Tafuta

Vatican News
Barua ya Kichungaji kutoka Jimbo Katoliki la Manzini, lililoko nchini Eswatini: Umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama ushuhuda wa imani yao kwa Kristo. Barua ya Kichungaji kutoka Jimbo Katoliki la Manzini, lililoko nchini Eswatini: Umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama ushuhuda wa imani yao kwa Kristo.  (Vatican Media)

Barua ya Kichungaji kutoka Jimbo la Manzini: Maisha na Utume!

Askofu José Luis Ponce de León., wa Jimbo Katoliki la Manzini, Eswatini katika ujumbe wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasiishi kwa wakati huu, wakitarajia kurejea tena katika maisha yao ya zamani! Kipindi hiki cha mapambano dhidi yaCOVID-19, kimekuwa kweli ni kipindi cha neema na baraka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila Mkristo anawajibika barabara kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa, wito ambao unabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayokita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbe, kwa njia ya neema ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanageuzwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa maisha na utume wa Kanisa, na hivyo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 uliongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”.  Kanisa linataka kuendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake.

Maadhimisho haya yamekuwa ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Umekuwa ni wakati muafaka kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa, tayari kutoka kifua mbele ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni ni kielelezo cha utume na ushuhuda wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Sherehe hii inaonesha kutukuka kwa mwili wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu, kiini cha imani na matumaini kwamba, daima Mwenyezi Mungu ataendelea kuambatana na binadamu katika hija yake ya maisha hapa duniani na kwamba, mbinguni, kila mtu anaandaliwa makazi ya milele. Kumbe, waamini wanapaswa kuishi hapa duniani wakiwa wanayaambata zaidi yale ya mbinguni, kama alivyofanya Yesu kwa kuunganisha mbingu na dunia!

Askofu José Luis Ponce de León, IMC., wa Jimbo Katoliki la Manzini nchini Eswatini katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasiishi kwa wakati huu, wakitarajia kurejea tena katika maisha yao ya zamani! Kipindi hiki cha mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kilichopelekea watu wote wa Mungu nchini humo kuwekwa chini ya karantini, kimekuwa kweli ni kipindi cha neema na baraka. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wameitwa, wakabatizwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Jimbo limetumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano kwa ajili ya sala, maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, tafakari pamoja na kuonesha matendo ya huruma, kwa kuwagawia maskini barakoa na mahitaji msingi katika kipindi hiki. Waamini wamejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuchangia miradi mbali mbali ya huduma kwa maskini na watawa wamejitahidi kuhakikisha kwamba, walau watu wanapata huduma msingi. Jimbo Katoliki la Manzini linalishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kwa kuwachangia kiasi cha Euro 40, 000 kwa ajili ya huduma kwenye Hospitali ya “Good Shepherd” iliyoko Jimboni humo. Waamini wameendelea kusali na kufanya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa hakika, waamini wameonesha mshikamano wa imani, upendo na matumaini; kwa kujaliana na kusaidiana kwa hali na mali. Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona,COVID-19, upendo na mshikamano wa dhati ndiyo silaha madhubuti kwa wakati huu.

Changamoto mamboleo kwa wakati huu ni pamoja na ukame wa maisha ya kiroho kutokana na waamini kushindwa kurutubisha maisha yao kwa Sakramenti za Kanisa na Sala Binafsi. Kwa baadhi ya familia, umekuwa ni muda wa neema wa kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani, lakini pia kwa baadhi ya watu, maisha ya kifamilia yamegeuka kuwa ni “uringo wa masumbwi kati ya baba na mama”, kila mtu, akitaka “kujimwambafai dhidi ya mwenzake”. Kwa baadhi ya watu wamejikuta wakitumbukia na hatimaye, kuzama katika ugonjwa wa sonona. Ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 umezua changamoto kubwa kiasi hata cha kuanza kumong’onyoa umoja na mafungamano ya kijamii kutokana na wasi wasi na hofu zisizokuwa na tija. Fursa za kazi na ajira kwa watu wengi kwa sasa ziko mashakani. Kumekuwepo na madhara makubwa katika mfumo wa elimu kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Madhara yake yataonekana kwa siku za usoni.

Askofu José Luis Ponce de León anapenda kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema maneno ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwamba, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga ujirani mwema na wale wote wanaowazunguka, ili kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Shrika la Afya Duniani, WHO linasema kwamba, Virusi vya Corona, COVID-19 vitaendelea kumwanadama mwanadamu hata baada ya kupatikana kwa chanjo kama yalivyo magonjwa mengine. Jambo la msingi ni kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Wakristo wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa majirani zao!

Jimbo la Manzini
23 May 2020, 14:57