Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIII ya Mwaka A wa Kanisa: Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa mashuhuda wa Imani kwa kristo Yesu na Kanisa lake. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIII ya Mwaka A wa Kanisa: Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa mashuhuda wa Imani kwa kristo Yesu na Kanisa lake. 

Tafakari Jumapili XIII: Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya Injili!

Yesu anatumia maneno makali kabisa kwa kila mmoja anayetaka kuwa mfuasi wake wa kweli. Anawaalika kumpenda zaidi Yeye kuliko baba, mama au watoto wake na kinyume chake basi huyo hastahili. Si kwamba Yesu anatualika kuwachukia wazazi au ndugu zetu la hasha ila basi wasiwe kikazwo kwetu katika safari ya ufuasi wetu. Kumbe, Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya utume!

Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.

Amani na Salama!Sehemu ya Injili ya leo, Jumapili ya XIII ya Mwaka A wa Kanisa ni hotuba ya pili ya Yesu kati ya hotuba zake tano katika Injili ya Mathayo na inayohusu juu ya kutumwa kwa wanafunzi wake. Na sehemu ya Injili ya leo inakamilisha hotuba hiyo ya Yesu juu ya utume wao wa kimisionari, wa kutoka na kwenda kuwa mashahidi wa Injili, mashahidi wa Habari Njema ya wokovu. Yesu anatumia maneno makali kabisa kwa kila mmoja anayetaka kuwa mfuasi wake wa kweli. Anawaalika kumpenda zaidi Yeye kuliko baba, mama au watoto wake na kinyume chake basi huyo hastahili. Si kwamba Yesu anatualika kuwachukia wazazi au watoto au ndugu zetu la hasha ila basi wasiwe kikazwo kwetu katika safari ya ufuasi wetu. Kila mfuasi wa Yesu anaitwa kujikatalia na kila mara kumpa nafasi ya kwanza Yesu. Kujitakatalia hata mahusiano yetu ya damu ikiwa ni kikwazo kwetu katika safari ya kuwa wafuasi wa Yesu na Injili yake. Tutaona japo kwa kifupi muktadha uliopelekea mpaka Yesu kutupa tahadhari hii kwa maneno makali na magumu si kwa wasikilizaji wake nyakati zile bali hata nasi kwetu leo.

Yesu anazidi kusema kuwa hakuja ulimwenguni kuleta amani bali kuleta upanga. (Mathayo 10:34). Ni lugha isiyokuwa rahisi kueleweka hata kwetu leo kwani Yesu tayari ameshahubiri kuwa  wana heri wale wanaokuwa wajumbe wa amani (Mathayo 5:9) na hata anatualika kuwapenda maadui zetu (Mathayo 6:44), hivyo haiwezekani Yesu awe anatuhamasisha nasi kuwa wavunjifu wa amani kwa kuwa watu wa mabavu au kulipiza kisasi au kuwaita watu kwake kwa upanga wa vita. Upanga anaouzungumzia Yesu hapa ni Neno lake, Ni ujumbe wa Injili. Unaokuwa na makali hivyo hata kuleta kutokuelewana na migawanyiko si tu katika jumuiya kubwa bali hata katika familia. Mwinjili Mathayo anaandika Injili yake wakati wa madhulumu na mateso ya Waamini Wakristo wa Kanisa lile la mwanzo. Wafuasi wa Kristo ili kubaki kweli wafuasi iliwabidi hata kukubali kutengwa si tu na masinagogi au wakuu wa dini ya kiyahudi bali hata na wazazi na ndugu na watoto wao. Marabi waliwatenga wale wote waliojulikana kuwa wafuasi wa Kristo Mfufuka, na walitengwa si tu wasishiriki katika ibada zao za Kiyahudi bali hata katika maisha ya kijamii na kisiasa na kibiashara, kiasi kwamba Myahudi anayeshika kweli dini yake hapaswi na hata ingempelekea kutengwa ikiwa atashirikiana na mkristo.

Wakristo si tu walitengwa katika majumba ya ibada bali hata na familia zao za damu, myahudi hakuruhusiwa si tu kununua kitu kutoka kwa mkristo bali hata kumuuzia kitu. Hivyo ni katika mazingira haya ya mateso na madhulumu makali kabisa Mwinjili Matayo anawaandikia wakristo wale wa kwanza kuwakumbusha maneno ya Kristo mwenyewe. Ni ujumbe ambao pia unatuhusu na kutugusa hata sisi wakristo wa miaka 2000 baada ya kifo na ufufuko wake Kristo. Yesu anawahimiza wanafunzi na wafuasi wake wanaopitia mateso na madhulumu kubaki waamini hata kama itawabidi kutengwa na baba, au mama, au watoto au jamii nzima. Mwanafunzi wa Yesu daima anasukumwa kwa nafasi ya kwanza ya upendo kwa Kristo na Neno lake. Yesu anatualika si tu kuwa tayari kupoteza mahusiano na mali au vitu bali kuwa tayari hata kuyatoa maisha yetu. Hivyo Msalaba unabaki ni ishara ya lazima kwa kila mmoja anayechagua kuwa mfuasi wa Injili ya Yesu Kristo. Kama vile Bwana na Mwalimu wetu alipitia njia ile ya mateso na kukataliwa basi hata nasi hatuna budi kuwa tayari kukataliwa na kutengwa na kuteswa kwa ajili ya Injili yake. Maisha ya kuwa mashahidi wa Injili daima ni maisha ya kujikatalia na kukubali kuubeba msalaba.

