Tafuta

Vatican News
Kanisa limeiweka siku hii kuwa pia ni siku ya wote wanaishi maisha ya wakfu ili kwa mfano wa Bikira Maria mama mwenye usafi wa moyo,waweze kuzidi kuyatakatifuza maisha yao kwa fadhila hii ya usafi. Kanisa limeiweka siku hii kuwa pia ni siku ya wote wanaishi maisha ya wakfu ili kwa mfano wa Bikira Maria mama mwenye usafi wa moyo,waweze kuzidi kuyatakatifuza maisha yao kwa fadhila hii ya usafi.  (Vatican Media)

Siku ya Kutolewa kwa Bwana Hekaluni:Yesu anaingia hekalu lake kulitakasa na kutangaza hukumu!

Katika sherehe ya kutolewa Bwana hekaluni,Yesu anaonekana kuutimiza unabii kwa kuingia kwa mara ya kwanza hekaluni akisindikizwa na Maria na Yosefu.Kwa upande mmoja anapelekwa kutekeleza mapokeo yaliyomhusu kama myahudi lakini kwa upande mwingine ni yeye anayeliingia hekalu lake kulitakasa na kutangaza hukumu.

Na Padre William Bahitwa- Vatican

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu.  Tafakari ya leo ni ya adhimisho la sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni, sherehe ya kiliturujia inayoadhimishwa tarehe 2 Februari, siku ya 40 baada ya kuzaliwa Yesu ambayo kadiri ya tamaduni za kiyahudi ni siku ya kutakasika kwa mama na siku ya kumtolea hekaluni mzaliwa wake wa kwanza wa kiume.

Somo la kwanza (Mal 3:1-4) ni kutoka kitabu cha nabii Malaki. Somo hili linatoa unabii juu ya ujio wa masiha ambaye kabla ya kuja kwake, Mungu atamtuma kwanza mjumbe atakayemtengenezea njia. Huu ni unabii unaoonekana kuelezea kwa ukaribu kabisa ujio wa Yohane Mbatizaji aliyemtayarishia njia Kristo Masiha. Wakati huo huo unabii huu wa nabii Malaki unaeleza kuwa Masiha huyu anayengojewa atatokea hekaluni- “naye Bwana mnayemtafuta atalijia hekalu lake ghafula”. Masiha anayetokea hekaluni ni masiha aliye kuhani. Sambamba na ujumbe wa jumla wa nabii Malaki, masiha kuhani atakuja kulitakasa hekalu na kuutakasa ukuhani dhidi ya kufuru zilizokuwa zikifanywa na makuhani wa wakati wake.  Katika sherehe hii ya kutolewa Bwana hekaluni, Yesu anaonekana kuutimiza unabii huu kwa kuingia kwa mara ya kwanza hekaluni akisindikizwa na Maria na Yosefu. Kwa upande mmoja anapelekwa kutekeleza mapokeo yaliyomhusu kama myahudi lakini kwa upande mwingine ni yeye anayeliingia hekalu lake kulitakasa na kutangaza hukumu.

Somo la pili (Heb 2:14-18) ni kutoka katika waraka kwa Waebrania. Ni somo linaloeleza kuwa Kristo, kwa kuzaliwa kwake, alitwaa asili ya ubinadamu. Na kwa asili hiyo aliyapitia yote wanayoyapitia wanadamu kwa jinsi ya mwili. Yeye ambaye ndiye kuhani mkuu na mpatanishi wa wanadamu na Mungu, amekubali kuyapitia yote wanayopitia wanadamu – mateso, majaribu na mahangaiko yao mbalimbali- ili apate kujua namna ya kuwachukulia kwa rehema. Ni katika mwanga wa somo hili tunaona kuwa kutolewa kwake hekaluni kunaenda sambamba na njia ya ubinadamu aliyoitwaa. Anakuwa tayari kutimiza mila na tamaduni zilizowahusu wayahudi kama ilivyoelekeza sheria ya Musa.

Injili (Lk 2:22-40) ni kutoka kwa mwinjili Luka. Ni injili inayoeleza tendo lenyewe la kutolewa Yesu hekaluni. Tendo hili ambalo kwa wayahudi lilikuwa la kawaida kabisa, kwa Yesu linakuwa ni tendo linaloambatana na tukio jingine ambalo si la kawaida; nalo ni ujio wa Simeoni. Huyu hakuwa kuhani. Anatambulishwa tu kama mtu mwenye haki na mcha Mungu. Na kwa vile hakuwa kuhani hakutegemewa pia kuwa hekaluni wakati huo lakini ghafla anafika, anamchukua mtoto,  anambeba na anatamka maneno mazito juu ya mtoto na juu ya mamaye. Anapombeba mtoto anamshukuru Mungu kwa kutimiza ahadi yake. Simeoni hamwiti mtoto kwa jina lake wala hamwiti kwa jina la jumla mtoto bali anamwita wokovu na nuru. Anapombeba anasema “macho yangu yameuona wokovu wako na nuru ya kuwaangazia mataifa”. Zaidi ya hapo, Simeoni anatabiri kuwa Yesu atakuwa ni kwa ajili ya kuanguka na kuinuka kwa wengi na atakuwa ishara ya kunenewa.

