Tafuta

Padre na Profesa Charles Nyamiti, Jaalimu wa CUEA kwa miaka 34 amefariki dunia tarehe 19 Mei 2020 huko Ipuli, Jimbo Kuu la Tabora nchini Tanzania. Padre na Profesa Charles Nyamiti, Jaalimu wa CUEA kwa miaka 34 amefariki dunia tarehe 19 Mei 2020 huko Ipuli, Jimbo Kuu la Tabora nchini Tanzania. 

Prof. Charles Nyamiti: Amefariki Dunia! Mwamba umeanguka!

Padre Charles Nyamiti alizaliwa kunako mwaka 1931. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, Mwaka 1962 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mwaka 1969 akajipatia shahada ya Uzamivu katika Mafundisho tanzu ya Kanisa. Mwaka 1976 hadi mwaka 1981 akafundisha Seminari Kuu ya Kipalapala. Mwaka 1983 hadi mwaka 2018 akafundisha CUEA. Tarehe 19 Mei 2020, akafariki dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora anasikitika kutangaza kifo cha Padre na Profesa Charles Nyamiti, kilichotokea tarehe 19 Mei 2020 kwenye Hospitali ya Mtakatifu Anna, Ipuli, Jimbo Kuu la Tabora. Mazishi yanatarajiwa kufanyika Alhamisi tarehe 21 Mei 2020 saa 4:00 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, huko Itaga. Padre na Prof. Charles Nyamiti ni mtoto wa Mzee Theophilus Chambi Chambigulu na Mama Helen Nyasolo, alizaliwa tarehe 9 Desemba 1931, huko Ndala Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 15 Agosti 1962 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu mwanzo alionesha kuwa na kipaji cha akili, kiasi kwamba, Jimbo kuu la Tabora kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 1969 likamtuma kwenda kujiendeleza zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Louvain, kilichoko nchini Ubelgiji na huko akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Katika ujana wake, akaonesha pia kubobea na kuzama katika masuala ya muziki. Baadaye alijiendeleza huko Vienna kwa masuala utamaduni wa mwanadamu.

Tangu mwaka 1976 hadi mwaka 1981 alipewa dhamana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kufundisha Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora. Licha ya kufundisha, pia alijihusisha na huduma mbali mbali za kichungaji kwenye Parokia za jirani kwa kuzingatia kwamba, mavuno yalikuwa ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana walikuwa ni wachache hasa ikizingatiwa mazingira na hali ya Kanisa kwa wakati huo! Kunako mwaka 1983 Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, likampatia dhamana na jukumu la kuwa ni kati ya waasisi wa Chuo Kikuu cha CUEA, dhamana ana utume ambao ameufanya kwa umahiri, weledi na ufanisi mkubwa kwa muda wa miaka 34. Kunako tarehe 14 Juni 2018, Jumuiya ya Chuo Kikuu cha CUEA ikaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kumuaga tayari kurejea nchini Tanzania akiwa na umri wa miaka 87.

Katika maisha yake, amebahatika kuandika vitabu 56. Wasomi zaidi ya 20 wamefanya tafiti za kisayansi kuhusu mawazo yake. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki la Mahenge amesema, familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati imempoteza Jaalimu aliyebobea katika taaluma ya kuhakikisha kwamba, anatawataalamisha wataalam wa baadaye kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Ni Jaalimu aliyewapenda sana wanafunzi wake, na akataka kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanalifahamu fika somo alilokua anawafundisha kwa sababu huu ulikuwa ni msingi wa maisha na utume wa Mapadre wa baadaye katika: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Alikazia dhana ya utamadunisho kwa Kanisa Barani Afrika.

Ni Jaalimu aliyewafundisha Maaskofu kama: Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam; Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki la Mahenge, Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma pamoja na Askofu Severin Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge Ngara. Wote hawa ni viongozi wa Kanisa waliofundwa na kufundika vyema! Askofu Ndorobo anasema, Padre Nyamiti amevipiga vita vilivyo vizuri, imani ameilinda, sasa wanamwombea ili aweze kukutana na Kristo Yesu, Uso wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, ili aweze kumkaribisha miongoni mwa watakatifu wake. Apumzike kwa amani! Mwamba wa taalimungu na harakati za utamadunisho wa imani, umeanguka yaani sipati picha! Askofu Mkuu Ruzoka katika taarifa yake anasema, Padre na Profesa Charles kimiti alistaafu shughuli ya kufundisha mwaka 2001 lakini akaendelea kubaki Nairobi akiandika vitabu na kufundisha masomo ya taalimungu na muziki katika Seminari kuu ya Shirika la Mitume wa Yesu, AJ. hadi mwezi Novemba 2019 aliporejea Jimboni Tabora.

Pd na Prof. Charles Nyamiti

 

 

19 May 2020, 14:01