Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu "Ufalme wako ufike" Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu "Ufalme wako ufike"  (ANSA)

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Kwaresima 2020: Ufalme wako Ufike!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawaalika kutafakari juu ya “Ufalme wa Mungu” katika kipindi cha Kwaresima cha mwaka huu wa 2020. Baada ya kupokea baraka na mwanga wa Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo Tanzania na Maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari Oktoba 2019, ni vema sasa tukaweka mkazo juu ya maana ya Ufalme wa Mungu kwa kutamka na kueleza bayana.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam.

UTANGULIZI: Wapendwa wanafamilia ya Mungu: Mapadre, Watawa, Waamini Walei na watu wote wenye mapenzi mema: “Neema na iwe kwenu, na Amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” (2 Thes. 1: 2). Tunafurahi kuwaandikia ujumbe huu katika kipindi hiki maalum cha Kwaresima, kipindi cha Neema na Baraka nyingi. Ujumbe wetu wa Kwaresima wa Mwaka 2019 ulilenga kuamsha roho, moyo, tabia, desturi na mila zetu za Kikristo za kuthamini utu katika maisha ya kifamilia. Maisha ya familia yasipojengwa vyema yanaweza kuwa kikwazo kwa Ufalme wa Mungu kufika katika maisha yetu. Tangu mwanzo maisha na mahusiano katika familia yanahitaji mahusiano mazuri ili ufalme wa Mungu ufike katika familia zetu.

Tunapomaliza kutafakari juu ya familia, ambayo ni kiini cha kwanza cha uhai wa jamii na kituo cha kawaida ambamo mtu anaweza kupata maendeleo ya kiroho na kimwili (rej. Ecclesia in Africa, No. 85), tunawaalikeni kwa mara nyingine tena kutafakari kwa pamoja ujumbe wa mwaka huu usemao “Ufalme wako Ufike.” Kwa kuzingatia hayo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawaalika kutafakari juu ya “Ufalme wa Mungu” katika kipindi cha Kwaresima cha mwaka huu wa 2020. Baada ya kupokea neema, baraka na mwanga wa Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo Tanzania na Maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari Oktoba 2019, ni vema sasa tukaweka mkazo juu ya maana ya Ufalme wa Mungu kwa kutamka na kueleza bayana.

Siku zote tutilie maanani kuwa Yesu mwenyewe aliishi katika jamii halisi kijijini Nazareti, na akakubali hali, tabia na maisha ya jamii, huku akihubiri Ufalme wa Mungu. Hivyo katika kipindi hiki tuendelee kutafakari kwa kina juu ya “Ukuu wa Mungu”, na namna Neno la Mungu linavyokuza Ufalme wa Mungu na Mamlaka ya Watu; na jinsi mazoezi ya kiroho yanavyoimarisha Ufalme huo. Tuombe tuendelee kukua katika Kristo, kwa kuifanya mioyo yetu iwake mapendo yake. Aidha tuendelee kuomba kwa ajili ya uongofu wa mioyo yetu ili iwe na hofu ya Mungu adumuye milele, ambaye ufalme wake ni ufalme usihoharibika na mamlaka yake hudumu hata mwisho.

SURA YA KWANZA UFALME WAKO UFIKE Katika Maandiko Matakatifu, Maneno “Ufalme wa Mungu” yanatoa tafsiri iliyojijenga juu ya imani ya Kibiblia kuwa Mungu ndiye Mkuu, Bwana wa mabwana na Mtawala wa vitu vyote (rej. Zab 103:19, 145:13). Hii ilitokana na ukweli kwamba, sura za kwanza za kitabu cha Mwanzo zinaweka wazi mpango wa Mungu wa kuanzisha ufalme wake ulimwenguni. Baada ya juhudi za shetani za kuvuruga mpango huo wa Mungu kwa njia ya Adam na Eva (rej. Mwa 3:15), na baada ya vizazi vingi kupita, Mungu alimwahidi Baba yetu wa imani Ibrahim, kuwa kwa njia yake mataifa yote ulimwenguni yatabarikiwa; na kupitia yeye watapatikana wafalme (rej Mwa 12:1-3, 17:6). Kwa zaidi ya miaka 400 baadaye, Mungu aliwakomboa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri na kuwafanya “taifa teule”, “ufalme wa makuhani” na “taifa takatifu” (Kut. 19:6).

AGANO LA KALE: Mungu alikusudia kulifanya Taifa la Israeli kuwa mfano wa Ufalme wake ujao kwa ulimwengu mzima. Kabla wana wa Israeli hawajaingia nchi ya ahadi ya Kanaani, Musa aliwaambia kuwa watapata mfalme ambaye atateuliwa na Mungu (rej. Kum 17:14-20). Kufuatia kuingia kwao nchi ya Kanaani chini ya uongozi wa Joshua, na kipindi kirefu cha Waamuzi (1400 – 1050 K. K.), wana wa Israeli walimpata Sauli ili awatawale kama mfalme wao wa kwanza (rej 1Sam 10:24). Hata hivyo, Sauli hakumtii Mungu na kwa sababu hiyo Mungu aliamua kumwinua Daudi badala yake (rej. 1 Sam. 16). Baada ya Daudi kuteuliwa kuwa mfalme wa Waisraeli (rej. 2Sam. 5:3-4), aliutwaa mji wa Yerusalemu uliokuwa umetekwa na maadui na kulirudisha sanduku la Agano na Mungu wao kwenye mji huo. Daudi alitamani kumjengea Mungu nyumba, yaani hekalu la kudumu badala ya tabernakulo pekee (rej. 2Sam. 7:1-3).

Kama jibu kwa matamanio hayo, Mungu aliahidi kumjengea Daudi “nyumba” na kuanzisha ufalme wa uzao wa Daudi milele (rej. 2Sam. 7:4-16). Basi, mpango wa Mungu wa kuanzisha ufalme ulimwenguni ulifikia hatua hiyo mpya kwa njia ya Agano hilo la milele na Daudi. 1.1.3 Hata utawala wa kifalme wa Waisraeli ulipoanza kutetereka, bado manabii walisimamia Agano la Mungu na Daudi. Manabii hao waliwatangazia wana wa Israeli matumaini ya wakati ujao ya ujio mpya wa Mfalme wa uzao wa Daudi, yaani Masiya, ambaye angeanzisha utawala wa Haki, Amani na Furaha (rej. Isa 9:6-7, 11:1-10, 40:9-10, 52:7, Dn. 7:13-14, Zek 9:9). Agano la Mungu na Daudi linatimia kwa kuzaliwa kwake Yesu (rej. Isa 9:2-7, Lk. 2:1-14, Mt. 1:1- 25). Yesu ndiye Mfalme ambaye Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake (rej. Lk 1:32).

AGANO JIPYA.: Katika Agano Jipya, neno “UFALME” laweza kufasiriwa kama “milki” au “utawala”. Ni Ufalme wa Mungu ambao uko mbele yetu. Umeletwa karibu na Neno aliyemwilishwa (rej. Yn. 1:14); unatangazwa katika Injili zote na umedhihirika katika kifo na ufufuko wa Kristo. Utume wa Yesu unaanza kwa tangazo la ufalme wa Mungu kuwa umekaribia (rej. Mk. 1:15, Mt. 3:2, 4:17, 23, 9:35, Lk. 4:18-19.) Tangazo hili ni kiini cha ujumbe wa mahubiri ya Yesu na ni nukuu kutoka kwa Nabii Isaya (rej. Isa. 61:1-2). Ujio wa ufalme wa Mungu umekuwa pia ujumbe mkuu katika mahubiri ya wafuasi wa Yesu (rej. Mt. 10:7, Lk. 9:2, 10:9).

Sala ya Baba yetu ambayo Yesu anawafundisha wafuasi wake imebeba ombi la msingi, “ufalme wako ufike…. duniani kama mbinguni” (rej. Mt. 6:20, Lk. 11:2). Sala hii inadokeza kuwa ufalme huo bado haujafika kikamilifu duniani; ni ufalme ujao katika utimilifu wake siku zijazo. Maneno “mapenzi yako yatimizwe” yanadokeza kuwa ufalme ni Mapenzi ya Mungu yanayopaswa kutimizwa na wanadamu. 1.2.3 Ombi hili pia linamaanisha ufalme wa Mungu tayari upo katika ukamilifu wake huko mbinguni, hata kama bado haujakamilika duniani. Hata mafundisho ya Yesu mlimani (rej. Mt. 5:2-12) yanaonyesha ufalme wa Mungu kama jambo ambalo bado lipo mbali, na muda wake haujatimia. Lakini, katika utume wa Yesu wa uponyaji, ufalme wa Mungu upo tayari na umeanza kuonekana (rej. Mt. 12:28, Lk. 11:20). Kwa maneno mengine, ufalme wa Mungu umeshafika kwa ujio wa Yesu Kristo. Yeye amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Lakini inatupasa kuendelea kusali “ufalme wako ufike” kwa sababu hapa duniani wapo watu ambao bado hawamwamini Yesu Kristo na hivyo hawajajiweka chini ya utawala wake, yaani utawala wa haki, amani na maridhiano!

