Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Kipofu anakuwa ni shuhuda wa Mwanga wa Kristo! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Kipofu anakuwa ni shuhuda wa Mwanga wa Kristo! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili IV ya Kwaresima: Shuhuda wa Mwanga

katika Biblia kulikuwa na dhana kwamba kama mmoja ni kipofu, mkoma na maskini huyo ametenda dhambi na amelaaniwa na Mungu: "Wanafunzi wa Yesu wakamwuliza wakisema, 'Rabi ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?" Yesu anajibu mara moja: "Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake."

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Roma.

Leo Yesu yuko karibu na Hekalu la Yerusalemu anamwona kipofu. "Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa." Kipofu wa kuzaliwa hajui chochote juu ya mwanga. Yaani mtu asiyeona, hawezi wala kupata picha ya maisha zaidi ya yale aliyo nayo. Mtu kipofu anaongozwa na wengine. Hatujui jina la kipofu bali tunaambiwa tu: "mtu, kipofu wa kuzaliwa". Kwa hiyo kipofu huyu anawakilisha binadamu wote wanaozaliwa bila kuona kutoka kuzaliwa. Aidha katika Biblia kulikuwa na dhana kwamba kama mmoja ni kipofu, mkoma na maskini huyo ametenda dhambi na amelaaniwa na Mungu: "Wanafunzi wa Yesu wakamwuliza wakisema, 'Rabi ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?" Yesu hataki kusikia fikra kama hizo ndiyo maana anajibu mara moja: "Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake." Maradhi ni tukio tu la maisha ya kibinadamu na siyo adhabu ya Mungu. Kwani kila binadamu anazaliwa kipofu na anahitaji kufunguliwa macho na mwingine. 

Tuzifuatilie hatua anazochukua Yesu katika kumponya kipofu huyu. Yesu akaanza kwanza kusema "Muda nilipo ulimwengu, mimi ni nuru ya ulimwengu." Baada ya kusema hayo, "Yesu akatema mate chini, akafanya tope kwa yale mate, akampaka kipofu kwa tope za macho." Mate (majimaji) ni mkusanyiko gandamizi wa hewa. Kadhalika hewa ni roho au DNA ya Mungu. Kitendo alichofanya Yesu alikifanya Mungu alipomwumba mtu wa kwanza: "Bwana akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai." (Mwa 2:7). Mate (hewa nzito) ya Mungu ndiyo iliyoupa uhai tope au udongo uliofinyangwa binadamu. Yesu kwa kujimwilisha kwake ameuvaa udongo (matope) yaani mwili wetu. Lakini mwili wake wa udongo umeungana tikitiki na roho ya Mungu ndani mwake. Kwa kujimwilisha ameiingiza roho ya kimungu duniani. Sasa Yesu alichukua udongo (mwili) wake yaani umwilisho wa ubinadamu wake halisi uliomwilishwa udongo au tope la duniani akachaganya na la Roho ya kimungu, na kuviweka machoni pa kipofu ili kumfungua macho.

Hapa ni dhahiri kuna maana ya kifumbo (metaphoric). Binadamu kipofu huyo hawezi kuona, yaani hana picha ya Yesu Kristu aliyejimwilisha ubinadamu wetu na mwenye roho kamili ya kimungu. Kitu pekee kitakachomfungua macho ni tope alilowekewa machoni mwake. Baada ya kumpaka tope machoni anamwagiza: "Nenda kanawe katika birika ya Siloamu" Neno hili shiloach kutoka Neno la kihebrabina shalua maana yake aliyetumwa. Mwinjili anataka kusema: "ukitaka kufunguka macho huna budi kwenda kwenye maji uliyotumwa kwenda." Sanasana kipofu anaambiwa kujiongeza, yaani kufanya kitu au kuchukua hatua ili aweze kufunguka macho. Picha hii ya kwenda kwenye maji ya aliyetumwa, inamaanisha kupokea paji la roho. Kipofu anapoteremka kwenda Siloamu kunawa maji, Yesu naye anafifia haonekani katika pilika-pilika hizo. Katika kipindi hicho kipofu anapitia changamoto za maisha mapya mbele ya vipofu wengine, yaani wale ambao macho yao bado hayajafunguka. Changamoto la kwanza, ni kutokutambuka. Kabla kipofu huyu aliketi na kuomba yala maskini sasa watu wanaulizana. "Je, huyu siye yule aliyekuwa ajkiketi a kuomba?" Wengine wakasema, "Ndiye." Wengine wakasema, "La; lakini amefanana naye." 

Hivi ni bayana kuwa mtu aliyeangazwa na Yesu hatambuliki kirahisi. Kabla ya kuponywa mtu huyu hakuweza lolote isipokuwa kutegemea wengine. Lakini sasa anaona, ni mtu mpya mwenye kufanya maamuzi yake mwenyewe. Ni mtu huru anatambua na kuelewa anakotaka kwenda, anafahamu anachokitaka katika maisha. Kabla yake alikuwa anasukumwa na vionjo na upofu wake, lakini sasa anasukumwa na roho. Kwa hiyo endapo kabla alikuwa na kiburi, mwenye majikuu, na mwenye majibu ya karaha, mwenye kufikiria pesa tu na kuiomba yala maskini, lakini sasa amegeuka na amekuwa mtu mwema, mwaminifu, na mwenye kujali wengine. Ndiyo maana wengine wanajiuliza kulikoni mabadiliko haya ya ghafla? Katika mashaka hayo, kipofu mwenyewe anawatolea uvivu na kusema: "Mimi ndiye." Baada ya majibu hayo, wakaendelea kumwulizia "Macho yako yaifumbuliwaje?" Naye akaanza kuwaelimisha: "Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho."  

