Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linasema kwamba, Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao; lakini hata hivyo kuna mambo msingi yamekuwa ni ya manufaa kwa wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linasema kwamba, Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao; lakini hata hivyo kuna mambo msingi yamekuwa ni ya manufaa kwa wengi.  (AFP or licensors)

Mang'amuzi Kuhusu COVID-19: Madhara na Uzuri wake?

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linakiri kwamba, kipindi cha watu kuwekwa karantini kimejenga na kuimarisha moyo wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; hali ambayo pia imegusa familia kubwa ya binadamu. Watu wamegundua kwamba, wanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtu anayeweza kujimwambafai kwamba, anajitegemea kwa kila jambo. COVID-19?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba, homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID- 19 kuwa ni Janga la dunia. Jumuiya ya Kimataifa na Serikali mbali mbali zimechukua hatua za kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huu ikiwemo kufunga shule na vyuo, kutoa elimu na kuhamasisha jamii kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwa kuepuka kukaa kwenye misongamano ya watu, kunawa mikono mara kwa mara, na pia, kuanzisha namba maalumu za kupiga ili kutoa taarifa za watu wanaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo au kupata taarifa sahihi juu ya ugonjwa huu wa COVID-19. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, hivi karibuni aliwaalika viongozi wa dini mbali mbali nchini Ufaransa kutoa mawazo yao kuhusu yale mambo msingi ambayo familia ya Mungu nchini Ufaransa imeweza kuyang’amua kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linakiri kwamba, kipindi cha watu kuwekwa karantini kimejenga na kuimarisha moyo wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; hali ambayo pia imegusa familia kubwa ya binadamu. Watu wamegundua kwamba, wanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtu anayeweza kujimwambafai kwamba, anajitegemea kwa kila jambo. Mawazo ya viongozi mbali mbali wa kidini nchini Ufaransa yamechapishwa na kuwekwa kwenye mfumo wa kitabu ambacho kimegawanyika katika sura kuu nne: Kumbukumbu! Mwili! Uhuru! Na Ukarimu! Katika kipindi cha Karantini, watu wamejitahidi kuishi kwa amani na utulivu. Silaha za vita zilikoma, Jumuiya ya Kimataifa ikajielekeza katika mapambano dhidi ya janga la Corona, COVID-19. Pengine, watu wanajiandaa kwa ajili ya vita ya biashara na uchumi. Amani na utulivu katika kipindi cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, ni chemchemi ya imani na matumaini kwa familia ya Mungu katika ujumla wake.

Familia ya Mungu nchini Ufaransa inayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa sababu katika miaka ya hivi karibuni, Ufaransa imekuwa ni nchi ambayo imeogelea sana kwenye machafuko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, kiasi hata cha kuhatarisha mafungamano ya kijamii na umoja wa kitaifa. Kwa waamini umoja na mshikamano ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga kila wakati. Uchu wa mali, fedha na madaraka pamoja na tabia ya baadhi ya watu kutaka kujimwambafai ni kati ya mambo ambayo yanapelekea: kinzani, mipasuko na mashindano ya kibiashara, kiuchumi na hata kivita. Lakini, ikumbukwe kwamba, mwanadamu anahitaji maendeleo fungamani yanayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, amani, ikipewa kipaumbele cha kwanza kwani hili ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Huduma ya upendo na mshikamano; sadaka na majitoleo kwa jirani ni kati ya tunu msingi ambazo watu wa Mungu katika ngazi mbali mbali wanapaswa kuziendeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 yamejitokeza na kusambaa kwa haraka kama “moto wa mabua”. Hii ni fursa ya kutafakari tena na tena kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, watu wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kumbe, wimbi hili la wakimbizi na wahamiaji linapaswa kushughulikiwa na Jumuiya ya Kimataifa, ikiwa imeungana kwa kutambua kwamba, binadamu wanategemeana na kukamilishana! Kipindi cha karantini, rasilimali muda ilionekana kuwa haina faida kwa watu wa Mungu waliokuwa wamefungiwa ndani “utadhani utumbo”. Lakini hiki ni kipindi ambacho watu wengi wamekaa nyumbani kwa utulivu na amani ya ndani, bila kukimbizana na shughuli za kila siku. Watu wameshiriki kazi mbali mbali za nyumbani bila hata ya wao wenyewe kutambua mchango wao. Kumekuwepo pia na uchafuzi kidogo wa mazingira kutokana na uzalishaji mdogo wa hewa ya ukaa. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linabainisha kwamba, maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 imekuwa ni fursa ya kugundua udhaifu mkubwa ulioko kwenye sekta ya afya hasa kuhusiana na rasilimali watu, miundo mbinu, dawa na vifaa tiba.

Kuna uhusiano na mshikamano mkubwa kati ya madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na viongozi wa huduma ya maisha ya kiroho hospitalini. Kila mtu anamshughulikia binadamu mkamilifu: roho na mwili. Kuna haja ya kuwa na majiundo endelevu yatakayowasaidia wadau katika sekta ya afya kujiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na majanga kama haya kwa siku za usoni. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kujizatiti katika malezi na majiundo makini kwa viongozi wa maisha ya kiroho pamoja na waamini walei, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika sekta ya afya. Jambo la msingi ni kuwasindikiza wagonjwa hatua kwa hatua ili kukabiliana na fumbo la kifo, kwa imani na matumaini juu ya maisha na uzima wa milele. Huruma na upendo kwa wagonjwa ni dawa muhimu sana inayoweza kuwaondolea wagonjwa upweke hasi, kwa kutambua kwamba, licha ya ugonjwa na hali yao tete, lakini bado wanapendwa na kuthaminiwa na jamii.

Kuna haja kwa familia ya Mungu kuweka siku ya kumbukumbu ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, ili watu wasijisahau na kuanza kuishi tena kwa mazoea na kusahau majanga makubwa yaliyosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna haja ya kuwekeza zaidi katika miundo mbinu, ili kuboresha makazi ya watu. Kwa hakika muda wa mapumziko unapaswa kutumiwa kikamilifu.

Ufaransa: Corona
12 June 2020, 10:53