Tafuta

Askofu Mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza anawaalika waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya sala, toba, wongofu wa ndani na kufunga. Askofu Mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza anawaalika waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya sala, toba, wongofu wa ndani na kufunga. 

Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande: Sala ya Kuomba Ulinzi

Askofu mkuu Renatus Nkwande anawaalika waamini kusali Sala ya Kuomba Ulinzi wa Mwenyezi Mungu dhidi ya hatari zote zinazomzungumka mwanadamu. Anawataka waamini kujikabidhi mikononi mwa Mungu, aliye mweza wa yote, ili pamoja na juhudi zinazofanywa na binadamu, aweze kuwanyooshea mkono wake wa huruma na mapendo na hatimaye, kuwaokoa katika haya yote.

Na Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, -Mwanza, Tanzania.

Amani na matumaini katika Fumbo la Msalaba ndio mwanzo wa mwaliko wa sala kutoka kwa Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania kwa ajili ya kuomba ulinzi juu ya hatari mbali mbali za maisha, lakini kwa wakati huu dhidi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Anasema kwa sasa jamii ya mwanadamu imekuwa ikikumbana na changamoto na hatari nyingi za kutisha, kutokana na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, magonjwa, majanga asilia nk. Kwa majuma kadhaa sasa, kumeibuka tishio kubwa dhidi ya ugonjwa wa unaosababishwa na virusi vya Corona, COVID-19. Dunia sasa imo katika hofu kubwa ya maambukizi yanayoenea kwa kasi na hatarishi kwa maisha ya binadamu.

Katika muktadha huu, Askofu mkuu Renatus Nkwande amewatumia waamini wa Jimbo kuu la Mwanza pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, Sala ya kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu dhidi ya hatari zote zinazomzungumka mwanadamu. Anawaalika waamini kujikabidhi na kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, Yeye aliye mweza wa yote, ili pamoja na juhudi zinazofanywa na binadamu, aweze kuwanyooshea mkono wake wa huruma na mapendo na hatimaye, kuwaokoa katika haya yote. Mtume Yakobo, anawasihi waamini kuungama dhambi na kuombeana kwa bidii, ili wapate kuponywa na hatari mbali mbali (Rej. Yak. 5:16).

Askofu mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza ameagiza Sala aliyowatumia watu wa Mungu Jimbo kuu la Mwanza isaliwe kila siku katika adhimisho la Ibada ya Misa takatifu, katika mkusanyiko wowote wa taasisi, vituo, Jumuiya na hata katika sala za familia. Kila mwamini ajibidishe kusali kwa bidii, katika nafasi binafsi na katika kujumuika na wengine. Waamini wote waendelee kufanya mfungo, toba na wongofu wa ndani, ili sala zao ziwe na nguvu ya kuzaa matunda wanayotumainia kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ifuatayo ndiyo sala yenyewe!

“Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako kwa maana zimekuwako tokea zamani” (Zaburi 25:6). Ee Mwenyezi Mungu Baba wa milele na Muweza wa yote, tunakuja tukiomba ulinzi kwako, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakumbana na changamoto na hatari nyingi zinazosababishwa na tamaa, husuda, kutokujali, visasi, magonjwa, mabadiliko ya tabianchi, majanga asilia na mengineyo mengi. “Moyo wangu unaumia ndani yangu, na hofu za mauti zimeniangukia. Hofu na tetemeko limenijia, na hofu kubwa imenifunikiza. Nikasema “Ningekuwa na mbawa kama njiwa, ningerukia mbali na kustarehe. Ningekwenda zangu mbali, ningetua jangwani. Ningefanya haraka kuzikimbia dhoruba na tufani” (Zaburi 55:4-8).

Tunakuomba Ee Mwenyezi Mungu, uwaangazie viongozi wa dini na serikali, pamoja na wanasayansi, kwa pamoja, wafanikiwe kutafuta suluhu ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona, na utuepushe na maambukizi yake. Uifanye mioyo yetu wanadamu, tupate kudumu katika upendo, kujali, kushikamana na kusaidiana kwa hali na mali, ili kila mmoja apate nafuu, na sote tujikwamue kutoka katika hatari za aina yeyote zinazotuzunguka. Udumishe amani, afya njema na utukinge na hila zote za yule Mwovu Ibilisi. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu…Amina.

Baba Yetu…

Atukuzwe Baba…

Tunakimbilia Ulinzi wako… Bikira Maria Afya ya Wagonjwa…

Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu…

Watakatifu wote wa Mungu… Mtuombee!

Sala ya Kuomba Ulinzi

 

19 March 2020, 15:33