Tafuta

Vatican News
Mama Olive Luena, Mwenyekiti WAWATA Taifa nchini Tanzania anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II amegusa watu wengi katika maisha na utume wake! Mama Olive Luena, Mwenyekiti WAWATA Taifa nchini Tanzania anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II amegusa watu wengi katika maisha na utume wake!  (ANSA)

Mama O. Luena: Mtakatifu Yohane Paulo II Amegusa Maisha ya Wengi

Mama Olive Luena: Kumbikizi la Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II binafsi linaendelea kunikumbusha mambo muhimu sana yaliyonigusa: maisha na utume wa Papa Yohane Paulo II. Aliniteua kuwa mjumbe wa Baraza la Kipapa la Walei:1991-1995. Kipindi hicho nilikuwa vile vile Mjumbe wa Bodi ya WUCWO nafasi niliyohudumu kwa vipindi vitatu (1983-1996).

Na Mama Olive Luena, Mwenyekiti WAWATA Taifa, - Dar Es Salaam.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2020 alisema kwamba, Papa Yohane Paulo II, alibahatika kuwa ni kiongozi na mfano bora wa kuigwa. Kwa hakika alikuwa ni mchungaji mwema aliyekita maisha yake katika sala; ukaribu kwa watu wa Mungu; akawaonesha upendo wa dhati; akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa vijana nchini Poland aligusia kwa ufupi kabisa historia ya maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II; Ibada kwa Huruma ya Mungu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na mwishoni aliwataka vijana kuthubutu kujiachia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwatumia kadiri ya mapenzi yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Poland.

Kumbukizi la Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu aliyeishi katika zama  zetu inazidi kutukumbusha kuwa kuishi wito wetu wa kuwa watakatifu inawezekana  kwa kuzingatia Mafundisho ya kanisa na kuiga Mfano wa Maisha ya Baba Mtakatifu huyu  na ya watakatifu wengine wengi wa zama zetu akiwemo Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta. Wanawake Wakatoliki katika Mkutano Mkuu wa Muungano wa Jumuiya za Wanawake Wakatoliki Ulimwenguni, WUCWO, UMOFC, uliofanyika mjini Dakar, Senegal kuanzia tarehe 15-22 Oktoba 2018, uliazimia kutekeleza mambo makuu manne katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka 2022. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kadiri ya mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.  Katika kuzingatia nafasi na wito wetu katika Kanisa, tulijikita katika Tafakari iliyosheheni maudhui ya “Wanawake Wakatoliki Wabebaji  Wa Maji ya Uzima kwa Dunia yenye kiu ya amani” (WUCWO Women, Carriers of “living water” to a world which thirsts for Peace)

Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kujali na kuzisaidia familia zinazoishi katika mazingira na hatarishi, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu! Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujifunga kibwebwe ili kutokomeza ubaguzi, nyanyaso na ukatili wanaofanyiwa wanawake majumbani kwa kuwa na maandalizi bora kwa wanandoa watarajiwa, ili kukuza na kushirikishana upendo wa dhati, ili kuwaimarisha wanandoa na hatimaye, waweze kutakatifuzana. Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujielimisha zaidi ili hatimaye, waweze kutikia wito wa utakatifu wa maisha! Jumuiya za Wanawake Wakatoliki Ulimwenguni, WUCWO, UMOFC, imechota utajiri wa maazimio haya kutoka katika Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Pili ni Wosia wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia.

Tatu ni Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ambao ni dira na mwelekeo wa maisha na shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kila kukicha! Nne ni Waraka wake wa kitume wa Papa Francisko “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Kumbikizi la Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, binafsi linaendelea kunikumbusha mambo muhimu sana yaliyonigusa kuhusu Mpendwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili. Binafsi nakumbuka upendeleo mkubwa alionijalia kwa kuniteua kuwa miongoni wa wajumbe wa Baraza la Kipapa la Walei: “Pontifical Council of the Laity”, kwa kipindi cha Miaka 5 (1991-1995) fursa iliyonisaidia sana katika utume wangu. Kipindi hicho nilikuwa vile vile Mjumbe wa Bodi ya WUCWO nafasi niliyohudumu kwa vipindi vitatu (1983-1996).