Yesu alitumia neno “Ufalme wa Mungu” kama dhana msingi ya mafundisho yake. Tunasoma, “Yesu alikuwa anakwenda kila mahali mkoani Galilaya akifundisha katika masinagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu.” (Mt.4:23). Ufalme wa mbinguni ni sehemu ya heri katika hotuba ya Yesu mlimani; “Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao.” (Mt. 5:3, 10). 6

Yesu analitumia neno “ufalme” mara nyingi katika mafundisho yake ili kuelezea utawala wa Mungu na mapenzi yake. Mara nyingi Yesu alitumia picha ya sherehe au mlo wa pamoja au tafrija ili kufundisha juu ya ufalme wa mbinguni. Yesu anasema, “Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni” (Mt. 8:11). Ufalme wa Mungu unaonekana wazi katika mafundisho na matendo ya Yesu. Maandiko Matakatifu yanaonyesha vigezo vya Ufalme wa Mbinguni kwa kadiri vinavyodhihirika katika maisha ya Kristo. Kwa mfano, pale Msalabani ni mtu aliyewapenda maadui zake; mtu ambaye haki yake ni zaidi ya ile haki ya Mafarisayo; anayetoa nira yake kwa wale wote wanaobeba mzigo wake na anayewaombea wote wanaomdhihaki (rej. Lk. 23:34). Anaonyesha kwamba msalaba sio kikwazo au pingamizi katika njia ya kwenda mbinguni, bali ni mwaliko wa ufalme wake.

Maisha na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa kujumuishwa na Sala ya Bwana, vyatualika sisi kujumuika naye kama watumishi katika Ufalme wa mbinguni. Hatimaye, tuweze kufanya kazi naye katika kusaidia mapenzi ya Mungu kufanyika duniani, kama ambavyo tayari yanafanyika mbinguni. Yesu anatufundisha njia ya kuuendea ufalme wa Mungu bila kujali tofauti zetu za kikabila, kitaifa, rangi, kidini, kiitikadi na kijinsia (rej. Gal. 3:28; 1 Kor 1:10-13).

KWA NINI TUNASALI “UFALME WAKO UFIKE?” Katika kipindi hiki cha Kwaresima, Tunasali “ufalme wako ufike” kwa ajili ya mwendelezo wa kueneza ufalme wa Mungu duniani, ili watu wote wajiweke kwa hiari yao chini ya utawala wa Yesu Kristo (rej. Flp. 2:6-11), na hivyo watimize mapenzi ya Mungu hapa duniani kama yanavyotimizwa katika ukamilifu wake wote huko mbinguni. Tunamwomba Mungu ili abadili mioyo ya maadui wake na kuwaleta kwake ili wamkiri Yesu Kristo na kumwamini kuwa ni Bwana wao (rej. Zab. 110) na kujiweka chini ya maongozi yake. Tunaomba kwa ajili ya ujio wa siku ambapo uovu, dhambi na uasi wote dhidi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu katika nyanja zote utakoma; na hivyo haki, upendo, amani na maridhiano vitatawala.

Tunasali Ufalme wa Mungu ufike, ili kila mtu aishi kadiri Mungu apendavyo. Wakristo lazima kwa moyo radhi watafiti namna ya kuupokea utawala wa Kristo katika maisha yao ya kila siku na huo utakuwa mwanzo wa kutimiza sala ya Bwana “Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.” Kwa mfano, makazi yetu lazima yawe kimbilio la wakosefu, maskini, wenye maradhi, wanaoonewa, wakimbizi, n.k. Urafiki wetu ukolezwe na neema, na shughuli zetu zote zifanyike kwa ajili ya utukufu wa Kristo (rej. Kol. 3:17, 23).

Tunaposali “Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni”, tunamwomba Mungu atutumie sisi kuonyesha nguvu ya ufalme wake leo, na jinsi mambo yatakavyokuwa hapo siku za usoni. Tukizingatia hilo, kutakuwa na jamii yenye kufuata sheria na amri za Mungu; yenye umoja na mshikamano; inayozingatia haki na amani; na hivyo kuwa na jamii yenye upendo isiyokuwa na migawanyiko. Kwa namna hiyo tutaishi vizuri kama atakavyo Mungu (rej. Ufu 11:15). Ili kufikia hapo ni lazima yaanzishwe mapambano thabiti kati ya “mwili na roho” (rej. Gal. 5: 16-25). Ni moyo ulio safi tu unaoweza kusema kwa ujasiri: “Ufalme wako uje.” Yeye anayetenda haki, katika matendo yake, mawazo yake na maneno yake, anaweza kumwambia Mungu: “Ufalme wako ufike.” (rej. Rum. 6: 12).

Sisi ambao tayari ni wana wa Ufalme na tumejiweka chini ya utawala wa Kristo tunaalikwa kuufanyia kazi ufalme wa Mungu ili kuwapa wengine mwanga wa Ufalme huo. Kwa upande mwingine tunaalikwa kufanya kazi tukiwa na matumaini makubwa kwamba juhudi zetu zitaleta mabadiliko, tukifahamu kuwa Bwana wetu atakuja kuyaweka mambo yote sawa. Kwa kuwa pale ufalme wa Mungu unapoongezeka, watu wa Mungu huwa “chumvi na mwanga” katika ulimwengu unaowazunguka (rej. Mt. 5:13- 16).

Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunaomba “Ufalme wa Mungu” uzidi kudhihirika wazi ulimwenguni ili kile anachotaka Mwenyezi Mungu kiwe kile kinachopaswa kutokea. Tunaombea mapenzi ya Mungu yatimizwe ulimwenguni, kwa nguvu ya Roho wa Mungu anayefanya kazi pamoja nasi na ndani yetu; na hii inatudai ushiriki wetu na kujitoa kikamilifu. Tunaposali, “Ufalme wako ufike,” tunasali kwa ajili ya ufalme (utawala) unaolinda daima uhuru kamili wa mwanadamu na unaopinga nguvu zinazoenda kinyume na mapenzi ya Mungu ulimwenguni. Uhuru wa mwanadamu unaotokana na ubinafsi, dhambi na uovu, huletwao na tamaa za kibinadamu, huzalisha matendo na tabia ambazo ziko nje ya mapenzi ya Mungu. Kwa mfano, kamwe si mapenzi ya Mungu kuwadhalilisha watoto, yatima na wajane. Mambo hayo yanapotokea ni kwa sababu ya msukumo wa dhambi za mwanadamu, kunakotokana na kutotii amri za Mungu, na si kwa sababu ya mapenzi ya Mungu.

Tunasali pia kwa ajili ya ufalme wenye nguvu kubwa ya kuzibadilisha nguvu ovu za mtu mmoja mmoja, taasisi, na ulimwengu kwa kuanza na sisi wenyewe. Tunasali “Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike,” ili utawala wa hapa duniani na utumishi wa kila namna uondokane na unyanyasaji; na msamaha umalize kabisa chuki; na kwamba upendo wa ufalme wa Mungu, usambaze mwanga wa Kristo ili neema, usawa na huruma vitawale katika kila eneo la maisha ya mwanadamu. Matokeo yake ni kuwa na jamii inayolinda utu wa mwanadamu mwenye sura na mfano wa Mungu (rej. Mwa 1:26-27).

HITIMISHO Tunaposali ili ufalme wa Mungu ufike tunaomba ili ufalme wa shetani utokomezwe. Tunapenda kuona kwamba shetani na nguvu zake, ujanja wake wote, ushawishi wake wa kiovu, uongo wake na uharibifu wake wote unatokomezwa. Vitu vyote vya ulimwengu na tamaa zake mbaya havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa yule mwovu. Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye mapenzi ya Mungu, ataishi milele. (rej. 1Yoh. 2:15-17

SURA YA PILI: NENO LA MUNGU LINAKUZA UFALME WA MBINGUNI: Lengo kuu la mahubiri na utume wa uchungaji katika Kanisa, daima lilikuwa, linabaki, na litabaki kuwa lile ambalo Mtume Paulo analitamka akisema:” Kwa hiyo navumilia yote kwa ajili ya wateule, ili nao wapate wokovu katika Kristo Yesu, ndio utukufu wa milele” (2 Tim 2:10). Kuupokea wokovu na utukufu wa milele, ndiko kuufanya Ufalme wa Mungu ufike. Mtume Paulo anamwandikia Timotheo waraka huu akiwa gerezani jijini Roma wakati ambapo anaonekana ameachwa na wengi wa marafiki zake (rej. 2Tim.1:15-18; 4:9-18) na anakabiliwa na kifo (rej. 2Tim. 3:6-8). Hivyo Mtume Paulo anamtia moyo Timotheo akimwambia “Nami katika hiyo (Injili) nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; Kwa ajili yake (Injili) navumilia mateso, hata nikifungwa minyororo kama mvunja sheria. Neno la Mungu halikufungwa” (2 Tim. 2:9).

Neno la Mungu ni tofauti na neno la mwanadamu. Mungu ndiye muumba wa mbingu na nchi na kila kilichomo; hata mwanadamu aliumbwa na Mungu mwenyewe. Mungu aliumba vitu vyote kwa Neno (rej. Mwa. 1:3-29). Hivyo, ni wazi kwamba Neno lake lina nguvu ajabu kiasi cha kutoweza kuzuiliwa na kitu chochote; ni kwa Neno hilo vyote vilifanyika na pasipo Neno kitu chochote kisingekuwepo ila Mungu mwenyewe (rej. Yn. 1:2-3). Neno linapaswa kutangazwa kadiri ya amri ya Mungu mwenyewe (rej. Mk. 16:15). Hivyo kwa Mkristo aliyepewa jukumu la kuhubiri Injili kwa ujasiri na kuimarishwa na paji la Roho Mtakatifu katika Ubatizo na Kipaimara (rej. Rum. 8:35- 37), ana jukumu la kuona kwamba ufalme wa Mungu unaenezwa bila kukata tamaa, licha ya changamoto anazokutana nazo.

