Tafuta

Vatican News
Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Ni Ushuhuda wa Kutukuka kwa Mwili wa Binadamu Mbinguni. Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Ni Ushuhuda wa Kutukuka kwa Mwili wa Binadamu Mbinguni. 

Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni: Ushuhuda na Utume wa Kanisa!

Sherehe inaonesha kutukuka kwa mwili wa binadamu mbele ya Mungu, kiini cha imani na matumaini kuwa, daima Mwenyezi Mungu ataendelea kuambatana na binadamu na kwamba, mbinguni, kila mtu anaandaliwa makazi ya milele. Kumbe, waamini wanapaswa kuishi hapa duniani wakiwa wanayaambata zaidi yale ya mbinguni, kama alivyofanya Yesu kwa kuunganisha mbingu na dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Tafakari ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Kristo Yesu baada ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, kwa muda wa siku arobaini aliwatokea wafuasi wake na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Alitumia fursa hii kwa ajili ya kuwaandaa kwa ujio wa Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana. Kanisa ni utimilifu wa Fumbo la Pasaka! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 24 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, unaongozwa na kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Kut. 10:2. Maisha yanakuwa ni historia. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anapembua kwa kina na mapana kuhusu mwingiliano wa hadithi na kwamba, si kila hadithi ni hadithi njema. Kuna hadithi ya hadithi; hadithi iliyopyaishwa na hatimaye kuna hadithi inayoendelea kumpyaisha mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao ukweli wa historia njema!  

Kristo Yesu Mfufuka kabla ya kupaa kwenda zake mbinguni aliwaambia wafuasi wake kwamba, amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani ambayo kimsingi ni nguvu ya Mungu na akawaahidia kuwapatia nguvu ya Roho Mtakatifu yenye utendaji na uweza mkuu unaounganisha mbingu na dunia, hili ndilo haswa Fumbo linaloadhimishwa kwa Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni Sherehe inayoonesha kutukuka kwa mwili wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu, kiini cha imani na matumaini kuwa, daima Mwenyezi Mungu ataendelea kuambatana na binadamu na kwamba, mbinguni, kila mtu anaandaliwa makazi ya milele. Kumbe, waamini wanapaswa kuishi hapa duniani wakiwa wanayaambata zaidi yale ya mbinguni, kama alivyofanya KristoYesu kwa kuunganisha mbingu na dunia! Lakini, waamini wanakumbushwa kwamba, licha ya Kristo Yesu kupaa mbinguni, lakini bado anaendelea kuwa pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahari.

Huko mbinguni anaonesha ubinadamu wake na wa watu wake na hivyo anaendelea kuwaombea kila kukicha, lakini kwa namna ya pekee kabisa anawaombea msamaha wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa kumwonesha Baba wa milele makovu ya Madonda yake Matakatifu, mwaliko wa kujiaminisha mbele yake kwani Yesu ni wakili wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa anakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu baada ya kuhitimisha kazi ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Katika utangulizi wa Sherehe hii tunasoma kwamba, kwa maana Bwana Yesu Mfalme Mtukufu, ameishinda dhambi na mauti. Amepaa mbinguni Malaika wakistaajabia. Amekuwa ni Msuluishi kati ya Mungu na wanadamu; Hakimu wa ulimwengu na Bwana mwenye enzi. Amepaa si kwa nia ya kutuacha yatima na wanyonge, bali tukae tukiamini kwamba, sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye, kichwa chetu na shina letu. Kupaa kwa Kristo Yesu mbinguni ni alama dhahiri ya kuingia ubinadamu wa Yesu ndani ya makao ya mbingu ya Mwenyezi Mungu, ambako toka huko atarudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Rej. Mdo. 1:11.

