Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 12 ya Mwaka A wa Kanisa: Msiogope kuwa Mashuhuda wa Injili ya Kristo! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 12 ya Mwaka A wa Kanisa: Msiogope kuwa Mashuhuda wa Injili ya Kristo! 

Tafakari Jumapili 12 ya Mwaka: Mashuhuda wa Injili ya Kristo!

Tangu mwanzo Yesu anawaonesha wanafunzi wake kuwa utume wa kuwa mashuhuda wake sio lelemama na unatutaka kujizatiti kwa hekima na busara itokayo kwa Mungu. Mwinjili Mathayo anaandika sehemu ya Injili ya leo mwanzoni mwa madhulumu ya Kaisari Domiciano, aliyetoa amri katika dola zima la Kirumi kuwekwe sanamu yenye sura yake na kuabudiwa kama mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Amani na Salama! Sehemu ya Injili ya leo ili kupata kuielewa vema inatanguliwa na Yesu akiwatuma mitume wake kumi na wawili na kuwapa tahadhari juu ya hatari zilizopo mbele yao, na hivyo kuenenda kwa hekima na busara lakini zaidi sana kudumu katika ujasiri. Tangu mwanzo Yesu anawaonesha wanafunzi wake na hata nasi leo kuwa utume wa kuwa mashahidi wake sio lelemama na unatutaka kujizatiti kwa hekima na busara itokayo kwa Mungu. Mwinjili Mathayo anaandika sehemu ya Injili ya leo wakati wakristo wale wa mwanzo wanapitia madhulumu ya Kaisari Domiciano, aliyetoa amri katika dola zima la kirumi kuwekwe sanamu yenye sura yake na kuabudiwa kama mungu. Hivyo wale wote waliokataa kuabudu sanamu ile waliteswa na hata kuuawa kwa amri ya mtawala yule wa kirumi. Hivyo madhulumu ya kwanza yalitoka kwa watawala wa kirumi na hasa Kaisari. Pia wakristo wa mwanzo waliokuwa wenye asili ya Kiyahudi walitengwa katika masinagogi kwa kuwa ni wafuasi wa Kristo Mfufuka.

Hivyo ni katika muktadha huo Mwinjili anaandika sehemu ya Injili ya leo kuwafariji na zaidi kuwakumbusha maneno ya Kristo mwenyewe wakati alipokuwa nao, maana sasa tunazungumzia kizazi cha pili cha Kanisa, na wengi hawakumuona Yesu uso kwa uso zaidi ya kupokea Habari Njema kutoka kwa mitume wake. Ni Kanisa teswa lililokuwa likiishi imani yake kwa hofu na kujificha huku wakigubikwa na hofu kubwa kutoka maadui wao wakubwa wawili ambao ni dola la utawala wa kirumi na wakuu wa masinagogi au wakuu wa dini ya kiyahudi. Mwinjili anawakumbusha Wakristo wale wa kwanza kuwa tayari Bwana na Mwalimu wao alishawatabiria juu ya magumu, mateso na madhulumu, hivyo sio kitu kigeni na hawapaswi kukata tamaa wala kurudi nyuma katika safari yao ya ufuasi na kuwa mashahidi wa Habari Njema ya ukombozi. Tunaona pia Mtume Paulo anapomwandikia kijana na mwanafunzi wake Timoteo anasema; ‘’Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe’’. (2 Timoteo 3:12). Mtume Paulo anaandika naye kipindi kile kile cha madhulumu na mateso ya Kanisa lile la mwanzo akimsihi Timoteo kuwa imara katika imani na pia wale wote waliokuwa watu wa njia yaani Wakristo.

Ni katika mazingira hayo ya mateso na madhulumu tunaona Yesu anawaalika wanafunzi wake kutoogopa, kutokukubali kurudi nyuma kwa sababu ya uoga na hofu. Tunasikia Yesu akiwaalika mara tatu ‘msiogope’. Uoga unaweza kuwa na upande chanya kututahadharisha na hatari inayokuwa mbele yetu na hivyo kuenenda kwa tahadhari lakini pia una upande hasi hasa pale tunapojiachia kutawaliwa na uoga na hofu. Kila tunaporuhusu uoga ututawale hapo tunakosa uhai na maisha, tunakosa pumzi na uwezo wa kuishi au wa kusonga mbele katika wito na utume wetu. Uoga ni adui wa uhai ndani mwetu. Wafuasi wa Kristo Mfufuka kutangaza na kushuhudia Neno lake kwenye nuru na juu ya nyumba, ndio kusema bila uoga wala hofu ili ulimwengu wote upate Habari Njema ya Wokovu. Ni wito wa kuwa majasiri katika kuishi imani yetu bila kificho wala uoga na katika hali zote iwe rafiki au hata pale tunaposongwa na hatari hata ikiwa ya kifo. Uoga ni adui mkubwa katika maisha yetu ya ufuasi. Tunakuwa waoga kupoteza nafasi zetu za heshima kwa kuwa tu wafuasi wa Yesu Kristo, kupoteza marafiki zetu, kupoteza mali na utajiri wa dunia hii, kudharauliwa na wengine, na mara nyingine hata kupoteza maisha yetu. Kila anayeruhusu kutawaliwa na uoga huyo anapoteza uhuru wa kweli. Anakuwa sawa na mmoja mwenye ugonjwa wa kiharusi kwa kukubali kutawaliwa na uoga. Uoga unasababisha kifo cha kiroho.

