Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Nyaisonga: Pasaka ni Sherehe ya Uhuru wa watoto wa Mungu waliokombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti; ni sherehe ya tafakari na ushuhuda! Askofu Mkuu Nyaisonga: Pasaka ni Sherehe ya Uhuru wa watoto wa Mungu waliokombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti; ni sherehe ya tafakari na ushuhuda!  (ANSA)

Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga: Pasaka: Uhuru wa Taifa la Mungu

Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga anasema, Pasaka ya Bwana ni Sherehe ya uhuru wa watoto wa Mungu. Ni muda muafaka wa kufanya tathmini, mahali walikotoka, walipo na wapi wanatarajia kwenda. Ni nafasi ya kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kumwilisha matunda ya Kwaresima katika maisha yao! Hii ndiyo Pasaka

Na Thompson Mpanji, Mbeya na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Umungu wa Kristo, unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, wa Jimbo Kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana tarehe 12 Aprili 2020 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, amesema, Sherehe ya Pasaka ni Siku kuu ya Uhuru wa Taifa la Mungu nchini Tanzania.

Ni wakati muafaka kwa Kanisa la Mungu nchini Tanzania kujitathmini, lilipotoka, lilipo na linapoelekea. Sherehe ya Pasaka ni kilele cha ukombozi wa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Kristo Mfufuka ameliondoa giza la dhambi na mauti kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Sherehe hii inawawajibisha Wakristo kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa jirani zao. Pasaka ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya Shetani, Ubilisi. Ni wakati muafaka wa kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuimarisha mchakato wa umoja, upendo na mshikamano. Pasaka ni siku ya ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwamba, huu ndio msingi wa imani ya Kikristo!

Pasaka ya Bwana anasema Askofu mkuu Gervas Nyaisonga, iwasaidie watu wa Mungu nchini Tanzania kuonja matunda ya Mfungo wa siku 40 za Kipindi cha Kwaresima. Huu ulikuwa ni muda wa sala, tafakari, matendo ya huruma na mkazo wa maisha ya Kisakramenti. Ni wakati muafaka kwa waamini kuchunguza dhamiri zao na kuona ni mahali gani ambapo wamefanikiwa hasa katika maisha ya kiroho? Je, wamefanikiwa kujijenga zaidi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji? Kwa Mapadre, Je, wameadhimisha vyema; kwa ibada na uchaji Sakramenti za Kanisa? Ikumbukwe kwamba, Sakramenti huweka msingi ya maisha yote ya Kikristo. Sakramenti zinawajalia waamini kushiriki hali ya Kimungu kwa kupata neema inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, na huo unakuwa ni mwanzo, kukua na malisho ya maisha ya kawaida. Wanaimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara na katika Ekaristi wanapokea chakula cha uzima wa milele. Hiki ni kielelezo cha utajiri wa Kimungu unaowasaidia waamini kufikia ukamilifu wa upendo.

Pasaka ya Bwana anasema Askofu mkuu Nyaisonga ni muda wa kutafakari mapungufu yaliyojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa! Janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, linatishia na kutesa roho na mwili. Hivyo kuna kila sababu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushirikiana na kushikamana ili kupambana na Corona, COVID-19, ili hatimaye, kuitokomeza kutoka katika uso wa dunia! Kuna baadhi ya nchi, Ibada ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, imehudhuriwa na Mapadre na watawa peke yao. Katika miji mikubwa, kumekuwepo na udhibiti mkubwa wa mahudhurio ya waamini Makanisani. Ugonjwa wa Corona, COVID ni tishio kubwa kwa maisha na usalama wa watu wote. Kuna kila sababu ya kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID. Huu ni wakati muafaka wa kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wa Serikali, ili waweze kusimama kidete, kuliongoza vyema Taifa nyakati hizi za janga la maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuzingatia maelekezo na maagizo yanayotolewa na viongozi wa Serikali na wataalamu wa afya, huku wakiendelea kuwasimamia na kuwalinda watoto wao. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna umati mkubwa wa watoto unaodhurura hovyo mitaani, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya watoto hawa. Kuna haja kwa wazazi na walezi kuwa karibu zaidi na watoto wao wakati huu!

Askofu Mkuu Nyaisonga: Pasaka 2020

 

15 April 2020, 10:49