Yaani ni kama angesema: nimefanikiwa kukutana na mtu mwenye utu wa kweli na aliyefanikiwa katika maisha"Akaniambia Nenda Siloamu ukanawe, baada ya kutoka huko, nimefunguka macho." Yaani huko kwenye maji ya aliyetumwa ni roho ya Mungu ukizamishwa unayabadili maisha yako. Yaani aliyebatizwa kwenye kisima cha maji ya ubatizo anaibuka binadamu mpya. Hali hiyo inaweza pia kutokea katika maisha yetu, kwamba mmoja anaweza kukiona kifo, ugonjwa, siasa, serikali, maisha ya ndoa nk, akayaona kwa namna tofauti kabisa na wanavyoona wengine. Hadi watu wakabaki kushangaa na kujiuliza. Kulikoni mmoja anaona ulimwengu kwa jicho tofauti na wanavyoona wengine. Kutokana na sintofahamu hiyo watu waliwakilishe shauri hilo kwa mafarisayo ili kipofu huyu akemewe kwa sababu anaonekana kuwa tofauti na wengine: "Basi wakampelekea kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani." Zaidi ya hapo wakambambatizia na kesi ya Yesu aliyeonekana kutofuata mapokeo na mila za utamaduni wao hususani wa kuvunja Siku ya Sabato.

Mafarisayo wanawawakilisha wale wote walio wafungwa na fikra zao na dhana zao bila ya kufunguka macho mbele ya mawazo mapya ya Injili. Katika muujiza huu tunaona mpito wa kutoka giza hadi mwangani hasa kwa wale waliojiruhusu kufunguliwa macho na Injili au habari njema na kuona sura ya Mungu ambayo ni upendo. Mafarisayo hao wanamsahili maswali kipofu aeleze jinsi gani alivyopata kuona. Mwanzoni alijibu: "Mtu yule aitwaye Yesu." Wanazidi kumdadisi tena kwa dharau bila kutaja hata jina la Yesu bali wanasema tu: "Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho?" Naye kipofu anaona aongeze sifa zaidi juu ya Yesu anawajibu kwa ufupi kabisa kiasi cha kuwakata maini: "Mimi binafsi ninamwona kuwa 'ni Nabii.'" Wayahudi hawa wanaompinga Yesu na Injili yake hawakusadiki ushuhuda wa kipofu wakaenda kuwadadisi tena wazazi wake. Wazazi, ni wale wanaowaingizia watoto thamani za kimila na utamaduni. Kumbe, sasa mtoto amekutana na Kristo hivi amegundua thamani ya maisha mapya. Wanawauliza wazazi: "Huyu ndiye mwana wenu ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa?" 

Wazazi wakaruka kesi, wanaogopa mkong’oto wa mawe. Kwamba hata nao hawajui chochote juu ya huu mwanga mpya. Wanachojua ni kwamba huyo ni mtoto wao na kwamba alizaliwa kipofu. Ni dhahiri kwamba wao wanaweza kutoa maelezo juu ya maisha ya kibaolojia waliyompa mtoto wao. Lakini huu ya maisha ya kiroho ya kufungua macho hayo hawajui. Hapa hata wazazi nao wanaogopa na wameshtushwa juu ya uponyi wa kuangalia mambo kwa mtazamo mpya. Kwa sababu hali hiyo itawalazimu wabadili mtazamo wao wa mambo. Mtoto wao amekiacha kile walichomwingizia mtoto wao kwa sababu amevumbua kitu kipya na kwamba sasa wazazi wataachwa peke yao katika mapokeo yao. Aidha wanaogopa kwa vile wakuu wa dini watawatenga na jumuiya ya kitamaduni wao. Katika awamu ya mwisho ya mazungumzo na Mafarisayo unaona jinsi wanavyojaribu kumlaghai kipofu afikiri kadiri ya mawazo yao. Katika majibu yake utagundua tabia nzima ya mtu aliyeangazwa. Awamu ya kwanza Mafarisayo hao walitofautiana fikra. Katika amamu hii wote wanatetea maslahi na mapendeleo yao. Awamu hii wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu wakamwambia: "Mpe Mungu utukufu, Sisi tunajua ua kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi." Yaani kwa sababu wewe sasa unaona basi wewe umshukuru Mungu tu, ila ishiana na yule mtu mdhambi.

