Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Jumapili ya Mchungaji Mwema: Sala ya Familia Kama Kanisa Dogo la Nyumbani, chemchemi ya miito mitakatifu! Maadhimisho ya Jumapili ya Mchungaji Mwema: Sala ya Familia Kama Kanisa Dogo la Nyumbani, chemchemi ya miito mitakatifu!  (AFP or licensors)

Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani: Ushuhuda na Sala!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya unaongozwa na kauli mbiu: “Maneno ya Miito” ambayo Baba Mtakatifu anasema ni: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, linawaalika waamini kuadhimisha Siku hii kwa kukuza na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho ndani ya familia, hasa kwa kusali zaidi ili kuombea miito mitakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Kanisa linatambua na kufundisha kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Familia ni kitalu cha miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Hapa ni mahali ambapo watu wa Mungu wanaanza kujifunza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Familia, Kanisa dogo la nyumbani ni chombo cha uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Hapa ni mahali pa kupokea na kunafsisha maagizo ya Mwenyezi Mungu katika uhalisia wa maisha.

Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani. Siku hii inaadhimishwa tarehe 3 Mei 2020. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya unaongozwa na kauli mbiu: “Maneno ya Miito” ambayo Baba Mtakatifu anasema ni: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, linawaalika waamini kuadhimisha Siku hii kwa kukuza na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho ndani ya familia, hasa kwa kusali zaidi ili kuombea miito mitakatifu. Kwa bahati mbaya, kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa mwaka huu wa 2020, hakutakuwa na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kuwapatia Majandokasisi Madaraja mbali mbali ya huduma ndani ya Kanisa.

Familia, Kanisa dogo la nyumbani linahimizwa kusali ili kuombea miito mitakatifu ya ndoa na familia, utawa na daraja takatifu ya upadre. Kanisa linawahitaji vijana: wema, wachapakazi, wachamungu na watakatifu watakaothubutu kujitosa katika miito mbali mbali pasi na kuogopa mawimbi mazito ya bahari kwani daima Kristo Yesu, yuko tayari kuwanyooshea mkono wake wenye nguvu na kuwakoa kama ilivyokuwa kwa Mtume Petro! Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID, watawa na wakleri wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa watu wa Mungu kiasi hata cha wengi wao kuhatarisha maisha na kwa hakika kabisa, kuna umati mkubwa wa Mapadre na Watawa ambao wamefariki dunia ndani na nje ya Hispania, wakati walipokuwa wanatoa huduma.

Kumbe, sala kwa ajili Siku ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2020 inabeba uzito wa pekee! Ni mwaliko kwa familia kusali na kuomba, ili Kanisa liweze kupata vijana watakaojitokeza kimasomaso kwa ajili ya huduma ya Neno, Sakramenti na Utume wa Kanisa. Vijana wawe wasikivu kwa sauti ya Mungu ili kila mmoja wao aweze kuitikia wito kadiri anavyojisikia kutoka katika undani wa maisha yake. Kanisa linawahitaji vijana watakaowasha moto wa Injili; vijana watakaoendeleza ari na mwamko wa kimisionari tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Familia, Kanisa dogo la nyumbani linaposali na kuombea miito, linaalikwa pia kuonesha mshikamano wa huruma na upendo kwa kuchangia katika mchakato wa kukuza na kuimarisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa!

Siku ya Miito Duniani 2020
28 April 2020, 12:13