AGANO LA KALE Katika agano la kale kuna mifano ya kutosha ya manabii waliohubiri Neno la Mungu kwa ujasiri bila kujali dhuluma na mateso waliyokutana nayo katika vifungo. Mungu aliponena na Musa na kumwambia aende nchini Misri kuwakomboa watu wake na kuwapeleka Nchi ya Ahadi (rej. Kut 3:10), Musa katika hali ya kibinadamu alijaribu kuweka mnyororo juu ya Neno hilo (rej. Kut 4:10). Pamoja na sababu alizozitoa mwishowe Musa alikwenda nchini Misri kadiri ya Neno la Mungu kwani hakuna kinachoweza kulifunga Neno la Mungu. Huko Musa alikutana na vikwazo vingi vilivyokuwa na lengo la kumkatisha tamaa ili ujumbe wa Mungu aliopeleka usitimie na lengo lisifikiwe. Lakini pamoja na hayo yote, wana wa Israeli walitoka nchini Misri na kuelekea katika Nchi ya Ahadi; na kila aliyejaribu kulizuia Neno la Mungu kutimia alipata mapigo makali (rej. Kut 7:8-11:1-9). 2.1.2 Ingawa hatuambiwi iwapo Nabii Isaya aliwahi kuhubiri akiwa mfungwa lakini mazingira hatarishi ya kisiasa ya wakati wake yalikuwa ni kama kifungo kwake.

Nabii Isaya alihubiri katika kipindi kigumu ambapo yeye pamoja na taifa zima la Israeli lilipitia shida za kisiasa hasa zile zilizosababishwa na uvamizi na ukandamizaji wa Waashuru wakati wa utawala wa Ahazi na Hezekia, wafalme wa Israeli na Yuda (736-700 K.K). Lakini pia Nabii Isaya hakuogopa hata kidogo kuwakemea wafalme na makuhani ambao walikosa uaminifu kwa Mungu, na alitamka waziwazi hukumu ya Mungu juu ya ukaidi wao bila kujali mateso ambayo yangempata mtu yeyote aliyemdhalilisha mtu wa cheo cha juu kama vile mfalme. Aidha Nabii Isaya kwa ujasiri mkubwa alilionya taifa la Israeli kwamba kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa Mungu lingeadhibiwa vikali na Mungu mwenyewe (rej. Isa. 6:1-13). 2.1.3 Mfalme Ahazi kwa mfano, alikuwa hana imani ya kutosha kwa Mungu. Hivyo alifanya mikataba ya kivita na mataifa jirani ili kuwashinda maadui wa Israeli. Lakini Nabii Isaya alimwambia mfalme Ahazi asiwaogope Waashuru na kwamba aombe ishara ya Imanueli, mfalme Masiya, ambayo nabii alitabiri kutimia kwake (rej. Isa. 6:6-12) ila mfalme alikaidi na alipata madhara makubwa.

Mfalme Ahazi alikosa imani na uaminifu kwa Mungu, akategemea nguvu za muungano na mapatano ya kijeshi zaidi na matokeo yake alipata madhara makubwa baadaye. Lakini pia taifa lote la Israeli lilikosa imani na uaminifu kwa Mungu na hivyo lilistahili adhabu na toba. Nabii Isaya alisisitiza kuwa Mungu mtukufu ni “Mtakatifu wa Israeli” aliyejiunga na Israeli katika Agano ili amkomboe. Njia ya kukombolewa kwake Israeli ni kumwamini Mungu, Mungu peke yake, katika haki na ukweli. Na kwa sababu Israeli hakumwamini Mungu atahukumiwa na ataangamizwa. Lakini waliobaki watamrudia Mungu na kuokoka (rej. Isa 4:3). Mfalme wao atakuwa Masiya mwana wa Daudi, atakayeweka duniani ufalme wa amani na haki, na “dunia itajawa na kumjua Mungu”, yaani watu wote watampenda na kumtii Mungu. Katika unabii wake, Isaya hakuuma maneno! Alihubiri Neno la Mungu bila kuogopa hatari zilizoonekana kumzonga au kumfunga asihubiri Neno la Mungu kwa ufasaha na uwazi.

Nabii Yeremia alijiona kuwa na umri mdogo hivyo hangeweza kutangaza Neno la Mungu (rej. Yer. 1:6). Pale nabii Yeremia alipojaribu kuweka mnyororo ili asifanye kazi hiyo ya Mungu, Mungu alimthibitishia kuwa umri siyo sababu ya kutotangaza Neno lake (rej. Yer. 1:7). Neno la Mungu halifungwi na chochote hata umri mdogo. Lakini pia nabii Yeremia alikutana na mazingira ya kifungo katika kuhubiri Neno la Mungu (rej. Yer. 32). Uaminifu na imani yake kwa Mungu vilimtia nguvu. “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je, kuna neno gumu lolote nisiloliweza?” (rej. Yer. 32:27). Kwa maneno mengine, “Neno la Mungu halifungwi minyororo.”

Katika Mwaka wa kumi wa Zedekia, mfalme wa Yuda, ambao pia ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza, nabii Yeremia alitabiri kuchukuliwa mateka kwa mji wa Yuda na mfalme Nebukadreza. Jambo hili halikumpendeza mfalme Zedekia, hivyo nabii Yeremia alifungwa gerezani ndani ya uwanda wa walinzi uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda. Hata hivyo nabii Yeremia aliendelea kuhubiri Neno la Mungu angali kifungoni; kifungo hakikumzuia kuendelea na kazi yake (rej. Yer. 33). Kama ilivyokuwa kwa Nabii Isaya vivyo hivyo na nabii Yeremia naye alikuwa na ujasiri mkubwa katika kuutangaza ukweli wa Neno la Mungu. Mara kadhaa alilumbana na wafalme Zedekia na Jehoiakimu katika kutetea Ukweli wa Neno la Mungu. Hii inadhihirisha kuwa Neno la Mungu halifungwi minyororo, linavuma katika mazingira yoyote kadiri ya mapenzi ya Mungu na si kwa matakwa dhaifu ya wanadamu.

Nabii mwingine aliyehubiri akiwa kifungoni ni Ezekieli. Nabii Ezekieli anadhaniwa kuwa mhubiri aliyewalenga Waisraeli waliokuwa uhamishoni Babeli (593-571 K.K). Lakini inasemekana pia kuwa kuna ujumbe aliutoa akiwa Palestina (rej. Eze. 2:1-3:9) na mwingine akiwa utumwani Babeli (rej. Eze. 1:4-28, 3:10-15). “Haya! Enenda uwafikie watu hao waliohamishwa, kwa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, ‘Bwana Mungu asema hivi’; kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia (rej. Eze. 3:11).” “Enenda ukajifungie nyumbani mwako. Lakini wewe, mwanadamu, tazama, watakutia pingu, nao watakufunga kwazo, wala hutakwenda nje kati yao. Nami nitaufanya ulimi wako ugandamane na kaakaa lako, hata utakuwa bubu, wala hutakuwa mwonyaji kwao, kwa kuwa wao ni nyumba yenye kuasi. Lakini hapo nitakaposema nawe, nitafumbua kinywa chako, nawe utawaambia, ‘Bwana Mungu asema hivi, Yeye asikiaye na asikie, naye akataaye na akatae’; maana wao ni nyumba yenye kuasi (rej. Eze. 3:24-27).” Hivyo, Neno la Mungu linawafikia watu wake hata kama wako kifungoni au latokea kifungoni, lenyewe linapenya tu.

Pia tundu la simba ambamo nabii Danieli alifungiwa jiwe kubwa, utukufu wa Neno la Mungu ulidhihirika kwa Waisraeli. Baada ya kuamka asubuhi mfalme alikwenda nje ya pango alimokuwa Danieli akalia na kuuliza kama Mungu wa Danieli alimwokoa. Ndipo Danieli alipothibitisha kwa kusema kuwa Mungu alimtuma malaika ayafumbe makanwa ya simba wasiweze kumdhuru hata kidogo. Mungu alinena na malaika, akatenda muujiza wa kumwokoa Danieli uliosababisha ongezeko la imani ya Mfalme Dario pamoja na watu wake (rej. Dan. 6). Hivyo Neno la Mungu halizuiliwi na chochote kilichoumbwa naye. 2.1.8 Nabii Amosi alishindana na kuhani Amazia ambaye alimkataza kuhubiri, ya kwamba hakuwa na haki ya kufanya hivyo. Amazia aliyafanya haya kwa sababu Amosi alitabiri kuwa Mfalme Yeroboamu ataangamia kwa upanga na Waisraeli watapelekwa utumwani. Utabiri huu haukumpendeza Amazia hivyo aliamuru nabii Amosi aondoke Betheli na aende kuwatabiria watu wa Israeli (rej. Am. 7:10-17). Lakini Amosi alimthibitishia Amazia kuwa yeye ni nabii halali na kwamba ndiye aliyeteuliwa na Mungu alipokuwa mchungaji na mtunza mikuyu kuwahubiria nyumba ya Israeli. Na papo hapo alimtangazia Neno la Mwenyezi Mungu (rej.Am. 7: 16-17). Maandiko hayo yanaonyesha jinsi gani Neno la Mungu haliwezi kuzuiliwa na yeyote au chochote.

