Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Masharti ya Ufuasi wa Kristo na Ukarimu wa Kiinjili. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Masharti ya Ufuasi wa Kristo na Ukarimu wa Kiinjili.  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili 13 ya Mwaka A: Utume na Ukarimu wa Kiinjili!

Kwanza anawaagiza wasijishikamanishe na familia na kwa maana anayempenda baba au mama kuliko yeye hamstahili. Pili anawataka wawe tayari kuyakabili majukumu yao hata katika ugumu wake. Na mwisho anawaambia wasitangulize mbele maslahi yao binafsi kwa maana anayetafuta kuyaokoa zaidi maisha yake kwa gharama ya utume atayapoteza. Ukarimu wa Kiinjili ni muhimu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 13 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (2Fal. 4:8-11, 14-16a) ni kutoka Kitabu cha Pili cha Wafalme. Ni somo linalotupatia mojawapo ya masimulizi ya matendo ya nabii Elisha. Ilitokea kuwa Elisha alikuwa akipita mara kwa mara katika mji huo unaotajwa, mji wa Shunemu. Wachambuzi wa historia ya Mji Mtakatifu wanatuambia kuwa mji huu ulikuwa kati ya miji ya Samaria na Karmeli ambako Elisha alikuwa akitolea unabii wake. Katika moyo wa ukarimu kwa watumishi wa Mungu, mama mmoja wa mji huo wa Shunemu anamkaribisha awe anafikia katika familia yake kumpunguzia mwendo na huenda pia na adha za safari kulingana na mazingira ya wakati huo. Tendo hili la ukarimu linageuka kuwa baraka kwa mama huyu ambaye kumbe alikuwa mgumba. Hakuwa na mtoto na mumewe alikuwa ni mzee. Elisha anamtabiria baraka mama huyo na mumewe kuwa watapata mtoto na kweli mwaka uliofuata wakabarikiwa kwa kujaliwa mtoto.

Simulizi hili ambalo huenda lingeonekana ni la kawaida, linapata maana nzito zaidi tunapoangalia kipindi cha historia na mazingira ya wakati huo ya Israeli. Katika kipindi hicho, picha nzima ya Israeli kiimani na kimaadili haikuwa nzuri. Ibada kwa miungu ya kigeni ilikuwa imeshamiri, maadili yalikuwa yameporomoka na watu walikuwa wameliacha pembeni kabisa Agano lao na Mungu. Katika mazingira hayo hakuna aliyemthamini nabii wa Mungu wala kumsikiliza. Katika mazingira hayo unahitaji ujasiri na moyo wa pekee sana kufanya kitendo ambacho mama huyu alikifanya kwa Elisha. Ni ujasiri na moyo huu unaokuzwa na kusifiwa katika somo hili la leo. Biblia inamsifu na kumweka mama huyu sambamba na akinamama wengine waliopokea baraka kubwa ya mtoto wakiwa katika umri wa uzee. Hapa tunamkumbua Sara mke wa Abrahamu, Hana mke wa Elkana aliyemzaa Samweli pamoja na Elizabeti mke wa Zakaria aliyemzaa Yohane mbatizaji. Ni somo linaloalika kutokukata tamaa kutenda mema hata tunapozungukwa na uovu. Thamani ya wema haiwezi kufunikwa na uovu. Itang’ara na daima italeta baraka za Mungu.

Somo la pili (Rum 6:3-4, 8-11) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili Paulo anaonesha muunganiko uliopo kati ya Kristo na yule anayebatizwa kwa jina lake. Kwa maneno mengine, Paulo anaandika kuonesha uhusiano uliopo kati ya Kristo na mkristo. Uhusiano huo ni kuwa kila anayebatizwa katika Kristo anabatizwa katika mauti ya Kristo. Kwa namna hii, ubatizo unakuwa ni ishara inayomuingiza mtu katika mauti ya Kristo ili kwamba kama vile Kristo alivyotoka katika mauti akafufuka basi na mkristo naye atoke katika mauti hayo aingie katika maisha mapya ya ufufuko. Hii inamaanisha kuwa ubatizo unakuwa ni mwaliko kwa mkristo kuyaacha maisha yake ya zamani na kuuvaa utu mpya ili kuyaanza maisha mapya ndani ya Kristo. Tunapoliangalia somo hili katika mwendelezo wa somo la kwanza, tendo lile la ukarimu na kumpokea mtumishi wa Bwana linapata maana nyingine kwa Kristo. Kumpokea Kristo kunakuwa ni kutafuta muungano kamili naye katika upya wa maisha yetu.

