Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili V ya Kipindi cha Pasaka: Mkazo wa pekee: Sala! Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Injili ya Upendo: Yesu ni njia, ukweli na uzima, ufunuo wa upendo wa Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili V ya Kipindi cha Pasaka: Mkazo wa pekee: Sala! Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Injili ya Upendo: Yesu ni njia, ukweli na uzima, ufunuo wa upendo wa Mungu. 

Jumapili V ya Pasaka: Sala! Neno! Sakramenti na Huduma!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka inakazia: Umuhimu wa maisha ya Sala, Utangazaji na Ushuhuda wa Neno la Mungu; Sakramenti za Kanisa kama chemchemi ya neema ya Mungu; Injili ya huduma inayomwilishwa katika matendo ya kiroho na kimwili; Umoja na mshikamano wa watu wa Mungu katika maisha ya utume wa Kanisa! Wazo la dhana ya Sinodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni, mwanadamu amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Pasaka ni kiini cha imani na zawadi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni kielelezo cha mshikamano na mafungamano kati ya binadamu na kazi nzima ya uumbaji kwa njia ya Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Mawazo makuu yanayoongoza tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka ni kwamba, Kristo Yesu amejifunua kuwa ni njia, ukweli na uzima, kumbe ni wajibu wa kila mwamini kujibidiisha kumfahamu, kumpenda, kumshuhudia na kumtangaza kwa njia ya maisha. Shida na changamoto za maisha na utume wa Kanisa, ziwasaidie waamini kujikita zaidi katika kunafsisha Injili ya huduma kwa watu wa Mungu kama sehemu muhimu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na mapaji mbali mbali mbali ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake.

Kwa njia hii, waamini katika ujumla wao watashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kanisa linajengwa kwa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Katika mchakato wa maisha ya Kipasaka, Jumuiya ya kwanza ya Wakristo inawachagua Mashemasi saba, alama ya utimilifu kwa ajili ya huduma ya upendo ili kukoleza mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Kipaumbele cha kwanza ni huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hili ni kundi la watu wasiokuwa na mtetezi! Katika Jumuiya hii ya kwanza, Mitume wa Yesu wanatoa msukumo wa pekee katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa njia ya sala na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Kwa maneno machache katika mazingira yetu, Mapadre wanayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, waamini walei wanashirikishwa huduma za Kristo Yesu: Kuhani, Nabii na Mfalme katika utume wa watu wa Mungu na wanautimiza mintarafu hali na mazingira yao katika Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Kwa kuyashughulikia malimwengu, humshuhudia Kristo Yesu kwa wazi zaidi na hivyo kusaidia mchakato wa wokovu wa roho za watu. Kimsingi, waamini walei wanapaswa kuwa ni chachu ya kuyachachua malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha unaopata chimbuko lake katika Sakramenti za Kanisa. Wao wamewekwa wakfu ili kufanywa ukuhani wa kifalme wa taifa takatifu ili watoe dhabihu za maisha ya kiroho kwa njia ya utendaji na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini wanapaswa kutekeleza dhamana na utume huu katika imani, matumaini na mapendo, ambavyo Roho Mtakatifu hueneza mioyoni mwa watoto wa Kanisa.

Lengo la Utume wa Kanisa ni wokovu wa wanadamu unaofumbatwa katika imani kwa Kristo Yesu na neema yake. Kumbe, waamini walei waendelee kujikita zaidi katika uinjilishaji sanjari na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Wanapaswa kupenyeza roho ya Kikristo katika mpango wa malimwengu na hasa kwa njia ya matendo ya huruma yanayopewa kipaumbele cha kwanza katika Somo la kwanza, kwa Kanisa la Mwanzo kuwachagua Mashemasi wema, wenye hekima na busara ili wawe ni wahudumu wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Katika umoja, upendo na mshikamano kati ya Mapadre na waamini walei, hapa tunaanza kupata wazo la dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto changamani inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama njia ya kusoma alama za nyakati!

Waraka wa Mtume Paulo kwa Watu wote, unatukumbusha kwamba, Kristo Yesu ndiye Jiwe kuu la pembeni, teule na lenye heshima. Maisha ya Kikristo ni sehemu ya mchakato wa upendo wa Kristo Yesu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Ufuasi wa Kristo ni zawadi inayowaunganisha waamini wote ili kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Kwa wale wote wanaomwamini, Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu na maisha ya uzima wa milele; ni kikolezo cha furaha, amani na utulivu wa ndani. Lakini kwa wale wasioamini ni jiwe la kujikwaa mguu na mwamba wa kuangusha. Kumbe, kila mwamini anapaswa kuwa na ushiriki mkamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani kwa njia ya ushuhuda! Katika shida, magumu na changamoto za maisha, waamini waendelee kushikamana kwa dhati!

Janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 linaweza kuligawa na kulichafua Kanisa kutokana na: ukame wa maisha ya kiroho sanjari na misimamo ya viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao! Kamwe, waamini wasikubali kupepetwa na kugalagazwa katika janga hili, bali wawe na ujasiri wa kusimama kidete na kumwendea Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Ni daraja kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kimsingi huu ni muhtasari wa imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kristo Yesu, amewahakikishia waja wake mahali salama na nafasi kwenye makao ya mbinguni, lakini hatuna budi kujibidiisha ili tuweze kufika huko, ili kushiriki maisha ya uzima wa milele. Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu wetu, kumbe, tunapaswa kumwendea kwa imani, matumaini na mapendo!

Kimsingi, Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa linajengwa kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa zinazotekelezwa na Mapadre kwa njia ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kanisa linatangaza, linashuhudia na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha, karama na tunu msingi za maisha ya waamini walei. Kumbe, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana katika kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa.

Tafakari J5 Pasaka

 

08 May 2020, 06:45