Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe wake wa Pentekoste kwa Mwaka 2020 linakazia: Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa na Mang'amuzi ya pamoja! Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe wake wa Pentekoste kwa Mwaka 2020 linakazia: Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa na Mang'amuzi ya pamoja! 

Maaskofu Hispania: Dhana ya Sinodi na Mang'amuzi ya Pamoja!

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2020, linawaalika watu wa Mungu nchini Hispania, kuendelea kushikamana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujizatiti katika mambo makuu mawili: “Dhana ya Sinodi na Mang’amuzi ya pamoja”. Ni wakati wa kupyaisha maazimio ya mkutano mkuu wa Halmashauri Walei!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linamwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika maisha na utume wake, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ndicho kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Mambo ya kuzingatia ni: Ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kupyaisha na kuendeleza ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Maadhimisho ya Sinodi ni mchakato wa Kanisa kutembea kwa pamoja kama sehemu ya utekelezaji wa utume na dhamana ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko.

Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, na linaihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Sinodi ndani ya Kanisa Katoliki, alilitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2020, linawaalika watu wa Mungu nchini Hispania, kuendelea kushikamana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujizatiti katika mambo makuu mawili: “Dhana ya Sinodi na Mang’amuzi ya pamoja”. Huu ni wakati muafaka wa kumwilisha Sherehe ya Pentekoste iliyopyaishwa mintarafu maazimio ya Mkutano Mkuu wa Halmashauri Walei nchini Hispania, uliofanyika mwezi Februari, 2020. Dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa kwa namna ya pekee, ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kanisa linabainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Waamini walei ni wadau pia katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Waamini walei wanapaswa kupandikiza mbegu hii katika maisha na utume wao, chini ya mwongozo wa Roho Mtakatifu. Umoja na mshikamano ni tunu msingi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji. Kanisa linapaswa kuendelea kutoa majiundo makini kwa waamini walei, ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Ni mwaliko wa kuzingatia umoja katika utofauti wake na kwamba, kila mtu anayo nafasi ya kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni mchakato unaopania kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari kwa kuishirikisha kikamilifu familia ya Mungu. Waamini wanategemeana na kukamilishana ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Kutokana na janga la maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, Jumuiya ya Kimataifa imegundua na kukiri umuhimu wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa upendo kwamba, hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba, anaweza kujitosheleza kwa kila jambo. Waamini wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuimarisha Jumuiya za Kikristo ili kweli ziwe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Huu ni wakati wa kuendelea kushikamana, ili kufanya mang’amuzi ya pamoja, ili kujitahidi kufahamiana na kuelewana. Kanisa halina budi kuwa ni chombo cha wokovu, imani na matumaini, kwa watu wa Mungu nchini Hispania, watu ambao kwa hakika wameguswa na kutikiswa sana na ugonjwa wa Corana, COVID-19.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, linasema, Mkutano Mkuu wa Halmashauri Walei, uliofanyika mjini Madrid, kuanzia tarehe 14-16 Februari 2020, ni tukio ambalo liliandaliwa kwa muda wa miaka miwili. Hili ni kati ya matukio muhimu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Hispania katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Hapa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ilijidhihirisha. Watu wa Mungu wakafanikiwa kuchangia: mawazo, maoni, tafakari na sala zao, huku wakionesha umoja na tofauti msingi, lakini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake.Huu ni wakati wa kuendelea kutekeleza maazimio ya Mkutano Mkuu wa Halmashauri Walei, kwa kujikita katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei wagundue ndani mwao umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo, inayowashirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu katika maisha yao. Sakramenti ya Ubatizo ni chemchemi ya karama mbali mbali kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mwendelezo wa utume wa Kanisa.

Maaskofu Hispania: Dhana ya Sinodi na Mang'amuzi ya Pamoja

 

 

04 June 2020, 13:09