Tafuta

Pentekoste 2020: Miaka 317 ya Maisha na Utume wa Shirika la Roho Mtakatifu, C.S.Sp., ndani ya Kanisa! Pentekoste 2020: Miaka 317 ya Maisha na Utume wa Shirika la Roho Mtakatifu, C.S.Sp., ndani ya Kanisa! 

Miaka 317 ya Maisha na Utume wa Shirika la Roho Mtakatifu

Claude P. Des Places aliasisi Shirika la Roho Mtakatifu tarehe 27 Mei 1703, Sherehe ya Pentekoste. Ni siku ya kuihuhisha karama ya Shirika ili iendane na mahitaji ya uinjilishaji kwa wakati wa sasa na kuwapa wanashirika moyo na ari mpya ya kuwa mwanga na ufunuo wa Uso wa Kristo, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Pentekoste ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Joseph Shio, C.S.Sp. – Roma.

Shirika la Roho Mtakatifu (Holy Ghost Fathers and Brothers) liliasisiwa na Kijana Claude Poullart Des Places (miaka 24), kule Rennes, Ufaransa, mnamo tarehe 27 Mei 1703, Sherehe ya Pentekoste. Tokea wakati huo, Pentekoste imekuwa ni siku ya kipekee kwa Shirika kuadhimisha kuanzishwa kwake; pia ni siku ya kuihuhisha karama ya Shirika ili iendane na mahitaji ya uinjilishaji kwa wakati wa sasa na kuwapa wanashirika moyo na ari mpya ya kuwa mwanga na ufunuo wa Uso wa Kristo, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Pentekoste ni Sherehe muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni adhimisho la zawadi ya kipekee sana ya Yesu kwa Kanisa na kwa kila mbatizwa. Kwa hiyo, leo kimsingi tunaadhimisha kuzaliwa kwa Kanisa na kuwekwa kwake wakfu kwa njia ya Roho wa Mungu. Kama tunavyosoma kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume: 2:1-11. Ni siku ile ya Pentekoste ya kwanza kule Yerusalem Kanisa lilizaliwa wakati wafuasi wa Yesu waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu, jambo lisilo la kwaida, lilitokea pale upepo wa nguvu ulipovuma, wafuasi wakaona ndimi za moto juu yao, milango ya nyumba walimokuwamo ikafunguka, wakavuviwa Roho Mtakatifu. Na mara uwoga wao ukaisha na wakaanza mara kunena kwa lugha mbalimbali kama walivojaliwa na Roho Mtakatifu.

Wafuasi wale walipata ujasiri, wakaimarika na chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu, wakajikita na kuzama katika kazi ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Waliweza kumshuhudia Kristo katika mazingira yote na tamaduni mbali mbali. Kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi kwa kwanza, sisi nasi tunahitaji kutambua kuwa hii nguvu ya Roho Mtakatifu tunayo. Roho Mtakatifu anatupatia ujasiri wa kuiendeleza duniani kote kazi ya uinjilishaji aliotuachia Kristo Yesu (missio ad gentes).  Na hasa katika kipindi hiki cha janga la maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Janga hili limetikisa mihimili yote ya kijamii, likiwemo kanisa. Tumeshuhudia hofu kama waliokuwa nayo Mitume wa Yesu, kabla ya Pentekoste ya kwanza ikiikumba dunia. Tumeshuhudia mamlaka za nchi zikihaha kama wakati wowote wa vita, watu wakapoteza uhuru wa kutoka, mikusanyiko na ibada za pamoja vikasitishwa kwa muda. Shughuli mbalimbali za watu na safari zikavurugika, mipaka ikafungwa, giza nene la mauti likatanda, mahusiano yaliozoeleka kati ya watu na hata kati ya mataifa yakabadilika ghafla “bin vu”! Miji mikubwa duniani ikatawaliwa na ukimya na utupu ambao haujawahi kuwepo.

Wakati huu wa janga la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 Kanisa lilibidi kubuni njia mbadala za kuweza kuwafikia waamini ili kutoa huduma za kiroho kwa watu wote. Ulikuwa pia ni wakati wa pekee kwa waamini kujitafakari, kuomba na kupokea nguvu na ari mpya ya kumtangaza na kumtolea Kristo ushuhuda katika ulimwengu mamboleo na uliogawanyika kutokana na tofauti za rangi, tamaduni, imani, kisiasa na kichumi.  Imekuwa ni desturi nzuri kila mwaka kwa Sherehe ya Pentekoste kutanguliwa na novena ya Roho Mtakatifu. Sote wabatizwa tuko kwenye “upper room” tukisali pamoja na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Mitume waliokusanywa pamoja kutokana na urafiki wao na Kristo Yesu, tukiomba mapaji ya Roho Mtakatifu. Huu ulikuwa ni wakati wa kujitathimini ni jinsi gani tumekuwa waaminifu katika wito wetu wa kumtangaza na kumtolea Kristo Yesu ushuhuda na kupafanya papya pale penye dosari. Basi, katika Sherehe ya Pentekoste tunamwomba Mungu atuondolee hofu na vikwazo vingine vyote: atujalie ndimi mpya za kunena na kuitolea Injili ushuhuda, ubunifu wa kuwa washiriki hai katika kazi yake ya kuufanya upya uso wa dunia, kuhubiri Injili kwa uaminifu katika mazingira ya sasa ya utandawazi, kumtolea Kristo ushuhuda kwa kuwapenda na kuwahudumia watu wote na hasa wale waliopembezoni mwa jamii, hasa maskini.

Mtume Paulo (1Korintho 12:3-7, 12-13) anasisitiza kuwa wajibu huu siyo wa wachache bali ni wa kila mbatizwa na kila aliyeimarishwa na kuyapokea Mapaji ya Roho Mtakatifu (Gal 5: 16, 22, 25).  Hivi tunaalikwa tutumie karama mbalimbali tulizojaliwa na Roho wa Mungu kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristu, yaani Kanisa ambalo lina wajibu wake wa kwanza wa kuwa sura na sauti ya mungu duniani – sauti ya upendo, haki, amani, umoja na kuwanenea wanyonge wasio na sauti katika jamii. Basi tutambue kuwa Imani yetu ni ya kimisionari kwa asili yake. Ni wito wa kuwashirikisha wengine makuu ya Mungu kwa njia ya unyofu wa matendo yetu. Ni wito wa kutoa huduma, kujenga umoja na undugu wetu na watu wote duniani, kujijengea uwezo wa kutoa na kupokea msamaha. Yote hayo yanawezeshwa na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Hivyo basi wanaomtafuta Mungu wamwone kwetu tunaojitahidi kuishi kwa matendo kile tunachoungama kwa nguvu ya Roho wa Mungu.

Shirika la Roho Mtakatifu
30 May 2020, 15:02