AGANO JIPYA: Yohane Mbatizaji alielewa umuhimu wa kuupata Ufalme wa Mungu alipotoa mwaliko, “Tubuni kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia “(Mt. 3: 2)”. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alitafuta faraja ya Neno la Mwenyezi Mungu. Aliamini kuwa Neno hilo litamfikia hata akiwa kifungoni katika mateso na kwalo angepata amani. Hivyo, Yohane Mbatizaji aliwatuma wanafunzi (rej. Mt. 11:2-6) kumwuliza Yesu ili apate kujua iwapo Yeye ndiye yule ajae au wamtarajie mwingine. Jibu lililorudi ni ushuhuda wa Neno la Mungu linavyoendelea kufanya kazi kati ya watu. Hivyo hakuna sababu ya kuwa na mashaka nalo. Neno la Mungu linavunja mipaka ya kifungo na kusafiri kwa urahisi bila ya pingamizi. Neno hilo halifungwi minyororo hata kama wale wanaolipokea wamefungwa minyororo. Aidha kilichompeleka Yohane Mbatizaji kifungoni na kuuawa ni Neno la Mungu ili asiendelee kulitangaza (rej. Mt. 14:1-12). Hata hivyo, akiwa kifungoni Neno la Mungu liliendelea kutangazwa na wengine (rej. Mk. 6:6-29).

Yesu alifungua Hotuba ya Mlimani kwa Heri nane. Heri hizo zinaunganisha tabia anayokuwa nayo mtu muda uliopo sasa na maisha yajayo. Heri ya kwanza na ile ya mwisho (Mt. 5: 3, 10), zote hueleza kuwa ufalme wa Mungu tayari upo hivi sasa miongoni mwetu na kati yetu. Heri sita ambazo zimo (Mt. 5: 4-9) huonyesha Ufalme utafikia ukamilifu wake siku ya mwisho. Heri za mwisho, (Mt. 5: 10-11) ni juu ya ulazima wa kuteseka kwa ajili ya Injili na baraka na utukufu wenye nguvu ya pekee tunavyovipata katika maisha yetu. Hakuna heri ambayo wanadamu wanaweza kuifikia inayokwepa mateso.

Katika Karamu ya Mwisho Yesu alisema, “Sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu” (Mk. 14: 25). Yesu Kristo mwenyewe akiwa katika praitorio anazungumza ukweli wa Neno la Mungu kwa ujasiri mkubwa (rej. Yn. 18-19:1-15). Kwa mfano, baada ya kuulizwa habari za mafundisho yake, Yesu Kristo anasema waziwazi kwamba hakuficha chochote. Alihubiri Neno la Mungu kwa uwazi hivyo hakuna sababu ya kuendelea kumhoji. Kwa hili Bwana wetu Yesu Kristo anapigwa kofi lakini naye anamjibu aliyempiga kwamba, aliyoyazungumza ni ukweli mtupu na kulikuwa hakuna sababu ya Yeye kupigwa kofi. Alisema haya bila kujali hatari ya kupigwa kofi tena. Neno la Mungu halifungwi kwa kupigwa kofi, au mijeledi, au kutemewa mate. Aidha Neno la Mungu alilolifundisha Bwana wetu Yesu Kristo na ukweli alioutangaza ndio uliomfikisha kwenye mateso makali na kifo cha Msalaba. Hata hivyo, siku ya tatu alifufuka na Neno la Mungu linaendelea kutangazwa (rej. Mt. 28:1-10).

Mitume Petro na Yohane na wengine wengi walianza kulitangaza Neno la Mungu baada ya Pentekoste; lakini walipelekwa gerezani kwa kuwa walilihubiri Neno la Uzima la Bwana wetu Yesu Kristo. Wangali bado gerezani, walipelekwa mbele ya baraza kuhojiwa. Kwamba ni kwa nguvu ya nani wanatenda? Mtume Petro kwa ujasiri mkubwa anazungumza juu ya habari za Yesu ambaye Wayahudi na viongozi wao walimsulubisha kuwa ndiye chanzo cha nguvu na mamlaka yao. Kristo ni jiwe walilolikataa waashi na limekuwa jiwe kuu la pembeni (rej. Mdo. 4:1-22). Neno la Mungu halifungwi minyororo!

Shemasi Stefano naye anapelekwa mbele ya baraza la Wayahudi kwa kuwa alitenda maajabu na ishara kwa jina la Yesu Kristo. Akiwa mbele ya baraza la Wayahudi anaendelea kutoa hotuba inayoshuhudia ukweli wa Neno la Mungu (rej. Mdo. 6:1-7:1-60). Stephano anaonyesha ujasiri wa hali ya juu kabisa. Anaonyesha imani yake kwa Bwana wetu Yesu Kristo bila kuogopa macho ya watesi wake. Anazungumza ukweli bila kuficha lolote. Mwishowe anauawa kwa sababu ya kusema ukweli uliowachoma Wayahudi. Kuuawa kwake hakuzuii Neno la Mungu kuendelea kutangazwa. Neno la Mungu halifungwi na minyororo ya mateso au kifo.

Mtume Paulo naye anafungwa gerezani mara kadhaa kwa sababu ya Neno la Mungu. Alipelekwa mbele ya baraza la Wayahudi na aliwaambia ukweli wa Neno la Mungu wajumbe wa baraza lote la makuhani na Wayahudi (rej. Mdo. 22:30-23:1-11, 24:24-26:32). Neno ambalo Mtume Paulo analihubiri akiwa kifungoni linaonyesha wazi kabisa kwamba Neno la Mungu halifungwi minyororo (rej. 2 Tim. 2:9). Fundisho hili linajirudiarudia sana katika maandishi ya Mtume Paulo katika barua zake (rej. Flm. 1:7-17, 9-13). Lakini zaidi katika Waraka wake kwa Wafilipi (rej. Flp. 1:13-17) na katika waraka kwa Waefeso (rej. Efe. 3:1-13). Neno la Mungu haliwezi kuzuiliwa na kitu chochote kuhubiriwa na kupenya katika mioyo ya watu.

Kwa njia ya haya yote, tunajifunza ujumbe mahususi kwamba Neno la Mungu hupenya sehemu yoyote. Mungu katika haya yote anatufunulia asili yake Mwenyewe kuwa ni Roho halisi na ukamilifu wake hauna mipaka. Yeye ni wa mahali pote. Bwana wetu Yesu Kristo anaushuhudia ukweli huu, “…watu hawa wakinyamaza, hata mawe yatasifu” (rej. Lk. 19:40). Hivyo, watu wakizuiwa kutangaza Neno la Mungu hata mawe yatalitangaza. Neno la Mungu halifungwi minyororo. Aidha mambo yote yapita, Neno la Mungu halitapita kamwe (rej. Lk. 21:33). 2.2.7 Neno la Mungu lina nguvu ya ajabu. Tunapaswa kulitafuta Neno la Mwenyezi Mungu siku zote na mahali pote na kwa nguvu zetu zote.

Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunaalikwa kutenga muda maalum wa kulisoma, kulitafakari, na kulitangaza kwa watu wote kwa maneno, matendo yetu mema na ushuhuda wa maisha yetu. Jukumu hili litekelezwe na mtu binafsi, familia, jumuiya, vyama vya kitume na Kanisa lote kwa ujumla (rej. Mk. 16:15-16). Kama asemavyo Mtume Paulo, “Litangaze Neno, sisitiza, hakikisha, onya, himiza kwa uvumilivu wote na elimu” (2Tim. 4:2); na Bwana wetu Yesu Kristo hatatuacha (rej. Mt. 28:20). Matunda ya Neno la Mungu ni haki, amani na furaha kwa mtu binafsi, familia, jumuiya, taifa na ulimwengu wote. Aidha wokovu na uzima wa milele ni matunda ya Neno la Mungu (rej. Yn.14:6, Mt. 22:29, Rum.1:16, Flp. 2:6-11). Neno la Mungu ni uhai wetu. “Mtu hataishi kwa mkate tu ila kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mt. 4:4). Tunapata uhai katika mateso na vifungo vya kimwili kwa sababu tunajishibisha kwa Neno wake Mungu, Yesu Kristo anayetufundisha na kutulisha. Neno la Mungu ni nuru yetu (rej. Yn. 3:19-20). Tuwapokee wanaotutangazia Neno la Mungu na tulizingatie. (rej. Mt. 10:40-42)

Neno la Mungu linatupatia uthabiti na kutuimarisha katika ukweli kwamba kwa neema ya Mungu, tunao uwezo wa kushinda dhambi na kuufanya Ufalme wa Mungu ufike. Neno la Mungu linasema kuwa yeye alifanywa mdhambi kwa ajili yetu sisi, alichukua dhambi zetu na adhabu katika mwili wake msalabani. Alifanywa kuwa laana kwa ajili yetu, na kwa ajili ya wale wote wanaoweka tumaini lao katika yeye kwao hao hakuna adhabu (rej. 1 Pet. 2: 21-24). Neno la Mungu linaleta matumaini kwamba hitaji la wanadamu kuokolewa limetekelezwa na Mungu tayari. Neno hili ndilo Habari Njema. Lakini Habari Njema hii inaleta pia wajibu kwa upande wa pili, yaani, waamini tunapaswa kumgeukia na kumrudia Mungu, na hiyo ndiyo maana ya kutubu na kuiamini Injili. Kwa namna hiyo Ufalme wa Mungu utakuwa unadhihirishwa maishani mwetu.

Neno la Mungu ni ukweli, na sifa moja ya ukweli ni kwamba hudumu daima bila kubadilika. Kwa vile Neno lake lina pumzi ya Roho wa Mungu, vile ambavyo Roho wa Mungu hafungwi, kadhalika na Neno la Mungu halifungwi na pingu au vizuizi au vikwazo vinavyoweza kumfunga Roho, kama ambavyo usivyoweza kufunga mnyororo upinde wa mvua. Neno lake li hai, tena lenye nguvu (rej. Ebr. 4:12-13); lina nguvu zaidi kuliko kitu chochote hapa duniani. Mambo yote mengine hayana uwezo wowote ukilinganisha na Neno la Mungu. Ilikuwa kwa njia ya Neno la Mungu kwamba mbingu ziliumbwa. Mungu anapotamka kinachotamkwa hufanyika na mambo yote hutii. Neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo kwa sababu ni nguvu isiyoweza kuzuiwa; ni yenye uwezo wa kutaalamisha na kuangaza na kuwafanya watu wengi bila idadi kwa pamoja wafanane zaidi na Kristo. Yesu Kristo ni Neno aliyetwaa mwili, hekima aliyemwilishwa, ukweli uliomwilishwa, na chimbuko lililomwilishwa la kila kitu. Kukosa ukweli, kukosa uwazi na u-ndimi mbili ni kinyume cha uhalisia wa Mungu na Ufalme wa Mungu. Popote ambapo mtu anamkana Kristo, atakuwa daima anaukataa ukweli.