Injili (Mt 10:37-42) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo.  Yesu anawapa mitume wake mafundisho yanayohusu utume wanaokwenda kuufanya. Katika sehemu ya kwanza anawaambia yale ambayo mtume anapaswa kuyafanya na hali anayopaswa kuwa nayo ili aweze kutekeleza vema utume wake. Kwanza anawaagiza wasijishikamanishe na familia na kwa maana anayempenda baba au mama kuliko yeye hamstahili. Pili anawataka wawe tayari kuyakabili majukumu yao hata katika ugumu wake. Hapo anasema asiyeubeba vema msalaba wake hamstahili na mwisho anawaambia wasitangulize mbele maslahi yao binafsi kwa maana anayetafuta kuyaokoa zaidi maisha yake kwa gharama ya utume atayapoteza. Katika hatua ya pili Yesu anaielekea jumuiya ambayo kwayo Mitume wataenda kufanya utume wao.  Hao anawaagiza ukarimu ili wampokee mtumishi wa Bwana kama kumpokea Kristo mwenyewe. Anasisitiza kuwa anayempokea nabii atapata thawabu ya nabii na kila atakayemnywesha walau maji atapata thawabu yake.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dhamira inayotawala katika masomo ya dominika hii ni mwaliko wa kumpokea mtumishi wa Bwana. Mwaliko huu unabeba umaana wake katika msingi kuwa mtumishi wa Bwana ni nafsi hai ya Kristo mwenyewe ambaye amemtuma. Kwa jinsi hii anayempokea mtumishi wa Bwana anampokea Kristo mwenyewe. Tangu Agano la Kale, uwepo wa mtumishi wa Bwana katika jamii umefananishwa na uwepo wa sauti ya Mungu katika jamii hiyo. Mtumishi wa Bwana amekuwa daima ni kama dhamiri inayoielekeza jamii kumgeukia Mungu. Kumbe, kumpokea mtumishi wa Bwana kumekuwa sawa na kumpokea Mungu mwenyewe na kumkataa mtumishi wa Bwana kumekuwa sawa na kumkataa Mungu mwenyewe.

Tunapotafakari leo juu ya mwaliko huu tunaalikwa katika nafasi ya kwanza kukubali kuguswa na kubadilishwa na sauti ya mtumishi wa Bwana. Hii ina maana tusiizuie sauti hiyo kupaa wala tusiufishe uwepo wa sauti hiyo katika jamii. Ni sauti ya Mungu mwenyewe. Mtakatifu Yohane Maria Vianney aliwahi kusema ukimwondoa Padre katika jamii kwa miaka 20, basi watu wataanza kuabudu miti. Maneno hayo ni kweli hasa yakichukuliwa katika mantiki kuwa uwepo wa Padre ni kielelezo cha uwepo wa Kristo mwenyewe. Katika nafasi ya pili tunaalikwa kuwa wakarimu katika kuuwezesha utume wa mtumishi wa Bwana. Kuuwezesha utume nao ni utume.   Mwaliko huu wa leo, kwa namna ya pekee unatoa changamoto kubwa kwa mtumishi wa Bwana kujitahidi kuwa kweli kile anachokiwakilisha, yaani kuwa nafsi ya Kristo pale anapotoa utume wake ili sura ya Kristo ambaye anamuwakilisha isififishwe katika udhaifu wa mtumishi wake.

Liturujia J13 Mwaka A
26 June 2020, 13:50