Tafuta

Kwaresima ni hija ya mfuasi wa Kristo katika jangwa la maisha yake yake ya kiroho kwa njia ya: sala, kufunga, kutafakari Neno la Mungu pamoja na matendo ya huruma! Kwaresima ni hija ya mfuasi wa Kristo katika jangwa la maisha yake yake ya kiroho kwa njia ya: sala, kufunga, kutafakari Neno la Mungu pamoja na matendo ya huruma! 

Kwaresima ni safari ya maisha ya Jangwa la Kiroho kwa Siku 40

Maisha ya kila mfuasi wa Kristo ni safari ya jangwani kama walivyosafiri wanawaisraeli walipotembea miaka 40 jangwani, Yesu aliyejaribiwa jangwani kwa siku 40 nasi sasa tunatenga siku hizi 40 za mfungo wa Kwaresima, lakini daima hatuna budi kuongozwa na Roho Mtakatifu kama alivyomwongoza Yesu. Hiki ni kipindi cha neema, toba na wongofu wa ndani, ili kuchuchumilia utakatifu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mama Kanisa katika Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresma, Somo la Injili ni juu ya majaribu ya Yesu jangwani kwa siku 40 mchana na usiku. Namba 40 katika Biblia ni namba kamilifu kwa maana si tu kwa kipindi fulani bali siku zote za maisha yake akiwa hapa duniani alijaribiwa na yule mwovu, na ndio nasi tunaalikwa safari ya siku hizi 40, ni kipindi cha neema tunapoalikwa nasi kusali, kufunga na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa kweli maisha ya kila mfuasi wa Kristo ni safari ya jangwani kama walivyosafiri wanawaisraeli walipotembea miaka 40 jangwani, Yesu aliyejaribiwa jangwani kwa siku 40 nasi sasa tunatenga siku hizi 40 za mfungo wa Kwaresima, lakini daima hatuna budi kuongozwa na Roho Mtakatifu kama alivyomwongoza Yesu. Ni kipindi cha neema hivyo hatuna budi kumruhusu Roho wa Mungu atuongeze nasi katika safari hii ya kuwa jangwani kwa siku 40.

Somo la Injili ya leo, linatupa maswali mengi, mmoja aliwahi kuuliza swali, wakati Yesu akiongozwa na yule Ibilisi mpaka mnara wa Hekalu la Yerusalemu; ni nani alitangulia mbele ni Yesu au yule mshawishi? Na labda swali hili linafungua maswali mengi mengine; mfano ni mlima gani mkubwa kiasi cha kuwa juu na kuona milki zote za ulimwengu? Iliwezekana vipi au tuna maelezo gani leo ya kisayansi kwa mwanadamu kuweza kufunga bila kula na kunywa kwa siku 40 mchana na usiku? Na je huyo mshawishi alikuwa katika umbo gani? Na labda ni nani alimsimulia Mwinjili Matayo masimulizi haya kwa usahihi wake? Na kwa kweli maswali yanaweza kuwa mengi juu ya sehemu ya Injili tuliyoisikia leo. Yafaa kama tulivyotafakari siku nyingine kujua tangu awali aina ya uandishi na nia ya mwandishi.

Mwinjili Marko 1:12-13 juu ya majaribu ya Yesu anaiweka kwa ufupi kabisa kwa aya 2 tu, ni kuwa Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu jangwani kwa siku 40 na huko akajaribiwa na Ibilisi. Ndio kusema kama tulivyosema hapo juu namba 40 haina budi kueleweka kuwa si tu kwa siku hizo tunazoweza kuzihesabu bali siku zote za maisha yake.  Namba 40 ni namba kamili inayoonesha siku zote za maisha yake. Jumuiya zile za mwanzo za waamini walikiri juu ya nyakati ngumu na za majaribu kwa Yesu Kristo.  Na hasa wakati ule akiwa pale juu Msalabani; Marko 15:34 ‘’Saa  tisa alasiri Yesu akalia  kwa sauti kubwa, akasema, Eloi, Eloi, lema sabakthani?. Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?’’ Yawezekana baadhi yetu maneno haya ya Yesu yakawa magumu kueleweka ila yafaa tukumbuke kuwa Yesu hapa alikuwa ananukuu sala ya kutoka Zaburi 22 kama alivyokuwa akifanya kila mara katika maisha yake. Maisha yake na kila wakati yalikuwa ni sala, yaliongozwa na Neno la Mungu.