Kupenda lisilo kweli, kutokuwa na msimamo kuhusu ukweli, kuubinafsisha ukweli, kuuweka ukweli na lisilo kweli katika ngazi moja, yote haya hupatikana katika kiini cha dhambi ya Adam na Eva (rej. Mwa. 3:1-24). 2.2.10 Kristo alikuja ili kuubomoa Ufalme wa uwongo na kuusimika Ufalme wake wa ukweli, kwa lengo la kumweka huru binadamu dhidi ya giza la uwongo na udanganyifu: “Kwa sababu hii nalitokea ulimwenguni, ili niushuhudie ukweli. Yeyote yule aliye wa ukweli huisikia sauti yangu” (Yoh. 18: 37). Yesu ndiye ukweli na uzima aliyekuja kuwaweka watu huru dhidi ya utumwa wa utawala wa shetani. Ukweli huu ni nafsi yake mwenyewe anayetualika tumsikie ili tupate kuwa raia wa ufalme wake na ili tupate hatimaye kufika kwa Baba. (rej. Yoh. 14: 6). Kumbe, Neno analotuambia Kristo ni ukweli unaotuonyesha njia ya kufikia uzima wa milele.

HITIMISHO: Kwa kushika Neno lake, tunafanyika warithi wa uzima wa milele na raia wa Ufalme wa Mbinguni. Katika kipindi hiki cha Kwaresima tunao uchaguzi wa kufanya. Tunaalikwa kuliishi Neno la Mungu kwa maneno na matendo yetu; na pia kulishuhudia kwa watu wengine ili ufalme wa Mungu uendelee kujidhihirisha kwetu na watu wengine. Hii ndiyo njia pekee itakayoyafanya maneno haya yatimie, “Ufalme wako Ufike”.

SURA YA TATU UFALME WA MUNGU NA MAMLAKA YA WATU: Katika Barua yake kwa Warumi, Mtume Paulo anachagua sura ya 13:1-7 kueleza uhusiano uliopo kati ya mamlaka au tawala za watu na ufalme wa Mungu. Mtume Paulo anatambua kuwa tawala zote za dunia zilizo halali zimewekwa na Mungu mwenyewe aliyeumba ulimwengu kwa upendo wake mkubwa. Hivyo kila mtu inabidi atii mamlaka hizo ili kuweza kuendana na mpango wa mwenyezi Mungu aliyeweka mamlaka hizo. Mungu anaendelea kuvileta viumbe vyote pamoja ili vibaki katika mpango wake wa uumbaji: kumjua, kumpenda, kumtumikia na hatimaye kuurithi uzima wa milele. Katika sura hii tunawaalika kutafakari uhusiano uliopo kati ya ufalme wa Mungu na mamlaka ya watu, tukiongozwa na Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa Katoliki.

AGANO LA KALE: Mwanzoni Taifa la Israeli lilikuwa tofauti na mataifa mengine kwani hawakuwa na mfalme bali walitambua utawala wa Yahweh pekee. Ni Mungu aliyeingilia kati kwa niaba ya Waisraeli kwa kupitia watu wenye karama kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Waamuzi. Watu wanamwendea aliyekuwa wa mwisho wa hao, Samweli, nabii na mwamuzi, wakimwomba awateulie mfalme (rej.1Sam. 8:5; 10: 18-19). Samweli anawaonya Waisraeli kuhusiana na athari za utawala dhalimu (rej.1Sam. 8:11-18). Hata hivyo, mamlaka ya Mfalme yanaweza kuonekana kama zawadi ya Mungu anayekuja kuwasaidia watu wake (rej. 1 Sam. 9:16). Mwishowe, Sauli anapakwa mafuta na kuwa mfalme (rej. 1 Sam. 10: 1-2). Matukio haya yanadhihirisha fadhaa iliyowafanya Waisraeli kuelewa ufalme kwa namna tofauti na vile ulivyokuwa ukieleweka kwa jirani zao. Mfalme, aliyeteuliwa na Mungu (rej. Kum. 17: 15; 1 Sam. 9:16) na aliyewekwa wakfu naye (rej.1 Sam. 16:12-14), anaonekana kama mtoto wa Mungu (rej. Zab. 72).

Mfalme, kwa hivyo, anakuwa mlinzi wa walio dhaifu na mdhamini wa haki kwa watu wake. Shutuma za manabii zinalenga haswa katika wafalme kushindwa kutekeleza wajibu hizo (rej. 1 Fal. 21; Isa 10:14; Amo. 2:6 – 8:48, Mik. 3:1-4). 3.1.2 Katika Agano la kale, kwa nyakati tofauti, Mungu anajionyesha kuwa ndiye anayewaongoza watu wake kwa mkono wa wale aliowachagua yeye mwenyewe kutenda kwa niaba yake. Anaeleza wazi kuwa, katika yeye, watawala na mamlaka yao hutekeleza kile kilicho ndani ya mpango wake mwenyewe (rej. Mith. 8:15). Mungu aliye mtawala pekee katika wateule wake, anazidi sana kuwajalia hekima na busara ya kutenda kwa niaba yake (rej. 1Fal. 3:4-15). Watawala wanakuwa vyombo anavyotumia Mungu kutekeleza kazi alizokusudia yeye mwenyewe kwa watu wake (rej. Isa. 11:2-5; Yer. 23:5; Sir. 10:4). Watawala nao kwa upande wao walijifungamanisha na upendo wa Mungu ili kuimarisha uhusiano mwema na Mungu wao. Aidha watawala wa Agano la Kale walitekeleza majukumu yao kadiri ya mapenzi ya Mungu. Hivyo waliheshimiwa kwa kazi zao hizo zilizowastahilisha wao wokovu na wale waliowaongoza (rej. Hek. 6:12, YbS.1:16). 3.1.3 Mungu mwenyewe aliwaweka watawala, akiwatarajia kuwaongoza watu na kuyafanya mawazo na matendo yao kuwa ya hekima, kwani Mungu alikusudia kutengeneza Taifa lenye heshima na mwenendo mwema (rej. Hek. 6:3; Zab. 2:10; Mith. 8: 15-16).

Watawala hao wa Agano la Kale pia walipaswa kuwa waamuzi kati ya watu. Kwa hiyo, iliwabidi kujaa hekima itokayo kwa Mungu ili wahukumu kwa upendo na haki maana walitenda mahala pa Mungu mwenyewe mwenye upendo na haki (rej. Hek. 6:4-7; Ayu. 34:17-19; YbS. 35:12). Mungu aliyekusudia hayo yote yafanyike, pia aliwasaidia watu kutii kanuni, taratibu, na sheria za mamlaka halali za watu. Sio tu wanadamu peke yao walipaswa kutii mamlaka hiyo bali kila kitu kilichoumbwa na Mungu (rej. Yer. 27:7-10; Jdt11:7). Kwa jinsi hiyo, watu walimtii Mungu na Watawala pia (rej. Yer. 27:5-7), ambao wanamwakilisha Mungu aliye chanzo cha mamlaka zote duniani.

AGANO JIPYA: Mtume Paulo katika waraka wake kwa Warumi anaongea juu ya kuheshimu serikali, yaani “kujisalimisha” kwa serikali, “kuwa chini” ya serikali au “kutii” serikali; kwani mamlaka zilizopo duniani zimetoka kwa Mungu (rej. Rum. 13:1). Mungu kwa huruma na upendo wake anawashirikisha baadhi ya wanadamu zawadi ya kuwa na mamlaka juu ya wanadamu wenzao. Ingawa Mungu ameamua kuwashirikisha baadhi ya wanadamu zawadi ya kuwa na mamlaka juu ya wanadamu wenzao, lakini namna ya kuchagua viongozi hao na jinsi wanavyoongoza ni jukumu la kibinadamu. Hii inafanya suala la kuongoza kuwa taasisi ya kibinadamu iliyowekwa na Mungu mwenyewe, hivyo watu wanahimizwa kuzitii mamlaka hizo (rej. Rum. 13:1-7).

Kwa kusema: “Hakuna mamlaka yasiyotoka kwa Mungu, na kila yaliyoko yamewekwa na Mungu” (Rum. 13:1), Mtume Paulo analinganisha utii kwa serikali na utii kwa Mungu. Utii huu wote ni wa lazima. Wakristo ambao hawatii kanuni, taratibu na sheria halali za serikali hawamtii Mungu. Hata Bwana wetu Yesu Kristo akiwa hapa duniani alitii mamlaka za kibinadamu zilizokuwa zikiongoza Taifa lake la Israeli wakati wake (rej. Lk. 2:51-52, Mt. 17:24-17). Hata hivyo, ni vema ijulikane wazi kuwa hatutakiwi kutii tu mamlaka halali zilizowekwa na Mungu bila kuzingatia dhamiri yetu njema (rej. Rum. 13:5) yenye kutambua wajibu na nafasi yetu katika jamii.

