Tafuta

Vatican News
Tutoe shukrani zetu za kawaida ya zawadi ya maisha na kulinda kwa dhati tusije kujutia jinsi tunavyonyanyasa mazingira yetu na maliasili, na kujua wajibu wetu kwa wanadamu wote kuelekea uumbaji wa Mungu. Tutoe shukrani zetu za kawaida ya zawadi ya maisha na kulinda kwa dhati tusije kujutia jinsi tunavyonyanyasa mazingira yetu na maliasili, na kujua wajibu wetu kwa wanadamu wote kuelekea uumbaji wa Mungu. 

Wajibu wa pamoja katika kutetea Dunia na mabadiliko ya Tabianchi

Tamko la dhati la Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni(WCC),Dk.Olav Fykse Tveit,lililozinduliwa hivi karibuni na kwa kupitia barua ya kichungaji juu ya mabadiliko ya tabianchi iliyoelekezwa kwa Makanisa na jamii ya ulimwengu, amehimiza kuchukua hatua mara moja juu ya hali inayoendelea.

Na Padre Richard Kashinje - Vatican

Mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kutokea ulimwenguni yanaathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya watu na mali zao. Makanisa yanafanya jitihada kubwa, kwa mshikamano na kwa umoja katika kuondokana na hali hiyo mbaya, lakini ulimwengu bado haujatambua na kuziunga mkono jitihada hizo. Hati ya Baraza la makanisa ulimwenguni juu ya mbadiliko ya tabianchi ni Tamko la dhati la Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC), Dk. Olav Fykse Tveit, iliyozinduliwa hivi karibuni, na pia Kuna barua ya kichungaji juu ya mabadiliko ya tabianchi iliyoelekezwa kwa Makanisa na jamii zote za ulimwengu; kwavyo, Dk. Tveit amehimiza kuchukua hatua mara moja juu ya hali tete ya mazingira inayoendelea hivi sasa.

Madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi

Kwa kuzingatia kwamba hatari na uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya anga ni kubwa zaidi kuliko ile ambayo imeonekana hadi sasa - kwa kasi ya ongezeko la joto duniani - na kwamba, hatua zinazochukuliwa ili kuondokana na tatizo hilo haziendani na ukubwa wa tatizo lenyewe, katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) anawaalika waamini wote kuchukua hatua mahususi na za kibunifu katika kutetea dunia ili isielemewe na athari zisizoweza kushughulikiwa za majanga ya kiikolojia. Na kiongozi wa asasi ya kiekumenia anasema: “japo tumechelewa sana kuchukua hatua, lakini bado tunaweza kufanya mabadiliko ikiwa tutachukua hatua sasa! Kile tutakachokifanya katika miaka kumi ijayo kitasaidia kupunguza joto duniani, kitaamua mustakabali wa nyumba yetu ya kawaida na ya kipekee, yaani Dunia, kwa maelfu ya miaka ijayo”. Zaidi ya hayo, wajibu wa kutunza mazingira ni wa vijana na watu wote waishio katika mazingira hayo hatarishi ambapo haifai kufumbia macho hali hiyo. Kwa mfano watu asilia waishio katika sehemu zilizoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, waishio kwa mtindo wa kuheshimu mazingira, wapaaze sauti zao katika kutetea uoto wa asili. Barua ya kichungaji inaendelea kusema kuwa “kama ushirikiano wa makanisa, ni jukumu la lazima kurudia juhudi zetu za kutoa mchango mkubwa ili kuepusha athari mbaya inayoendelea katika mazingira yetu.

