Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linasema, ukweli umefahamika na haki imetendeka baada ya Kardinali George Pell kushinda rufaa yake Mahakama kuu ya Australia sasa ni mtu huru! Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linasema, ukweli umefahamika na haki imetendeka baada ya Kardinali George Pell kushinda rufaa yake Mahakama kuu ya Australia sasa ni mtu huru! 

Maaskofu Katoliki Australia: Ukweli umefahamika na Haki imetendeka!

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linasema, watu wengi wameipokea hukumu hii kama kielelezo cha ukweli na haki kutendeka. Watu wengi wameteseka sana wakati wote wa mchakato wa kesi dhidi ya Kardinali George Pell, sasa kesi hii imefikia ukomo. Hata hivyo, Kanisa litasimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na makuzi ya watoto wadogo dhidi ya nyanyaso mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limepokea kwa mikono miwili hukumu iliyotolewa na Mahakam kuu ya Australia ya kumwachia huru baada ya Kardinali George Pell kushinda rufaa yake dhidi ya shutuma za nyanyaso za kijinsia zilizokuwa zinaelekezwa dhidi yake. Mahakama Kuu imeamuru kwamba, Kardinali Pell aachiliwe huru mara moja! Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linasema, watu wengi wameipokea hukumu hii kama kielelezo cha ukweli na haki kutendeka. Watu wengi wameteseka sana wakati wote wa mchakato wa kesi dhidi ya Kardinali George Pell, sasa kesi hii imefikia ukomo. Hata hivyo, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na makuzi ya watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ambazo kwa miaka ya hivi karibuni, zimechafua maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Mahakama nchini Australia ilimtia hatiani Kardinali George Pell, mwenye umri wa miaka 77 wakati ule kwa kupatikana na kosa la kunyanyasa watoto wadogo, kwenye miaka 1990 wakati alipokuwa Askofu msaidizi wa Melbourne kati ya mwaka 1987-1998, kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Melbourne na kuongoza kati ya mwaka 1996-2001. Kuanzia mwaka 2001-2014 alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Sydney nchini Australia; na kuteuliwa kuwa Kardinali kunako mwaka 2003. Kunako mwaka 2013 kama sehemu ya mageuzi makubwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, Baba Mtakatifu Francisko akamteua Kardinali Pell kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uchumi! Kesi hii kwa mara ya kwanza iliibuliwa kunako mwaka 2014, Kardinali Pell alipotakiwa kwenda kutoa ushahidi Mahakamani kwa shutuma ya kuwalinda mapadre waliotuhumiwa kujihusisha na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Wakati wote, Kardinali Pell amekanusha madai haya kwamba, hakuwa na taarifa zozote kuhusu nyanyaso za kijinsia zilizotokea katika Jimbo Katoliki Ballarat. Kunako mwaka 2016 Kardinali akahojiwa mjini Roma na tarehe 26 Julai 2018 akatakiwa kuwepo Mahakamani ili kuweza kujitetea mwenyewe. Kardinali George Pell amekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia sanjari na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baba Mtakatifu Francisko. Baraza la Maaskofu Katoliki Australia likaonesha mshikamano wake wa dhati na Kardinali Pell na kwamba, sheria ni msumeno; watu wote wako sawa mbele ya sheria. Taarifa iliyotolewa na Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican wakati ule ilieleza kwamba, Vatican inapenda kuchukua fursa hii kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Australia kutambua uamuzi wa Mahakama nchini humo, hata kama habari hizi zimepokelewa kwa majonzi makubwa sehemu mbali mbali za dunia. Vatican iliendelea kusuburi hukumu ya mwisho, baada ya Kardinali Pell kukata rufaa! Ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka, Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchukua tahadhari, kuanzia wakati huo, Kardinali George Pell alisimamishwa kufanya shughuli za kichungaji hadharani na wala hakuruhusiwa kukutana tena na watoto wadogo kadiri ya sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwa sasa!

Maaskofu Australia
10 April 2020, 14:27