Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Wafuasi wa Yesu wanahitaji jicho la imani kuweza kutambua uwepo wake endelevu kati yao! Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Wafuasi wa Yesu wanahitaji jicho la imani kuweza kutambua uwepo wake endelevu kati yao!  (ANSA)

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Tunahitaji Jicho la Imani!

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Kwa muda wa siku arobaini, Kristo Yesu aliwatokea wanafunzi wake, akala na kunywa pamoja nao. Akawafundisha juu ya Ufalme wa Mungu na utukufu wake ulikuwa bado umefunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Kwa Kristo Yesu kupaa mbinguni maana yake ni kurudi kwa ubinadamu wake katika utukufu wa Mungu unaojionesha kwa wingu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mwinjili Matayo juu ya kupaa Bwana mbinguni hatuelezei wala kutuonesha tukio hilo kama tunavyosoma kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume, na badaya yake anatumia ishara nyingine kutuonesha tukio hilo hilo. Pia tofauti na Injili ya Luka na ile ya Yohana hatuoneshi kuwa Kristo Mfufuka alikutana na wafuasi wake Yerusalemu bali Galilaya. Ndio kusema kwa Mwinjili Matayo kutuonesha eneo la kijiografia la Kaskazini kuna ujumbe wa kiteolojia. Mwisho wa masimulizi ya Injili sio tamati bali ni mwanzo wa misheni ya Yesu Kristo kwa Kanisa lake. Mwinjili anataka kutuonesha leo kuwa misheni na utume wa wafuasi wa Yes una hasa kundi lile dogo la Mitume linaanzia pale walipoanzia utume wao tangu walipoitwa na Yesu, yaani katika mkoa ule wa Galilaya. Galilaya ulikuwa ni mkoa uliodharaulika kati ya Wayahudi kwani kule waliishi wayahudi waliochanganyika na watu wa mataifa ambao kwao ni wapagani. Si tu waliishi pamoja na watu wa mataifa kwani ni mkoa wa mpakani bali hata na wayahudi wa sehemu zile hawakuonekana kuwa ni wayahudi safi na kamili, kwa sababu hiyo hiyo ya mwingiliano wao na watu wengine. Na ndio tunasoma kutoka Kitabu cha Nabii Isaya 9:1, Galilaya ya mataifa. Hata Nikodemo wakati alipotaka kumtetea Yesu alikumbushwa kuwa kutoka Galilaya kusingeweza kutokea Nabii. Yohane 7:52.

Mwinjili Mathayo leo anatuonesha kuwa Kristo Mfufuka anataka Mitume na rafiki zake kuanza utume wao katika mazingira haya ya watu waliokuwa nusu wapagani. Yerusalemu kwa jinsi ulimvyomkataa Masiha umepoteza fursa na upendeleo ule na sasa utume wa Kristo Mfufuka unaanza kutokea Galilaya. Walienda katika mlima ule ambao Yesu aliwaonesha, ila Mwinjili hasemi waziwazi na wala kuutaja mlima huo. Ila daima tunatambua mlima katika Maandiko Matatifu ni sehemu ya Agano na kukutana na Mungu, ni mahali ambapo Mungu anajifunua na kujidhihirisha. Ni pale juu mlimani Yesu anawafundisha wanafunzi wake juu ya maisha ya heri, ikiwa ndio katiba na mwongozo wa maisha ya mkristo, kama vile Musa alivyopokea amri za Mungu juu ya mlima Sinai, pia Yesu anatoa mafundisho yake ya heri pale juu mlimani. Hivyo ni mlimani wanapaswa kubadili vichwa vyao kwa maana ya kuanza maisha mapya kadiri ya Neno na maagizo yake Yesu Kristo Mfufuka.

Wanafunzi wale tunasikia walikuwa bado na mashaka na wasiwasi, na ndio katika mashaka na wasiwasi hapo imani inahitajika na si kinyume chake. Hakuna uhitaji wa imani pale tunapokuwa na hakika na kuona kila kitu kwa uwazi, hakuna anayehitaji imani juu ya uwepo wa jua na mwezi kwani ni vitu tunavyoviona na kuwa na hakika navyo. Jumuiya ile ya mwanzo ya mitume kama nasi leo kila mara tunaitikia wito wa Kristo Mfufuka tunajawa na mashaka na wasiwasi na hivyo kualikwa kuwa na imani kwa kila njia na misheni anayotuitia na kututuma. Mitume wanaalikwa sio kumwona Kristo Mfufuka kwa macho ya nyama, bali kwa macho ya imani, ndio kuona kule kunakutambulishwa kwa kitenzi cha Lugha ya Kigiriki οραω (orao), kuona kwa ndani kabisa kwa jicho la imani, tofauti na aina ya pili ya kuona nayo ni βλεπω (Blepo), kuona kwa macho ya nyama, kuona kwa nje na juujuu tu bila kuwa na imani. Nasi leo tunaalikwa kukutana na Kristo Mfufuka kwa jicho la imani na daima anajidhihirisha na kujifunua kwetu.

