Tafuta

Vatican News
Jumapili ya Matawi inafungua maadhimisho ya Juma Kuu ambamo waamini wanazamishwa kutafakari: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Jumapili ya Matawi inafungua maadhimisho ya Juma Kuu ambamo waamini wanazamishwa kutafakari: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.  (Vatican Media)

Jumapili ya Matawi: Mateso, kifo na ufufuko wa Yesu: Kiini cha Ukombozi wetu

Kristo Yesu anaingia mjini Yerusalemu kwa shangwe ili kwenda kuyakabili mateso yake kama utimilifu wa Maandiko Matakatifu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ndiye yule mtumishi mwaminifu wa Mungu anayewasaidia waja wake kuona maana na hatima ya mateso ya mtu asiye na hatia! Mateso ya Kristo ni kiini cha ukombozi wetu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari masomo ya dominika ya Matawi, dominika inayoliingiza kanisa zima katika Juma kuu. Liturujia yenyewe ya dominika hii ya Matawi, inaunganisha maadhimisho mawili makubwa. La kwanza ni tukio la Yesu kuingia Yerusalemu kwa shangwe na la pili ni la Mateso aliyoyakabili ndani ya Yerusalemu. Leo pia Kanisa linaadhimisha Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kijana, nakuambia: Inuka.” Lk. 7:14. Vijana wanakumbushwa mambo msingi yaliyojiri katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyofanyika mwezi Oktoba 2018 mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito. Tafakari hii inaongozwa na kitenzi “Inuka” yaani ufufuko na maisha mapya maneno ambayo yanajitokeza sana katika Wosia wa Kitume mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana: "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi” pamoja na Hati ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018.

 

Somo la kwanza (Isa. 50:4-7) ni kutoka kitabu cha Nabii Isaya. Katika somo hili, Isaya anamzungumzia mtu mmoja anayemtaja kwa jina la Mtumishi wa Bwana. Katika yale ambayo Isaya anayaeleza kuhusu huyu mtumishi, kuna mambo mawili ambayo hayakuwa ya kawaida kabisa katika fikra za mwisraeli. La kwanza ni namna yake ya kuyakabili mateso na la pili ni sababu zake za kuteseka. Katika jambo la kwanza, Isaya anachora picha ya mtu ambaye ni kama anapoona mbele kuna mateso yeye badala ya kuyaepuka anayafuata. Tena anayafuata bila kupinga bali anajisalimisha na kuyapokea hadi tone la mwisho. Hii haikuwa kawaida. Jambo la pili ambalo pia halikuwa la kawaida ni kwamba Isaya haelezi huyu mtumishi amekosea nini hadi ateseke hivyo. Badala yake tangu mwanzo anamuelezea kama ni mtu mwaminifu, mtiifu na aliye karibu na Mungu. Hili halikuwa la kawaida kwa sababu kadiri ya mapokeo yao, mateso aliyapata mtu kwa sababu ya makosa yake.

Unabii huu wa Isaya unalenga kudokeza dhana mpya katika Taalimungu ya Agano la Kale, nayo ni dhana ya “Mateso ya yule asiye na hatia”. Katika mazingira ya wakati wa Isaya, iliweza kutafsiriwa kuwa inawezekana ni Isaya mwenyewe alikuwa akijizungumzia kama ndiye yule anayeteseka bila hatia kwa sababu ya ugumu alioupata katika utume wake wa unabii. Katika nafasi nyingine, ilionekana kuwa Isaya anaizungumzia Israeli nzima kama taifa la Mungu kuwa ndiye mtumishi anayeteseka bila hatia kwa sababu ya tukio lake la kupelekwa utumwani. Pamoja na tafsiri zote hizi, unabii huu unaonekana kumuelekea moja kwa moja Kristo kama ndiye mtumishi wa Bwana ambaye bila kuwa na hatia yoyote aliyakabili mateso.  Ni kwa Kristo pia tafsiri hii inapata maana kwa sababu ni yeye anaonesha pia ni nini thamani au matokeo ya kuyakabili mateso bila hatia.

Somo la pili (Fil 2:6-11) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Somo hili linaendeleza dhana ya somo la kwanza juu ya Kristo mtumishi anayeyakabili mateso bila ya kuwa na hatia. Mtume Paulo anaionesha dhana hii kwa kukazia juu ya unyenyekevu na utii aliokuwa nao Kristo. Mtume Paulo anaonesha katika somo hili kuwa isingekuwa rahisi kwa mtu asiye na kosa kukubali kuwekwa katika kundi la wakosaji na tena akiwa huko kuteswa vikali namna alivyoteseka kama hana unyenyekevu na kama hana utii. Mtume Paulo anaenda mbali zaidi kuliko Isaya na anaonesha ni nini kilitokea sasa baada ya mateso hayo. Baada ya mateso hayo Mungu alimtukuza mno na akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina ili katika jina hilo kila goti lipigwe na kila ulimi ukiri kuwa Yesu Kristo ni Bwana kwa utukufu wa Mungu Baba.  Somo hili linatoa uhakika wa utukufu unaokuja baada ya mateso yaliyopokelewa kwa unyenyekevu na utii. Pamoja na uhakika huo, somo hili pia linatoa mfano na njia ya kufuata kwetu sote tunaoitwa wakristo. Kama njia aliyoifuata Bwana wetu ndiyo hiyo, basi nasi hatuna budi kujibidiisha kuipitia njia hiyo hiyo ili tushiriki naye utukufu wake.