Utekelezaji katika kupambana na madhara hayo

Baada ya makubaliano ya kihistoria ya hali ya hewa kufikiwa huko Paris nchini Ufanransa, bado utekelezaji wake haujaridhisha katika mataifa mengi duniani. Na baada ya mazungumzo ya kikao cha 25 cha Mkutano wa Mataifa wa Jumuiya ya Mfumo wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi (COP 25) uliofanyika katika wiki mbili za kwanza za Desemba mwaka 2019 huko Madrid nchi Hispania, uchunguzi wa Tveit uligundua kuwa mataifa 200 yameshindwa kuchukua hatua stahiki katika kupambana na hali hiyo mbaya inayosababisha mabadiliko ya tabianchi. Matokeo yake yamekuwa yakukatisha tamaa kwani yanaweza kutafsiriwa kuwa ni ukosefu wa makubaliano makubwa ambayo yanalenga kutafuta zana muhimu katika kutatua shida hiyo. Kwa sababu hii, Wakristo kote ulimwenguni wamealikwa kuhamasika kwa nguvu ili kuweka shinikizo kwa maafisa wa umma kuchukua hatua nzuri katika kupambana na janga hilo la mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizo zitawapatia wakristo hao imani, kuwaondolea wasiwasi na kuamsha matumaini katika mioyo yao kwa siku zijazo.

Ulazima wa kujitolea kuunda masharti ambayo yanalenga uwekezaji wa kifedha

Tamko hilo pia linaongeza kuwa, viongozi wa mataifa yaliyoendelea zaidi kwa uchumi, ambao ndio wanaowajibika zaidi kwa uzalishaji wa hewa chafu aina ya kaboni, na vile vile wazalishaji wapya na wanaoibuka wa uchafuzi huu, lazima wazidi kujitolea kuunda masharti ambayo yanalenga uwekezaji wa kifedha kwa niaba ya jamii hizo ambazo zimeathirika sana kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa hiyo, kuna haja ya dharura ya kuendeleza miradi ili kupunguza uzalishaji wa gesi hatari usio na udhibiti, kuchangia fedha za kutosha na za ziada ili kuweza kutoa elimu ya kuweza kupambana na athari hizo na hatimaye joto la dunia lihifadhiwe kwa kiwango cha kawaida. Tveit anaonya kuwa, mipaka ya kitaifa kamwe haiwezi kupunguza kupanda kwa viwango vya bahari, gesi chafu, vimbunga na ukame.

Kuchukua hatua ya pamoja katika kulinda mazingira

Na barua ya kichungaji inasisitiza kuwa, ni wajibu wa kila mmoja tena kwa kujitoa kabisa kupambana na mabadiliko hayo ya tabianchi, kwani ni matokeo ya dhambi zetu za kiikolojia. Inaonekana dhahiri kwamba tumeshindwa muda mwingi kuzingatia mahitaji ya mazingira. Barua hiyo inabainisha pia kwamba tusipochukua hatua tutakuja kujutia kwani tutakumbuka ya nyuma (metanoia), na kama wahenga walivyosema “majuto ni mjukuu”. Ni jambo la lazima sasa kutafuta mioyoni mwetu na katika kanuni zetu za msingi za imani, mabadiliko mapya ya kiikolojia na mwongozo wa kimungu kwa hatua zetu zijazo, zinazolenga kujenga ujasiri katika changamoto hii isiyo ya kawaida ya milenia. Kama watu wa imani na nia moja ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kuungana, tukiimarishwa na mila zetu za kidini, kulinda uumbaji na viumbe vyote vilivyo hai, leo na vizazi vijavyo.

Mwaliko wa kutopoteza matumaini kwa Kristo Mwokozi

Tamko alilolitoa katibu mkuu Dk. Tveit linamalizia kwa kuwapa Wakristo wote mwaliko kwamba, kamwe wasipoteze tumaini kwa Kristo Mwokozi ambaye anatamani waishi kwa utulivu na ustawi wa maisha, na pia Kristo kamwe hamwachi mwanadamu peke yake katika nia yake njema ya kuunda ulimwengu bora. Na Rais wa Baraza la Makanisa ya Ulaya (KEK) Christian Krieger hivi karibuni alisema kuwa kutenda bila kuchelewa ni njia bora ya kumtukuza Mungu kama muumbaji pamoja na kutoa shukrani zetu za kawaida kwa zawadi ya maisha na kujutia jinsi tunavyonyanyasa mazingira yetu na maliasili, na kujua wajibu wetu kwa wanadamu wote kuelekea uumbaji wa Mungu.

MAZINGIRA
15 January 2020, 11:44