Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili IV ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni mwanga wa maisha na uzima wa milele. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili IV ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni mwanga wa maisha na uzima wa milele.  (AFP or licensors)

Tafakari Neno la Mungu Jumapili 4 ya Kwaresima: Mwanga wa Mataifa

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kwaresima inajulisha mambo makuu mawili; la kwanza ni kuwa Kristo ni mwanga wenye kumwangazia kila mtu; ukijitenga naye utaingia katika gizani la dhambi, hutakuwa na furaha na matokeo yake ni kifo. La pili ni kuwa: kila mkristo anaangazwa na Kristo na anapaswa kuingia katika mwanga na kuonesha njia kwa wengine wanaomzunguka.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, domenika ya nne ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Domenika hii inajulikana kama domenika ya furaha. Ni dominika ya furaha kwa sababu Kanisa linafurahi kwa kuwa tumekwishamaliza zaidi ya nusu ya kipindi cha kwaresma na tunakaribia kuadhimisha mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hata wimbo wa mwanzo unasema; furahi Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao. Katika domenika hii linafanyika takaso la pili la Wakatekumeni watakaobatizwa katika Kesha la Pasaka. Domenika hii inajulisha mambo makuu mawili; la kwanza ni kuwa Kristo ni mwanga wenye kumwangazia kila mtu; ukijitenga naye utaingia katika gizani la dhambi, hutakuwa na furaha na matokeo yake ni kifo. La pili ni kuwa: kila mkristo anaangazwa na Kristo na anapaswa kuingia katika mwanga na kuonyesha njia kwa wengine wanaomzunguka.

Somo la kwanza la Kitabu cha kwanza cha Samweli linaeleza kuwa licha ya Daudi kuwa mdogo kabisa kati ya kaka zake, Mungu aliamua kumchagua na kumpaka mafuta kupitia mikono ya Samweli ili awe mfalme, ili aanzishe kipindi kipya katika historia ya wokovu. Hivi Mungu humchagua ye yote anayemtaka kwa kazi yake bila kujali umri au hadhi aliyonayo katika jamii au familia, kimo wala urefu. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Waefeso anatukumbusha na kutufahamisha kwa wasiofahamu kuwa Mkristo ameingia katika mwanga wa Kristo kwa njia ya Ubatizo hivyo hatupaswi kuchanganya mienendo yetu ya kikristo na matendo ya giza bali tuyakemee kwani ni ya aibu.

Katika Injili ilivyoandikwa na Yohane, simulizi la kuponywa kwa kijana aliyezaliwa kipofu latufundisha mambo makuu mawili. Kwanza ni unyenyekevu katika kupokea ujumbe wa Mungu na pili ni kuwa mpango wa Mungu ni kinyume na matazamio yetu, ulemavu wa viungo sio laana bali kwa mlemavu bali Mungu amemfanya hivyo ili utukufu wake udhihirike. Kipofu amefunguliwa macho apate kuona mwanga tena. Basi tutafakari kidogo wazo la kuona mwanga. Yohane anatumia ishara ya mwanga na giza mara kwa mara kufafanua Maandiko Matakatifu. Kwa Yohane; Mwanga ni ishara ya uzuri, furaha, utakatifu na uzima ambavyo ni vya Mungu mwenyewe. Na giza ni ishara ya ubaya, masikitiko, dhambi na kifo na chanzo chake ni shetani. Mwanga na giza haviwezi kuwa mahali pamoja kwa wakati mmoja. Uwepo wa kimoja huondoa kingine. Kumbe, wajibu ni kuchagua mwanga au giza, Maisha au kifo, kuwa upande wa Mungu au upande wa shetani. Kuwa upande wa Mungu ni kumsikiliza na kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo Nuru na mwanga wa kweli, yeye mwenyewe anasema; mimi ndimi nuru ya ulimwengu; yeye anifuataye hataenda gizani kamwe bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele (Yoh 8:12).

Yesu ni nuru ya kila mkristo aliyebatizwa, tena ni nuru imtiaye uzima, nuru inayotakasa na kuponya, nuru inayoleta furaha. Yesu katika kumponya kijana aliyezaliwa kipofu amefanya tendo hilo hatua kwa hatua. Kwanza anamuonea huruma na kumwendea, kisha akatema mate akatengeneza tope, alimpaka machoni kwa hiyo tope, akamwambia aende kunawa katika Birika-Kisima cha Siloamu, Maana ya Siloamu ni aliyetumwa. Aliyetumwa ni Kristo. Yeye ndiye Kisima chetu kama Isaya anavyotwambia “kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu” ndiye Kristo katika sakramenti hasa ubatizo na kitubio, naye akaenda, akanawa, akarudi anaona. Naye anapoulizwa alivyopona, anaeleza kwa ufasaha na usahihi hatua hizi alizofanya Yesu. Anashuhudia kuwa ni yeye aliyezaliwa kipofu, na anakiri kwa ushujaa na ujasiri kuwa Yesu ndiye aliyemponya naye ni Nabii, hana dhambi akisema, Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye shambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake; humsikia huyo. Hajawahi sikika mtu yeyote ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo. Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.