Injili (Mt. 26:14-27:66) Injili ya dominika hii ni historia ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo kadiri ya Mwinjili Mathayo. Kati ya mafundisho mengi yaliyomo katika simulizi hili, Mathayo hakuacha kuonesha pia kuwa Yesu ameshitakiwa, ameteswa na kufa msalabani kama mtu asiye na hatia. Mathayo analionesha hili katika vipengele vitatu vya simulizi analolitoa. Kipengele cha kwanza ni wakati wa Yesu kukamatwa. Mathayo anaonesha kuwa kukamatwa kwa Yesu kulitokana na usaliti wa mmoja wa wanafunzi wake aliyeitwa Yuda Iskarioti na sio kwamba alifanya kosa lolote liliopelekea kukamatwa kwake. Ni Yuda Iskarioti aliyewauliza wakuu wa makuhani “ni nini mtakachonipa ili nimtoe kwenu”? Na wao wakamuahidi vipande 30 vya fedha.

Kipengele cha pili ni juu ya mashataka yake. Mathayo anaonesha kuwa Yesu alishitakiwa katika mahakama mbili, moja ya kidini na nyinigine ya kisiasa. Katika mahakama ya kidini ambayo ndiyo Baraza kuu la Wayahudi yalitajwa makosa mawili; kwamba amesema atalivunja hekalu na kwamba amejiita mwana wa Mungu. Hata katika haya Mathayo haachi kutaja na kurudia rudia kuwa ulikuwa ni ushahidi wa uwongo ili wapate kumuua. Huenda ndo sababu hawakumhukumu kwa kupigwa mawe kama ilivyokuwa desturi ya mahakama hii kwa sababu walijua hana hatia. Wakaamua wampeleke kwenye mahakama ya kisiasa kwa Pilato. Wakiwa kwa Pilato mashitaka sio tena kutaka kuvunja hekalu wala kujidai mwana wa Mungu bali ni kuwa amejiita mfalme wa wayahudi. Pilato anashindwa kuona kosa hilo kwa Yesu lakini pia anashindwa kumuachia huru kwa kuogopa shinikizo la watu.

Kipengele cha tatu ni maneno ya akida baada ya Yesu kufa Msalabani. Baada ya hayo yote kuwa yametokea, Akida (askari anayeongoza kikosi cha askari 100) aliyekuwa pale chini ya msalaba akakiri na kutamka “hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu”. Katika Injili ya Luka, akida huyu huyu anaripotiwa kusema “hakika mtu huyu alikuwa mwenye haki” (Lk. 23:47). Mtu mwenye haki ni mtu asiye na hatia. Katika mwanga huo, tunayaelewa zaidi maneno ya Mwinjili Mathayo kuwa akida anapokiri kuwa Yesu ni mwana wa Mungu anakiri kuwa Yesu hakuwa na hatia. Ni kwa namna hii Injili hii inakamilisha unabii wa nabii Isaya katika somo la kwanza kuwa Yesu ndio yule mtumishi asiye na hatia ambaye amekubali kuyapokea mateso ili kwa mateso yake aweze kumkomboa mwanadamu na kumuingiza katika utukufu wa Mungu Baba.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, mambo mawili makubwa ambayo Kanisa linayaadhimika katika dominika ya Matawi ni tukio la Yesu kuingia Yerusalemu na kumbukumbu la mateso yake. Ndiyo maana katika liturujia ya matawi tunafuata utamaduni wa tangu kale wa kubariki matawi na kuandamana nayo na pia kusikiliza katika injili historia ya mateso ya Yesu. Kihistoria, tangu karne ya 5, huko Israeli katika dominika hii wakristo walikusanyika  katika mlima wa Mizeituni na kufanya maandamano hadi Yerusalemu wakiwa na matawi ya mizeituni. Ibada hii ilisambaa hata nje ya Israeli na maandamano yakaanza kufanyika kukumbuka tukio hilo la Yesu kuingia Yerusalem. Utamaduni huu umeingia katika Liturujia, na sasa sio tu tendo la kumbukumbu ya kihistoria bali ni tendo la kukiri hadharani imani na utayari wetu wa kumfuata Kristo ambaye kwa mateso yake sisi tumepona. Ndiyo maana hata katika kipindi hiki ambacho maandamano hayawezi kufanyika kwa sababu ya kuepuka maambukizi ya homa ya mapafu inayosabishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bado alama ya tendo lenyewe inabaki.

Matawi yanayobarikiwa ni Kisakramenti. Tangu mwanzo wakristo wamekuwa wakiyapeleka nyumbani na kuyatunza kwa uchaji ili kuzikinga nyuma, mashamba na mifugo dhidi ya mashambulizi ya pepo wabaya. Wasafiri katika vyombo vya maji wamekuwa wanatunza pia matawi katika vyombo vyao wakiamini katika nguvu ya Mungu kuwakinga dhidi ya machafuko ya bahari yanayoweza kuvizamisha vyombo na kuleta mauti.  Dhamira ya pili ambayo ni ya mateso ya Kristo ina lengo la kukazia kuwa kwa Yesu mateso hayo hayakuwa jambo lililomkuta kwa bahati mbaya au bila kutarajia kama vile ajali inavyotokea bali ulikuwa ni ndani ya mpango wa Mungu wa wokovu kwa mwanadamu. Kama ilivyokuwa imetabiriwa kuwa mateso ya mtumishi asiye na hatia yataleta wokovu kwa wengi, Kristo amejidhihirisha kuwa ndiye huyo mtumishi aliyetabiriwa na ameingia katika mateso hayo ili awakomboe wengi na kuwaingiza pamoja naye katika utukufu wa Baba.

Jumapili ya Matawi
04 April 2020, 09:10