Kristo Mfufuka anawakaribia, na kuwakaribia ndio kuwasaidia wao kuweza kumuona na kumtambua, kuuona Uso wa Mungu wa kweli, kuwadhihirishia vile alivyo, ili waweze kumtambua. Na ndio upendo wa Mungu kwa mwanadamu ulivyo, sio sisi tunaomtafuta Mungu bali Mungu anawaka na upendo ule wake hivyo kila mara anakaribia kwako na kwangu, anatukaribia tukiwa katika kila hali za maisha yetu, itoshe kufunua macho ya imani ili tuweze kuuona uso wake. Kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, Yesu aliwatuma Mitume wake kwenda kutangaza Habari Njema kati ya Wayahudi na si kati ya mataifa au wapagani. Mathayo 10:5-6 Ni baada ya Pasaka tunaona misheni na utume wao sasa unakuwa bila mipaka, si tu kwa wayahudi au watu wa Israeli bali kwa watu wa mataifa yote. Yesu ni nuru si tu inayowaka na kuangazia Galilaya kwa watu waliokuwa gizani bali sasa kwa ulimwengu mzima. Sasa anakuwa nuru kwa ulimwengu mzima. Mathayo 4:16 na Isaya 42:6

Anawaalika Yesu leo Mitume wake kwenda, ni kitendo cha kutoka, si tu katika nchi na taifa lao bali kutoka katika tamaduni na mitazamo yao ya awali, ni kuwaalika kubadili vichwa na kuwa na mtazamo mpya, ndio ule wa Kristo Mfufuka. Kutoka katika mipaka ile ya utaifa kati yao na watu wengine, mipaka ya jinsia, mipaka ya makuhani na wanaume wengine na mipaka hata ile ya kuhani mkuu na makuhani wengine, ni kutoka katika mitazamo yote ya awali iliyokuwa inawazua kuwa ndugu, kuwa kaka na dada, kwani Kristo sasa anatualika sote kuwa ndugu bila kuangalia tofauti zetu mbali mbali. Na ndio Jumuiya mpya ya wanakanisana, sote tunakuwa ni ndugu na tunaunganishwa na imani kwa Kristo Mfufuka. Pia anawaalika kwenda kuwafundisha, kwa kweli sio kuwafundisha kanuni za imani bali kuiishi imani, kuishi upendo ule wa Kristo Mfufuka na wengine. Hivyo mafundisho yetu kwa wengine wote ni ushuhuda wa maisha yetu, ni kwa kuishi Injili wengine watatutambua kuwa sisi kweli ni wanafunzi na rafiki zake Kristo Mfufuka, ndio utume huo Kristo anatuachia kabla ya kupaa kwake Mbinguni.

Na kuwabatiza kwa Jina la Baba, la Mwana na la Roho Mtakatifu. Neno Ubatizo linatokana na neno la Kigiriki βατιζειν (Batizein) likiwa na maana “zamisha”. Na hivyo kubatiza hapa ina maana mbili, ya kwanza ndio ile ya kuingiza katika Jumuiya ya waamini kwa Sakramenti ile ya kwanza ya imani, hapa mmoja anazamishwa na kutolewa nje. Ila Neno batiza lina maana ya pili nayo ndio kuzamisha moja kwa moja, ndio maisha ya mkristo tunapaswa kuzamishwa katika maisha ya Mungu mwenyewe bila kukengeuka au kurudi nyuma, ni kuwaza, kutenda na kuishi pamoja na Mungu mwenyewe katika Utatu Mtakatifu, ni kuishi maisha mazimamazima na Mungu katika ukamilifu wote. Ni hapo tunaweza kutimiza utume wa Kristo Mfufuka wa kuwafundisha kuyashika yote, ni kwa kuonesha wengine na kuiishi pamoja nao ile amri yake ya Upendo kwa Mungu na jirani. Upendo inaweza kuchukua sura mbali mbali ila ni mwito na mwaliko wa kila mmoja wetu kuwa mwalimu kwa maisha yetu, kuyashika sio akili tu bali kuyashika na kuyashuhudia katika maisha yetu ya siku kwa siku.

Ni wazi tunapotambua udogo na uduni wetu tunajawa na mashaka na wasiwasi juu ya uwezo wetu wa kuishi haya anayotualika Kristo Mfufuka, ila tunahakikishiwa na kupata faraja kutoka kwa Kristo Mfufuka kuwa anabaki nasi siku zote mpaka ukamilifu wa dunia. Yeye ni Mungu pamoja nasi, Yeye ni Emanuele, anakuwa nasi hata tunapopita nyakati ngumu za maisha yetu kama wakristo, Kristo hatuachi kamwe katika safari yetu hata nyakati za mashaka na wasiwasi mkubwa kama za siku hizi za ugonjwa wa homa kali ya mapafuinayosababishwa na Virusi vya COVID-19, tuwe na hakika kuwa yupo pamoja nasi na anatuona na kutulinda kwani Yeye ni mwaminifu daima. Ninawatakia mwendelezo mwema wa Novena kwa ajili ya Ujio wa Roho Mtakatifu. Tumwombe Mungu atuwezeshe kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini.

22 May 2020, 09:41