Sehemu ya pili ya Injili Yesu anawaahidia wale wote wanaowapokea wahubiri na mashuhuda wa Injili. Kwa kweli kuwapokea hapa Yesu hamaanishi zaidi juu ya kuwapa msaada wa mahitaji yao tu ya siku kwa siku bali kuwa tayari kuupokea ujumbe wake yaani Injili yake, Habari Njema ya wokovu. Ujumbe wa wafuasi wa Yesu si mwingine bali ni Injili ya Yesu Kristo, ambao ni Neno la Mungu. Na ndio Yesu anasema hata kitendo kidogo kabisa cha kumpa maji baridi mjumbe wa Habari Njema basi hicho ni kitendo cha thamani kubwa mbele ya Mungu kwani mmoja anakuwa amempokea mjumbe wa Mungu mwenyewe. Na ndio wajibu wa kila mmoja kuwategemeza na kuwasadia wale wanaotolea maisha yao kwa ajili ya Injili, na kuwa muhubiri wa Injili kamwe tusisukumwe na mali au vitu bali upendo usio na mashaka kwa Kristo na Kanisa lake, na ndio maana hata leo Kanisa Katoliki linaalika watumishi wake kwa maana ya makasisi na watawa kuishi maisha ya ufukara, kujitakalia kwa ajili ya Injili na Ufalme wa Mungu. Kabla ya mahitaji mengine yote ya kawaida yafaa tukumbuke kila mtangazaji au mhubiri wa Habari Njema ana uhitaji wa kuwa na kujisikia nyumbani kila mahali anapotumwa kueneza Habari Njema ya Wokovu na ndio mwaliko wa kumpa japo kikombe cha maji baridi, ni kumfanya awe mmoja wetu, ajisikia nyumbani pamoja na sisi, na kamwe tusiwafanye wajisikie wageni au watu wakuja tu bali mkristo anampokea kila mjumbe wa Mungu na kumfanya ajisikie nyumbani.

Kuwa nyumbani ndio kujisikia ndugu na jamaa ya watu wale wanaoshiriki naye imani moja, meza moja ya Neno na ya Ekaristi Takatifu. Ulimwengu mamboleo umekumbwa na changamoto kubwa ya kutokuwafanya wengine kujisikia nyumbani, sisi Wakristo wabatizwa hatuna budi kuwasaidia wengine kila mara wajisikie nyumbani iwe kwa upendo wetu na hata majitoleo yetu mbali mbali ya hali na mali. Ulimwengu leo unashuhudia ubaguzi wa kila aina iwe wa rangi, imani au dini, utaifa, ukabila, itikadi za kisiasa, ukanda, uwezo wa kiuchumi, nafasi zetu katika jamii mbali mbali, na kila aina ya ubaguzi tunaoweza kuufikiria au kukutana nao katika maisha, ubaguzi wa aina yeyote ile ni kinyume kabisa na Injili, hivyo ujumbe wa Injili ya leo unanialika mimi na weye kujivua iwe akilini iwe katika matendo au hulka zetu kila aina ya ubaguzi maana kwao unakuwa ni kikwazo kwa Injili na Habari Njema ya Wokovu. Kristo anatualika leo kuwa watangazaji na hasa mashahidi wa Habari Njema na pia anatupa wajibu wa kuwapokea wengine wanaofika kwetu kama wajumbe wa Habari Njema.

Habari Njema au Injili ya kwanza ni ya maisha yangu na yako, hivyo kabla hatujatoka kuhubiri hatuna budi sisi wenyewe kuwa Habari Njema, kuwa harufu nzuri ya Upendo wa Kristo kwa watu wote. Kristo anatualika kupenda sio tu wanaotupenda na kututakia mema bali hata wale wasiotupenda na kututakia mema, dunia leo inahitaji kutoka kwetu wakristo, sio kweli za mafundisho yetu mazuri na labda yenye ushawishi mzuri wa kifalsafa bali ushahidi wa maisha yetu kama wakristo. Watu wanapaswa kututambua kwa maisha yetu ya siku kwa siku. Niwatakie Dominika na tafakari njema.

24 June 2020, 13:28