Tarehe 15 Agosti, 1988, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika kuadhimisha Mwaka wa Bikira Maria alitoa Waraka Muhimu sana uitwao Utu na Wito wa Wanawake: “Mulieris Dignitatem” ambao tulipata fursa kama wanawake kuujadili katika ngazi mbalimbali za Wanawake Wakatoliki na hadi leo ni mwongozo mzuri sana tunaoendelea kuutafakari katika utume wetu na wito wa kuwa watakatifu. Katika tafakari hiyo ya Utu na Wito wa Wanawake Baba Mtakatifu Yohane Pili anatupa uelewa wa kina kuhusu uumbaji wa Binadamu kwamba “Mwanawake na Mwanaume wote wameumbwa kwa kwa sura na mfano wa Mungu Mwenyewe” huku kunamaanisha usawa wa binadamu machoni pa Mungu. Kupitia tafakari hiyo tunapata fursa ya kuelewa vizuri nafasi ya Mama Bikira Maria, kama Mwanamke katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu na wanawake waliotangaza na kushuhudia ufufuko wa Yesu kama mifano hai ya utu na wito wa wanawake.

Tafakari pamoja na maelezo ya kina kuhusu nafasi ya Mwanamke katika familia, jamii na Kanisa kama Mama, Mwalimu au Dada inataja mifano mingi ya Wanawake watakatifu ambao ni mifano hai ya kuigwa katika safari yetu ya wito wa kuwa watakatifu. Wanawake Wakatoliki wakiwa sehemu Kubwa ya waamini walei, Hati hiyo ya Utu na Wito wa Wanawake vilevile inaenda sambamba na ile hati yake inayohusu: Wito wa Utume wa Walei: “Christifideles laici” aliyoitoa tarehe 30 Desemba1988 baada ya Sinodi ya Maaskofu iliyotafakari nafasi na wito wa walei katika Kanisa na ulimwengu. Sitasahau mahubiri aliyoyayatoa akiwa Pale Jangwani Dar Es Salaam, tarehe 2 Septemba 1990 ambapo alisitiza umuhimu na nafasi ya familia kama shule ya sala kwa kukazia: Sala binafsi na sala za kifamilia. Familia ni shule ya uaminifu na upendo, changamoto na mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kukuza na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Familia ni shule ya huruma na msamaha unaopaswa kubinafsishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Kumbukizi hili la miaka 100 imenifanya vile vile nikumbuke ile barua iliyosomwa na kutajwa sana aliyowaandikia Wanawake tarehe 29/6/1995 kwa ajili ya Mkutano wa Wanawake wa Beijing ambayo alitaja makundi mbalimbali ya Wanawake Duniani kama mama, mke, binti na dada. Wanawake wafanyakazi, wanawake katika miito ya kitawa,na Wanawake wote kwa ujumla na kutanabaisha kwa kifupi  wajibu katika miito yao na kwa kuzingatia pia Hati yake ya Kipapa ya “Mulieris dignitatem”.  Nakumbuka niliratibu ushiriki wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) katika Mkutano huo wa Ulimwengu  wakati huo,  nikiwa katibu Mkuu wa WAWATA  ambapo tulipeleka ujumbe wa WAWATA 11 na kumchangia Mwanamke mmoja wa dini ya  Kiislam kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini katika uhalisia wake. Wakati huo huo nikiwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Hiari Tanzania (TANGO) niliratibu ushiriki ujumbe wa akina mama 110 toka vyama vya hiari Tanzania walioshiriki Mkutano Beijing NGO Forum wakiwemo WAWATA. Naendelea kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo 11 aliyegusa maisha yangu na ya Wwatu wengi kwa ujumla na anaendelea kutuombea mbinguni. Nakumbuka kila mara tulipopewa fursa ya kukutana naye tukiwa kwenye Baraza lake la Kipapa daima mioyo yetu iliruka kwa furaha isiyo na kifani!

Mama Luena
26 May 2020, 13:36