngumu au rahisi. Kama vile uaminifu ni wa muhimu hata kati ya marafiki ni zaidi sana kati ya watu wa maisha ya ndoa na hata wale wanaoitwa kuishi maisha ya wakfu kama makasisi na watawa. Uaminifu hapa sio tu ule wa kutopeana talaka na kuacha au kutengana. Badala yake ndio hali ya kujitoa mzima mzima kwa mwingine, kumuona mwingine ni kujiona wewe mwenyewe. Inachukua muda kuingia katika mahusiano.

Inachukua muda kuwa huru na wazi mbele ya mwingine. Jinsi muda unavyosonga katika mahusiano na ndio mwingine anapata kukujua na hata kugundua si tu mema na mazuri yako bali hata mabaya na madhaifu yako. Uaminifu daima ni hatarishi! Hivyo ujasiri unahitajika ili kubaki katika mahusiano hasa pale unapogundua madhaifu na mabaya ya mwingine. Ni kwa njia ya Ekaristi pekee tunapata nguvu kama ile ya Kristo mwenyewe hata baada ya kugundua kusalitiwa na kukanwa na hata kukimbiwa bado anatoa Mwili na Damu yake kwangu na kwako. Yesu hata leo anaendelea kujitoa kwa ajili yetu sisi tunaomsaliti, kumkana na hata kumkimbia mara nyingi.  Kifo kinapobisha hodi hapo mahusiano yetu yanakuwa matatani na hata tunakosa maneno ya kuongea kwani sote tunagubikwa na machungu na hofu kuu. Katika karamu ya mwisho mbele ya Yesu ni kifo kwani alishajua kuwa saa yake sasa imewasili na hana budi kutimiza mapenzi ya Mungu Baba.

Ni katika muktadha huo hatuoni Yesu akiwasusa na kuwaacha wanafunzi wake ambao kwa kweli kila mmoja sasa hataki tena kutambulika kama mwanafunzi wake bali anatoa Mwili na Damu yake kwa ajili yao na yetu mpaka leo. Kifo na maisha yetu ya kijinsia ya maumbile kuna uhusiano mkubwa hata kama tunabaki kushangaa kwanza. Katika Agano la Kale, ni kwa njia ya uzao tu mmoja anakuwa na hakika ya kuendelea kuishi hata baada ya kifo chake, na hii ipo sana katika tamaduni zetu za kiafrika, labda hata unaposhirikisha wazazi na ndugu na jamaa wazo la kuwa kasisi hata mtawa utasikia kwa hiyo utakufa bila kutuachia mjukuu au bila kutuachia sura yako. Hapa kila mmoja ajaribu kuingia katika mila na tamaduni zake tutakubaliana kuwa uzao ni faraja kubwa mmoja anaouacha nyumba baada ya kifo chake. Uzao wanabaki kubeba jina na sura ya mzazi wao. Na hata leo pia bado mtazamo huo upo. Kwa akina mama wanapojifungua saa ile wanaona ni saa ya kupambana kati ya uzima na kifo.

Na ndio utasikia mama leo anasema tumbo la uzazi linamuuma pale mtoto wake anapopatwa na mabaya au magumu.Hebu fikiria leo wamama wazazi wanaojifungua wakiwa na shida mbali mbali za uzazi tena katika mazingira duni ya nchi yetu na bara letu na hata ulimwenguni kote, fikiria leo akina mama wenye maambukizi wa ukimwi na wanapaswa kujifungua watoto salama, fikiria leo wamama wajawazito wasiokuwa na uwezo au jinsi ya kupata huduma bora za uzazi na mengi ya namna hiyo. Katika Kristo pekee upendo unashinda kifo! Upendo wa Mungu Baba kwa Mwana tunaona unashinda nguvu ya mauti na kifo.  Hivyo kama kweli tendo la ndoa ni kitendo cha upendo basi daima kifo hakiwezi kuwa na neno la ushindi. Mama pamoja na maumivu na hofu kubwa ya kuwa kati ya uzima na kifo bado anaendelea kutaka mtoto wa pili na watatu na kadhalika na kadhalika kwani anasukumwa na upendo kwa watoto. Hapa hatuna budi kuonja na kuthamini upendo wa mama zetu.

Jamii zetu leo tunaona zinagubikwa sana na agenda ya mahusiano au maumbile ya kijinsia yaani ukoloni wa kiitikadi, lakini kila mara tunakosa ukina na upana wa maana yake. Ukristo hauna budi kuonesha uzuri na maana yake na hivyo narudia Kanisa halipaswi kuanza kwa kufundisha sheria za makatazo na nini linaruhusu bali kuweka mbele ya waamini uzuri wake. Tabia zetu za kimahusiano ya kijinsia hazina budi kuwajenga watu katika heshima na mapendo yanayoakisi pande zote mbili kwa usawa.  Zinapaswa kuponya madonda na kuvunja ukimya. Yanapaswa kujengeka katika uaminifu na pia kutoa nafasi kwa watu kuyaingia huku wakijua pia magumu na changamoto zake na jinsi ya kuyakabiri. Kanisa halina budi kutenga muda wa kuwaanda vema wale wote wanaopenda kuingia katika mahusiano ya mume na mke. Ndoa nyingi leo zinajikutaka katika mitafaruku isiyoishia kwa kuwa hata waliingia bila kujua nini maana pana na ya kina ya ndoa. Ndoa haina budi kuakisi karamu ile ya mwisho. Ndoa ni sakramenti ya upendo, upendo unaakisiwa na ule wa Yesu, upendo usiangalia hatari ya kusalitiwa, kukanwa wala kukimbiwa bali unaojikabidhi mzima mzima kwa mwingine bila kutanguliza mashaka na kukosa imani kwa mwingine.

Sehemu kubwa ya tafakari hii nimehariri sehemu ya Kitabu cha Padre Timothy Radcliffe, OP’Christians and Sexuality in the Time of AIDS’’, 2008. Nawatakia tafakari njema na hasa kwa wanandoa tunapoadhimisha Dominika hii sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.

13 June 2020, 12:01