Tafuta

Askofu Ludovick Joseph Minde wa Jimbo Katoliki Moshi amesimikwa rasmi tarehe 19 Machi 2020: Kauli mbiu "Sala na Kazi: Ora et Labora". Askofu Ludovick Joseph Minde wa Jimbo Katoliki Moshi amesimikwa rasmi tarehe 19 Machi 2020: Kauli mbiu "Sala na Kazi: Ora et Labora". 

Askofu Ludovick Joseph Minde: Jimbo Katoliki Moshi: Sala na kazi

Mwaliko wa kumpokea Askofu Ludovick Minde kama zawadi na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Moshi, ambalo kwa sasa linaongozwa na kauli mbiu “Sala na Kazi, Ora et Labora” katika shughuli za kichungaji. Maaskofu wametumia fursa hii kutoa Tamko kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Agapito Mhando na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Ludovick Joseph Minde wa Jimbo Katoliki la Moshi, amesimikwa rasmi tarehe 19 Machi 2020 katika Sherehe ya Mtakatifu Josefu, Mume wake Bikira Maria. Hii ni changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kumpokea Askofu Ludovick Minde kama zawadi na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Moshi, ambalo kwa sasa linaongozwa na kauli mbiu “Sala na Kazi, Ora et Labora” kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetumia fursa hii kutoa Tamko kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa muda wa siku mbili, yaani kuanzia Jumamosi tarehe 21-22 Machi 2020, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limekuwa katika kipindi cha sala, mafungo na tafakari kwa ajili ya kuomba huruma ya Mungu katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimekuwa ni tishio kwa usalama na maisha ya watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Askofu Ludovick Joseph Minde amesimikwa rasmi katika Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu, changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Moshi kutambua kwamba, Mtakatifu Yosefu ni baraka na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama alivyo Askofu Ludovick Joseph Minde.

Askofu Antony Lagweni Gasper wa Jimbo Katoliki Mbulu ndiye aliyeongoza Ibada ya Masifu ya Jioni, Mkesha wa Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria. Hii ni siku ambayo Askofu Minde alikabidhiwa fuguo za Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi. Familia ya Mungu ilitumia fursa hii kumkaribisha na kumwombea neema, heri na baraka katika maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Moshi. Haya yalikuwa ni masifu ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi na baraka ya Mtakatifu Yosefu, Msimamizi wa familia ya Mungu katika ujumla wake. Mtakatifu Yosefu alishiriki safari ya ukombozi kwa imani, matumaini, haki na usafi kamili. Akaruhusu mpango wa ukombozi upitie mikonini mwake, akazipokea changamoto zake kwa imani na matumaini makubwa, kiasi hata cha kukirimiwa  neema ya kuwa ni baraka na zawadi kwa watu wa Mungu.

Mtakatifu Yosefu alikuwa ni Baba mlishi wa Yesu na mchumba mwaminifu wa Bikira Maria na hatimaye, akalipokea Fumbo la Umwilisho katika imani, haki na usawa. Akasimamia utu na heshima ya Bikira Maria, mfano bora wa kuigwa katika: Ibada, Sala na Sadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia. Alisimama kidete kuilinda na kuitetea Familia Takatifu ya Nazareti, akaiokoa na hatari zote za kiroho na kimwili; akaonesha uhodari wake kama Baba wa familia katika hali ya unyenyekevu na kimya kikuu, huku akiruhusu mpango wa Mungu katika maisha yake. Tunu ya uaminifu, uchaji wa Mungu na ushirikiano wa kifamilia mambo muhimu sana hata kwa wazazi na walezi wa nyakati hizi ambazo, familia kama Kanisa dogo la nyumbani linakabiliana nazo! Askofu Antony Lagweni Gasper anasema, hii ni changamoto ya wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanatimiza vyema nyajibu zao kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Askofu Ludovick Joseph Minde anapaswa kuendeleza ari na moyo wa: kikuhani, kinabii na kichungaji; awe ni Baba mwaminifu, hodari na mchapa kazi, ili kweli aweze kuwa ni baraka na zawadi kwa watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Moshi. Atumie zawadi, karama na mapaji aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kuwaongoza watu kwa upendo; kwa kuwalisha kwa Neno la Mungu pamoja na Sakramenti za Kanisa. Awe ni mlezi na mtetezi wa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Moshi, awafundishe watu wake maisha ya sala na kanuni maadili na utu wema, kwa kuzingatia ukweli wa kinabii. Askofu Minde awe na moyo wa kibaba kama kiongozi na mchungaji kwa kutambua kwamba, yeye ni zawadi na baraka ya watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Moshi. Askofu Minde atende kwa haki na uaminifu; na aendelee kutunza hazina na amana ya imani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, Mtumishi mwaminifu wa Mungu. Asimamie kweli za kiimani, maadili na uchaji wa Mungu, ili kwa njia ya ushuhuda na mafundisho yake, asaidie kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani kama ilivyo mbinguni. Haya ndiyo matamanio halali ya watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Moshi.