Kuna fundisho zito lililofichika hapa; kujitegemea mwenyewe na kujitosheleza vinakwamisha njia yetu ya kumwamini Yesu; wokovu hauwezekani kwa yeyote anayetegemea hekima au nguvu zake mwenyewe. Kwa yule aliyeponywa; kuweza kuona tena ilikuwa tu hatua ya kuendea zawadi kubwa zaidi; imani kwa Yesu Kristo. Kuna makundi mbali mbali yaliguswa sana na muujiza huu; kundi la kwanza ni watu walioona na kushuhudia ule muujiza, hawa wapo walioshangaa na kuuliza yuko wapi wamfuate na wapo ambao walibaki katika kushangaa. Kundi la pili ni wazazi wa aliyezaliwa kipofu. Walichukulia ule muujiza kama maudhi, kwa maana uliwaletea usumbufu kwa viongozi wa kidini, ndio maana jibu lao walipoulizwa ameponaje wanasema, yeye ni mtu mzima, mwulizeni mwenyewe (Yoh 9:21). Wanakwepa uwajibikaji.

Kundi la tatu ni la Viongozi. Majivuno na chuki viliwazuia wasimfuate Yesu; walijiona wamekamilika na hii ilikuwa kikwazo kwao cha kumkiri Kristo ndiyo maana wanasema, tunajua kuwa huyu mtu ni mdhambi, sisi ni wafuasi wa Musa (Yoh 9:25-29) kinyume kabisa na Yule aliyezaliwa kipofu. Kwake yeye kila hatua katika tukio la kuponywa kwake ilimleta karibu zaidi na Yesu na kumjua zaidi kuwa ni nabii Yoh 9:17. Mchamungu kwani Mungu anamsikiliza yule amchaye na kutenda mapenzi yake (Yoh 9:31), uwezo wake wa kuponya ni kwa sababu ametoka kwa Mungu, anasema, Kama huyu hakutoka kwa Mungu asingeweza kufanya haya (Yoh 9:33). Kuteseka kwa ajili ya Yesu kulimleta kijana kipofu aliyeponywa karibu zaidi na Yesu kwani alifukuzwa na kutengwa na Jumuiya ya Wayahudi waliosali katika Sinagogi. Na hiki ndicho walikuwa wanaogopa wazazi wake kwani ilikuwa ni adhabu mbaya kwa myahudi. Yesu aliendelea kumtafuta na katika maongezi yake kati yake na yule mtu tunavutiwa na sehemu hii ya injili; Unamwamini Mwana wa mtu? Mwalimu, niambie yeye ni nani ili niweze kumwamini. Ndiye unayemwamini, ndiye anayesema nawe. Bwana, naamini. Akamwabudu.

Hapa tunaonja upendo wa Yesu na furaha yake katika imani thabiti ya yule kipofu, tunaonja furaha na amani itokayo katika moyo wa mtu anapojikabidhi kwa Yesu. Huu ni ukweli, kila mtu anayemwamini Kristo katika kweli na roho anapitia hatua hizi alizopitia huyu kipofu. Kwa hiyo tukio hili linatuhusu sisi pia; linaanza na huruma kwa upande wa Yesu, halafu inafuata kutambua hali yetu ya dhambi na kutojiweza kwetu, taratibu tunatambua upendo wake, wema wake, huruma yake na ukarimu wake, lakini tu kama tutayapokea mateso na madhulumu yanayotokana na kukiri imani yetu kwake. Ana heri yule asiyekata tamaa na kuishia njiani bali anavumilia mpaka mwisho mpaka imani kwa Yesu itakapomleta chini ya miguu yake.

Mkristo aliyeangazwa na Kristo anapaswa wakati wote kuwa taa inayomwangazia kila mtu anayekuwa karibu naye ndivyo mtume Paulo anawaambia wakristo wa Efeso katika somo la pili; wakati fulani mlikuwa gizani lakini sasa ninyi ni mwanga katika Kristo, kuweni kama watoto wa mwanga katika wema na katika kuishi vema katika kweli (Efe. 5:9). Mkristo ni mtu aliyeangazwa na Kristo ambaye anamtazama Mungu, anajitazama mwenyewe, anawatazama watu, anavitazama vitu vilivyomzunguka kwa macho ya Mungu yaani kwa mtazamo wa kimungu. Kwake Mungu ni baba anayempenda katika chochote kinachotokea katika maisha kwa njia ya matukio ya furaha na huzuni. Anajiona kuwa mtoto wa Mungu anayepaswa kutimiza mapenzi yake kwa upendo kila wakati. Tunapozidi kukaribia sikukuu ya pasaka Kanisa linatualika kutambua umaana wa ubatizo wetu kwa kuchunguza dhamiri zetu tuende kunawa katika bwawa la sakramenti ya upatanisho ili tusijebaki katika giza wakati Yesu akiujaza ulimwengu mzima kwa mwanga wa pasaka.

 

20 March 2020, 14:03