Na ndio maana Yesu anarudia mara tatu nzima ili kututahadharidha na hatari ya uoga katika maisha ya ufuasi. Kila mfuasi wa Yesu Kristo Mfufuka anaalikwa kutoogopa bali daima kujitegemeza kwa Kristo Mwenyewe katika maisha ya ufuasi na katika kuwa mashahidi wa Habari Njema ya Wokovu. Anayepelekwa kutangaza Habari Njema anaweza kutawaliwa na uoga wa kushindwa katika utume yake. Na ndio maana Yesu anatukumbusha kuwa hata kama tutakutana na magumu daima Injili yake itaenea na kusambaa ulimwenguni kote. Yesu kwa kutuhakikishia hilo anafanya marejeleo kwa marabi wa nyakati zake ambao walibaki na wanafunzi wao na kuwafundisha sirini mpaka pale mmoja alipohitimu ndipo aliruhusiwa kwenda kufundisha katika viwanja na masinagogi. Ndio kusema Yesu anatusisitizia hata pale tunapoona kwamba kazi yetu haina mafanikio makubwa kwa macho na mitazamo yetu ya kibinadamu, hakika bado Neno lake litazaa matunda ni kama vile mbegu iliyozikwa ardhini. Mfano wa wazi ni watesi wa Yesu mwenyewe mara baada ya kumuua na kumzika na kuweka jiwe kubwa katika mlango wa kaburi walijiridhisha na kujihakikishia kuwa sasa wameshinda na kufaulu kumnyamazisha mtu yule kutoka Galilaya. Siku ya tatu akafufuka na kuwa mzima tena! Amefufuka kama mbegu iliyokuwa imezikwa ardhini na sasa imechipua na kuleta matumaini na mwanga mpya.

Sababu ya pili inayoweza kutulewesha uoga na hofu ni madhulumu na mateso na hata kifo. Na ndio Yesu pia anatuhakikishia kuwa hakuna ushindi wowote unaoweza kupatikana kwa wale wanaotesa mwili kwani kila anayekuwa tayari na jasiri kumfuasa Yesu na kuwa shahidi wa Injili huyo anajaliwa uzima wa milele, maisha ya kweli sasa na hata milele. Kila mfuasi wa kweli huyo anapokea sio tu maisha ya kibailojia bali maisha ya muunganiko na Mungu mwenyewe, hivyo ni maisha ya hapa duniani na ya milele yote. Mtume Paulo anapowaandikia Warumi anawakumbusha pia ukweli huo; ‘’Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo?’’. (Warumi 8:35-39). Lakini anaendelea Yesu na kututahadharisha kumuogopa mmoja anayeangamiza si mwili tu bali pamoja na roho. Kwa kweli tafsiri sahihi sio kitu kinachokuwa nje yetu bali kila mmoja wetu anacho ndani mwake tangu kuzaliwa kwetu, ndio nguvu ile ya muovu inayotuambia kila mara kuenenda kinyume na njia na mipango yake Yesu Kristo. Kila wazo linalopinga mpango mzima wa Yesu huwa linapelekea katika angamio langu na lako kwani tunaangamia si tu mwili bali pamoja na roho. Kila mmoja wetu anajua ni nini katika maisha yake kinamkinza katika kuiishi na kuwa shahidi wa Injili, na tukichunguza tunaona jambo au kitu hicho asili yake ni ndani mwetu.

Leo dunia nzima tumekumbwa na hofu na uoga mkubwa juu ya janga na hatari ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni haki kabisa ila Injili leo inatukumbusha kuogopa kirusi kinachoshambulia roho zetu, ndio kirusi cha chuki, wivu, ubinafsi, ubaguzi, uchoyo, masengenyo na yote mabaya yanayotutenga na Mungu na jirani. Injili inatualika kuwa karibu na Mungu na jirani. Kirusi cha hatari ni kile kinachoniweka mbali na Mungu na jirani, ndio kile kinachoangamiza si tu mwili bali na roho pia. Kama tunavyochukua tahadhari kupata maambukizi ya Corona, COVID-19, basi pia tuchukue tahadhari kubwa zaidi dhidi ya kirusi cha kiroho. Sababu ya tatu inayotuepelekea kuogopa sasa inagusa si tu sisi bali hata na wale wanaokuwa karibu nasi. Na ni hapo Yesu anatuhahakishia ulinzi wa Mungu Baba kwani sote tu wa thamani kubwa mbele yake. Anatumia mifano ya shomoro na nywele. Shomoro kwa nyakati za Yesu walihesabiwa kuwa ni viumbe wadogo na wasio na thamani kwani pia walikuwa ni ndege waharibifu kwa mazao na hasa ngano ikiwa bado shambani.

Hivyo Wayahudi walipowabariki viumbe vyote vya Mungu hawakuwabariki shomoro kwani ni waharibifu, ila leo Yesu anatuonesha kuwa mbele ya Mungu kila kiumbe kina thamani kubwa, hivyo kutuhakikishia kuwa hatuna sababu ya kuwa na uoga wala hofu hata kama mbele yetu kuna mateso na madhulumu makubwa. Mungu anajua hata hesabu ya unywele mmoja, vile sisi hatuwezi kuhesabu nywele lakini mbele ya Mungu sisi sote kama viumbe vyake tu wa thamani kubwa. Yesu anamalizia kwa ahadi kuwa kila anayemkiri mbele ya watu huyo atamkiri mbele za Baba yake wa Mbinguni. Ni hakika kuwa tunatambuliwa na Mungu hata sisi tukiwa kweli wafuasi wa kweli wa Kristo bila kujali hatari zinazoweza kutukabili na hata kutuzuia kuwa mashahidi, daima mfuasi hana budi kumtegemea Mungu katika kila hali za maisha ya ufuasi. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

19 June 2020, 13:59