Tena tutii tukijua kuwa yatupasa kuzitii mamlaka zilizo halali ili tuweze kuuona ufalme wa Mungu. Tunahimizwa kutimiza wajibu wetu kwa Mungu, kwa mamlaka za kidunia na kwa jamii (rej. Mt. 22:21) ili kuwepo haki, amani, furaha, maelewano, na kuchangia maendeleo ya jamii zetu; kwa mfano, kwa kulipa kodi (rej. Rum. 13:7, Mt. 22:21). Mtume Paulo aliamini kuwa Wakristo na raia wote kwa ujumla lazima walipe kodi kwa serikali, ili Serikali nayo kwa upande wake, itoe huduma nzuri za kijamii ikitumia mali ya raia wake kwa ukweli na uaminifu. Raia kwa upande mmoja, na serikali kwa upande mwingine, tunapaswa kufanya vivyo hivyo, tukizingatia kanuni, taratibu na sheria zetu.

Watawala kwa upande wao, wanaowaongoza watu, wanatakiwa wawaelekeze namna ya kuenenda kadiri ya mpango wa Mungu, wakiwakumbusha kanuni, taratibu, na sheria za msingi za kufuata. Iwapo raia watakosea, basi namna inayofaa kadiri ya mpango wa Mungu, itumike kuwakosoa. Kumbe, watawala wameshirikishwa hadhi ya Baba mwenye upendo na huruma ambaye anahukumu kwa haki na ambaye anakemea na kukaripia ikiwa ni kwa uvumilivu na mafundisho (rej. 2Tim. 4:2). 3.2.4 Hata hivyo, Watawala wanalo jukumu la kuwaadhibu watu waovu kwa mujibu wa sheria halali za nchi. Raia wema hawana sababu ya kuwaogopa watawala. Watu ambao hufanya vitendo vibaya lazima watarajie kuadhibiwa na watawala wao. Kwa hiyo, watu waovu wana sababu ya kuogopa watawala wao (rej. Rum. 13:3-4). Kile kinachoweza kuonekana kuwa ni uasi wa raia, kinaweza kuhesabiwa haki ikiwa tu sheria ya serikali inapingana waziwazi na sheria ya Mungu.

Mtakatifu Petro anawasihi Wakristo asemapo, “Tiini kila kiamriwacho na watu kwa ajili ya Bwana” (1 Pet. 2:13). Mfalme na watawala wake wana wajibu “wa kuwaadhibu watenda mabaya na kuwasifu watenda mema” (1 Pet. 2:14). Mamlaka yao hayo sharti “yaheshimiwe”, yaani, yatambuliwe kwa sababu Mungu anadai mwenendo sahihi” (1 Pet. 2:17). Uhuru usitumike kwa kusisitiza ubaya, bali kumtumikia Mungu (rej. 1 Pet. 2:16). Msisitizo ni juu ya utii ulio huru wa kuwajibika kwa mamlaka iwezeshayo haki kuheshimika, ikihakikisha manufaa kwa wote.

Kwa upande mwingine, Kanisa linatufundisha kwamba hatuna ruhusa ya kuwatii viongozi wetu pale wanapotuamuru kutenda kinyume na Amri za Mungu. Ni muhimu kuzingatia kuwa kujiweka chini ya mamlaka haya hakumaanishi kwamba ni lazima tutii kama vipofu amri inayotolewa na dola ambayo ni mbaya au inakwenda kinyume na Amri ya Kristo ya kuwapenda jirani zetu. Hoja ni kwamba raia wanapotii mamlaka iliyoko, mamlaka hiyo nayo lazima imtii Mungu. Hivyo, mamlaka inapoacha kutunuku matendo mema au tabia njema, au inapoacha kuadhibu maovu, na badala yake ikaamrisha mambo yaliyo kinyume; mamlaka hiyo inapoteza nguvu au uwezo wake wa kimaadili wa kuongoza watu. Mamlaka ya kiraia yamewekwa ili kudumisha utulivu katika jamii. Hivyo basi, raia ni lazima wafanye kile ambacho ni sahihi ikiwa wanataka kuepukana na hukumu au adhabu. Tuitii mamlaka kwa sababu ya dhamiri zetu sahihi. Kwa maneno mengine, dhamiri zetu zituelekeze kwamba Mungu, ambaye ndiye mwenye mamlaka kuu kupita zote, ameweka ngazi mbalimbali na kuweka sheria ili kuhakikisha kuwa kuna utulivu na utaratibu. Aidha, kupingana na ngazi hizo ni kupingana na mpango wa Mungu wenye lengo la kuwa na jamii yenye utulivu. (rej. Mdo. 4:18-20).

Kwa kuwa Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni, ni wajibu wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake, awe mtawala au mtawaliwa, kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu (rej. Lk 12:31). Ufalme wa Mungu tutaupata kwa kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu na kutimiza wajibu wetu itupasavyo katika nafasi zetu. Kila mmoja wetu ni kiongozi wa nafsi yake mwenyewe, hivyo tujifunze kuzitii dhamiri zetu njema zinazotuongoza kutenda mema na kutuzuia kutenda mabaya. Kwa kufanya hivyo tutaweza kueneza utawala wa Mungu maishani mwetu, utawala wa haki, amani na furaha. Basi, utawala wa watu au mamlaka ya watu iwe na lengo la kuuleta ufalme wa Mungu karibu zaidi katika maisha ya kila siku ya watu.

MAFUNDISHO YA MTAGUSO MKUU WA PILI WA VATICAN. Kadiri ya mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican moja kati ya maeneo yaliyotiliwa mkazo ni uhusiano kati ya Ufalme wa Mungu na utawala wa watu, hususani katika Hati ya Kichungaji juu ya Kanisa na Ulimwengu (Gaudium et Spes-GS). Utambuzi hai wa hadhi ya binadamu katika mahali pengi duniani, unaamsha juhudi ya kuunda utaratibu wa kisiasa na kisheria ambapo haki za binadamu katika maisha ya hadhara zinalindwa vema zaidi. Nazo ndizo haki za kujumuika na kuunda umoja kwa uhuru, haki ya kila mmoja kutoa maoni yake na kukiri imani yake akiwa peke yake au hadharani.

Maana, ulinzi wa haki za binadamu ni sharti la lazima ili raia, kila mmoja peke yake au kama wanachama, waweze kushiriki kimatendo maisha ya umma na uongozi wa mambo yanayowahusu. (rej. GS. 73). Pamoja na maendeleo ya kiutamaduni, kiuchumi na kijamii, hamu ya walio wengi ya kuchukua wajibu mkubwa zaidi katika kuratibu maisha ya jumuiya ya kisiasa inazidi kupata nguvu. Katika dhamiri ya watu wengi bidii ya kuhifadhi haki za makundi ya wachache katika nchi zao inastawi, lakini bila ya makundi hayo ya wachache kusahau wajibu zao mbele ya jumuiya ya kisiasa. Aidha, inazidi kukua heshima mbele ya watu wenye maoni au dini tofauti. Na wakati huohuo ushirikiano mpana zaidi unaundwa; nao unalenga kwa raia wote (rej. GS. 73). Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote. Pia ni kuuimarisha msimamo wa msingi mintarafu maumbile halisi ya jumuiya ya kisiasa; tena kuhusu lengo, matumizi halali na mipaka ya wajibu wa serikali (rej. GS. 73).

Utawala wa kisiasa, uwe unatekelezwa na jumuiya yenyewe au na vyombo vinavyowakilisha dola, ni lazima daima ufanyike ndani ya mipaka ya sheria ya kimaadili. Lengo lake ni kuyafikia manufaa ya wote, tena manufaa yenye maendeleo yake, kadiri ya kanuni za utaratibu wa kisheria uliokwisha kuwekwa, au wa kuwekwa. Na hapo ndipo raia wanapolazimishwa kutii kwa sababu ya dhamiri zao (rej. GS. 74). Aidha katika Hati ya Kanisa katika Ulimwengu mamboleo (GS), Mtaguso unasisitiza kuwa utekelezaji wa madaraka ya kisiasa daima ukusudie katika kumuunda mtu mwadilifu, mtulivu, na mkarimu kwa wote, kwa manufaa ya familia nzima ya wanadamu.

Ili kukuza maisha ya hadhara ya kisiasa, sharti ipatikane miundo ya kisiasa na kisheria inayowawezesha zaidi na zaidi raia wote – bila ubaguzi wowote – kushiriki kwa uhuru na kwa matendo katika kutengeneza misingi ya kisheria ya jumuiya ya kisiasa. Lengo lake ni kuongoza mambo ya dola, katika kuainisha uwanja wa kazi na mipaka yake kwa taasisi mbalimbali, na hatimaye katika kuwachagua viongozi. Kwa sababu hiyo, raia wote wakumbuke haki yao, ambayo pia ni wajibu, ya kutumia kura yao huru kwa minajili ya kuhamasisha manufaa ya wote. Kanisa linasifu na kuthamini wale ambao, kwa ajili ya kuwatumikia wanadamu, wanajitoa kwa manufaa ya dola na kubeba uzito wa wajibu husika (rej. GS. 75).

Katika nyakati zetu hizi, ugumu wa masuala yanayojitokeza unazilazimisha serikali kujihusisha zaidi katika fani za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni ili kuleta mazingira yanayofaa zaidi, kusudi raia na makundi waweze kuyafuatilia kwa bidii na kwa uhuru manufaa kamili ya binadamu. Uhusiano mzuri miongoni mwa watu na uwezo wa kujiratibisha na kujiendeleza kwa mtu binafsi, unaweza kufikiriwa kwa namna tofauti katika nchi mbalimbali za ulimwengu na kwa mujibu wa maendeleo ya mataifa. Raia hawana budi kustawisha upendo kwa taifa lao kwa ari na unyofu, lakini si kwa mtazamo finyu, yaani hivi kwamba wayazingatie daima mema ya familia nzima ya wanadamu inayounganika kwa vifungo mbalimbali kati ya makabila, mataifa na nchi (rej. GS. 75).