Simeoni yaliashiria njia ya mateso ya Yesu

Atakuwa ni kwa ajili ya kuanguka na kuinuka kwa sababu ni yeye atakayekuwa kipimo cha uhusiano mpya ambao Mungu anakwenda kuuanzisha na watu wake. Wale watakaompokea kama kipimo na mwongozo wa maisha yao watainuka lakini wale wasiompokea wataanguka.  Neno “ishara ya kunenewa” katika muktadha wa majadiliano lilimaanisha hali ambapo wazungumzaji wanapopishana kauli. Tunapoyaangalia maisha ya Yesu hasa katika yale aliyokuja kuyakabili katika mashitaka, mateso na kifo msalabani tunaona ishara hii aliyozungumzia Simeoni haikuwa kupishana kauli tu bali ilienda zaidi ya hapo kumaanisha mapambano yaliyokuwa yakimsubiri. Kwa namna hii tunaona wazi kuwa maneno haya ya Simeoni yaliashiria njia ya mateso ya Yesu. Na sio mateso yake peke yake bali hata kwa Maria mamaye ambaye upanga mkali utaupenya moyowe. Maneno haya ya Simeoni ni maneno ya kinabii juu ya umasiha wa Yesu. Yesu mwenyewe atayarudia mara nyingi kwa wanafunzi wake kuonesha yeye ni Masiha wa namna gani. Ni katika unabii huu tunarudi kwa Simeoni na kuona kuwa katika ukawaida wake alikuwa pia ni mtu aliyejaa Roho Mtakatifu. Simeoni alikuwa anawakilisha kundi la wale watu wema, wenye haki na  wacha Mungu katika Israeli ambao walikuwa na matumaini ya kweli juu ya masiha.

Sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni ni sherehe ambayo Kanisa limeipatia alama nyingi 

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, sherehe hii ya kutolewa Bwana Hekaluni ni sherehe ambayo Kanisa limeipatia alama nyingi za kutusaidia kumuelewa, kumpokea na kumuishi Kristo masiha wa Bwana katika maisha yetu ya ufuasi. Kati ya alama hizo ni alama ya mwanga na ya usafi wa Maria. Sherehe hii pia huitwa sherehe ya mishumaa ambapo mwanzo wa Misa mishumaa hubarikiwa na waamini huingia huandamana na mishumaa inayowaka kuingia kanisani. Mishumaa hii ni ya kumkiri Kristo aliye mwanga halisi ambaye katika injili Simeoni anamkiri kama nuru ya kuwaangazia mataifa. Mwanga wa mishumaa unaingia kulijaza kanisa kama alivyotabiri nabii Malaki kuwa Kristo atalijia hekalu lake na kulijaza na utukufu wake. Kutoka katika tamaduni za kiyahudi, kwa sherehe hii Bikira Maria alitekeleza tamaduni za kutakasika kwake. Kwa Bikira Maria aliyezaliwa bila doa la dhambi huu haukuwa utakaso wa dhambi. Tunaweza kuliona hili kama tendo la Yesu kubatizwa ili kutimiza haki (Mt 3:15). Pamoja na hayo, kanisa limeiweka siku hii kuwa pia ni siku ya wote wanaishi maisha ya wakfu ili kwa mfano wa Bikira Maria mama mwenye usafi wa moyo, waweze kuzidi kuyatakatifuza maisha yao kwa fadhila hii ya usafi.

Wakfu wa sakramenti ya daraja, nadhiri na sakramenti ya ndoa

Fadhila hii ya usafi wa moyo sio kwa ajili ya wanaoishi maisha ya wakfu pekee, ni kwa ajili ya wote: walio ndani ya maisha ya wakfu kwa sakramenti ya daraja au nadhiri na hata walio nje ya maisha ya wakfu kwa sakramenti ya ndoa au wanaoishi peke. Sherehe hii ya leo inatualika kwa mfano wa Mama Bikira Maria kutafuta kutunza usafi katika fikra, katika maneno na  katika matendo. Na tena kujibidiisha kuziishi kiaminifu nadhiri na kutafuta kuutii na kuufuata mpango wa Mungu katika mahusiano. Kristo wokovu wetu na mwanga wa Mataifa azidi kutuongoza katika maisha yetu ya ufuasi na ya kumshuhudia.

KUTOLEWA KWA BWANA
31 January 2020, 16:20