Maandiko Matakatifu yanatukumbusha kwamba, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu. Rej. Kol. 3:3. Kristo Yesu akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya Hekalu, anaomba daima kwa ajili ya waja wake. Kama Mshenga anayetuhakikishia kumiminwa kwa daima kwa Roho Mtakatifu. Kwa maadhimimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, huu unakuwa ni mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa hadi atakaporudi tena kuwahukumu wazima na wafu. Tukio hili ni changamoto kubwa kwa Mitume wa Yesu, linalowataka kurejea tena Galilaya kwa ari na moyo thabiti ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika, limepewa dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa; kwa Kubatiza na kuwa ni Sakramenti ya Wokovu. Somo la Pili kutoka katika Waraka Mtume Paulo kwa Waefeso: 1:17-23, ni sala ya kuwaombea Wakristo wa Efeso ili waweze kuwa na roho ya hekima na ufunuo, tumaini, nuru, utajiri wa utukufu wa urithi pamoja na ubora wa ukuu wa uweza wake katika Fumbo la Pasaka. Mtume Paulo anadadavua Fumbo la Kupaa Bwana Mbinguni kama mwanzo mpya wa maisha na utume wa Kanisa.

Sehemu hii ya Neno la Mungu ni muhtasari wa Fumbo la Kupaa Bwana Mbinguni linaloadhimisha na Mama Kanisa. Kristo Yesu ni mwanga angavu wa Kanisa lake. Ni Daraja la Kanisa lililopo hapa duniani na Kanisa lile lijalo katika utukufu na ubora wake. Mwinjili Luka na Mathayo wanapenda kuonesha Kanisa hai, lakini Paulo Mtume analielezea Kanisa kama Taasisi, Kanisa kama Fumbo. Hii ni changamoto ya kuliangalia Kanisa kama Taasisi na Kanisa ambalo ni Fumbo lililofichika. Kumbe, tunaweza kusema kwa ufupi kabisa kwamba, Kanisa ni taasisi ya Kimungu inayoendeshwa na kuratibiwa na binadamu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa njia ya Fumbo la Pasaka Kristo Yesu aliwavuta wote kwake. Akawapelekea wanafunzi wake Roho Mtakatifu na kuliweka Kanisa kuwa ni Sakramenti ya wokovu kwa wote. Amepaa mbinguni kwa Baba yake, lakini anaendelea kuwalisha wanafunzi wake kwa Sakramenti na Neno la Mungu. Rej. LG. 8. Kimsingi kuna Kanisa linaloonekana na lile lisiloonekana na limewekwa duniani kama Jumuiya ya imani, matumaini na mapendo kama muundo unaoonekana na daima hulilisha na kwa njia yake hueneza kwa watu wote ukweli na neema.

Hii ni Jumuiya inayoundwa na viungo vya kihierakia na Mwili wa Fumbo la Kristo; Jumuiya ya maisha ya kiroho. Kanisa linalosafiri na Kanisa lililoko mbinguni, hili ni Kanisa lenye asili ya Kimungu na Kibinadamu. Kanisa ni takatifu kwa sababu limeanzisha na Kristo Yesu. Hili ni Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Kutokana na udhaifu wa watoto wa Kanisa, basi linapaswa kujitahidi kutubu, kuongoka na kutakaswa kwa sababu Kanisa pia linawakumbatia wadhambi. Mwili wa Fumbo wa Kristo unapaswa kujengwa katika: umoja, unyenyekevu, upole, uvumilivu na upendo, kila mtu akitumia vyema karama zake. Lengo ni kuweza kufikia umoja wa imani, ili kulifahamu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katika muktadha huu, waamini wanapaswa kushika kweli katika upendo! Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni chemchemi na nguvu ya kusonga mbele, ili kuliimarisha Kanisa hapa ulimwenguni. Kristo Yesu anaendelea kutembea pamoja na Kanisa lake katika imani, matumaini na mapendo. Wakati wa raha na majonzi. Kristo Yesu kwa njia ya Kanisa anaendeleza uwepo wake. Kanisa linaendelea kujengeka na kudumishwa kwa njia ya Neno, Sala na Sakramenti za Kanisa sanjari na ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Mfufuka kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni
20 May 2020, 14:16