Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, limetoa mwongozo unaopaswa kufuatwa kama tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya Corona, COVID-19 nchini Tanzania. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, limetoa mwongozo unaopaswa kufuatwa kama tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya Corona, COVID-19 nchini Tanzania.  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Tahadhari ya Corona!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuzingatia Tamko la Serikali kuhusu tahadhari ya kusambaa kwa Virusi vya Corona, COVID-19 limetoa mwongozo unaopaswa kufuatwa na waamini wa Kanisa Katoliki kuhusu: Sala, ushiriki katika ibada na Liturujia ya Kanisa; Huduma za Sakramenti za Kanisa, Maadhimisho ya Juma Kuu pamoja na kusitisha kwa muda makongamano na mikutano.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam.

Wapendwa, Maaskofu, Mapadri, Watawa na Waamini wote, Tumsifu Yesu Karisto.Wapendwa Taifa la Mungu, Sisi Maaskofu wenu kwa kuzingatia taarifa ambayo ilitolewa na serikali kuhusu kugundulika kwa watu wenye maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, hapa nchini na maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kasim Majaliwa tarehe 17/3/2020 ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivi nchi nzima, tunatoa maelekezo yafuatayo kwa waamini wote kuhusiana na huduma zetu za Kichungaji Katoliki;

A. SALA: Tunawaomba waamini wote kusali sala maalumu ili kumwomba Mungu atukinge dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, COVID-19. Tumwombe Mungu aendelee kutulinda kwa mkono wake na kuwaponya wale wote ambao wamepata maambukizi haya. Na wataalamu wetu wapate ufumbuzi wa kisayansi kuzuia kuenea kwa virusi hivi. Sala hii ni jukumu la kila mtu mmoja na jukumu la pamoja kama Kanisa kitaifa. Na Kutakuwa na sala maalumu itakayotolewa na maaskofu lakini kila mmoja wetu anaweza kusali sala inayomfaa kadri inavyoelekezwa na Askofu Jimbo. Ni wakati sasa wa kusali na kufanya toba kama taifa ili kujiunganisha na Muumba wetu.

B. KWENYE IBADA MBALIMBALI ZA LITURUJIA: Tunaagizwa kuzingatia taratibu za kujikinga na virusi vya Corona kadri serikali ilivyoagiza.  Hakikisha kutumia maji safi kwa kuosha mikono kwa sabuni mara kwa mara unapokuwa nyumbani kwako na unapokwenda kujumuika na wengine katika shughuli za kiibada. Maji ya baraka ya kuchovya kwenye milango yatasitishwa kwa muda na tutatakiwa kutumia maji ya baraka kadri tutakavyoelekezwa kijimbo. Wakati wa kutakiana amani tusipeane mikono na waamini wafumbe mikono na kuinamiana kwa heshima. Waamini watakomunika kwenye mikono tu, mapadri wazingatie hili wanapowakomunisha watu. Mapadri wanapoadhimisha Misa pamoja, watakomunika maumbo yote mawili kwa kuchovya Hostia Takatifu.  Waamini wote wanaombwa kutoshiriki ibada na Jumuiya ndogondogo kama unajisikia kuumwa. Badala yake washiriki ibada na huduma kwa njia ya redio na njia nyingine zitakazoelekezwa. Kila mwamini ajitahidi kutumia vitabu vya ibada vya kwake. Wale wote wanaohesabu fedha za matoleo watumie sanitizers kwa ajili ya kusafisha mikono.

C. HUDUMA ZA MASAKRAMENTI: Wagonjwa watapakwa mafuta kwa kutumia pamba na padri aambatane na mhudumu wa afya anapokwenda kwa wagonjwa. Wakati wa kupokea Sakramenti ya Kitubio, Padri anayeungamisha na mwamini wasiangaliane uso kwa uso, na kiti cha kitubio kisitumike bali maungamo yafanyike katika sehemu ya wazi kwa kuzingatia sheria za maungamo.

D. MAADHIMISHO YA JUMA KUU: Ibada ya kuabudu msalaba ishara ya wokovu wetu, itafanyika kwa kuinamia msalaba bila kuugusa. Sisi Maaskofu wenu tutaendelea kutoa maelekezo kadri serikali yetu itakavyoendelea kutoa miongozo na maelekezo ya jinsi ya kudhibiti maambukizi katika nchi yetu.

E. MIKUTANO NA MAKONGAMANO: Mikutano yote ya vikundi vya sala na vyama vya kitume itasitishwa kwa muda. Neema na Amani ya Kristo viwe nanyi nyote,

Ni sisi Maaskofu wenu,

+ Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga.

Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Maaskofu Tanzania: Tamko

 

26 March 2020, 14:13