Tafuta

Marehemu Padre Serenus Rupia, OSB: Mtawa, kiongozi na mwalimu aliueyejisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi: kiroho na kimwili! Marehemu Padre Serenus Rupia, OSB: Mtawa, kiongozi na mwalimu aliueyejisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi: kiroho na kimwili! 

Marehemu Padre Serenus Rupia, OSB: Atakumbukwa na watanzania wengi!

Kanisa nchini Tanzania linamkumbuka na kumwombolezea Marehemu Padre Serenus Rupia, OSB, aliyefariki dunia tarehe 12 Februari 2020 na kuzikwa huko kwenye makaburi ya Abasia ya Hanga, Jimbo kuu la Songea, tarehe 19 Februari 2020. Ni mtawa, kiongozi na mwalimu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi katika uhai wake!

Na Ivetha Kimburu, Agatha Kisimba; Songea na Padre Richard A. Mjigwa, Vatican.

Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu, ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!

Baba Mtakatifu Francisko akitafakari kuhusu Fumbo la kifo anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbu kumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili waweze kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Kifo kitakuja tu kwa wakati wake, kinaweza kuwahi au kuchelewa, lakini mwanadamu akumbuke kwamba, iko siku atakufa tu na hivyo kuungana na wahenga kwenye usingizi wa amani. Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao.

Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Ni katika muktadha huu, Kanisa nchini Tanzania linamkumbuka na kumwombolezea Marehemu Padre Serenus John Rupia, OSB, aliyefariki dunia tarehe 12 Februari 2020 na kuzikwa huko kwenye makaburi ya Abasia ya Hanga, Jimbo kuu la Songea, tarehe 19 Februari 2020. Ibada ya Misa imeongozwa na Askofu mkuu Damian Dallu wa Jimbo kuu la Songea. Katika mahubiri yake, Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki la Mbinga, aliwataka waamini kujitahidi kuishi maisha mema, adilifu na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu na jirani. Wahakikishe kwamba, wanatumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amewataka waamini kujitosa kikamilifu kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani zao, ili yale matendo mema wanayoyafanya yawe ni kumbu kumbu endelevu na urithi kwa wale wanaobaki hapa duniani!

Marehemu Padre Serenus  John Rupia alijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa njia ya maisha ya kuwekwa wakfu. Katika maisha na utume wake, ameliachia Kanisa hazina na utajiri mkubwa. Ataendelea kukumbukwa kwa karama na mapaji aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Alikuwa ni kiongozi makini, aliyekosoa na kukemea kwa wale waliokuwa wamepoteza dira na njia ya maisha. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa ni mlezi na mwalimu katika Seminari Ndogo ya Kaengesa, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Seminari Ndogo ya Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma, Seminari kuu ya Hanga, Jimbo kuu la Songea na Kibosho, iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi. Kanisa linamkumbuka na kumwombea, ili sasa aweze kupata maisha na uzima wa milele baada ya kuhitimisha hija ya maisha yake huku bondeni kwenye machozi.

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Padre Serenus John Rupia, OSB alizaliwa tarehe 10 Januari 1924 kwenye Parokia ya Kate, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya malezi na majiundo yake ya kikasisi, kunako tarehe 19 Agosti 1950 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Sumbawanga na baadaye kunako mwaka 1985 akajiunga na Shirika la Wabenediktini, OSB. Akaweka nadhiri zake za kwanza tarehe 6 Julai 1986 na nadhiri za daima tarehe 11 Julai 1992. Padre Serenus John Rupia amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96. Amefundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Padre kwa miaka 70 na kama mtawa miaka 34! Ndiyo maana, Familia ya Mungu nchini Tanzania ina kila sababu ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya mtumishi wake Padre Serenus John Rupia! Sasa apumzike katika usingizi wa amani!

Marehemu Padre Rupia

 

21 February 2020, 14:36