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO (01.01.2019) Baba Mtakatifu Francisko, katika Ujumbe wa Siku ya Kuombea Amani Duniani mwaka 2019, wenye kauli mbiu ya “Siasa safi ni huduma ya amani”, aliangalia mambo kadhaa, kwa kuzingatia kuwa Injili ya amani ni sehemu ya utume wa Kanisa. Mambo hayo ni a) Changamoto za siasa safi; b) Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; c) umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; na d) kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa amani.

Changamoto za siasa safi: Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka, na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini siasa ikitumiwa vibaya inaweza kuwa chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Kuhusiana na hilo naye Papa Paulo VI alikuwa na haya, “Siasa ikichukuliwa katika umuhimu wake kuanzia ngazi ya kijiji, kimkoa, kitaifa na kidunia- ni kukubali wajibu wa kila mtu kukiri ukweli na thamani ya uhuru ambao unatolewa kwake na jamii kuufanyia kazi kwa manufaa mazuri ya mji, taifa na binadamu wote,” (rej. Octogesima Adveniens, 14 Mei 1971, 46).

Upendo na fadhila za kiutu ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani: Baba Mtakatifu Fransisko akimnukuu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, “Kila mtu ajitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu” (rej. Benedict XVI, Caritas in Veritate 29 June 2009). Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tena, anapaswa kuwa mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, awe tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri.

Siasa safi inajengeka katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu: Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa chombo cha upendo. Umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani: Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi. Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao, tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa Amani: Siasa ya namna hii inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano, watu kuaminiana, kuthaminiana na kujenga upendo. Haya yatafuta dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija. Jamii inawahitaji wanasiasa ambao watakuwa wajenzi wa amani, watakaokuwa watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha.

HITIMISHO Hivyo, basi tunaalikwa tuwaombee viongozi wetu waweze kutawala kadiri ya mapenzi ya Mungu (rej. Dn. 4:17). Daima watawala watambue kuwa uongozi ni utumishi, dhamana, uwakili, na kuwa watatakiwa kutoa hesabu ya utumishi wao kwa Mungu na kwa jamii. Hata hivyo, tunaamini kuwa watawala ni wajumbe wa Mungu ambao licha ya ubinadamu wao, neema ya Mungu huwasaidia katika kutimiza majukumu yao (rej. Mith. 8:15-16). Ndiyo maana ni muhimu kuwaombea watawala. Mtakatifu Paulo alipendekeza hata alipokuwa akiteswa, kuwa “sharti pawepo dua, sala, maombi na sala za shukrani kwa Mungu kwa ajili ya watu wote, kwa ajili ya wafalme na watu wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema” (1Tim 2:1 – 2).

SURA YA NNE MAZOEZI YA KIROHO NA UFALME WA MBINGUNI. Ni ukweli usiopingika kwamba mazoezi ya kimwili yana faida nyingi, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa mwili na akili, kujenga mahusiano mema baina ya watu katika jamii, na faida nyingine nyingi. Lakini, mazoezi ya kiroho yana faida zaidi, faida za kila namna na pekee. Kwani humuandaa mwanadamu kwanza kuwa na mahusiano mema na wenzake katika jamii, na zaidi humuandaa kwa maisha ya umilele mbinguni; “Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaaokuwapo baadaye” (rej. 1Tim. 4: 8).

KWA NINI MAZOEZI YA KIROHO? Mazoezi ya kiroho ni matendo yanayofanywa mara kwa mara ili kuiweka roho katika hali ya uhusiano mzuri na Mungu kwa njia ya muunganiko wa ndani na Bwana wetu Yesu Kristo (rej. Yn. 15: 1-17). Matendo hayo ni sala, kufunga lakini pia kutenda matendo mema kwa wote. Utii kwa mapenzi ya Mungu, unyenyekevu, kushiriki maadhimisho ya mafumbo matakatifu kwa ibada na uchaji mkubwa, kupokea Sakramenti, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, kusoma na kutafakari maisha ya Watakatifu, kusoma vitabu mbalimbali vya maisha ya kiroho, n. k. Mazoezi ya kiroho yanahitaji zaidi msukumo wa ndani wa mtu binafsi ili kuweza kuleta mafaa katika maisha yake ya kiroho (rej. Yoe. 2:17). Mazoezi haya yanahitaji sana msaada wa neema ya Mungu ili mtu aweze kuuvua utu wa kale, avae utu mpya na kujibidisha katika kuufanya upya utu wa ndani unaodhihirishwa na matendo mema ya nje.

Kwaresima ni kipindi cha “Mazoezi zaidi ya Kiroho”. Mama Kanisa anatualika katika kipindi hiki cha Kwaresima kwamba tufanye mazoezi ya kiroho, yaani kujiandaa katika kuvishwa taji ya Utukufu mbinguni: taji isiyoharibika. Hiki ni kipindi maalum kwa ajili ya waamini kujitafiti katika maisha ya kiroho, ili pale walipokosea basi waombe toba na kuanza maisha mapya. Ni mwaliko wa kujitafakari kwa kina, na kwa ndani kabisa; kuutafakari uhusiano wetu na Mungu, na kuyaacha yote yale yanayotufanya tuwe mbali na Mungu. Ni kipindi cha kujifunza kutenda mema, kama tunavyoalikwa na Nabii Isaya anaposema:” Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane” (rej. Isa. 1:17).

Mazoezi ya Kiroho huimarisha uhusiano wetu na Mungu. Kwa asili mwanadamu si mkamilifu kama Mungu alivyo; mara kwa mara huanguka katika dhambi. Kwa sababu hiyo Kanisa limeweka utaratibu wa mazoezi ya kuendelea kuutafuta ushirika na Mungu tunaoupoteza kwa sababu ya dhambi. Ni mwaliko wa pekee kutaka na kutamani sana kuuchuchumilia Utakatifu ambao ndio wito wa kila mbatizwa. 4.1.4 Kwaresima ni kipindi kizuri cha kufanya tafakari, kusali, kufunga, na kufanya matendo ya huruma kwa mwili na kwa roho bila ya kujali cheo, umri au jinsia. Mama Kanisa anamwalika kila mkristo mkatoliki kujifunza unyenyekevu, huruma kwa maskini, utu wema, mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Hiki ni kipindi cha kutafuta ushirika na Mungu na Kanisa kwa njia ya toba na maungamo, ili kuyaondoa majeraha yaliyomo ndani yetu.

AINA YA MAZOEZI YA KIROHO Biblia inaonyesha aina mbalimbali za mazoezi ya kiroho, mfano: 4.2.1 Kufunga na kusali (rej. Mt. 6:6): Sala ni kuinua akili na mioyo yetu kwa Mungu, na kuongea naye. Hili ni zoezi la kwanza kabisa la kiroho ambapo mwanadamu anakutana na Mungu, muumba wake na kuongea naye (rej. Zab. 4:4) ili kujua mapenzi yake (ufalme wake) na kuyatimiza, akimwomba msamaha wa dhambi zake (rej. 1Yn. 1:9), akipumzika kwake (rej. Mt. 11:28 – 30) pamoja na kuisikiliza sauti ya Mungu wake (rej. Lk.10:39). Katika Agano la Kale pia, tunamwona nabii Danieli akifunga na kuwaombea watu wake ili Mungu awasamehe maovu yao (rej. Dn. 9:3 – 6). Aidha, katika Agano Jipya, Bwana wetu Yesu Kristo anatuonyesha mfano bora wa kusali na kufunga (rej. Mt. 4:2, 10:1 – 4, Mk. 3:13 –19, Lk. 6:12 – 16). 4.2.2 Matendo mema yafaa Zaidi: Kutokula kwafaa sana lakini kutoa ambacho sitakula kwa wahitaji kwafaa zaidi.

Kusaidia wahitaji kwafaa sana lakini kusaidia bila ya kujionyesha mbele ya watu kwafaa Zaidi (rej. Mt. 6:16-18); “maana imeandikwa, unapotoa sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume.” (Mt. 6:3). Kuwasaidia wahitaji wakati wa sikukuu kwafaa sana lakini kuwasaidia kila mara unapojaliwa chochote kwafaa zaidi. Hivyo, matendo yetu ya nje yafaa kuwa ya unyenyekevu ili yazifaidie roho zetu, tusiwe sawa na wanafiki ambao hufanya mambo yao kwa matangazo makubwa na kupenda kujulikana na kila mtu kwamba wao ndio waliotenda jambo hili ama lile (rej. Mt. 6:1). Kusoma kiaminifu Neno la Mungu na kulitafakari: Kama tulivyodokeza hapo juu, na hili ni mojawapo ya mazoezi muhimu sana ya Kiroho. Ili kuwa imara kiroho yatupasa kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu mara kwa mara na kulielewa. Kwa kulisoma Neno la Mungu, kulitafakari na kulielewa tunapata ulinzi wa Mungu (rej. Isa. 30:12), tunapewa hekima ya kimungu (rej. Yak.1:5), tunapata faraja (rej. Zab 23:4), na mwangaza wa kiroho (rej. Zab119:18).