Kumbe, kipofu hataki kuchanganywa anawajibu bila woga wala makunyanzi: "Kwamba yeye ni mwenye dhambi mimi hilo sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona." Wanampeleleza tena: "Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani?" Sasa wanatafuta mwanya wa kumshika Yesu kwa vile amevunja sabato (siku ya Bwana). Kwa hiyo wanamdai kipofu aachane mara moja na mdhambi huyo. Lakini kwa vile kipofu yule sasa ni mtu huru hajali kutoa majibu hata yale yanayoweza kumponza. Anawajibu: "Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena?" Aidha anawaudhi zaidi: "Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?" Hapo Mafarisayo wanachefuka nyongo na kumkashifu: "Wewe u mwanafunzi wake yule;" hawasemi Yesu. "Sisi tu wanafunzi wa Musa. Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako." Majibu haya yanaashiria woga waliokuwa nao watu wenye mamlaka. Wanashindwa kupambana kwa kihoja mbele ya mwanga mpya wa Injili. 

Kipofu anaendelea kuwajibu: "Hii ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho! Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafunua mapenzi yake, humsikia huyo. Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo. Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lolote."  Mafarisayo kumkashifu zaidi kipofu: "Ama! Wewe ulizaliwa katika Dhambi tupu, nawe unatufundisa sisi?" Hapohapo wakamtenga na jumuiya: "Wakamtoa nje." Hebu sasa tuione tabia ya mtu aliyetoka gizani, sasa ameangazwa na yuko katika mwanga wa Kristu na anaifuata Injili. Tabia ya kwanza, ni kutokuelewa ili kueleweshwa. Mafarisayo walimwuliza kipofu: "Ni nani mtu huyo?" Kipofu anajibu tu kifupi: "Mimi sijui". Kadhalika wazazi na majirani wa kipofu wanajibu "Hatujui." Wakuu wa dini (Wayahudi) wanapothibitisha: "sisi tunajua kuwa huyo ni mdhambi." Yeye anajibu tu "mimi sijui." Baadaye anapokutana na Yesu anayemwuliza "Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?" 

Kipofu anatoa jibu lilelile: "Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?" Kutokana na jibu hili, kipofu huyu anabakia daima kuwa ajenda ya majadiliano. Yaani, kipofu hana mazingira ya kujitetea mwenyewe. Kwa sababu ukweli daima unakubalika kwa wenyewe. Hakuna sababu ya kuogopa ukweli kwa sababu ukweli unatoka kwa Mungu. Kule kukubali kutokujua ndiko kunakoletesha mwanga wa ukweli mpya. "Kubali yaishe!" Tabia ya pili, mtu aliyeangazwa anajijua yeye ni nani na kwamba amebadilika. Kwa hiyo pale wanapohangaika kuulizana na kumfananisha, yeye mwenyewe anajitambulisha: "Mimi ndiye". Tabia ya tatu, anajijua kuwa ni mtu huru na anaeleza ukweli anaouamini na kuuishi."Ukweli utawafanya kuwa huru."  Hasa baada ya kuupokea mwanga mpya. Tabia ya nne, mtu huyu anamwabudu kwanza Mungu, anamtanguliza Kristu na Injili yake. Kisha anaheshimu viongozi wa dini, serikali na siasa. Lakini hawaogopi kama vile wangekuwa miungu. Anapochokozwa anaonesha uhuru wake wote bila woga. Hana chochote cha kupoteza wala cha kupata. Mtu aliyeangazwa hajiruhusu kunyanyaswa au kuwa mnyonge. Hata kama anaonewa, kutukanwa hadi kusukumwa nje. Yeye anabaki ngangali kutetea ukweli. Yaani sio mwoga hata mbele ya madhulumu kwani yu mtu huru.

Wakati wa malumbano haya yote, kipofu yule alikuwa na roho ya Kristo, ingawaje Yesu mwenyewe hakuonekana kwa macho. Mtu aliyeangazwa hahitaji uwepo wa moja kwa moja wa Yesu. Kwani Yesu alimwacha ili kipofu ajiongeze mwenyewe na nguvu ya roho aliyempata. Baada ya mizengwe yote na kufukuzwa nje. "Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alienda kumtafuta." Kisha alimwuliza: "Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?" Naye akajibu akasema, "Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?" Kuamini maana yake ni kupokea katika maisha yangu. Kusadiki ni chaguo la upendo. Ushahidi wa imani wa mtu huyu katika neno analoliona, ufunuo wa mwana wa Mungu, anayemwalika kumpokea katika maisha yake. Hivi kama walivyomdhulumu mwana wa Mungu, hata wale wanaompokea na kumfuata watafuata njia hiyo hiyo. Yesu akamjibu: "Umemwona naye anayesema nawe ndiye." Toka hapa Yesu anatoa hukumu yake ya ukombozi kwamba yabidi kujihadhari sana na chaguzi tunazofanya. Mafarisayo wanajishuku na kujitilia wasiwasi juu ya kuona kwao. "Je, sisi nasi tu vipofu?" Hata sisi tujiulize swali hilo. Kuzaliwa kipofu siyo dhambi ila kuukataa mwanga wa Injili ni dhambi na upofu. Dhambi ni kuacha kujimwilisha ndani mwetu yule mtu wa kweli Yaani Yesu na kuwepo binadamu sawa na watoto wa Mungu.

21 March 2020, 18:05