Askofu Ludovick Joseph Minde katika salam na shukrani zake, kwa namna ya pekee kabisa amemshukuru Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu Francisko, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Kahama na Moshi. Alionesha shukrani zake za dhati kwa Mwenyezi Mungu na kwa Serikali kiasi hata cha kufanikisha maadhimisho haya licha ya changamoto kubwa iliyoko mbele ya watu wa Mataifa kwa sasa yaani: maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Tukio la kusimikwa kwake kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, ilikuwa ni sawa na kulazwa Msalabani. Tangu alipoteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Moshi, aliingia katika kipindi cha hofu na mahangaiko makubwa, lakini kwa utii mkubwa amekuja kutekeleza mpango wa Mungu kwa watu wa Mungu Jimboni Moshi. Askofu Ludovick Joseph Minde anamshukuru Mungu kwani ni kwa nguvu na neema yake inayomsadikisha kuanza utume kwa ari na moyo mkuu, huku akijiaminisha kwa Mwenyezi Mungu anayemtia nguvu katika udhaifu na mahangaiko yake ya kibinadamu!

Askofu mkuu Marek Solczyn’ski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ameonesha upendo wa pekee kwa Jimbo Katoliki la Moshi na hatimaye, limepata mchungaji mkuu. Kumbe, hizi ni shukrani kwa Baba Mtakatifu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha ambaye ameliongoza Jimbo Katoliki la Moshi kwa muda wa miaka 10. Kwa hakika amefanya kazi kubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Moshi! “Mzee wa Mwondoko” ataendelea kukumbukwa na wengi! Katika mahubiri kwenye Sherehe za kusimikwa kwa Askofu Ludovick Joseph Minde, Askofu mkuu Isaac Amani Massawe alibainisha sifa kuu za Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria na kuwataka wanaume katika familia kusimama kidete kulinda, kutetea na kutekeleza dhamana na majukumu yao badala ya “kukimbilia mitini” na kuzitelekeza familia zao. Amemshukuru Askofu Minde kwa kukubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake! Ameitwa, akateuliwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika kipindi cha miaka 19 kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Askofu Ludovick Joseph Minde aliwapenda watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kahama na alikuwa na sera na mikakati safi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao, lakini ameacha yote na kumtii Mungu. Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Moshi, ilisali sana kumwomba Mwenyezi Mungu ili awapatie mchungaji atakayestawisha, wema, utakatifu, haki, ukweli, umoja na amani; tunu ambazo zinapaswa kutekelezwa na watu wote wa Mungu Jimbo Katokiki la Moshi ambalo kwa sasa limetimiza umri wa miaka 67 tangu kuanzishwa kwake. Jimbo hili limehudumiwa na Maaskofu nane! Wanapaswa kushiriki kikamilifu kwa sala na matendo yao, ili kufurahia matunda ya imani. Kumbukumbu ya Miaka 70 ya Zawadi ya Imani Jimbo Katoliki Moshi, iwe ni fursa kwa waamini kujiandaa kikamilifu, ili kweli zawadi ya imani waliyo ipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo iweze kujidhihirisha kikamilifu, ili miito mitakatifu ndani ya Kanisa iweze kuchipua na kuchanua maua ya utakatifu wa maisha!

Waamini wajitahidi kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaendelea na maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa linaloongozwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu chemchemi ya uzima wetu”. Kongamano hili linatarajiwa kuadhimishwa katika Jimbo Kuu Katoliki la Tabora. Ibada ya Misa Takatifu katika kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 5 Julai 2020. Lengo ni kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa nchini Tanzania. Umoja na mshikamano wa watu wa Mungu pamoja na Askofu wao, ni jambo muhimu sana katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili!

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka watanzania kuwa makini kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali pamoja na Kanisa ili kusalimisha maisha ya watu dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hiki ni kipindi cha sala, toba na wongofu wa ndani. Baraza la Maaskofu Katoliki limetenga siku mbili kwa ajili ya kusali na kuomba huruma na neema ya Mungu dhidi ya janga hili ambalo limekuwa ni tishio kubwa kwa usalama na maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Watu wakumbuke pia kwamba, UKIMWI bado upo! Vitendo vya nyanyaso dhidi ya watoto wadogo pamoja na kuwanyanyapalia wagonjwa viachwe mara moja na badala yake, watu wajenge moyo wa huruma, upendo na mshikano wa dhati. Ameishukuru familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Kahama na kuwaomba watu wa Moshi kumpokea na kumpatia ushirikiano mkubwa Askofu Minde. Kwa pamoja wanapaswa kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni wakati wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi ya haki, amani na maridhiano; kwa watanzania kujisadaka na kujituma kikamilifu: kiroho na kimwili!

Askofu Ludovick Joseph Minde
23 March 2020, 11:41