Ndio kusema waamini wale wa Kanisa la Mwanzo daima waliielewa Agano Jipya kwa kufanya rejea na kuongozwa na Agano la Kale. Na ndio aina ya uandishi anayotumia Mwinjili Matayo. Daima kuelewa ujumbe wake hatuna budi kuusoma sehemu nyingi kwa kuhusianisha na Agano la Kale. Kama vile Israeli ilivyokuwa Taifa teule lililoitwa kutoka katika nchi ya utumwa Misri ndivyo Yesu alivyo mwanapekee wa Mungu, aliyebaki mwaminifu daima katika misheni ya Mungu Baba. Na ndio mtindo wa Haggadah Midrashic unaotumika daima na Mwinjili Mathayo. Ili kuweza kuelewa Agano Jipya hatuna budi kulisoma na kulihusianisha au kupewa mwanga wa Agano la Kale.

Tunaona Yesu katika majibizano yake na yule mshawishi anafanya rejea kwa kunukuu sehemu tatu kutoka katika masimulizi ya Kutoka: Manung’uniko na malalamiko ya wanawaisraeli wakiwa jangwani kwa kukosa chakula na Mungu kuwashushia manna. (Kutoka 16), Tukio la kukosa maji (Kutoka 17), na kuabudu ng’ombe wa dhahabu (Kutoka 32). Hivyo Yesu anatembea na kusafiri na watu wake katika historia yao.  Yesu anajaribiwa majaribu yale yale yaliyowakuta wanawaisraeli wakiwa safarini jangwani. Na ndio Mama Kanisa katika safari hii ya Kwaresma anatualika katika Dominika hii ya kwanza kukumbuka kuwa nasi si tu kwa siku hizi 40 bali siku zote za maisha yetu tutapitia majaribu kama waliyopitia wanawaisraeli na Yesu mwenyewe wakati wa maisha yake hapa duniani.

Yesu anapitia majaribu matatu, ni majaribu yanayogusa hasa mambo matatu, mahusiano yetu na vitu(mali), na Mungu na wengine. Hivyo maisha yetu yote yanagusa sehemu kuu hizo tatu, aidha vitu yaani mali, Mungu mwenyewe na wenzetu. Ni kipindi cha neema kujiangalia tena ndani mwetu kila mmoja katika maisha yake ni kwa namna gani tunahusiana na vitu, Mungu na wenzetu. Jaribu la kwanza: ‘’Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate’’ Bila chakula hakuna maisha, kwani chakula kinatuwezesha kuishi maisha ya kibailojia. Kula ni moja kati ya vitenzi vinavyotumika mara nyingi. Katika Agano la Kale tu linatumika mara 910, hivyo kuonesha ni kwa kiasi gani kula ni jambo la lazima na msingi kwa maisha ya kila mwanadamu.

Wanawaisraeli wakiwa jangwani Mungu anawapa manna kutoka mbinguni. Anawaalika kila mmoja kuchukua kiasi kile tu kinachomtosha kwa siku, ndio kusema tayari Mungu anamwandaa mwanadamu kuwa na kiasi na kufikiria wengine katika mahitaji ya siku kwa siku. Tunaona wanakosa imani kwa wema na ukarimu wa Mungu na badala yake wanaanza kujilimbikizia na hivyo kwenda kinyume na maagizo ya Mungu. (Kutoka 16) Kamwe hata nasi leo hatuwezi kutosheka na mali au vitu vya ulimwengu huu kwani jinsi tutakavyozidi kujilimbikizia ndio hamu na shauku ya kupata zaidi na zaidi. Yesu leo anatuonesha kiu na njaa ya kweli haipo katika mali au vitu au vyakula au vinywaji bali kiu yetu na njaa yetu itajibiwa kwa Neno la Mungu, kwa kumsikiliza na kumtii Mungu, ni kwa kuenenda kwa kuongozwa na Neno lake la uzima. Ni kwa kukubali kuongozwa tu na Neno la Mungu hapo tunapata kweli chakula na kinywaji kwa ajili ya nafsi zetu.

