Tafuta

Vatican News
Liturujia ya Neno la Mungu: Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka: Maandalizi ya Sherehe ya Pentekoste, Zawadi ya Roho Mtakatifu Mfariji, Roho wa kweli! Liturujia ya Neno la Mungu: Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka: Maandalizi ya Sherehe ya Pentekoste, Zawadi ya Roho Mtakatifu Mfariji, Roho wa kweli! 

Jumapili VI ya Pasaka: Roho Mtakatifu Mfariji, Roho wa kweli!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka ni maandalizi kwa ajili ya ujio wa Roho Mtakatifu. Lengo ni kuwasaidia waamini kumfahamu vyema zaidi Kristo Yesu. Mama Kanisa anafundisha na kukiri kwamba, Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mwenye uwamo mmoja na Baba na Mwana anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu tulipoadhimisha Sherehe ya Pasaka, Liturujia ya Neno la Mungu imekuwa ikituongoza kumtafakari Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka ni sehemu ya maandalizi ya Sherehe ya Pentekoste: Siku Kanisa lilipozaliwa rasmi, Mitume wakatoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ujio wa Kristo Yesu, Masiha na Mpakwa wa Bwana, uliandaliwa na Manabii, ukatangazwa na kushuhudiwa na Yohane Mbatizaji. Lakini ujio wa Roho Mtakatifu unaandaliwa na Kristo Yesu ambaye aliwaambia wafuasi wake “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.  Yn. 14: 15-16. Huyu ndiye Roho Mtakatifu Mfariji, Roho wa kweli.

Somo la kwanza: Mdo. 8:5-8; 14-17 linaonesha jinsi ambavyo Jumuiya ya Wakristo mjini Samaria walivyotangaziwa na kushuhudiwa Neno la Mungu na kuziona ishara zikitendwa na Mtakatifu Filipo, Mtume. Pepo wachafu waliwatoka watu, wagonjwa na viwete wakaponywa. Ishara zote hizi zikawa ni chemchemi ya furaha ya Injili mjini Samaria. Mitume Petro na Yohane walipofika wakawawekea mikono na hapo Roho Mtakatifu akawashukia! Wasamaria wakabatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu, huo ukawa ni mwanzo wa maisha mapya katika Kristo Yesu, Mfufuka. Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka ni maandalizi ya kina kwa ajili ya ujio wa Roho Mtakatifu. Lengo ni kuwasaidia waamini kumfahamu vyema zaidi Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Mama Kanisa anafundisha na kukiri kwamba, Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mwenye uwamo mmoja na Baba na Mwana anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Roho Mtakatifu ndiye aliyenena kwa vinywa vya Manabii, anayewawezesha waamini kusikiliza Neno la Mungu, anayewafafanulia na kuwa tayari kumkaribisha katika imani. Roho Mtakatifu amefunuliwa na Kristo Yesu ndiye anayewafundisha na kuwakumbusha waamini yale mambo msingi aliyofundisha Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anakaa katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; anakaa katika Mapokeo ya Kanisa; katika Mamlaka rasmi ya ufundishaji wa Kanisa “Magisterium”, katika Liturujia ya Sakramenti ambazo huwaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu na zaidi ya hayo yuko katika maisha ya kitume na kimisionari. Rej. KKK namba 683-688 kwa ufafanuzi wa kina!

Somo la Pili, ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote:1 Pet. 3: 15-18, Mtakatifu Petro anawataka Wakristo kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani mwao, lakini kwa upole na kwa hofu na katika mwenendo mwema. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Mungu! Kimsingi, waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukweli! Mwinjili Yohane katika Sura ya 14: 15-21 anamwelezea Roho Mtakatifu kuwa ni Roho wa kweli na huyu ndiye Roho Mfariji. Paji la upendo wa Mungu na Mpako wa Kristo Yesu. Kwa ufupi tunaweza kusema kwamba, Roho Mtakatifu ambaye Kristo, kichwa anammimina katika viungo vyake, anajenga, anahuisha, analitakasa Kanisa Sakramenti ya umoja wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na wa watu. Rej. KKK namba 747.

Roho Mtakatifu ni Mfariji na chemchemi ya faraja ya Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu aliwapenda waja wake upeo! Anatambua udhaifu wao wanapokumbana na matatizo na changamoto za maisha. Kwa kutambua hili, Kristo Yesu amewawekea wanafunzi wake mpango mkakati unaofumbatwa katika Amri ya Upendo ambayo ni chemchemi ya faraja ya Mungu! Nabii Isaya 40:1 anasema, watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu. Watu wa Mungu wakati huu wanakabiliwa na hofu kubwa ya kifo na hali ya kujikatia tamaa kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni katika muktadha huu, Paulo Mtume, anawakumbusha watu wa Mungu kwamba, Mungu wao ni Baba wa huruma na faraja yote. Yeye ndiye anayewafariji katika dhiki zao zote, ili wao pia waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja ya Mungu kwa jirani zao. Rej. 2 Kor. 1:3-4.

Huruma ya Mungu imenafsishwa kwa namna ya pekee katika Kristo Yesu ndiyo maana katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho yake makuu anasema, Heri wenye huzuni maana hao watafarijika. Rej. Mt. 5:4. Anawaalika wale wote walioelemewa na mizigo kumwendea ili aweze kuwapumzisha. Rej. Mt. 11:28. Kwa hakika, Roho Mtakatifu Mfariji ataendelea kubaki na waamini milele yote. Rej. Yn. 14:7. Faraja ya Mungu ni upendo wake uliomiminwa katika Nafsi ya Kristo Yesu. Mwenyezi Mungu anawafariji wanyenyekevu wa moyo, ili nao waweze kuwa ni chemchemi ya faraja, upendo, umoja, mshikamano na furaha inayobubujika kutoka kwa Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Tafakari Jumapili 6 ya Pasaka

 

13 May 2020, 13:21