Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu la Mbeya nchini Tanzania amewataka watanzania kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa licha ya tofauti zao msingi Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu la Mbeya nchini Tanzania amewataka watanzania kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa licha ya tofauti zao msingi  (AFP or licensors)

Askofu mkuu Nyaisonga: Dumisheni, umoja na mshikamano wa kitaifa

Askofu mkuu Nyaisonga asema: Umoja, amani na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa watanzania ni tunu ambayo imeleta mvuto sana kwa mataifa mbali mbali duniani. Mwalimu Nyerere ni kiongozi aliyejitahidi sana kutumia karama na mapaji aliyokuwa amekirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeeo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Na Thompson Mpanji, - Mbeya na Padre Richard A. Mjigwa, Vatican.

Sherehe ya Pentekoste ni adhimisho llinalohitimisha kipindi cha Pasaka ya Kristo Yesu kwa kumminina Roho Mtakatifu anayewakirimia waamini nguvu na jeuri ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Ni siku ya kutafakari juu ya uwepo endelevu wa Roho Mtakatìfu katika maisha na utume wa Kanisa. Sherehe hii imekuwa ni fursa kwa waamini kuomba Mapaji saba ya Roho Mtakatifu pamoja na matunda ya Roho Mtakatifu ili kukuza na kudumisha umoja wa familia ya Mungu inayowajibika. Kwa waamini wa Jimbo kuu la Mbeya nchini Tanzania, Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2020 imekuwa ni fursa ya kutafakari umoja na mshikamano wa watanzania pamoja na kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie hekima, umoja na amani na aendelee pia kuwasaidia kudumisha uhuru na umoja. Huu ni utajiri na urithi mkubwa kutoka kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Muasisi wa Taifa la Tanzania. Ni kiongozi aliyejipambanua katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuyaunganisha makabila zaidi ya 100 yaliyoko nchini Tanzania na hivyo kuweza kuzungumza lugha moja ya Kiswahili.

Mwalimu Nyerere, alijitahidi kuhakikisha kwamba, watanzania hata katika tofauti zao msingi, wanaungana na kuwa wamoja. Umoja, amani na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa watanzania ni tunu ambayo imeleta mvuto sana kwa mataifa mbali mbali duniani. Mwalimu Nyerere ni kiongozi aliyejitahidi sana kutumia karama na mapaji aliyokuwa amekirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeeo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, iliyofanyika kwenye Kanisa la Roho Mtakatifu, Parokia ya Ruanda, Jimbo kuu la Mbeya. Umoja, mshikamano na ujasiri, uliwawezesha Mitume kujitokeza hadharani na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Sherehe hii ya Pentekoste ya Wayahudi ilikuwa imesheheni: mahujaji, watalii na wageni kutoka pande mbali mbali za dunia. Lakini Mitume wa Yesu walipokuwa wanatangaza Habari Njema ya Wokovu, kila mtu aliwasikia kwa lugha yake mwenyewe, matendo makuu ya Mungu.

Hii ndiyo ahadi ya Baba wa milele na nguvu ya Mungu iliyowawezesha waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hata waamini katika ulimwengu mamboleo wanapaswa kumwita Roho Mtakatifu ili aweze kuwaangaza kutoka mbingu, na kuwakirimia mapaji yake saba! Aweze kuwafariji na kuwajalia pumziko, afute machozi na kuwajaza waamini mwanga wenyeheri na neema mioyoni mwao. Aoshe machafuko, anyeshee pakavu na kuponya majeraha. Alegeze ukaidi, awashe moto wa uadilifu na kunyoosha upotovu wa waamini wake. Roho Mtakatifu awajalie waamini Mapaji yake saba na hatimaye, awajalie heri ya milele! Askofu mkuu Nyaisonga amesema haisaidii kwa waamini kunena kwa lugha ikiwa ndani mwao wamegubikwa na chuki, choyo, wivu, uhasama, masengenyo na matukano. Kunena kwa lugha hakuna mashiko, ikiwa kama waamini wamejaa rushwa, wizi, unyang’anyi, ukaidi na mambo kama haya!

Waamini wanaalikwa na kuhimizwa kujichimbia katika maongozi ya Roho Mtakatifu ili awafunde somo la upendo, imani na matumaini. Watu waliweza kusikia Mitume wa kinena katika lugha zao, yaani waliweza kuonja upendo katika maisha yao! Askofu Nyaisonga anawahimiza waamini kuendelea kumwilisha imani katika matendo kwa kuwasaidia waathirika wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Ifuatayo ni Senkwensia ya Roho Mtakatifu kadiri ya Mapokeo ya Kanisa!

1.      Uje Roho Mtakatifu, tuangaze toka mbingu, Roho zetu kwa mwangao

2.      Uje Baba wa maskini, uje mtoa wa vipaji, Uje mwanga wa mioyo

3.      Ee Mfariji mwema sana, ee rafiki mwanana, Ewe raha mustarehe

4.      Kwenye kazi u pumziko, kwenye joto, burudiko, U mfutaji wa machozi

5.      Ewe mwanga wenye heri, uwajaze waamini, Neema yako mioyoni

6.      Bila nguvu yako wewe, mwanadamu hana kitu, Kwake yote yana kosa

7.      Osha machafuko yetu, panyeshee pakavu petu, Na kuponya majeraha

8.      Ulegeze ukaidi, washa moto wa uadili, Nyoosha upotevu wote

9.      Wape waumini wako, wenye tumaini kwako, Paji zako zote saba

10.    Wape tuzo ya fadhila, wape mwisho bila hila, Wape heri ya milele

Amina aleluya, amina aleluya, Amina aleluya.

Askofu Mkuu Nyaisonga: Pentekoste 2020
04 June 2020, 13:24