Kutoa sadaka na dhabihu: Tunapaswa siku zote kutoa sadaka iliyo ya kweli na dhabihu safi kwa Mungu ili kuweza kutakatifuzwa katika maisha yetu na kupata mafaa yetu sisi na Kanisa zima. Katika kitabu cha Mwanzo, tunaambiwa Abeli alitoa sadaka yake kwa Mungu pasipo kuwa na choyo na hivyo kubarikiwa na Mungu, lakini Kaini alitoa kwa choyo na kwa sababu hiyo alilaaniwa (rej. Mwa. 4:3 – 15).

Kufanya toba: Zoezi hili la kiroho linahitaji zaidi msukumo wa ndani wa mtu wa kuwa tayari kukiri na kutubu uasi wake kwa mapenzi ya Mungu, yaani kuwa tayari kukiri na kutubu uasi ili kupokea huruma na msamaha wa Mungu ambao siku zote unasubiri utayari wetu wa kurudi na kusema Baba tumekosa. Katika Agano la Kale, nabii Yona alikuwa tayari kufanya zoezi la kiroho la kutubu hata akasamehewa dhambi zake (rej. Yon. 2:2-9). Kitabu cha Esta pia kinabeba fundisho la zoezi hili la kiroho la kufanya toba (rej. Esta 4:17). Aidha Mwana mpotevu alikuwa tayari kurudi kwa baba yake na kukiri kwamba amekosa na hivyo kufanya zoezi la kiroho kwa kutubu na kuomba msamaha (rej. Lk. 15:11 – 32). Lakini pia yule mwizi aliyetubu pale msalabani, anatupa fundisho la kufanya toba hata kama ni dakika zetu za mwisho hapa duniani ili tuweze kuurithi uzima wa milele. (rej. Lk. 23:40 – 43).

FAIDA ZA MAZOEZI YA KIROHO KATIKA KUUTAFUTA UFALME WA MBINGUNI: Mtume Paulo katika barua yake ya kwanza kwa Wakorintho (9:24-27), anaongelea faida ya mazoezi ya kiroho kuwa ni: Uzima wa milele: Anayetoa tuzo hiyo ni Mungu aliye hai na wa milele. Hivyo mtu anayefanya mazoezi ya kiroho vizuri na kwa ufanisi mwisho atapata tuzo hiyo, uzima wa milele ambao pia ni ufalme wa mbinguni. Mtakatifu Paulo anasisitiza hili akifuata maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye daima aliwaasa Mitume wake waishi kwa namna ambayo watatoa kipaumbele kwa maisha yajayo, yaani ya umilele (rej. Mt. 6:19-21). Mazoezi ya kiroho pia husaidia kuvumilia mateso na kushinda majaribu mbalimbali ya shetani (Ayu.1:21- 2:10b): mazoezi ya kiroho ya Ayubu yalimsaidia kukabiliana na majaribu yaliyompata, na kwa njia hiyo alizidi kuimarika hata katika matatizo.

Hivyo basi, akaweza kuvumilia na kumshinda shetani, akiyazingatia daima mapenzi ya Mungu. 4.3.3 Mazoezi ya kiroho hutusaidia kuwa raia wema na wana wa Mungu na hivyo twaweza kuurithi ufalme wa Mungu. Mtume Petro anawaambia waamini waliokuwa wamekusanyika katika nyumba ya Korneli, kuwa yeyote anayeshiriki mambo ya Kimungu ataurithi ufalme wa Mungu bila kujali ukoo au mahali alipozaliwa mtu huyo (rej. Mdo.10:34-35). 4.3.4 Mazoezi ya kiroho pia humsaidia Mkristo kuujua ufalme wa Mungu: Mazoezi mbalimbali ya kiroho kama vile semina za maisha ya kiroho husaidia watu kupata elimu juu ya ufalme wa Mungu, kama anavyofundisha Nabii Isaya “…. Mimi ni BWANA, Mungu wako nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari” (48:17-18).

Mazoezi ya kiroho hutusaidia kuishi imani yetu kwa matendo: Kama Mtume Yakobo anavyotuambia katika barua yake kwa watu wote (rej. Yak. 2:14-26), imani yetu inapoonekana katika matendo yetu hapo ndipo kweli twaweza kusema tu watu wa imani, yaani wana wa Mungu tunaosubiri kwa matumaini kuurithi uzima wa milele, na imani yetu inakuwa ya kweli. Mazoezi ya kiroho hali kadhalika hutusaidia kuwa makini katika mambo ya kiroho zaidi kuliko mambo ya kimwili: Wanaotafuta kwa nguvu kubwa mambo ya kimwili waweza kupuuzia yale yote yanayohusu ufalme wa Mungu, lakini wanaotafuta ya kiroho kwanza basi watakuwa katika njia nzuri ya kuurithi ufalme wa Mungu (rej. Ebr. 13:5-19, 1Yn. 2:15-17, Mwa. 3:6, Mith. 27:20, Yer. 45:1-5). Katika Injili ya Mathayo (6:25-33), Bwana wetuYesu Kristo anatusihi kuhangaikia zaidi kuurithi uzima wa Kimungu hasa kwa njia ya mazoezi ya kiroho. 4.3.7 Mazoezi ya kiroho hutusaidia pia kuishi maisha ya upendo, haki, amani na furaha katika jamii yetu, nchi yetu, taifa letu na ulimwengu wote kwa ujumla. Matunda ya mazoezi ya kiroho hujidhihirisha kati yetu tangu ulimwengu huu mpaka ulimwengu ujao. Tujibidishe zaidi kufanya mazoezi ya kiroho.

Mazoezi ya Kiroho Hujenga Mazoea Katika kipindi hiki cha Kwaresima, kufunga, kusali na kujitoa kwa wahitaji hakuna maana kwamba tunamhonga Mungu ili atusamehe au atupokee kwake mbinguni. La hasha! Pia haina maana kwamba vipindi vingine vyote hatupaswi kufanya matendo hayo. La hasha! Maana yake ni kufanya mazoezi ili iwe ni mazoea katika maisha yetu ya kila siku kama wakristo; kama vile mwalimu amwandaavyo mwanafunzi wake aweze kufanya vyema au kocha aandaavyo wachezaji wake, vivyo hivyo Kanisa huwaandaa waamini katika kufanya yale yampendezayo Mungu na kuendelea kuwahimiza mazoezi hayo yawe sehemu ya maisha yao.

HITIMISHO Wapendwa Taifa la Mungu, sisi Maaskofu wenu tunawatakieni kila baraka katika safari hii ya kukua na kukomaa kiroho. Tumwombe Mungu athibitishe imani yetu iweze kujidhihirisha katika maisha na matendo yetu ya kila siku katika kuzingatia haki na kutenda mema. Katika kipindi hiki tunapenda tuchukue maneno ya Yesu mwenyewe yawe dira yetu: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa” (Yoh. 18:36). Hivi sisi pia ufalme wetu sio wa dunia hii kwani tunashirikishwa ufalme wa Yesu kwa sakramenti mbalimbali na kwa njia ya mateso katika Kanisa.

Yesu Mwenyewe alisema anaenda kutuandalia makao ili alipo nasi tuwepo. Hivyo kama vile Yesu asivyo wa ulimwengu huu hali kadhalika sisi nasi ufalme wetu sio wa dunia hii. Daima tunawakumbusha kuwa; maisha yetu si ya kudumu. Hivyo yatupasa kumtanguliza Mungu daima. Ikiwa sisi sio wa dunia hii tunapaswa kutafuta yaliyo juu Kristo aliko “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Kol. 3:1). Hata hivyo hatuwezi kuyapata haya bila ya kufanya mazoezi ya kiroho. Mazoezi ya kiroho tunayoalikwa tuyafanye yatusaidie: Kukua kiimani katika kumwelekea Mungu yaani kuufikia Utakatifu.  Kuwa karibu zaidi na Mungu. Kufika mbinguni baada ya maisha ya hapa duniani. Kuelewa kuwa matendo ya huruma na huduma ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Tuendelee kuziombea falme zote za dunia zipate kujua kuwa Mungu ndiye Bwana peke yake (rej. Isa. 37:20, Yoe. 3:17) na zitimize mapenzi yake. Mungu aweze kuwa pamoja na falme hizo na watu wote kwa ujumla (rej. Isa. 7:14, 8:8, 10, Zab. 46:8, 12). Hali za falme hizo na watu wote kwa ujumla ziboreshwe: laana ziondolewe, magonjwa yaponywe, Mungu aendelee kufanya maajabu makuu zaidi, ambapo haki, amani na furaha vitawale milele yote (rej. Joe. 4:1-21). Hatimaye tunawatakieni matunda tele ya kipindi hiki cha Kwaresima na mwishowe furaha za Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Ni sisi Maaskofu wenu, 1. Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu, Mbeya 2. Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Geita 3. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora 4. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Dar es Salaam 5. Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Dodoma 6. Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu, Songea 7. Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, Arusha 8. Mhashamu Askofu Mkuu Renatus Nkwande, Mwanza 9. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Iringa 10. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi 11. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga Ujumbe wa Kwaresima - 2020 40 12. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge 13. Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar 14. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara 15. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba

16. Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba (Askofu Msaidizi) 17. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS, Askofu, Moshi 18. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe 19. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma 20. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga 21. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same 22. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, (Askofu Msaidizi), Dar es Salaam 23. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara 24. Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa 25. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga 26. Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Mtwara 27. Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS, Kigoma 28. Mhashamu Askofu Prosper Lyimo, (Askofu Msaidizi), Arusha 29. Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Shinyanga 30. Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Singida 31. Mhashamu Askofu Beatus Urassa, Sumbawanga 32. Mhashamu Askofu Anthon Lagwen, Mbulu 33. Mhashamu Askofu Filbert Mhasi, Tunduru-Masasi.

TEC: Kwaresima: Ufalme wa Mungu

 

 

 

26 February 2020, 16:18