Kwaresima ni kipindi cha kuingia katika maisha yetu na kuangalia tena upya mahusiano yetu na mali na vitu vya ulimwengu huu. Ni kujiuliza kama maisha yangu na yako mintarafu mali za ulimwengu huu yanaongozwa na mashauri au Roho ile ya Injili, Roho ile anayotualika Yesu kuongozwa nayo si tu siku hizi 40 bali maisha yetu sote. Jaribu la pili: ‘’…Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu jitupe chini…imeandikwa usimjaribu Bwana Mungu wako’’ Ibilisi anamjaribu Yesu, Mwana wa Mungu kwa kunukuu Neno la Mungu, ni Ibilisi anayejipa sura isiyo yake. Lengo la Ibilisi kujaribu mahusiano ya Yesu na Mungu Baba.  Ni majaribu yanayokuja hata katika maisha yetu ya siku kwa siku kama wafuasi wa Yesu. Ni kishawishi cha kuanza kutilia mashaka upendo na uwezo wa Mungu katika maisha yetu. Kama wanawaisraeli walivyotilia mashaka wema na uwezo wa Mungu hivyo nasi kuna nyakati tunapitia sote katika maisha yetu, yule mshawishi anatutaka tuingie nasi katika mashaka ya namna hiyo.

Yesu alibaki mwaminifu hata katika nyakati zile ngumu kabisa katika maisha yake, na anabaki kuwa kielelezo kwetu kuwa hata nasi katika maisha yetu kuna nyakati ngumu tunapitia lakini hatuna budi kubaki waaminifu kwa wema na uwezo wa Mungu. Yesu alibaki daima katika mahusiano mema ya Mungu Baba na ndio anatualika nasi leo kwa njia ya sala kubaki katika mahusiano na Mungu. Sala sio kwa ajili ya kumtaka Mungu atende kama tunavyotaka sisi bali kumuomba neema na baraka zake ili tuweze kukubali mapenzi yake katika maisha yetu hata yakitutaka kutoa sadaka kubwa. Jaribu la tatu: ‘’…hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu…’’ Ni jaribu hasa juu ya kishawishi cha kuwa wakubwa na watawala au watu wa maana katika ulimwengu huu na badala yake Yesu anatualika wanafunzi na rafiki zake kuwa wadogo na watumishi daima. Mara nyingi katika maisha yetu tunajikuta njia panda kati ya ukubwa/utawala na utumishi/udogo. Ni kishawishi cha kuwa watu wa maana, watu wanaotumikiwa na kuabudiwa kwa ukubwa wao bali sisi tunaalikwa kuwa watumishi wasio na faida kwani ni Mungu pekee wa kuabudiwa.

Wanawaisraeli wakiwa jangwani wakamwacha Mungu na kujitengenezea mungu wa ndama wa dhahabu, ndio miungu ya mali au vitu ya ulimwengu huu, miungu tunayoitengeneza kwa mikono yetu. Hapa tunaweza kutoa msururu wa mambo au vitu tunavyovigeuza kuwa miungu yetu na kumpa kisogo Mungu wa kweli. Tunapogeukiwa viumbe na kumwacha Mungu hapo nasi tunageuka kumpigia magoti yule mwovu na kumwasi Mungu wetu. Yesu kamwe hakupigia magoti miungu ya dunia hii iwe watawala wa kisiasa wa nyakati zake, pesa, utumiaji wa silaha na mabavu kwa kujilinda na kujitetea, kusaka urafiki na watu wanaoonekana na kuitwa wa maana katika ulimwengu huu, hata fikra na falsafa za mafanikio kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu bali daima aliongozwa na kuishi Neno la Mungu Baba.

Katika safari ya siku hizi 40 ni fursa nyingine tunajaliwa tena mwaka huu ili kuangalia maisha yetu ya siku kwa siku mintarafu mahusiano yetu na mali, Mungu na wengine. Ni kipindi cha sala ili tutimize mapenzi ya Mungu, kufunga na matendo ya huruma. Yote lengo na shabaha yake ni ili tuweze kuwa na mahusiano mema zaidi na Mungu na jirani, ni mazoezi ya kiroho yanayotuweka karibu na Mungu na jirani. Kwaresma ni kipindi cha neema kwani kinatuleta tena karibu na Mungu na jirani, Pasaka ni kilele kwani kila anayekula kalamu ile ya Pasaka ni yule anayekuwa na mahusiano mapya na Mungu na jirani. Nawatakia tafakari na Dominika njema na Kwaresima njema.

29 February 2020, 09:31